Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

KHAWAARIJ                   Inaendelea ...

Amirul-Muuminina; Aliy-Allah amuwiye radhi-alipo maliza suala la Khawaariji, akawaamrisha wafuasi wake kwenda Shamu kupigana na Muawiya na washirika wake. Wakamwambia: Ewe Amirul-Muuminina! Hakika tumeishiwa zana za vita, mishale imetuishia, panga zetu na mikuki yetu imekuwa butu. Basi hebu na turudi mjini kwetu ili tufanye maandalizi.

Maneno yao haya, yanafahamisha kwamba watu wale tayari wamesha vunjika moyo na wamekimwa na vita. Ikiwa hiyo ndio hali ya jeshi, basi usije kushangaa hali iliyo mpata Amirul-Muuminina Aliy bin Abi Twaalib. Nguvu zake zikaanza kupungua kila siku, naye kila muda akiutumia ufasaha wake alio pewa na Allah kuwahimiza na kuwatia mori wa kuipigania dini. Lakini wapi, yote hayo hayakuwazidishia ila ulegevu, ni wachache tu miongoni mwao ndio walio mtakashia kauli na maneno. Kutokana na hali hiyo, Khawaariji wakapata nguvu na hoja yao waliyo iunda nayo si nyingine ila kwamba yeye amehukumiana na watu katika dini ya Allah na ilhali hapana hukumu ila ya Allah tu.

Na akawa katika jumla ya walio muasi Imamu, ni Al-Khiriit bin Raashid An-naahiy na kundi la watu mia tatu la ukoo wa Naahiya, akamuendea Imamu Aliy, akamwambia: Ewe Aliy! Wallah, sitaitii amri yako na wala sitaswali nyuma yako na hakika mimi nitajitenga nawe kesho. Imamu akamwambia: Kwa kufanya hivyo utakuwa umemuasi Mola wako Mlezi na utakuwa umeitangua ahadi yako. Na (kwa kufanya kwako hivyo) hauidhuru ila nafsi yako. Hebu niambie, kwa nini unafanya hivyo? Akajibu: Ni kwa sababu wewe umefanya “tahkiimu” na wale watu na umeinyongesha haki na umeegemea upande wa madhaalimu. Ni kwa ajili hiyo basi, mimi ninajitenga nawe na wao ni mwenye kuwalipia kisasi. Sayyidna Aliy akamwambia: Njoo nikusomeshe kitabu cha Allah na nifanye nawe mdahalo katika Sunna. Na nikupe ufunguzi wa mambo ambayo mimi ninayajua sana kuliko wewe. Basi huenda wewe ukayajua hivi sasa haya unayo yapinga. Akasema: Mimi ninakupa ahadi. Imamu akamwambia: Shetani asikughuri na wala wasikupaparishe watu majaahili. Wallah, ukitaka maongozi yangu na ukayakubali, bila ya shaka nitakuongozea kwenye njia ya uwongofu. Lakini wapi, Al-Khiriit hakuyasikia maneno mazuri hayo, huyo akaelekea upande wa Nafar na kundi lake.

Akamtuma Ziyaad bin Hafsah Al-Bakriy kuwafuatia na akamwambia: Nenda mpaka ufike kwenye maboma ya Abu Mousa, usubiri amri yangu hapo. Ziyaad akaenda mpaka akafika kwenye maboma ya Abu Mousa. Baada ya kuondoka kwake, Qurdhwah bin Ka’ab Al-Answaariy akamtumia ujumbe Imamu Aliy, akimwambia ya kwamba wafuasi wa Al-Khiriit wamemuua mmojawapo wa machifu ambaye alikuwa amesilimu. Kufuatia khabari hiyo, Sayyidna Aliy akampelekea ujumbe Ziyaad ya kwamba awafuatilie na awatake wamtoe mtu aliye muua mtemi muislamu. Akisha mtia mkononi, amrejeshe kwake na iwapo watakataa, apambane nao.

Ziyaad akaipokea amri ya Amirul-Muuminina, akawafuatilia mpaka akawakuta nyanda za juu, Ziyaad akamwambia Al-Khiriit: Ni lipi lililo kufanya uwe na kinyongo kwa Amirul-Muuminina na kwetu sisi, mpaka ukajitenga nasi? Akajibu: Mimi sijamridhia mtu wenu huyo kuwa Imamu (kiongozi) na wala sikuuridhia mwenendo wenu kuwa ndio mwenendo wa kufuatwa. Kwa minajili hiyo basi, nikaona bora nijitenge na nijiunge na lile kundi litoalo wito wa shura. Ziyaad akamuuliza: Hivi kweli watu wanaweza kukusanyika kwa mtu anaye lingana na mtu wako huyu uliye jitenga naye, kwa kumjua Allah, kanuni zake na kitabu chake. Pamoja na udugu wake na Mtume wa Allah na utangu wake katika Uislamu? Al-Khiriit akasema: Mimi sisemi hapana katika yote hayo. Ziyaad akamuuliza: Ikiwa hivyo ndivyo, basi ni kwa lipi umemuua muislamu uliye muua? Akajibu: Sikumuua mimi, lakini ameuawa na kundi la wafuasi wangu. Akamwambia: Basi wasalimishe (hao wauaji) kwangu. Akasema: Mimi sina njia ya kulifanya hilo. Kwa kukataa kwake kuwasalimisha wauaji ili wachukuliwe kisasi, kamanda Ziyaad akalazimika kupambana nao. Akapambana nao mpaka usiku, wakazidiwa nguvu na kiongozi wao Al-Khiriit akakimbia.

Ziyaad alipo uona utimua mbio huo, na kusambaratika kwa genge la waasi hao, akaamua kurejea Basrah ili kuwaganga majeruhi alio nao. Na akamtumia Imamu Aliy taarifa ya kazi aliyo mtuma na namna mambo yalivyo jiri. Kisha ndipo akamtuma Ma’aqal bin Qays Ar-riyaahiy kukiongoza kikosi cha askari elfu mbili, kwenda kupambana na Khawaariji. Na akamwandikia waraka Ibn Abbas aliyeko Basrah, amuongezee nguvu kwa kikosi cha watu elfu mbili cha wenyeji wa Basrah, kiongozwe na mtu mwenye weledi wa vita. Ma’aqal akasonga mbele na ikaungana nae ile nguvu ya wazalendo wa Basrah, wakawakuta Khawaariji karibu ya mojawapo ya majabali ya Raamahurmuz. Wakaingia mapambanoni nao mpaka wakauawa katika watu wa Ma’aqal kiasi cha askari sabini, Al-Khiriit na baadhi ya wafuasi wake wakazidiwa nguvu, wakatimua mbio tena. Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-akamuamrisha kamanda Ma’aqal awafuatilie mpaka awasage wote na kuukata mzizi wa fitina. Kamanda Ma’aqal akaipokea amri hiyo, haraka akawafuatilia, akawaangushia kisago kikali mpaka akawafyeka wote na akamuua na kiongozi wao Al-Khiriit.

Baada ya hapo, likafumuka wimbi la uasi dhidi ya Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy, yakaasi makundi mengi ya Khawaariji. Kila alipo jaribu kuuzima moto wa fitina wa kundi moja, ndipo lilipo ibuka kundi jingine.

Ama tukirejea kwa upande wa Muawiyah, yeye tangu alipo pewa kiapo cha utii cha ukhalifa, mambo yalimuendea vema huko Shamu. Na watu wake wakawa ni jeshi la kupigiwa mfano katika utii kwa kiongozi wao. Kutokana na unyoofu huo wa hali na mambo, akaona sasa ni fursa yake ya kuwakusanya Waislamu wote chini ya utii wake, kama alivyo kuwa akitaka kufanya hivyo Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi. Katika kuitekeleza kivitendo fikra yake hii, akaamua kumtuma balozi wake Misri; Amrou bin Al-Aaswi. Na khabari ya Misri ilikuwa kwamba Imamu Aliy alikwisha pata kiapo cha utii kutoka kwa watu wa huko. Alimtuma huko Qays bin Sa’ad bin Ubaadah, kama tulivyo tangulia kueleza. Balozi huyu wa Imamu kwa watu wa Misri, alipo fika huko wengi wa watu wa Misri walimkubali Sayyidna Aliy na wakambai. Isipo kuwa kundi dogo miongoni mwao, ambalo lilijitenga katika sehemu ya “Kharabtaa”, likiongozwa na Yazid bin Al-Haarith Al-Mudlajiy. Kundi hili lilishikilia na kuyatumia mauaji ya Sayyidna Uthman, kufanya uasi dhidi ya Amirul-Muuminina na kuitumia fursa hiyo kupata waunga mkono. Akajiunga na kundi asi hili, Maslamah bin Mukhallad, gavana Qays yeye akajizuia kujiunga nalo, kwa kujua kwamba hilo si kundi hatari. Imamu Aliy alipo lifahamu hilo, akamuandikia Qays waraka amrishi/elekezi, akimuamrisha kuwapiga vita waasi hao, kwa kuuzingatia msingi usemao “Chanzo cha moto mkubwa, ni cheche ndogo”. Qays akamuandikia Imamu Aliy waraka rejezi: (Ama baad...Ninakushangaa, unaniamuru kuwapiga vita watu ambao wamejizuia kukufanyia uadui na ambao wanashughulika na adui yako! Na tutakapo waghadhibisha, watamsaidia adui yako dhidi yako. Basi nakuomba unitii, ewe Amirul-Muuminina na uachane nao. Kwani fikra sahihi ni kuwaacha. Wassalaamu).

Kufuatia kuikaidi kwake amri halali ya Amirul-Muuminina, Sayyidna Aliy akamuuzulu katika kiti cha ugavana wa Misri na akamtawaza mahala pake Muhammad bin Abubakar As-siddiq. Gavana mteule; Muhammad alipo fika Misri, akasema: (Kila sifa za jinsi kamali ni stahiki yake Allah, ambaye ametuongoza sisi na nyinyi katika ile haki waliyo khitalafiana kwayo watu. Na ambaye ametuonyesha sisi nanyi yale ambayo wamepatwa upofu nayo watu majaahili. Ehee fahamuni ya kwamba Amirul-Muuminina amenitawalisha uongozi wenu na ameniusia mliyo yasikia. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Allah, kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea. Basi mkiona katika uongozi wangu na kazi zangu utii, muhimidini Allah kwa hayo kwani hakika Yeye ndiye Muongozi. Na iwapo mtamuona mtendaji wangu yeyote hakutenda haki, basi leteni mashitaka kwangu na mnilaumu kwa sababu yake. Kwani mimi nitafurahi sana ikiwa mtafanya hivyo, nanyi mnastahiki kufanya hivyo. Allah atuwezeshe sisi nanyi kutenda matendo mema kwa rehema zake). Alipo maliza khutba yake akashuka mimbarini.

Na baada ya mwezi mmoja tangu kuwasili kwake Misri, akawatumia ujumbe watu wale walio jitenga huko Kharabtaa, akiwapa khiyari ya ama kumtii Amiri au kuondoka Misri. Wakamjibu sisi hatuyafanyi yote hayo, hebu tuache tuangalie suala letu litakuwaje, usifanye haraka kutupiga vita. Gavana mteule akawakatalia hilo. Nao wakajitia ngomeni na kuwa katika hali ya tahadhari na gavana Muhammad. Ilipo patikana tahkiimu, wakawa na tamaa nayo na wakamtupia maneno ya kejeli. Kufuatia uchokozi huu gavana akaamua kuchukua hatua, akawapelekea kikosi kuwapiga, waasi wale wakakizidi nguvu kikosi cha gavana Muhammad na wakamuua kiongozi wake. Akatuma kikosi kingine, nacho pia akauwa kiongozi wake. Kisha akatoka Muawiya bin Khudeiji As-sakuuniy akitaka kisasi cha damu ya Sayyidna Uthman. Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-alipo pata khabari hiyo, akaona hali ya Misri imesha kuwa tete na kwamba Muhammad hawezi kupambana. Ndipo akafikia uamuzi wa kumuengua na nafasi yake ikashikwa na Al-Ashtar bin Al-Haarith An-nakh’iy. Na akamuandikia usia ambao alikusanya ndani yake siasa ya Dunia na utengevu wa Akhera. Kwa bahati mbaya, gavana huyu mpya akafa akiwa njiani kuelekea Misri kukalia kiti cha ugavana. Muhammad bin Abubakar kukamuwia uzito kuuzuliwa kwake, kufuatia hali hiyo Imamu Aliy akamuandikia waraka:

(Ama baad...Hakika imenifikia khabari ya kughadhibika kwako kutokana na kumteua kwangu Al-Ashtar kushika nafasi yako. Nami sikulifanya hilo ila ni kwa ajili ya kuongeza jitihada zako kwangu, lau kitakuponyoka kilichoko mkononi mwako, nitakutawalisha kilicho chepesi kwako na kinacho pendeza mno kwako. Hakika huyo mtu ambaye nilikuwa nimemtawalisha uongozi wa Misri, alikuwa ni mtu mwenye nasaha kwetu na ni mwenye nguvu kwa adui yetu. Naye amekwisha zikamilisha siku zake za kuishi na amekutana na mauti yake hali ya kuwa sisi tu radhi naye, basi tunamuomba Allah naye amuwiye radhi na amrudufishie thawabu.

Msubirie adui yako na uvipanyie vita na ulinganie kuelekea kwenye njia ya Mola wako Mlezi, kwa hekima na mawaidha mema. Na kithirisha kumdhukuru Allah na kumuomba msaada, na umkhofu naye atakutoshea na ya kutatizayo na atakuauni {atakusaidia} katika utawala wako).

Muhammad naye akamuandikia Amirul-Muuminina kumjibu waraka wake: (Ama baad ... Nimeupokea na kuufahamu waraka wako na hapana yeyote katika watu anaye iridhia mno rai ya Amirul-Muuminina, wala mwenye kumtaabisha mno adui yake, wala mwenye huruma mno kwa mtawalishwa wake, kuliko mimi. Nami nimekwisha toka na kupiga kambi na nimewapa amani watu wote ila wale walio tuwashia moto wa vita na kutukhalifu. Nami ninaifuata amri ya Amirul-Muuminina na ninailinda. Wassalaamu).



 


 | Tuandikie |