Kusema
kwao ya kwamba Allah hakumteremshia mwanaadamu chochote, na Allah
kumlakinia (kumfundisha) Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-jibu
rejezi linalo ufedhehi uongo wao.
Allah
Ataadhamiaye anasema: “NA HAWAKUMKADIRIA ALLAH KWA HAKI YA KADRI
YAKE, WALIPO SEMA: ALLAH HAKUMTEREMSHIA MWANAADAMU CHOCHOTE. SEMA:
NANI ALIYO TEREMSHA KITABU ALICHO KUJA NACHO MUSA, CHENYE NURU NA
UWONGOFU KWA WATU. MLICHO KIFANYA KURASA KURASA MKIZIONYESHA, NA
MENGI MKIYAFICHA. NA MKAFUNZWA MLIYO KUWA HAMYAJUI NYINYI WALA BABA
ZENU? SEMA: ALLAH. KISHA WAACHE WACHEZE KATIKA POROJO LAO”. [06:91]
Wanazuoni
wetu-Allah awarehemu-katika kuelezea sababu za kushuka kwa aya hii,
wametaja riwaya nyingi. Miongoni mwazo, ni kwamba Maalik bin
As-swaif; Muyahudi, huyu alizozana na Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-katika mas-ala fulani. Mtume wa Allah akamwambia: Mimi
ninamuapia Allah wewe hupati (aya) katika Taurati (inayo sema) kwamba
Allah anamchukia mtu mzima mnene – na huyu Ibn As-swaif alikuwa ni
mnene. Ndipo (Ibn As-swaif) akasema: “Allah hakumteremshia
mwanaadamu chochote”. Baadhi ya wafuasi wake wakasema: Ole ni wako
na wala si wa Musa. Ndipo Allah Ataadhamiaye akaiteremsha aya hii.
Maana
ya aya:
Ni
kwamba Mayahudi hawa hawakumuadhimisha Allah Ataadhamiaye ipasavyo
kumuadhimisha. Na hawakumjua ipasavyo kumjua katika kuwaonea kwake
upole na huruma waja wake. Lakini wao wakazinyongesha kwa kiwango
kikubwa haki zake na hilo likawapelekea kupotea upotovu mkubwa, kwa
kuwa wao walikanusha kuletwa kwa Mitume na kuteremshwa kwa vitabu.
Ndipo wakayasema yale maneno yao mabaya, nayo si mengine ila ni kule
kudai kwao ya kwamba Allah Ataadhamiaye hakumteremshia mwanaadamu
chochote. Walilo likusudia kwa maneno yao haya mabaya: Ni kuutukana
utume wa Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na kuitukana
Qur-ani kuwa haitoki kwa Allah.
Allah
Ataadhamiaye akamuamrisha Mtume wake awajibu kwa majibu rejezi
yatakayo zitia ububu ndimi zao, akasema: “SEMA: NANI ALIYO TEREMSHA
KITABU ALICHO KUJA NACHO MUSA, CHENYE NURU NA UWONGOFU KWA WATU”.
Yaani: Sema, ewe Muhammad! Waambie hao wanao dai ya kwamba Allah
hajamteremshia mwanaadamu chochote. Basi hebu waulize ni nani aliye
iteremsha Taurati, ambayo ni kitabu alicho kuja nacho Musa, kikiwa ni
“NURU NA UWONGOFU KWA WATU”. Yaani: Ni mwangaza unao zagaza
kutoka kwenye kiza cha ujaahili, tena ni uwongofu unao hifadhi dhidi
ya batili na upotofu.
Kisha
Allah-utakati wa mawi ni wake-akabainisha upotoshaji wa maana na
ubadilishaji wa maana ulio fanywa na wapingaji kwenye vitabu vyake,
akasema: “MLICHO KIFANYA KURASA KURASA MKIZIONYESHA, NA MENGI
MKIYAFICHA”. Yaani: Mnakifanya kitabu hiki ambacho Allah
Ataadhamiaye amekiteremsha kuwa ni nuru na uwongofu, mnakifanya kuwa
kurasa kurasa zilizo tapanyika. Mnafanya hivyo ili mpate upenyo wa
kukidhihirisha kile mnacho kitaka nyinyi kidhihirike na kifahamike na
watu katika kurasa hizo. Na myafiche mengi katika kurasa hizo kwa
mujibu wa matashi ya nafsi zenu zenye maradhi na matamanio yenu yenye
madhambi.
Muradi/mapendeleo
ya sentensi hii tukufu, ni kuwalaumu na kuwaumbua wale wanao
badilisha vitabu vya Allah. Ambao makusudio yao ya nyuma ya pazia la
upotoshaji/ubadilishaji huo, ilikuwa ni kuutukana utume wa Nabii
Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Na kupata njia ya mkato ya
kuyafikia matashi na matamanio yao.
Na
kauli yake Allah “NA MKAFUNZWA MLIYO KUWA HAMYAJUI NYINYI WALA BABA
ZENU”. Yaani: Na mkafundishwa kupitia ulimi wa Muhammad, yale
ambayo nyinyi wala baba zenu hamkuwa mkiyajua. Mkafundishwa
maarifa/elimu ambazo mtu mweledi hapati shaka kwamba elimu hizo ni
uteremsho wa Mungu Mwenyezi.
Na
kauli yake Allah: “SEMA: ALLAH. KISHA WAACHE WACHEZE KATIKA POROJO
LAO”. Yaani: Sema ewe Muhammad, uwaambie hao wakanushaji: Allah
Ataadhamiaye ndiye ambaye aliye mteremshia Musa kitabu. Kisha baada
ya kuwaambia maneno hayo ya upambanuzi, waache katika batili yao
wacheze na porojo lao.
Na
Allah kumuamrisha Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-awajibu, amri
hiyo inaleta hisia ya kwamba jawabu ni lazima na hakuna imkani ya
njia nyingine. Na ni uzindushi ya kwamba wao wamepigwa na butwaa
kiasi cha kushindwa kutoa jawabu.
Kwa
maelezo haya basi, aya tukufu inakuwa imewarudi kwa jawabu madhubuti
lifikishalo mno ujumbe. Jawabu lililo waacha wao katika
utoshewa/udangani na lililo wafanya watu weledi kustaajabu kuipinga
kwao hata Taurati ambayo Allah Ataadhamiaye alimteremshia Nabii
Musa-Amani imshukie-kwa ajili ya kuwaongoza wao.
|