Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

WARITHI WA ROBO NA SHARTI ZA KURITHI KWAO

  1. Wapatao (wenye kurithi) robo (1/4) na sharti za kurithi kwao hiyo robo:

Katika mbea za warithi, wanao stahiki kupata robo (1/4) ya tarika, ni watu wawili:

  1. MUME:

Mume wa maiti anastahiki kurithi robo ya mali yote iliyo achwa na marehemu mke wake, kwa sharti ya kuwa marehemu asiwe ameacha:

  1. Mtoto wake mwenyewe, au

  2. Mtoto wa mtoto wake mwanamume na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu.

Ni mamoja mtoto aliye achwa na marehemu, ni wa mume huyu (mrithi) au si wake, na ni sawa sawa mtoto huyo ni wa kike au wa kiume.

Na dalili/ushahidi wa hili, ni kauli yake Allah Atukukiaye: “...WAKIWA NA MTOTO BASI FUNGU LENU NI ROBO YA WALICHO KIACHA...”. [04:12]

Tumesha tangulia kusema na tunasema tena hapa: Ya kwamba mtoto wa mtoto wa kiume (mjukuu wa maiti kwa mtoto wake wa kiume), ni kama/sawa na mtoto wake maiti. Usawa huo ni katika kurithi, hajbu (kuzuia kurithi) na katika uasaba.

  1. MKE/WAKE:

Mke/wake wa marehemu anastahiki/wanastahiki kupata robo ya tarika, kwa sharti kwamba marehemu hakuacha:

  1. Mtoto wake mwenyewe, au

  2. Mtoto wa mtoto wake mwanamume, na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu. Japo huyo mtoto/mtoto wa mtoto wake huyo hakuzaa na mke/wake hao.

Na ushahidi wa hili, ni kauli yake Allah Atukukiaye: “...NA WAKE ZENU WATAPATA ROBO MLICHO KIACHA, IKIWA HAMNA MTOTO...”. [04:12]



  1. Wapatao thumni (1/8) na sharti za kurithi kwao hiyo thumni:

Anaye rithi thumni katika tarika ya maiti, ni mke/wake. Fungu la wake ni hiyo hiyo thumni hata kama watakuwa ni wane, watagawana hiyo. Mke/wake watarithi thumni kwa sharti ya kwamba maiti ameacha:

  1. Mtoto wake mwenyewe, au

  2. Mtoto wa mtoto wake mwanamume, na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu.

Ni mamoja huyo mtoto au mtoto wa mtoto mwanamume wa marehemu, ni mwanamume au mwanamke.

Dalili ya hili, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “MKIWA MNA MTOTO BASI SEHEMU YAO NI THUMNI YA MLICHO KIACHA...”. [04:12]



SOMO LA SABA

  1. Wapatao theluthi mbili (2/3) na sharti za kurithi kwao hizo theluthi mbili:

Wanao rithi theluthi mbili katika warithi, ni mbea nne za wanawake, na kila mbea inazo sharti zake stahikishi, tunazitaja kama ifuatavyo:

  1. BINTI WAWILI NA ZAIDI WA MAITI:

Kumeshurutizwa katika kurithi kwao theluthi mbili ya tarika, sharti moja tu, nalo ni kutokuwepo na ndugu yao mwanamume (Asaba) – ambaye ni mtoto mwanamume wa maiti.

Na ushahidi wa kurithi kwao hizo theluthi mbili, ni kauli yake Allah Atukukiaye: “...NA IKIWA WANAWAKE ZAIDI YA WAWILI, BASI WATAPATA THELUTHI MBILI ZA ALIZO KIACHA MAITI...”. [04:11]

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwahukumia mabinti wawili wa Sa’ad kupata theluthi mbili ya tarika ya baba yao”. Tirmidhiy [2093] & Al-Haakim [04/334]-Allah awarehemu.

  1. BINTI WAWILI WA MTOTO MWANAMUME WA MAITI, NA KWENDA CHINI KWA KUPITIA KWA WANAMUME WATUPU:

Hawa watastahiki kurithi theluthi mbili kwa kupatikana sharti mbili hizi:

  1. Maiti asiwe na mtoto wake mwenyewe, au mtoto aliye karibu kwa daraja kuliko yeye.

  2. Wasiwe pamoja na ndugu mwanamume, wa daraja moja (ambaye ni Asaba).

Na dalili ya mabinti wa mtoto mwanamume wa maiti kurithi theluthi mbili, hakika si vinginevyo ni qiyaasi kilicho twaliwa kwa mabinti wa maiti mwenyewe (shangazi zao hao watoto). Au dalili ni kule kuingia kwao chini ya tamko “MABINTI”, kwa kujengea hoja ya kwamba tamko hilo hutumika katika hakika yake na katika majaazi (uazimwa) yake.

  1. DADA WAWILI NA ZAIDI WA MAITI WA KWA BABA NA MAMA (SHAQIQA):

Hawa wanarithi theluthi mbili kwa sharti tatu:

  1. Wasiwe pamoja na ndugu mwanamume (kaka), wa daraja moja (ambaye kwao ni Asaba).

  2. Maiti asiwe na mtoto wake mwenyewe. Au mtoto wa mtoto wake mwanamume na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu.

  3. Maiti asiwe na baba au babu.

Na dalili ya kurithi kwao theluthi mbili, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “...NA IKIWA WAO NI NDUGU WA KIKE WAWILI, BASI WATAPATA THULUTHI MBILI ZA ALICHO ACHA MAITI...”. [04:176]

  1. DADA WAWILI NA ZAIDI WA MAITI WA KWA BABA TU:

Hawa watarithi theluthi mbili kwa sharti nne; zile tatu tulizo tangulia kuzitaja kwa madada shaqiqa. Na sharti ya nne inayo ongezeka, ni: Maiti kutokuwa na ndugu mwanamume wa kwa baba na mama au ndugu mwanamke wa kwa baba na mama.

Na dalili ya kurithi dada wawili wa maiti wa kwa baba tu, ni Ijmaa. Kwani Ijmaa imekongamana ya kwamba aya hiyo iliyo tangulia kutajwa hapo juu, hakika si vinginevyo, imeshuka ikiwakhusu dada wa kwa baba na mama (SHAQIQA) na dada wa kwa baba tu, bila ya dada wa kwa mama.

Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Abdillah-Allah amuwiye radhi-amesema: Niliugua, akaja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kunikagua (kunijulia hali), akanikuta nimezimia. Akaja akiambatana na Abubakar na Umar wakitembea kwa miguu. Basi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatawadha, kisha akanimwagia maji yake ya udhu, nikazinduka. Nikasema: Ewe Mtume wa Allah! Nihukumu (nigawe) vipi mali yangu? Au nifanyeje katika mali yangu? Mtume hakunijibu kitu. – Na alikuwa na dada tisa – Mpaka ilipo teremka aya ya mirathi: {WANAKUOMBA UHUKUMU; SEMA: ALLAH ANAKUPENI HUKUMU JUU YA MKIWA...”. [04:176]

Tirmidhiy [2098]-Allah amrehemu.

Ukamilifu wa aya: “...IKIWA MTU AMEKUFA, NAYE HANA MTOTO, LAKINI ANAYE NDUGU WA KIKE, BASI HUYO ATAPATA NUSU ALICHO ACHA MAITI. NA MWANAMUME ATAMRITHI NDUGU WA KIKE IKIWA HANA MWANA. NA IKIWA WAO NI NDUGU WA KIKE WAWILI, BASI WATAPATA THULUTHI MBILI ZA ALICHO ACHA MAITI. NA WAKIWA NDUGU WANAUME NA WANAWAKE, BASI MWANAMUME ATAPATA SEHEMU ILIYO SAWA NA YA WANAWAKE WAWILI. ALLAH ANAKUBAINISHIENI ILI MSIPOTEE; NA ALLAH NI MJUZI WA KILA KITU”.

Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Aya hii imeshuka ikinikhusu (kwa sababu yangu).

  1. Wapatao theluthi moja (1/3) na sharti za kurithi kwao hiyo theluthi:

Wanao pata fungu la theluthi moja (1/3) miongoni mwa warithi, ni wawili tu, nao ni:

  1. MAMA:

Mama wa maiti, atarithi theluthi ya tarika ya mwanawe kwa sharti mbili hizi:

  1. Maiti asiwe na mtoto wake mwenyewe. Au mtoto wa mtoto wake mwanamume, na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu.

  2. Maiti asiwe na ndugu mwanamume au mwanamke zaidi ya mmoja. Wakiwa ndugu hao ni wa kwa baba na mama (MASHAQIQI), au wa kwa baba tu, au wa kwa mama tu.

Dalili ya mama kurithi theluthi moja kwa sharti hizi tulizo zitaja, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “...AKIWA HANA MTOTO, NA WAZAZI WAKE WAWILI WAMEKUWA NDIO WARITHI WAKE, BASI MAMA YAKE ATAPATA THULUTHI MOJA...”. [04:11]

  1. NDUGU ZAIDI YA MMOJA WA KWA MAMA TU; WANAMUME AU WANAWAKE:

Ndugu wa maiti wa kwa mama yake wanarithi theluthi ya tarika ya marehemu ndugu yao. Wote hawa wanamume na wanawake watashirikiana kurithi hiyo theluthi (1/3) kwa usawa; bila ya tofauti baina ya wanamume na wanawake. Watapata theluthi kwa sharti zifuatazo:

  1. Maiti asiwe na mtoto wake mwenyewe. Au mtoto wa mtoto wake mwanamume na kwenda chini kwa kupitia wanamume watupu.

  2. Maiti asiwe na baba au babu.

Dalili ya kurithi kwao theluthi, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “...NA WAKIWA ZAIDI KULIKO HIVYO, BASI WATASHIRIKIANA KATIKA THULUTHI”. [04:12]

Na ushirikiano huu unao tajwa na aya, unahukumia usawa baina yao, kama tulivyo kwisha kusema.

Naam, hivyo ndivyo ilivyo, lakini babu naye anarithi theluthi katika baadhi ya hali zake anapo kuwa pamoja na ndugu. Ufafanuzi wa hili utaelezwa katika mlango wa babu na ndugu, INSHALLAH.

   



| Tuandikie |