|
Uislamu
ni ujumbe wa kheri na salama/amani na upole kwa jamii yote ya
wanaadamu. Na Allah Ataadhamiaye amekwisha mwambia Mtume wake: “NASI
HATUKUKUTUMA ILA UWE NI REHEMA KWA WALIMWENGU WOTE”. [21:107]
Na
sura zote za Qur-ani Tukufu zimeanzwa na
“BISMILLAAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM” – Kwa jina la Allah, Mwingi wa
rehema, Mwenye kurehemu.
Lakini
mbwa mwitu walio jificha nyuma ya sura ya binaadamu, hawataki ila
kuikingama rehema/huruma huru hii. Na wakaweka miamba katika mapito
yake ili kuzuia mito ya rehema/huruma isiwafikie watu. Kwa minajili
hiyo basi, watu waangamie katika mawanda ya udangana na ujaahili
kutokana na kuyakosa maji ya mito ya rehema. Kwa ajili hiyo basi,
ndio ikawa hapana budi kuviondosha vikwazo hivyo na kuwafanyia ugumu
wadau wa vikwazo hivyo. Na siku utakapo katika upinzani na ukaidi wao
huo, ndipo rehema hii jumuishi itakapo waenea. Na rehema hii haina
mapungufu, lakini hakika si vinginevyo, mapungufu yako kwa yule aliye
inyima nafsi yake fungu katika rehema hiyo. Hivi ewe ndugu msomaji
mwema, huoni ya kwamba rehema ya Allah imevienea vitu vyote! Lakini
pamoja na ukweli huo basi, rehema hiyo hatoipata mshirikina wala
mkanusha Mungu: “...NA REHEMA YANGU IMEENEA KILA KITU. LAKINI
NITAWAANDIKIA KHASA WANAO MCHAMNGU, NA WANAO TOA ZAKA, NA WALE AMBAO
WANAZIAMINI ISHARA (aya) ZETU. AMBAO KWAMBA WANAMFUATA HUYO MTUME,
NABII, ASIYE SOMA WALA KUANDIKA...”. [07:156-157]
Kama
unavyo sema: Ukumbi huu una uwezo wa kuchukua watu elfu moja, lakini
haruhusiwi kuingia humo ila tu yule aliye na tiketi. Basi baadhi ya
watu watakao kataa kukata tiketi za kuingilia na hilo likapelekea wao
kuzuiwa kuingia ukumbini, kwa sababu ya kutokuwa na tiketi. Wakabakia
nje, kubakia kwao huko nje, hakuwi ni dosari katika ukunjufu (ukubwa)
wa ukumbi.
Na
mfano wa hilo, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Umati
wangu wote wataingia peponi, ila yule atakaye kataa. Wakauliza
(maswahaba): Ni nani huyo atakaye kataa? Akajibu: Atakaye nitii, huyo
ataingia peponi. Na atakaye niasi, huyo ndiye aliye kataa”.
Bukhaariy-Allah
amrehemu.
Na
hupata kutokezea mara nyingine rehema ya kweli, ikavaa chapa ya
ukatili, lakini kihakika si hivyo kabisa. Sote tumepata kushuhudia
watoto wetu wakisindikizwa kwa bakora kwenda shule na wanahifadhi
masomo yao kutokana na ukali wa mwalimu. Hili katika taswira yake ya
nje linaweza kuonekana kuwa ni ukatili kwa watoto, ambao wanahitajia
mno huruma ya wazazi na jamii kwa ujumla. Lakini sivyo kabisa, kwani
lau watoto wetu hao wataachwa kufuata matashi na mapenzi yao hayo ya
kitoto; yasiyo jua maslahi na manufaa yao. Basi bila ya shaka,
wangeli angamizwa na pumbao na mchezo na wangeli fikia umri wa
majukumu (ujana) wakiwa hawana walijualo si tu katika dini yao bali
pia hata katika Dunia yao. Na tabibu pale anapo upasua mwili wa
mgonjwa, hutumia kisu chake kikali ili kukata nyama. Na pengine
hulazimika kuvunja mfupa na hata kukata kiungo. Hili nalo laweza
kuonekana kuwa ni ukatili, lakini ukweli ni kwamba daktari hafanyi
hivyo ila ni kwa kumuhurumia mgonjwa na kutaka arejewe na afya yake
aliyo pokonywa na ugonjwa huo.
Haikuwa
rehema ni hisia huba zisizo ambatana na akili na wala si upendo unao
kinzana na uadilifu na nidhamu/utaratibu. La hasha! Si hivyo kabisa,
hakika rehema ya kweli, ni zile hisia zinazo zichunga haki zote hizi.
Bila ya shaka mandhari ya mtu aliye hukumiwa kunyongwa, akiwa
ananing’inia manyongeoni ilhali mwili wake ukiwaya waya hewani. Na
macho yake yaingiayo kiza yakiutamani mwanga na kutafuta uwokovu.
Hayo ni mandhari yanayo vuta hisia za huruma, na lau hisia hizo
zingeli itikiwa haraka na muuaji akaachiwa huru, basi kwa yakini
ardhi ingeli jaa fujo/ghasia na uhovyo hovyo. Hiyo ndio huruma ya
yale yanayo itwa mashirika ya kutetea haki za binaadamu, yanayo piga
kelele za kufutwa kwa adhabu ya kifo. Hivi ni kweli binaadamu ana
huruma zaidi kwa binaadamu mwenzake, kuliko Yule aliye waumba?! Hebu
tuwe wakweli na tuwe huru, tusiongozwe na akili za viumbe kama sisi.
Tukubali kuwa rehema/huruma ya kweli imo ndani ya kutozipa nafasi
hisia kama hizo “MTAKUWA NAO UHAI MZURI KATIKA KULIPIZA KISASI ENYI
WENYE AKILI, ILI MSALIMIKE”. [02:179]
Enyi
wanaadamu! Hakika rehema ya Allah kwenu ni kubwa kwa hii hukumu ya
kisasi. Kwa fadhila ya kisasi jamii yenu ina hakika kupata maisha ya
amani na salama. Haya ni kwa kuwa mwenye kutaka kuua akijua kuwa naye
atauawa, atajizuia kutenda alilo likusudia. Kwa hiyo yeye na yule
ambaye angeli uawa wanahifadhika. Wenye akili na wazingatie faida ya
sharia ya kisasi, hilo litawapelekea kuutambua upole wa Allah kwao
kuendea njia ya uchaMngu, na kuzifuata amri za Allah.
Hakika
ukatili unao laaniwa na kushutumiwa na Uislamu, ni ule ukavu/ugumu
uliomo ndani ya nafsi ambao hauna mafungamano na mantiki wala
uadilifu. Hakika ukatili huo ni maovu yaliyo jaa ubaya/uovu na
adha/kero/bughdha, yanayo anzishwa na ubinafsi/umimi menyu na
matamanio pofu. Ama rehema/huruma, hakika hiyo ni athari ya uzuri wa
Kimungu, iliyo salia katika tabia/hulka/silka ya watu, inayo
waongozea na kuwapelekea kwenye wema. Athari hiyo ndio inayo
watunukia katika nyakati za mizozo songefu, upepo roho mwanana unao
changamsha maisha na kuburudisha nyoyo. Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-amesema: “Hakika
Allah Ataadhamiaye siku alipo umba mbingu na ardhi, (pia) aliumba
rehema mia moja. Kila rehema moja ni tabaka baina ya mbingu na ardhi.
Akaweka katika ardhi rehema moja kutoka kwenye (tabaka) hilo. Katika
hilo mzazi humuonea huruma mwanawe na mnyama mwitu na ndege (huoneana
huruma) wao kwa wao”. Muslim-Allah
amrehemu.
Kama
ambavyo inavyo mea na kukua akili kwa kupata elimu/maarifa mbali
mbali, ndivyo hivyo rehema hii nayo humea na kukua kwa njia mbali
mbali na ikatanuka. Ama ikiachwa hivi hivi tu, basi hunyauka na
hatimaye hufa na hapo ndipo mwenye nayo huwa kuni ya Jahannamu.
Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira-Allah amuwiye
radhi-amesema: Nilimsikia
ambaye yeye ni Mkweli; mwenye chumba hiki, Abul-Qaasimu-Rehema na
Amani zimshukie-akisema: “Haiondolewi rehema ila kwa mtu muovu”.
Abu
Daawoud-Allah amrehemu.
Na
Uislamu umewatanabahisha Waislamu ya kwamba yapo makundi maalumu ya
watu ambao jamii inatakiwa iwape ziada ya rehema/huruma na uangalizi.
Miongoni mwao ni “Dhawil-Arhaam” – hawa ni ndugu wa umamani.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Wenye
kuwahurumia (wenzao) watarehemewa na Allah Ataadhamiaye, waoneeni
huruma walioko ardhini atakuhurumieni aliyeko mbinguni. Ar-rahimu –
uzawa ni udugu utokanao na Rahmaani – Mwingi wa rehema. Atakaye
uunga, ataungwa na Allah na atakaye ukata, naye atakatwa na Allah”.
Tirmidhiy-Allah
amrehemu.
Na
ni wajibu wa muislamu kutekeleza haki za ndugu/jamaa zake na
auimarishe udugu wake wa damu kwa mapenzi ya daima. Na wanao ustahiki
mno wema wake na ambao wanatakiwa kupewa kipaumbele kabla ya watu
wengine, ni wazazi wake wawili, Allah Ataadhamiaye anatuagiza: “NA
WAINAMISHIE BAVU LA UNYENYEKEVU KWA KUWAONEA HURUMA. NA USEME: MOLA
WANGU MLEZI! WAREHEMU KAMA WALIVYO NILEA UTOTONI”. [17:24]
Kisha
wanao fuatia ni wanawe. Imepokewa kutoka kwa Al-Baraau, amesema:
“Abubakar
alikwenda kwa (binti yake) Aysha akiwa amepatwa na homa, akasema:
Unajionaje ewe binti yangu na akambusu shavuni”. Bukhaariy-Allah
amrehemu.
Na
lionekanalo kwa watu mafedhuli ni kwamba hisia/mawazo yao hayachukui
nembo hii ya upole na huruma, kwani katika hulka na maneno yao kuna
ukavu karahishi. Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira-Allah
amuwiye radhi: “Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimbusu Hasan au Husein bin Aliy,
akiwa na Al-Aqrau bin Haabis At-tamiimiy. Al-Aqrau akasema: Mimi nina
watoto kumi na kamwe sijambusu yeyote miongoni mwao. Mtume wa Allah
akamuangalia na kusema: “Asiye na rehema harehemewi”.
Na
katika riwaya/upokezi mwingine alisema: “Mimi
similiki kwako Allah kuondosha rehema moyoni mwako”.
Bukhaariy-Allah
amrehemu.
Na
imepokewa kutoka kwa Sayyidna Anas-Allah amuwiye radhi: “Tuliingia
pamoja na Mtume wa Allah kwa Abu Saifi muhunzi na alikuwa ni baba wa
kunyonya wa Ibrahimu; mtoto wa Mtume wa Allah. Mtume wa Allah
akamtwaa mwanawe akambusu na kumshumu. Kisha tukaenda tena nyuumbani
kwake siku nyingine na Ibrahimu akiwa katika hali ya kukata roho,
macho ya Mtume wa Allah yakaanza kububujika machozi. Ibn Auf
akauliza: Ewe Mtume wa Allah, nawe (pia unalia)? – kama kwamba yeye
aliona ajabu Mtume kulia – (Mtume) akasema: “Ewe mwana wa Auf!
Hakika hayo (machozi) ni rehema”. Kisha akazidi kububujikwa na
machozi na akasema: “Hakika jicho linatoa machozi na hakika moyo
unanyenyekea. Na wala hatusemi ila yale yanayo mridhi Mola wetu na
hakika sisi tuna huzuni kuu kutengana nawe, ewe Ibrahimu”.
Muslim-Allah
amrehemu.
|