Makala
Mwanzo
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao

 

  MASWALI NA MAJIBU  


Majibu : Swali na 1                              
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kutuwafikisha kukuletea majibu ya maswali yako na tunamtakia Rehma na Amani Mtume wetu Muhammad pamoja na jamaa na mashaba wake.

1. Tuelewe kwanza kabisa kuwa Mbwa ni najisi kwa maneno ya wanazuoni walio wengi. Wanaosema kuwa mbwa ni najisi wametegemea hadithi iliyopokewa toka kwa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- kuwa alialikwa katika nyumba, akakataa kwenda alipoulizwa alijibu “Katika nyumba ya fulani kuna mbwa” akaambiwa : na katika nyumba ya fulani kuna paka, akasema Mtume “Hakika paka si najisi”. Maneno haya yanajulisha wazi kuwa mbwa ni najisi. Pia wanategemea hadithi iliyopokewa na Abu Hurairah toka kwa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- “Anapoingiza (kinywa chake) katika chombo cha mmoja wenu basi na amwage (kilichomo) na aoshe chombo chake mara saba mojawapo (achanganye) na mchanga” Muslim. Amesema Imaam Malik ambaye ameiona hadithi hii lakini anasema Mbwa sio najisi, na kusafisha huku ni kwa ajili ya ibada tu. Ifahamike pia kuwa kuna hadithi iliyopokewa na Abdullah bin Omar – Allah awawie radhi- kuwa mbwa walikuwa wanapita (kwenda na kurejea) msikitini zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani zimshukie- wala hawakuwa (masahaba) wakimwagia kitu mahali alipopita.Bukhaariy. Pia wametegemea aya ya nne katika suratil Maidah “NA KULENI WALICHOKUSHIKIENI (mbwa)” Dalili yao ni kuwa Mwenyezi Mungu hakuamrisha kuosha kilichoshikwa na mbwa hao. Kwa hivyo ndugu yangu mbwa ni najisi kwa maneno ya wanazuoni waliokuwa wengi, hata hivyo ukiwa na mtihani wa kuwa na mbwa wa ulinzi nyumbani basi unaweza ukategemea maneno ya wanazuoni wanaosema si najisi kama Imaam Malik. Ama ikiwa unafuga kwa mchezo tu (hobby) basi ukumbuke hadithi ya Mtume -Rehema na Amani zimshukie- isemayo “Malaika hawaingii kwenye nyumba yenye mbwa”

2. Suala la kupangusa juu ya soksi : ni jambo la kustaajabisha kuwa kuwa kuna watu wanaopangusa juu ya soksi, tungependa kujua khabari zao. Kuhusu suala lako, tunaamini kuwa unafahamu wazi kuwa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- alipangusa juu ya KHOFU na hukmu yake itakuja kwenye Fiqhi, kwa ufupi ni kama viatu vya ngozi au mfano wake vyenye kufunika hadi kwenye vifundo, na hutumiwa sana kwenye sehemu za baridi kama uturuki. Miongoni mwa shuruti zake ni kuwezekana kuzitembelea juu yake, zisizoingiza maji ila penye kiungio, zimewekwa juu ya tahara na hazina najisi. Hadithi ya khofu imepokewa na Bukhariy na Muslim. Ama kupangusa juu ya soksi, kuna hadithi iliyopokewa na Mughira kuwa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- alipangusa juu ya soksi zake na viatu vyake. Hadithi hii imepokewa na Tirmidhiy, lakini ni dhaifu kama alivyobainisha hayo wanazuoni wengi miongoni mwao akiwa Imaam Nawawiy kwenye kitabu chake Majmuu, Juzuu ya kwanza. Yeye ameeleza kwamba ameidhoofisha hadithi maimamu wa hadithi kama Imaam Ahmad bin Hanbal, Muslim, Sufyanu Thawriy, Yahya bin Muin Aliy bin Almadiniy na wengineo.

3. Kuswali na viatu inafaa, Mtume -Rehema na Amani zimshukie- aliswali na viatu kama ilivyopokewa kwenye Hadithi ya Bukhariy na Muslim. Imepokewa pia kuwa aliwahi kuvua viatu ndani ya swala na kuwaambia masahaba kuwa Jibril alimwambia kuwa viatu vyake vina najisi. Kwa hivyo kuswali ndani ya viatu inafaa kama viatu havina najisi. Lakini, tuiangalie misikiti yetu na misikiti ya wakati wa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- Misikiti ina mazulia na msikiti wa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- ulikuwa wa udongo bila hata busati tusije kuanza kuzua vitu vipya ndani ya misikiti yetu, ikiwa sisi hatutaki mgeni kuingia nyumbani mwetu na viatu kwa kuwa sitting room zetu zina mazulia na ataichafua, vipi kuhusu nyumba za Mwenyezi Mungu, hizo ni haki zaidi kuziheshimu.


Forum | Guestbook | Tuandikie |