|
FALSAFA (HEKIMA) YA FUNGA
(SWAUMU)
ATHARI ZA SWAUMU: KINAFSI,
KIROHO, KIAFYA NA KIJAMII.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafaradhishia waislamu kufunga (swaumu) katika mwezi wa
Ramadhani. Mwezi ambao imeshuka ndani yake Qur-ani Tukufu. Ameifaradhisha
swaumu ili iwe ni ngome na kinga ya wachamungu dhidi ya shari za nafsi.
Swaumu huinasua nafsi katika maumbile yake ya kupenda mno shari na kuivika
twaa na uchamungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia kuhusiana na swaumu: “ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA
WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH” SIKU CHACHE TU (kufunga
huko)……..” (2:183-184) Aya inafumbuliza wazi kuwa lengo la kufaradhishwa
funga kwa waumini ni kuwafinyanga kuwa wachamungu. Tena kufunga huko ni
masiku machache tu, yaani mwezi mmoja tu, mwezi wa Ramadhani. Amesema kweli
Allah, mtu ana uhuru wa kula, kunywa na kufanya mambo yake yote ya halali
katika miezi kumi na moja ya mwaka mzima na afunge mwezi mmoja tu, Naam, ni
kweli ni masiku machache lakini yenye faida katika kipindi kizima cha mwaka.
Lengo la masiku haya machache ni kuacha athari njema katika nafsi za
wafungaji, athari itakayodumu na kuendelea katika kipindi chote cha mwaka.
Baada ya mwezi huu wa Ramadhani kumalizika ionekane athari ya malezi yake kwa
waumini wafungaji yawepo mabadiliko ya wazi katika tabia na mienendo yao.
Zoezi la kuidhibiti nafsi na yaliyo halali liendelezwe katika kuidhibiti na
yaliyo rahamu. Swaumu ilete siha njema kwa kuunguza mafuta na ziada ya
chakula kilichohifadhiwa mwilini bila ya kutumika katika kipindi cha miezi
kumi na moja. Muislamu ambaye anajizuilia kula chakula cha halali pamoja na
kutambua kwamba maisha (uhai) yake yanategemea chakula. Pamoja na ukweli huu
bado anakubali kuacha kula, kwa nini? Muumini anafanya hivi kwa sababu ya
kutaka radhi ya Mola wake Mtukufu kwa kuitekeleza amri yake yenye manufaa
makubwa kwake mwenyewe. Anafanya hivyo kwa kuchelea kufikwa na adhabu kali ya
Mola wake kwa kuikhalifu na kuipinga
amri yake. Na anafanya hivyo kwa tamaa ya kupata rehema adhimu ya Mola wake.
Ikiwa muumini huyu ameweza na
anachokihitajia ambacho hana budi nacho ili aweze kuishi. Itakuwa ni ajabu
kwa muumini huyu huyu kushindwa kujizuia na haramu ambayo hainamchango wowote
katika uhai wake na wala haihitajiki kabisa. Mfungaji hasemi uongo,
hadanganyi, hafanyi khiyana, havunji wala kukhalifu ahadi, hafanyi riyaa,
halaani na wala hasemi ila haki na kweli. Mfungaji hujiepusha na utesi na
usengenyi, huuzuilia mkono na ulimi
wake, hufanya sana wema na huwa mkweli,
mwenye kutekeleza ahadi. Mfungaji huwa muaminifu, mwenye subira katika shida
na matatizo, na huidhibiti na kuitawala nafsi yake. Hivi ndivyo swaumu
inavyomfinyanga na kumuandaa mja kuwa mchamungu katika miezi kumi na moja
inayofuatia baada ya Ramadhani.
SWAUMU NI MWALIMU WA ROHO NA MLEZI WA MATASHI
(MATAKWA)
Swaumu ni miongoni mwa masomo makuu ya kiamalia
(pratical) ambayo hulenga kumuandaa mfungaji mkweli kuwa mchamungu. Hulenga
kumuandaa kukabiliana na magumu ya maisha ya kila siku. Kwa mantiki hii funga huyalea matashi (matakwa),
mfungaji akaweza kusema na nafsi yake wakati inapotaka kutenda la haramu au
lililo nje ya uweza wake. Swaumu ni mwalimu anayetoa mafunzo ya kiroho, mafunzo ambayo hupandikiza moyo wa
subira katika nafsi ya mfungaji, ili yote haya yapatikane na athariyake
ionekane ni lazima mja aitakase ibada yake hiyo, yaani afunge kwa ajili tu ya
Allah.
Kwa nini subira? Subira ina athari na
umuhimu gani katika maisha yao kila siku?.
Kwa hakika swaumu (funga) si tu kujuzuia na
matamanio ya tumbo (kula na kunywa) na matamanio ya tupu (jimaa). Bali ni
wajibu kujizuia na hayo kuambatana sambamba na kujizuia na tabia mbaya na
baki ya madhambi mengine. Hii ndio maana ya kauli ya Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie:
“Asiyeacha maneno ya uongo/uzushi na kuyafanyia kazi, Allah hana haja na
kuacha kwake kula na kunywa” Bukhaariy.
Swaumu kwa maana hii ni mazoezi ya kimwili na
kiroho ambayo humtayarisha mwanadamu kukabiliana na matukio ya ghafla yenye
kuhuzunisha na kutia simanzi kwa kuwa matukio kama hayo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na hapana budi yatamtokea kama si leo, basi kesho, kwa
namna moja au nyingine. Ikawa hapana budi, mwanadamu huyu aandaliwe na kupatiwa mazoezi ya jinsi ya kukabiliana na kupambana na matukio hayo
pindipo yanapojitokeza tena bila ya taarifa. Yakimtokea asipapatike bali akae
chini na kutafakari njia bora ya kukabiliana nayo na kuyatatua. Lolote
linaweza kutokea maishani, mtu anaweza kufilisika akawa masikini baada ya kuwa tajiri asiyejua
kukosa. Inawezekana kabisa mtu akawa
mgonjwa taabani kitandani baada ya kuwa mzima mwenye siha njema
inayomuwezesha kwenda huku na kule na kufanya mambo yake yote mwenyewe. Si
muhali mtu kuwa dhahiri mnyonge baada ya kuwa alikuwa mtu mtukufu mwenye
kuheshimika na jamii yake, leo akawa hajulikani tena wala kutajwa. Inatokea
mtu akawa na mke mzuri waliyependana na kuishi maisha mazuri na dhuria
(watoto) yao lakini Allah akawachukua wote na kumuacha peke yake bila ya kuwa
na wa kumliwaza. Yote hayo na mengine mfano wa haya kuna imkani ya kumtokea
mtu katika maisha. Na ni ukweli usiopingika kwamba matukio haya yana taathira
kubwa kwa nafsi. Taathira ambayo huweza kumfikisha mtu kutoona raha na
starehe ya uhai (maisha) huu na hivyo kufikia uamuzi wa kujitoa uhai (kujiua)
ili kumuepusha mwanadamu huyu kufika mahala hapo pabaya ni lazima apate
mazoezi ya kiamalia ya mwili na roho (swaumu) kila mwaka mara moja kwa
uchache. Ili nafsi yake iweze kuzoea kukosa inavyovipenda na kustahamili.
Mtu kusubiri (kustahimili) kuacha kile ambacho ni
halali yake ni jambo zito sana, katika nafsi ya mwanadamu kuliko kusubiri
kuacha kile kilicho haramu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ikiwa mtu ameweza kuitawala nafsi yake na
kuacha lililo halali yake, hakuna sababu ya kushindwa kuidhibiti nafsi yake
na kuacha lililo la haramu. Kuacha lililo la halali kunahitaji nguvu na
subira nyingi kuliko kuacha lililoharamishwa. Mtu ambaye huitazama neema
aliyonayo kwa jicho la amana aliyopewa na Mola wake na anaweza kuichukua
wakati wowote. Mtazamo huu humsahilishia kusubiri kuondoka kwa neema hiyo na
kuridhia na kusalimu amri kwa lile alilolikadiria Mola wake. Ni dhahiri iliyo
bayana kwamba kila mwanadamu anahitaji subira katika maisha haya. Mwanafunzi
anahitajia sana subira katika kazi yake ngumu ya kulima, ndipo aweze kuvuna
matunda ya jasho lake. Hata rais (kiongozi) wa nchi pia anahitajia subira ya
kutosha katika kufanikisha kuiongoza nchi. Kwa ujumla kila mmoja wetu hana
budi kuwa na subira katika maisha
hata kuishi na watu majumbani, makazini na hata mitaani pia kunahitaji
subira. Kwa hiyo itakudhihirikia kwamba subira ni kitu azizi na muhimu sana
katika kurahisisha na kuchanganyika kimaisha. Ni kutokana na umuhimu na ugumu
wa suala zima la subira ndio ikawa ujira wake ni mkubwa usiojulikana ila na
Allah pekee, yeye ndiye ajuaye amewaandalia nini wenye kusubiri,
tusome:”…………….NA BILA SHAKA WAFANYAO SUBIRA (wakajizuilia na maasia na
wakaendelea kufanya ya twaa) WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HISABU” (39: 10).
Subira hii ni mojawapo ya mafunzo na malezi yanayotolewa
na chuo hiki kikuu cha nne cha Uislamu (swaumu). Chuo hiki kinamuandaa
mwanachuo (muumini) kuwa na subira katika kukabiliana na magumu ya maisha
ikiwa ni pamoja na kuzoea hali ya kupata na kukosa. Mwanachuo huyu akihitimu
mafunzo yake ya mwezi mmoja chuoni kila mwaka hutunukiwa shahada ya juu ya
subira. Subira ambayo itakuwa ni silaha kubwa katika maisha yake ya miezi kumi na moja ifuatayo
baada ya mafunzo. Website yako (WEBSITE UISLAMU) inazidi kuamini kuwa
unaelewa sasa kwa nini unafunga, unaelewa kuwa falsafa ya amri hii ya Mola
wako, kwa hivyo utajitahidi kufunga kama alivyoamrisha Mola wako.
|