Lengo
na madhumuni ya nasaha hizi ni kujaribu
kukumbusha utukufu, ubora na fadhila za mwezi
huu mtukufu ambao ni msimu wa kheri nyingi. Ni
kutokana tu na kuujua mwezi wa Ramadhani ni
mwezi wa namna gani, ndio tunaweza kuupa hadhi
na haki yake inayostahili. Kuutukuza na kuupa
mwezi huu haki yake kwa kujituma kwa makusudi
na bidii zetu zote bila kuchoka kuyatenda yale
yote tunayotakiwa kuyafanya ndani yake
miongoni mwa mambo ya kheri na twaa. Na athari
ya mambo hayo kuonekana katika miezi kumi na
moja ifuatayo baada ya Ramadhani kuonyesha
shukrani zetu kwa Mola Muumba wetu kwa neema
hii ya mwezi wa Ramadhani. Isitoshe ni ishara
na dalili ya wazi
ya kunadi sada (kutanakiwa).
Walengwa
wa hadia hii ya Nasaha za Ramadhani ni wale
watu wema waliojihakikishia mafanikio ya
duniani na kahera kwa kutekeleza kwao
maamrisho na makatazo ya Mola wao. Wale watu
ambao wamejipamba na sifa zote za utu na kuwa
kigezo kwa kila mpenda haki. Wale
walioandaliwa na Mola wao samahani (maghfirah)
na ujira adhimu. Wale wanaotajwa na kauli hii
ya Allah,
“BILA
SHAKA WANAUME WENYE KUFUATA VIZURI NGUZO ZA
UISLAMU, NA WANAWAKE WANAOZIFUATA VIZURI NGUZO
ZA UISLAMU, NA WANAUME WANAOAMINI VIZURI NGUZO
ZA IMANI, NA WANAWAKE WANAOAMINI VIZURI NGUZO
ZA IMANI, NA WANAUME WASEMAO KWELI, NA
WANAWAKE WASEMAO KWELI, NA WANAUME
WANAOSUBIRI, NA WANAWAKE WANAOSUBIRI, NA
WANAUME WANAONYENYEKEA NA WANAWAKE
WANAONYENYEKEA, NA WANAUME WANAOTOA (zaka na)
SADAKA, NA
WANAWAKE WANAOTOA (zaka na) SADAKA, NA WANAUME
WANAOFUNGA NA WANAWAKE WANAOFUNGA, NA WANAUME
WANAOJIHIFADHI TUPU ZAO NA WANAWAKE
WANAOJIHIFADHI, NA WANAUME WANAOMTAJA ALLAH
KWA WINGI NA WANAWAKE WANAOMTAJA ALLAH (kwa
wingi), ALLAH AMEWAANDALIA MSAMAHA NA UJIRA
MKUBWA” (33: 35).
Tunarajia
kwa fadhila zake Allah kuwa wewe msomaji wetu
ni miongoni mwa watu hawa na kwa hivyo,
utanufaika na kufaidika na nasaha hizi za
Ramadhani.
Tunakutakia
Ramadhani njema iliyosheheni rehma, maghfirah,
radhi za Allah, taq-wa na kuachwa huru na
moto.
“MOLA
WETU! USIZIPOTOE NYOYO ZETU BAADA YA
KUTUONGOZA, NA UTUPE REHEMA ITOKAYO KWAKO,
HAKIKA WEWE NDIO MPAJI MKUU” (3:8).
SWAUMU
(FUNGA) KATIKA UISLAMU
TUJIULIZE:
KWA NINI TUNAFUNGA?
Mwenyezi
Mungu Mtukufu amemuumba mwanadamu katika
sehemu kuu mbili, mwili (kiwiliwili) na roho.
Akaziunganisha pamoja roho na mwili pamoja na
tofauti ya maumbile na tabia zao na kuwa
mwanadamu kamili. Akamweka kiumbe huyu
mwanadamu katika daraja ya kati, baina ya
wanyama na malaika. Juu yake kuna malaika
watakasifu watoharifu ambao “…..HAWAMUASI
ALLAH KWA AMRI ZAKE, NA WANATENDA
WANAYOAMRISHWA (yote)” (66:6). Na chini yake
kuna wanyama ambao hawakupewa akili wala
amana, wao kuendeshwa na kusukumwa na matashi
na matamanio yao. Katikati ya makundi haya
mawili ndio akamuweka mwanadamu aliyemkirimu
kwa kumpa akili ambayo ndio neema pekee
inayomtofautisha na hayawani wengine.
Akamletea na muongozo wa maisha na akampa
uhuru na khiyari ya kuchagua – kuufuata
muongozo huo au kutokuufuata, “NA SEMA: HUU
NI UKWELI
ULIOTOKA KWA MOLA WENU, BASI ANAYETAKA
NA AAMINI NA ANAYETAKA NA
AKUFURU”…..(18:29).
Kisha
akambainisha matokeo ya matumizi mazuri au
mabaya ya uhuru na khiyari aliyompa
“……NA KAMA UKIKUFIKIENI MUONGOZO UTOKAO
KWANGU, BASI WATAKOUFUATA MUONGOZO WANGU HUO
HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA HAWATAHUZUNIKA
LAKINI WENYE KUKUFURU NA KUYAKADHIBISHA MANENO
YANGU, HAO NDIYO WATAKAOKUWA WATU WA MOTONI,
HUMO WATAKAA MILELE” (2: 38 – 39).
Sasa
basi, mwanadamu atakapoitumia vema neema hii
ya akili, muongozo na khiyari aliyopewa
akayashinda matamanio yake maovu. Hupanda
daraja mpaka kuwa juu ya malaika, mahala
ambapo Mola wake alipomuweka: “NA
(wakumbushe watu khabari hii): TULIPOWAAMBIA
MALAIKA MSUJUDIENI ADAM (yaani muadhimisheni
kwa ile elimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA
WOTE ISIPOKUWA IBILISI, AKAKATAA NA
AKAJIVUNA……..” (2:34).
Hii
ndio nafasi ya mwanadamu atakapoushinda unyama
ambao ni sehemu ya maumbile yake, huwa mtukufu
na karibu zaidi na Mola wake kuliko hata
malaika. Ama akiuachia unyama umshinde na
kutawaliwa na matamanio maovu, huporomoka
daraja na kuwa chini kabisa ya wanyama: ‘JE
UMEMUONA YULE ALIYEFANYA MATAMANIO YAKE (kile
anachokipenda) KUWA MUNGU WAKE? BASI JE
,UTAWEZA KUWA MLINZI WAKE (ukamuhifadhi
nahayo, na hali ya kuwa hataki?) AU JE,
UNAFIKIRI YA KWAMBA WENGI KATIKA WAO WANASIKIA
AU WANAFAHAMU? HAWAKUWA WAO ILA NI KAMA
WANYAMA, BALI WAO WAMEPOTEA ZAIDI NJIA” (25:
43-44)
Mwenyezi
Mungu Mtukufu amemzawadia mwanadamu huyu mfumo
sahihi wa maisha (Uislamu) uliogusa nyanja
zake zote za maisha. Akamuwajibishia ndani ya
mfumo huo ibada za aina mbalimbali ambazo
lengo jumla lake ni kuleta manufaa na
kuondosha madhara. Ibada hizi kama
atazitekeleza kama ipasavyo zitampa kinga
kubwa dhidi ya unyama na matamanio maovu.
Amemfaradhishia swala mathalan ili imkinge na
mambo maovu na machafu na kumuweka katika
mazingira ya kumtii Mola wake kwa kuamrika
katika maamrisho na kukatazika katika
makatazo: “SOMA ULIYOLETEWA WAHYI
(uliyofunuliwa) KATIKA KITABU (hiki
ulicholetewa) NA USIMAMISHE SWALA
BILA SHAKA SWALA (ikiswaliwa vilivyo)
HUMZUILIYA (huyu mwenye kuswali na) MAMBO
MACHAFU NA MAOVU, NA KWA YAKINI KUMBUKO LA
ALLAH (la kumzuilia mtu na mabaya). NA ALLAH
ANAJUA MNAYOYATENDA”.
(29:45)
Mwenyezi
Mungu Mtukufu kwa kumtambua vema mwanadamu na
udhaifu wa maumbile yake kutokana na kumuumba
mwenyewe. Ili asishindwe na unyama unaotokana
na umbile lake na asiangushwe mweleka na
matamanio maovu, akampa msaada. Akamtayarishia
ibada ya funga mwezi mmoja kila mwaka ili
imtoe katika unyama na kumpeleka katika utu.
Imtoe katika
ulimwengu wa vitu na kumpeleka katika
ulimwengu wa roho ambapo atayashinda matamanio
maovu. Imuonyeshe udhaifu wake mbele ya Mola
Muumba wake na haja yake kwa Mola wake.
Imuondoshee moyo wa ubinafsi na imjengee moyo
wa huruma na upendo kwa kuhisi tabu ya njaa na
kiu. Ikivunjilie mbali kiburi chake na kumvika
taji la unyenyekevu. Kauli jumla, muislamu
ameamrishwa kufunga ili swaumu (funga) iwe ni
chuo cha malezi ya nafsi. Ndani ya chuo hiki
nafsi ya mja inajengewa mazingira ya
kustahimili wakati wa shida (kukosa). Nafsi
inapewa chanjo/ kinga dhidi ya maasi na
matamanio. Chuko hiki humtunukia mja shahada
ya umiliki wa nafsi na utawala
wa unyama na matamanio maovu. Utu na
ukamilifu wa mwanadamu unatokana na uwezo wake
katika kuimiliki na kuitawala nafsi yake
ambayo: ….KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE
KUAMRISHA SANA MAOVU ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA
WANGU AMEIREHEMU……..” (12:53).
Uwezo
huu wa kuimiliki nafsi na kuikalia juu ndio
unaompatia mja daraja na nafasi njema mbele ya
jamii bali hata mbele ya Mola wake. “NA AMA
YULE ALIYEOGOPA KUSIMAMISHWA MBELE YA MOLA
WAKE, AKAIKATAZA NAFSI YAKE NA MATAMANIO
(maovu). BASI (huyo) PEPO NDIYO ITAKAYOKUWA
MAKAZIYAKE”. (79: 40-41)
“BILA
SHAKA AMEFAULU ALIYEITAKASA (nafsi yake). NA
BILA SHAKA AMEJIHASIRI ALIYEIVIZA (nafsi
yake)”
(91: 8-9).