Yale
ambayo swala huyatekeleza mara tano kila siku,
swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani
huyatakeleza mara moja kila mwaka. Katika
kipindi chote cha swaumu yaani tokea kuchomoza
kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua magharibi,
hatuli hata chembe moja ya chakula na wala
hatunywi walau tone moja tu la maji. Tunajizuia
hivyo il-hali tunavyo vya kuvila na kunywa. Ni
lipi basi litufanyalo hata tukavumilia kwa hiari
zetu machungu haya ya njaa na joto la kiu ?
Tukijiuliza swali hili hatutapata jawabu zaidi
ya kuvimilia kwetu taklifu zote hizi kunatokana
na imani yetu thabiti kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu
na kumcha yeye na kuiogopa siku ya Kiyama ambayo
Mwenyezi Mungu ametuasa tuiogope :
“NA
IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH,
KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE
WALIYOYACHUMA NA HAWATADHULUMIWA” [2:281]
Kwa
hivyo basi itabainika kwamba funga ni suala
linalofungamana na imani na ndio maana Mwenyezi
Mungu alipotuamrisha kufunga katika aya ya
swaumu, akatuita kwa jina la imani, akasema :
“ENYI
MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA
WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE
KUMCHA ALLAH” [2:183]
Jua
na ufahamu ndugu yangu Muislamu kwamba saumu ni
mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, ambazo
Uislamu haukamiliki ila kwa kupatikana zote. Kwa
mantiki hii, yeyote atakayeikanusha na kuipinga
nguzo hii ya swaumu na kusema si wajibu, huyo
atakuwa amekufuru, Tunasoma katika hadithi ya
Bwana Mtume : “Uislamu umejengwa juu ya nguzo
tano; kushuhudia kwamba hapana Mola apasaye
kuabudiwa kwa haki ila ALLAH na kwamba Muhammad
ni mjumbe wake, na kusimamisha swala na kutoa
zaka na kufunga Ramadhani na kuhiji nyumba ya
Mwenyezi Mungu” Bukhariy na Muslim kutoka kwa
Ibn Umar.
Ibada
hii ya funga ni ibada kongwe sana, haikuanzia
kwa umma huu wa Nabii Muhammad bali ni ibada
iliyokuwa ikifanywa na nyumati zingine
zilizopita kabla yetu. Ushahidi wa hili ni kauli
yake Mola Mtukufu : “ENYI MLIOAMINI
MMELAZIMISHWA KUFUNGA KAMA WALIVYOLAZIMISHWA
WALIOKUWA KABLA YENU …” [2:183]
Tukivipekua
vitabu vya historia tutakuta vinatuambia kwamba
Mwenyezi Mungu mtukufu ameufaradhishia ummah huu
ibada ya funga katika mwezi wa Shaaban {mwezi wa
nane kwa mpangilio wa miezi ya kiislamu} mwaka
wa pili wa Hijra {yaani tangu bwana Mtume
kuhamia Madinah} kabla ya vita vya Badri.
Mwenyezi Mungu anatuambia “ENYI MLIOAMINI!
MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) ….” Hebu
tujiulize, kufunga swaumu ni nini ? Kwani
tukijua swaumu ndio tutaweza kufunga kama
alivyotuamrishwa na funga hiyo kutupelekea
kwenye ucha Mungu (taq-wa) ambalo ndio lengo la
swaumu. Neno SWAUMU/FUNGA linatafsirika kwa
maana mbili;maana ya kilugha na ile ya kisheria.
Tukilitizama neno SWAUMU/FUNGA kwa darubini ya
lugha, tutalikuta linatoa maana ya KUJIZUIA na
chochote kile. Mtu akijizuia kula anaambiwa
kafunga, akijizuia kuzungumza anaambia kafunga
na …. na ….. Maana hii ya funga katika lugha
mafaqihi hawakulitoa kichwani bali wameichukua
ndani ya Qur-ani Tukufu : “HAKIKA MIMI
NIMEWEKA NADHIRI KWA (ALLAH) MWINGI WA REHEMA YA
KUFUNGA, KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU”
[19:26]
Bibi
Maryam, mama yake Nabii Isa –Amani ya Allah
ziwashukie wote – alipokwishajifungua mwanawe
kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu bila ya baba,
ilimpata tabu kuu ya kufikiri atawaambia nini
jamaa zake hata wamsadiki na kuamini kuwa
ujauzito ule unatokana na uweza wa Mola Mtukufu
na hautokani na uchafu wa zinaa. Ni katika hali
hii ya kutafakari jawabu la kuwajibu jamaa zake
watakapomuuliza habari za mtoto wake, hapo ndipo
Mwenyezi Mungu aliyetawalia suala lile
akamwambia : “…NA KAMA UKIMUONA MTU YEYOTE
(akauliza habari ya mtoto huyu) SEMA HAKIKA MIMI
NIMEWEKA NADHIRI KWA (ALLAH) MWINGI WA REHEMA YA
KUFUNGA, KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU”
Bi
Maryam aliposema kuwa kaweka nadhiri ya kufunga,
hakuwa na maana ya kufunga Ramadhani bali neno
“funga” hapa limetumika kwa maana ya
kujizuia kusema/kuzungumza na jamaa zake. Hapa
ndipo imepatikana maana ya funga kilugha kuwa ni
kujizuia na lolote lile.
Swaumu/Funga
katika sheria ina maana ya kujizuiliya kula,
kunywa na mambo yote yanayofunguza swaumu kwa
namna maalum na muda maalum. Muda huu ni tangu
kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua.
Kujizuiliya huku ni lazima kuambatane na nia.
Hii
ndio maana ya funga kwa ujumla. Je, hii ndio
khasa aliyokusudia Mwenyezi Mungu katika aya ya
swaumu. Ni nini ukweli/uhakika wa swaumu ?
Swaumu ya kweli mbali na kujizuia kula na
kunywa, inampasa muislamu ajizuiliye viungo
vyake kama vile masikio, macho, ulimi, mkono,
mguu na utupu na yale yote yaliyokatazwa na
Mwenyezi Mungu. Ayazuiliye masikio yake
kuyasikiliza yale yote yaliyokatazwa
kuyasikiliza kama vile kusikiliza maneno ya watu
bila ya ridhaa yao, kusikiliza utesi na
useng’enyi, ayahifadhi macho yake kuwaangalia
wanawake/wanaume wasio maharimu zake, asiangalie
ndani ya nyumba ya mtu bila ya idhini yake,
asiangalie nyuchi, asimtazame mtu kwa jicho la
dharau na kadhalika. Hali kadhalika avizuiliye
viungo vyake vingine vilivyosalia na kila ambalo
limekatazwa na sheria kulitenda. Muislamu
atakapoweza kulizuia tumbo lake kula na kunywa
na akavizuia viungo vyake vingine na yale yote
ya haramu, hapo ndipo atakuwa amefunga kama
alivyoagiza na kuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu
na hiyo ndio funga itakayotoa natija ya
ucha-Mungu ambalo ndilo lengo mama la
swaumu/funga.
Imepokelewa
hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah – Allah
amuwie Radhi – amesema: Amesema Mtume wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie – “Haikuwa
swaumu ni kujizuiliya kula na kunywa (tu) bali
ni swaumu ni kujiepusha na upuzi na mambo
machafu. Basi yeyote atakayekutukana au
kukufanyia upuuzi, basi mwambie hakika mimi
nimefunga” Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan. Na
akasema tena Bwana Mtume – Rehema na Amani
zimshukie – “Asiyeacha maneno ya
urongo/uzushi na kuyafanyia kazi, Mwenyezi Mungu
hana haja na kuacha kwake chakula na kinywaji
chake” Al-Bukhariy.
Itakuwazikia
na kukubainikia kutokana na hadithi hizi kuwa
funga ya kweli haikomelei katika kula na kunywa
tu. Pia ni vema ikafahamika kuwa funga ndio
ibada pekee isiyoweza kuchezewa na shetani, ndio
ibada pekee isiyoingiwa na riyaa, ndio ibada
pekee isiyoandikwa thawabu zake na Malaika, hii
ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema : “Funga ni
yangu na ni mimi ambaye nitakayeilipiza”
HEKIMA/FALSAFA
YA FUNGA :
Baada
ya kuona funga ya kweli, hebu sasa tujiulize ni
kwa nini Mwenyezi Mungu ametulazimisha kufunga
na kutuacha tuteseke na machungu ya njaa na joto
la kiu ? Je, funga ni adhabu kwetu ? Bila ya
shaka Mwenyezi Mungu hawezi kutuamrisha jambo
ila huwa mna ndani ya jambo lile manufaa,
maslahi, na faida kwetu sisi waja tulioamrishwa.
Elewa ewe Muislamu kuwa funga ina faida nyingi
sana; faida za kiroho, kijamii na kiafya. Funga
hukibomoa na kukivunjilia mbali kibri cha
mwanadamu na humfanya auone unyonge na udhaifu
wake. Yeye kama kiumbe anahitajia chakula, maji
na hewa ili aweze kuishi, kwa mantiki hii
binadamu hawezi kujitegemea mwenyewe bali daima
anamuhitajia Mwenyezi Mungu Muumba ambaye ndiye
humpa hiba ya chakula, maji na hewa. Amesema
Mwenyezi Mungu Mtukufu : “ENYI WATU! NYINYI
NDIO WENYE HAJA KWA ALLAH; ALLAH NI MKWASI (na
nyinyi hakuhitajieni) ASIFIWAYE (kwa neema zake
juu ya viumbe wake vyote)” [35:25]
Funga
ni mwalimu wa subira. Funga humfinyanga na
kumuandaa binadamu kuwa na subira katika
kukabiliana na majanga mbali mbali ya maisha.
Humfanya azoee machungu ya njaa na joto la kiu
wakati wa ukame, vita, awapo gerezani, aunguapo
na kushindwa kula. Kwa kuwa binadamu huyu
atakuwa ameipata shahada ya uvimilivu/subira
kutoka chuo kikuu cha subira; Ramadhani, na ni
dhahiri kuwa atakuwa thabiti na imara katika
kukabiliana na matatizo mbali mbali maishani
mwake. Na Mola Mtukufu amewaahidi wenye kusubiri
ujira/malipo makubwa aliposema : “ …NA BILA
SHAKA WENYE KUSUBIRI WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO
HESABU” [39:10]
Funga
ya Ramadhani ni chuo cha uaminifu. Funga
inamfundisha Muislamu kuwa mkweli katika
mahusiano yake na waja wenzake. Inamfundisha
kuidhibiti na kuichunga nafsi yake, inamfanya
amuone Mola wake kuwa yu naye kila wakati na
kila mahala na hivyo kuipanda khofu ya Mwenyezi
Mungu ndani ya moyo wake. Natija ya kumuogopa
Mwenyezi Mungu ni nafsi kujiepusha na yote
yaliyoharamishwa na kutenda yale iliyoamrishwa.
Funga
humfanya Muislamu kuwa na huruma kwa wenziwe na
ni huruma hii ndio impelekeayo kumsaidia
masikini, mgonjwa, yatima, mjane na baki ya
wanyonge wengine waliomo katika jamii zetu.
Funga
ina athari kubwa, kwa mfungaji, na athari hizi
hudhihiri katika tabia na nafsi, funga ni silaha
ya ajabu sana ambayo Mwenyezi Mungu ameileta ili
kuuvunja unyama wa binadamu, ambao huu ndio
humfanya binadamu akawa mbaya kuliko hata mnyama
wa mwitu kiasi cha kuona ni jambo dogo tu kuitoa
roho ya mwanadamu mwenziwe. Funga humtoa huku na
kumpeleka katika ubinadamu na utu na hapo ndipo
utamuona mfungaji namna alivyo mnyenyekevu,
mpole, mnyonge na mwenye huruma.
Funga
huyavunja matamanio mabaya ya nafsi. Kwani
hapana kiwezacho kuivunjavunja nafsi ya
mwanadamu kama njaa. Kwa ujumla, funga humpamba
muislamu na sifa njema kwa sababu humkalifisha
kuvizuia viungo vyake na mambo ya haramu na
kumfanya kuwa kuwa mkweli, muaminifu,
mnyenyekevu, mpole, mkarimu na baki ya sifa
nyinginezo nzuri, tukufu. Kwa hivyo funga ni
chuo kinachotoa mafunzo juu ya kuidhibiti na
kuimiliki nafsi na kumpamba muislamu na sifa
njema na kumuepusha na tabia mbaya.
Mwenyezi
Mungu, Mtenegenezaji, Mpangaji, na Mpitishaji wa
mambo yote, Mwenye hekima na busara, Mtunga
sheria aliye mjuzi ameiwajibisha funga kwa
hekima/falsafa za juu sana kama tulivyoona.
TUNDA
LA RAMADHANI :
Karibu
tena ewe ndugu yangu uburudike na tunda la
Ramadhani.
- Imepokelewa
(hadithi) kutoka kwa Ya’alaa Ibn Murrah
–Allah amuwie Radhi- amesema: Amesema
Mjumbe wa Allah – Rehema na Amani
zimshukie - : “Allah anayapenda mambo
matatu; kuharakia kufuturu, kuchelewa (kula)
daku na kufumbatanisha mikono miwili mmoja
juu ya mwingine katika swala” Twabraaniy.
MAELEZO
: Haya muislamu, hayo ndiyo mambo matatu
ayapendayo Mola wako na yote yamo ndani ya uweza
wako na bila shaka kama Allah anayapenda pia
atakuwa anawapenda wayafanyayo mambo hayo. Je,
wewe ndugu yangu, hutaki kupendwa na Mola wako ?
haya shime “!
- Imepokelewa
kutoka kwa Anas bin Maalik – Allah amuwie
Radhi – amesema : Amesema mjumbe wa Allah
– Rehema na Amani zimshukie - : “Kuleni
daku, kwani hakika mna baraka katika daku”
Ibn Hibban.
MAELEZO
: Kula daku ni suna na mwenendo wa Bwana Mtume,
alikuwa hafungi bila ya kula daku. Hii
haimaanishi kuwa kama mtu hakula daku, funga
yake haikubaliwi, la hasha bali atakosa fadhila
kwa kuiwacha Sunna ya Nabii Muhammad. Wakati wa
kula daku huanzia nusu ya usiku (saa sita) mpaka
kabla kabla ya kuchomoza alfajiri kwa muda
mchache. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya swahaba
wa Mtume : Zayd bin Thaabit –Allah amuwie
Radhi - : “Tulikula daku pamoja na Mtume wa
Allah –Rehema na Amani zimshukie – kisha
akainuka kwenda kuswali (Alfajiri) nikamuuliza :
kilikuwepo kitambo gani baina ya adhan ya
alfajiri na huko kula daku ? Akasema : Kiasi cha
kusoma aya khamsini” Bukhaariy na Muslim.