Hii ni kutokana na mnasaba wa
kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani. Minbari ya
Ramadhani itakuwa ikikuletea mawaidha
yahusiyanayo na funga ya Ramadhani, ili uweze
kuijua funga na hatimaye uweze kufunga kama
alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kama
alivyofunga Bwana Mtume -Rehema na Amani
zimshukie - ambaye ndiye kigezo chetu chema.
Sambamba na Minbari ya Ramadhani, website yako
itakuwa ikikuletea TUNDA LA RAMADHANI. Kupitia
tunda la Ramadhani utajifunza hadithi mbili tatu
za Mtume zihusianazo na funga tukufu ya Mwezi
mtukufu wa Ramadhani. Hadithi hizi zitakuwa
zikifuatiwa na maelezo mafupi ili kuziweka wazi
kwa wasomaji.
i) MINBARI YA
RAMDHANI NA KHUTBA YA MTUME KATIKA KUUKARIBISHA
MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI :
Jueni na eleweni enyi ndugu
zanguni Waislamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu
amejaalia mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi,
yenye kwisha na kuondoka, na mafanikio ya akhera
ndiyo yenye kusalia/kubakia milele. Haya
mafanikio ya kudumu, hayapatikani ila kwa
kupitia barabara ngumu ya "TAQ-WA"
kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata
Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie-. Katika
jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu
mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Allah
ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe. Nao kama
mjuavyo ndio mwezi ambao imeteremshwa ndani yake
Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo kwa watu wote.
Muongozo uliosheheni hoja wazi za uongofu na
upambanuzi baina ya haki na batili. Ramadhani
pia ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake
milango ya pepo na kufungwa milango ya moto. Ni
kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa
Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake
tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe
katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Imepokelewa na Salmaan Alfaarisy
- Allah amuwie Radhi - amesema : Alitukhutubia
Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani
zimshukie - katika siku ya mwisho ya mwezi wa
Shaabani, akasema : "Enyi watu,
umekufikieni mwezi mtukufu wenye baraka. Ndani
ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku
ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi
Mungu amejaalia funga ya mwezi huu kuwa ni
FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake
kuwa ni SUNA. Atakayejikurubisha (kwa Mola wake)
ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo lolote la
kheri, (malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama mtu
aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na
atakayetekeleza fardhi katika mwezi huu, atakuwa
ni kama mtu aliyetekeleza fardhi sabini katika
miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA,
nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni REHEMA na
katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA ALLAH na
mwisho wake ni KUACHWA HURU NA ADHABU YA MOTO.
Yeyote atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi
huu, (ujira wa futari hiyo) utakuwa ni maghfira
ya madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru
na adhabu ya moto na atapata ujira kama aupatao
mfungaji bila ya kupungua chochote katika
ujira/thawabu zake (mfungaji)". Tukasema :
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza
kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji.
(Mtume) akawajibu : "Mwenyezi Mungu humpa
thawabu hizi yule atakayemfuturisha mfungaji
ndani ya mwezi huu kwa onjo/funda ya maziwa au
(kokwa ya) tende au funda ya maji. Na
atakayemshibisha ndani ya mwezi huu mfungaji,
itakuwa ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya
madhambi yake (mshibishaji) na Mola wake
atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda
moja ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na
atakuwa na ujira kama aupatao mfungaji bila ya
kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji).
Na atakayempunguzia kazi mtumishi/mfanyakazi
wake ndani ya mwezi huu, Mwenyezi Mungu
atamghufiria madhambi yake na kumuacha huru na
adhabu ya moto. Basi kithirisheni sana ndani ya
mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu
kwa kutenda mambo mawili kati ya manne hayo; na
mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama
hayo mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu
ni shahada (kushuhudia kwamba hapana Mola
apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH) na mumtake
maghfira. Na ama yale mambo mawili msiyojikwasia
nayo ni mumuombe Mola wenu pepo na
mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya
moto". Ibn Khuzaymah katika sahihi yake.
MAELEZO : Ikiwa tunafuatana
pamoja, tunaweza tukaigawa hadithi hii tukufu
ambayo ni khutba kongwe iliyo hai hadi leo na
itaendelea kuwa hai mpaka mwisho wa dunia.
Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana
Mtume katika kuukaribisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu
au tuseme ina vipengele vikuu vitatu.
Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa khutba
yake, Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie -
anawafahamisha maswahaba na umma mzima juu ya
utukufu, ubora, cheo na nafasi ya mwezi wa
Ramadhani. Kuna hekima/falsafa gani ndani ya
maelezo haya ? Mtume anauelezea mwezi wa
Ramadhani ni mwezi wa namna gani ili muislamu
aujue, kwani waswahili husema asiyekujua
hakuthamini. Akishaujua atauthamini na kuupa
hadhi yake unayostahili. Kuuthamini na kuupa
heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA
kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya namna mbali mbali
za ibada na mambo mengine ya kheri.
Sehemu ya pili ya hadithi, Bwana
Mtume anataja fadhila/faida na ubora wa mwezi wa
mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote
inayofanywa ndani ya mwezi huu hailingani
kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa
katika miezi mingine. Kwa hiyo basi, Ramadhani
ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana
Mtume anatuelezea malipo na thawabu adhimu
anazozipata mja mwenye kumfuturisha nduguye
muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani. Hapa
Bwana Mtume anaashiria moyo wa ukarimu na upendo
utakiwao waislamu wajipambe na kuwa nao. Kwani
waislamu wakipendana watakuwa ni wamoja na
mshikamano, na wakishikamana watautawala
ulimwengu na hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda,
si magharibi wala mashariki.
Kisha ndipo Bwana Mtume
akaikhitimisha khutuba yake kwa kutoa wito
muhimu kwa waislamu. Akawataka wakithithirishe
sana kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya
shahada na wamtake sana maghfira. Hali kadhalika
akawataka waislamu wakithirishe mno kumuomba
Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto wa
jahanamu. Ili kuutekeleza wito huu ndipo
wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu-
wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani ya
mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni ile
sehemu ya mwisho ya hadithi. Uradi wenyewe ni
huu :
ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU
NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA WANA'UDHU
BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN,
TUHIBBUL-AFWA FA'FU 'ANNAA YAA KARIIM
Tunashuhudia kuwa hapana Mola
apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah, Tunakuomba
maghfira (msamaha wa madhambi) Ewe Allah,
Tunakuomba pepo na tunajikinga kwako na moto,
Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda
msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.
Haya shime ndugu zanguni
waislamu, tukithirishe kuuleta uradi huu ndani
ya mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeuitikia wito wa
Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.
TUNDA LA RAMADHANI :
Karibu ndugu yangu muislamu
katika bustani ya Bwana Mtume -Rehema na Amani
zimshukie - uchume utakavyo na kula kiasi chako
matunda matamu, mazuri yasiyokwisha hamu;
matunda ya Ramadhani. Ili ufaidike na kunufaika
na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya
bustani hii tukufu kwa unyenyekevu, utulivu,
adabu, heshima na usikivu.
TUNDA LA KWANZA - DUA YA
KUFUTURU
Amepokea Ibn Majah kutokana na
hadithi ya Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume) :
YUNA MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA
ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila ya
kipingamizi)". Ni kwa sababu hiyo ndiyo
Mtume alikuwa akisema (wakati wa kufuturu) :
[ALLAHUMMA INNIY LAKA SWUMTU
WA'ALAA RIZQIKA AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA
QADDAMTU WA MAA AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU
WABTALLIT-'URUQU WATHABATAL AJRU IN-SHAALLAHU
TAALA]
Maana yake : "Ewe Mola wa
haki ni kwa ajili yako tu nimefunga na
nimefuturu kwa riziki yako. Basi (nakuomba)
unisamehe dhambi zangu zilizotangulia na zijazo.
Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira
umethibiti pindipo atakapo Mwenyezi Mungu
Mtukufu"
Haya shime ndugu zanguni
waislamu, tumuige Mtume wetu katika hili na
mengineyo ili tutengenekewe duniani na akhera.
Usikubali kuipoteza fursa hii adimu ya
kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.
TUNDA LA PILI : FADHILA ZA
KUHARAKIA KUFUTURU :
Imepokelewa hadithi kutoka kwa
Abuu Hurayrah - Allah amuwie Radhi - amesema,
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na
Amani zimshukie- "AMESEMA MWENYEZI MUNGU :
HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE
WAHARIKIAO KUFUTURU" Ahmad na Tirmidhi.
MAELEZO : Ni vema mtu akafanya
haraka kufuturu, maadam ana uhakika wa
kutua/kuzama kwa jua. Ikiwa hana uhakika, basi
ni vema akasubiri adhana ili asije akafuturu
kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola
wako.