|
KUMUHALALISHA MTOTO WA ZINAA
Kumuhalalisha mtoto wa zinaa
au mtoto wa nje ya ndoa kama ijulikanavyo leo ni
miongoni mwa mila potofu na desturi mbaya
zilizoenea na kutapakaa katika jamii zetu kiasi
cha kuonekana kuwa ni jambo zuri linalokubalika.
Mila hii ni zao na matokeo ya mwanamume na
mwanamke kuchukuana kinyumba na kuishi maisha ya
mke na mume bila ya kufunga ndoa kwa mujibu wa
sheria. Pengine hili hupata baraka zote za
wazazi wa pande zote mbili, upande wa mtoto wa
kiume na ule wa mtoto wa kike. Hili hufanyika
pale wazee wa upande wa mtoto wa kiume
wanapokwenda kwa wazazi wenzao, wazazi wa mtoto
wa kike kufunga kile kinachojulikana kama
“PAMVU” Baada ya pamvu kufungwa ndipo mtoto
wa kiume hupata ruhusa na uhuru wa kuchanganyika
na binti kama atakavyo, huku wazazi wa kiangalia
na kufurahia tu bila ya kuona kuwa hilo ni jambo
baya ambalo wao kama wazazi wanapaswa kulikemea
na kulikataza ili kuzuia na kuepusha ufisadi na
uharibufu katika jamii. Hali hii huweza kufikia
kilele cha vijana hawa kuishi pamoja kama mume
na mke, na matunda ya hali hii ni kupatikana
mtoto /watoto wa zinaa (nje ya ndoa). Maisha
haya ya kinyumba ni kinyume kabisa na sheria ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenyezi Mungu
amelikataza jambo hili kutokana na madhara na
athari yake mbaya inayoikumba jamii ya wanadamu.
Tusome na tuzingatie “………NA
(mmehalalishiwa kuwaoa) WANAWAKE WEMA WA
KIISLAMU NA WANAWAKE WEMA KATIKA WALE WALIOPEWA
KITABU KABLA YENU. (Ni halali kwenu kuwaoa)
MTAKAPOWAPA MAHARI YAO, MKAFUNGA NAO NDOA, BILA
KUFANYA UZINZI (kwa mwanamke huyu na huyu), WALA
KUWAWEKA (wanawake) KINYUMBA ……..” (5:5)
kwa mujibu wa aya hii ni haramu kwa mtu
anayemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuishi
na mwanamke kinyumba bila ya kufunga ndoa kwa
mujibu wa sheria na bila ya kumpa mwanamke
mahari yake. Maisha ya kinyumba ni uzinzi
usiokubalika na sheria. Baada ya watu hawa,
mwanamme na mwanamke kuamua kwa khiyari zao
wenyewe kumuasi Mola wao na kuzitupilia mbali
sheria zake, wakaishi maisha ya kinyumba kama
mtu na hawara yake bila ya kupata radhi za
Mwenyezi Mungu kupitia ndoa watu hawa huweza
kuruzukiwa watoto katika maisha haya batili ya
uzinzi. Sasa inapofikia watu hawa kuzinduka na
kutaka kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria ili
kuanza ukurasa mpya wa maisha ya ndoa. Au
inapofikia mtoto amekuwa mkubwa anataka kuolewa,
ili baba apate uhalali wa kuwa walii wa binti
huyu hapo ndipo hujitokeza suala lijulikanalo
kama kumuhalalisha mtoto. Tendo hili haramu la
kumuhalalisha mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa
(katika maisha ya uzinzi) hukamilika kwa huyu
baba mzinzi kupigwa faini na kisha kumuoa
mzinifu mwenziwe (mama wa mtoto). Baada ya faini
na ndoa hiyo, huyu mtoto wa zinaa hunasikishwa
na baba huyu mzinifu na kutambulika na jamii
husika kama mtu na mwanawe. Baba huyu huwa na
mamlaka kamili kwa mtoto huyu kama mzazi na
hivyo kuwa na uhalali/ haki ya kuwa walii wa
binti huyu aliyempata katika maisha ya kinyumba.
Mahari ikapokelewa, khutuba ya ndoa ikasomwa na
hatimaye baba huyu asiyetambulika na sheria
akamuozesha yule anayedai kuwa binti yake na
wali ukaliwa. Huku ni kuendeleza uchafu, kwa
sababu kwa mujibu wa sheria huyu si baba na
hivyo hawezi kuwa walii kwani mtoto yeyote
anayezaliwa nje ya ndoa huwa ni wa mama, hana
nasabu. Bwana Mtume Rehema na amani zimshukie
– anatuasa :-
“Yeyote atakayejinasibisha
na asiye baba yake (halali) na il-hali anajua
kwamba si baba yake basi pepo ni haramu kwake
(mtu huyu).” Bukhaariy na Muslim.
Hii ndiyo athari mbaya
inayoweza kuikumba jamii ya wanadamu kutokana na
kuendeleza mila na desturi hii mbaya ya kuishi
maisha ya unyumba kisha kupelekea kuzaa mtoto wa
zinaa. Mtu ataozesha kwa kuamini kuwa ana haki
ya kufanya hivyo, na huyu ataamini kuwa
kaoa/kuolewa na hivyo kuwa ni mme/mke wa mtu.
Wakaishi katika dhana hiyo na kupata watoto huku
wakiamini kuwa ni watoto wao, watu wakarithi na
kurithiwa. Lo! Masikini kumbe ukweli na haki ni
kinyume cha wanavyodani au kuamini kwani kwa
mujibu wa sheria huyu si baba bali ni mzinifu
tu. Kwa hivyo hana halali wa kuwa walii na kwa
sababu ya kukosekana walii ambaye ni mmoja wapo
wa nguzo za ndoa, ndoa haipo yaani haikusihii
kisheria. Hivyo wawili hawa mbele ya sheria si
mume na meke ndio maana tunasema huku ni
kuendeleza uchafu juu ya uchafu. Vijana hawa
wanazinishwa kwa sababu tu ya mtu mmoja
aliyekiuka sheria na kuishi na mwana mke
kinyumba yeye kafanya makosa na anasababisha
watu wengine kufanya makosa wakiwa wanajua au
hawajui. Huyu ni mtu mbaya sana, atabeba mzigo
wake wa dhambi zinazotokana na kitendo chake
hiki chenye athari mbaya sana, atabeba mzigo
wake wa dhambi zinazotokana na kitendo chake
hiki chenye athari mbaya kwa jamii na pia
hataepuka kubeba mzigo wa dhambi za aliowapoteza
kwa kuwazinisha. Tusome “(wanapoteza watu
hivi) ILI WABEBE MIZIGO (ya madhambi) YAO KAMILI
SIKU YA KIAMA, NA (pia) SEHEMU YA MIZIGO YA WALE
WANAOWAPOTEZA BILA YA KUWA NA ILIMU (hao
wanaowapoteza) .SIKILIZENI! NI MIBAYA MNO HIYO
(mizigo) WANAYOIBEBA” (16:25) Mfasiri Mkuu wa
Qur-ani Tukufu, Bwana Mtume – Rehema na Amani
zimshukie – anatufafanulia aya hiyo pale
aliposema :- “yeyote
atakayeanzisha/atakayeasisi mwendo (suna) mwema
katika Uislamu, atapata ujira wake (mwendo huo)
na ujira wa watakaoufuata mwendo huo baada yake
(Mtu huyo) bila ya kupungua chochote katika
ujira wao (watendaji) Na atakayeasisi katika
Uislamu mwendo mbaya (kwa maasi aliyoyafanya)
atakuwa juu yake (mzigo wa) dhambi za mwendo huo
na dhambi za watakaomfuata katika mwendo huo
baada yake bila ya kupungua chochote katika
madhambi yao (watendaji).” Muslim. Kukaa na
mwanamke kinyumba ni zinaa ambayo ni miongoni
mwa madhambi makubwa baada ya kufru, shirki na
kuua na ni uchafu aliouharamisha mwenyezi Mungu
Mtukufu: ‘WALA MSIKARIBIE ZINAA. HAKIKA HIYO
(zinaa) NI UCHAFU (mkubwa) NA NI NJIA MBAYA
(kabisa)” 17:32 Mwenyezi Mungu Mtukufu
ametukataza uchafu wa zinaa ili kutuhifadhi na
madhara yake sambamba na athari zake mbaya kwetu
ambazo ni wazi mble ya macho ya kila mmoja wetu.
Miongoni mwa hekima/falsafa ya kuharamisha zinaa
kwa aina zake zote ikiwa ni pamoja na maisha ya
unyumba ni :
1. Kuchunga/kuhifadhi utukufu
na heshima ya mwanadamu. Mwanadamu atofautiane
na hayawani wengine; hayawani wasio wanadamu wao
wana tendo la ndoa tu hawana ndoa na wigo wa
tendo la ndoa kwao ni mpana sana kiasi cha
kuweza kufanya tendo hilo na mama yake/baba
yake.
Sasa ili kudhihirisha utukufu
wa huyu binadamu juu ya baki ya hayawani wengine
ndipo Mola, Muumba wake akamuwekea utaratibu
mzuri ndoa. Aoe kwanza ndipo apate uhalali wa
kufanya tendo la ndoa. Mwanadamu anapoacha
utaratibu huu na kuanza tendo la ndoa kabla ya
ndoa, tendo lake hilo humshushia hadhi na
thamani yake na kuwa kama mnyama au chini zaidi
kuliko mnyama “……. HAO NI KAMA WANYAMA
BALI WAO NI WAPOTEVU ZAIDI ” (7:179)
2. Kuchunga na kuhifadhi
nasabu ya mwanadamu na ukoo wake. Hayawani wasio
na akili hawana nasabu wala ukoo. Huwezi kusema
mathalan : Ng’ombe huyu anaitwa Fulani bin
Fulani wa ukoo Fulani. Lakini mwanadamu ni
lazima kisheria atambulike nasabu na ukoo wake.
Aozwe au kuolewa kwa nasabu hiyo, kadhalika
ajulikane hivyo katika shughuli zote za maisha
ya kibinadamu. Sasa watu wanapoamua kuishi
kinyumba na kuzaa watoto, huko ni kujidhalilisha
na kujivunjia hadhi na heshima yao na
kujitangazia unyama wao na pia wana hatia ya
kumpotezea mtoto aliyezaliwa nasabu na heshima
yake machoni pa jamii ikiwa ni pamoja na
kumkosesha haki zake za msingi kama mtoto.
Ni kutokana na athari hizi
mbaya kwa jamii ndio Mwenyezi Mungu
akauharamisha na kuukemea vikali uzinifu ambao
ni pamoja na kuwekana kinyumba ambako huzaa
haramu nyingine ya kuhalalisha mtoto wa zinaa,
dhambi juu ya dhambi na uchafu juu ya uchafu.
Eeh! Ubaya uloje wa mila mbaya hizi tulizozizua
na kuacha utaratibu mzuri aliotuwekea Mola
Muumba wetu. Hizi ni nasaha za wiki, kunasihika
au kutonasihika hiyo ni juu yako. Amua ama
kunasihika kwa manufaa ya nafsi yako na jamii
kwa ujumla au acha kunasihika kwa mangamizi ya
nafsi yako na jamii kwa jumla na ubebe mzigo wa
dhambi zako na za jamii ikiwa ni matokeo ya
ukaidi wako.
|