|
Leo tena kwa msaada wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu, jukwaa, lako la Nasaha
za wiki linaendela kukuletea na kukuchambulia
mila na desturi zinazopingana na kukhalifiana na
sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Karibu
unasihike pamoja nasi.
2. WACHUMBA KUZOEANA TABIA
Hii ni ada na desturi ambayo
inaishi na kuchukua nafasi katika baadhi ya
familia katika jamii zetu. Binti anapoposwa na
kijana na kufungwa kile kinachoitwa “pamvu”,
kitu ambacho uislamu haukitambui. Pamvu ni kile
kitu ambacho hupelekwa kwa wazazi wa binti ili
kufunga mlango wa posa na kuonyesha kuwa tayari
binti yao amekwishachumbiwa. Baada ya kufungwa
kwa pamvu, kijana wa kiume huwa na fursa ya
kufika nyumbani kwao na binti na kupokelewa kwa
mapana na marefu. Akapikiwa, akala na kunywa kwa
raha na furaha. Akawa na uhuru wa kukaa peke
yake na binti faraghani wakazungumza na kucheka
kwa furaha. Zaidi ya yuote hayo, kijana anaweza
kumchukua binti na kwenda kutembea nae kokote
apendako. Haya yote hufanyika chini ya kivuli ya
kile kinachoitwa “kuzoeana kitabia” kabla ya
kuishi pamoja kaitka maisha ya ndoa. Desturi hii
na yaliyomo ndani ya desturi hii hayakubaliki na
hayana nafasi kabisa katika uislamu. Haijuzu kwa
mujibu wa sheria mchumba kuzungumza na mchumba
wake hata kwa njia ya simu seuze kutokana na
matembezi kukaa nae faraghani bila ya kuwepo
baina yao maharimu wa mtoto wa kike kama vile
Babu, baba au kaka. Kisheria kijana wa kiume
anaruhusiwa kumuangalia mtoto wa kike uso na
mikono anapotaka kumposa bila ya kumgusa na hili
hufanyika mbele ya wazazi wa pande zote mbili.
Hekima ya mkutano huu na kuonana huku ni kuwapa
vijana hawa fursa ya kumuona yule atakayekuwa
mwenza wake katika maisha na pia kuamua kukubali
kuoa au kuolewa ama kukataa. Hili tu ndilo
linaloruhusiwa na sheria. Baada ya kuonana huku,
wachumba hawa hawana ruksa ya kuzugumza au
kuonana tena mpaka watakapooana kwa misingi na
taratibu zote za kisheria ambapo binti sasa
hutambulika kama mke wa mtu na kijana kama mume
wa mtu.
Yaliyozuliwa na watu kinyume
na utaratibu huu tuliowekewa na sheria ni HARAMU
isiyokubalika na yenye adhabu kali mbele ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na athari yake
mbaya kwa jamii. Uzoefu umeonyesha na
kuthibitisha kuwa ada hii ya “kuzoeana
kitabia” katika hatua ya uchumba imefanya ndoa
nyingi zisifungwe. Kijana wa kiume akishapata
nafasi ya kukutana na binti na kufanya tendo la
ndoa kabla ya ndoa, matokeo yake ni kumtia mimba
mtoto wa kike. Baada ya mimba hupatikana
mojawapo ya mambo mawili haya:
- Ama kijana ataukubali mzigo wake ule,
akalea mimba na wakaja kufunga ndoa baadaye
wakiwa na mtoto wa haramu/njeya ndoa.
- Au ataukana mzigo ule uwa si wake na hivyo
kumuacha mtoto wa kike ahangaike na kuteseka
pake yake naye akashika nia kwenda
kuendeleza fisadi na uharibifu wake mahala
pengine.
Sasa ili ili kuzuia haya yote
yasitokee, ndio uislamu ukaamua kuufunga kabisa
mlango huu wa fisadi na uharibifu kwa maslahi
yetu wenyewe. Tufuatane pamoja katika hadithi
ifuatayo ya Bwana Mtume, ili tuone jinsi uislamu
ulivyoharamisha mwanamume kumuangalia mwanamke
ajnabia (wa kando na kando – yaani si maharim
wa mwanamume yule):-
Imepokelewa na Umu Salamah
– Allah amuwiye radhi – amesema: Nillikuwa
mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na
Amani zimshukie - akiwa na Maimunah (mkewe),
akaja/akaingia Abdullah Ibn Ummi Maktuum
(kipofu). Na hili lilikuwa baada ya kushuka aya
za hijabu, akatuambia Mtume; “Jificheni
nae,” tukamwambia; Ewe Mtume wa Mwenyezi
Mungu, je, yeye si kipofu ? Hatuoni na wala
hatujui ? Mtume akatuambia; “Je! Na nyinyi ni
vipofu, hamumuoni ?” Abuu Daawoud na
Tirmidhiy.
Haya, ikiwa huyu ni kipofu
haoni na bado Bwana Mtume anawaamrisha wakeze
waondoke mbele yake, wasimuone kwa kuwa ni
mwanamume. Vipi leo, vijana wetu wa kike na wa
kiume ambao wote wawilli si vipofu wanaona wakae
pamoja wakitazamana na kuzungumza kwa tabasamu
pevu na vicheko vya furaha. Ruksa hii na uhalali
huu wanaupata wapi na il-hali Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – anatuonya;
“Asikae faragha mmoja wenu pamoja na mwanamke
ila (atakapokuwa mwanamke huyo) pamoja na
maharimu wake.” Bukhaary na Muslim. Bwana
Mtume, anatukataza katika hadithi hii kukaa
faraghani (yaani mwanamume na mwanamke peke yao
tu) pamoja na mwanamke ambaye si maharimu yetu.
Mwanamke asiye maharimuni yule ambaye kisheria
hakuna kizuizi wala kipingamizi chochote kwetu
kumuoa. Haya ni maelekezo, maagizo na amri ya
Bwana Mtume ambayo sisi kama waislamu tunapaswa
bali imetulazimu na kutuwajibikia kuifuata na
kiutekeleza mara moja bila ya kuzitii na
kuzifuata amri na maelekezo ya Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie. Na ni vema ikatiwa
akilini kuwa kumtii na kumfuata Bwana mtume ni
amri ya mwenyezi mungu mtukufu, tusome na
tutekeleze. “………………NA ANACHOKUPENI
MTUME (ANACHOKKUAMRISHENI BASI POKEENI), NA
ANACHKUKATAZENI JIEPUSHENI NACHO
………………...” (59:7)
Tusome tena kwa mazingatio na
kasha tufuate: “SEMA: IKIWA NYINYI MNAMPENDA
ALLAH, BASI NIFUATENI; (HAPO) ALLAH ATAKUPENDENI
NA KUKUGHUFIRIENI MADHAMBI YENU” (3: 31)
Aya hizi na nyinginezo ndizo
zinazotulazimisha kumfuata na kumtii Bwana Mtume
katika maelekezo, maamrisho au makatazo yote
atakayotupa kwa maslahi na manufaa yetu wenyewe.
Kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu mtukufu
ametukamilishia dini hii kupitia kwa Mtume wake.
Dini hii haikusaza lolote lenye manufaa na faida
kwetu katika maisha haya ya dunia na yale yajayo
ya akhera ila imetueleza jambo hilo na namna ya
kulitekeleza. Kadhalika haikuacha lolote lile
lenye madhara na kasoro kwetu ila
imetuabainishia na kututahadharisha nalo na
kutuonya tusilitende au kulifuata. Sasa ikiwa
dini hii imekamilika na kila jambo linalohusu
nyanja mbalimbali za maisha yetu ya kila siku
limekwisha bainishwa na kuwekewa utaratibu wake
wa kulitekeleza au kulienda. Kwenda kinumbe na
utaratibu huo, kunamaanisha:
- Dini hii haikukamilika kama anyavyosema
Mwenyezi Mungu mtukufu
- Kumkadhibisha mwenyezi mungu na Mtume
wake, jambo ambalo ni maasi.
- Sisi tunayo mamlaka na madaraka ya
kujitungia sheria kinyume na sheria za
Mwenyezi Mungu mtukufu.
- Tuna uamuzi na khiyari ya kufuata ama
kutokufuata sheria/ hukumu za Mwenyezi Mungu
mtukufu.
- Sheria na taratibu zetu tulizojipangia ni
bora na zinafaa zaidi kuliko zile za
mwenyezi mungu
- Kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Kwa ujumla kutokumfuata Bwana
Mtume ni kumhalifu na kumpinga, jambo ambalo
Mwenyezi Mungu mtukufu ametukataza tusome na
tuzingatie: “ ................BASI WAJIHADHARI
WALE WANAOKAIDI AMRI YAKE USIJE UKWAPATA MSIBA
AU UKAWAFIKA ADHABU IUMIZAYO.” (24: 63)
Leo kwa sababu ya ukaidi na
kukhalifu kwetu amri ya Bwana Mtume – Rehema
na amani zimshukie- na tukaruhusu mila na
desturi hii ya kuzoeana tabia iitawale jamii
yetu, tayari tumeshafikwa na kupatwa na msiba.
Msiba huu si mwingine bali ni wimbi na janga la
watoto wa haramu/nje ya ndoa na pengine hata
hawa tuwaitao leo watoto wa mitaani ni natija ya
kuendekeza na kufuata mila tamaduni n a desturi
hizi mbaya. Taathira na athari na ada hizi
potofu ziko wazi na bayana kwa kila mmoja wetu.
Haya sasa ndugu zanguni waislamu, tuamue ama
kumfuata Bwana Mtume tupate salama au
kutokumfuata na kuendeleza mila tamaduni na ada
zetu wenyewe tufikwe na msiba na adhabu kali
iumizayo. Mwisho ni vema tukakumbuka na kukiri
kuwa hizi ni hasaha za wiki, kunasihika au
kutonasihika huo ni uamuzi wako wewe mwenyewe.
|