|
Mwenyezi Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia ndani
ya Qur-ani Tukufu:"ENYI MLIOAMINI !INGIENI
KATIKA HUKUMU ZA UISLAMU ZOTE, WALA MSIFUATE
NYAYO ZA SHETANI, KWA HAKIKA YEYE KWENU NI ADUI
DHAHIRI".
Hili nitangazo na agizo la Mwenyezi Mwenyezi
Mungu Mtukufu kwa kila ambaye ameukiri na
kuukubali uislamu kwa khiyari yake mwenyewe.
Katika tangazo na amri hii analazimishwa kila
muislamu kuufuata uislamu mzima kama mfumo wa
maisha yake yote. Aufuate uislamu katika maisha
yake ya kijamii, kiuchumi,kielimu, kiulinzi,
kiibada na baki nyanja nyingine za maisha yake.
Atambue kuwa uislam kama dini ndio mfumo sahihi
wa sheria, mila na utamaduni umfaao mwanadamu.
Ni mfumo ulio kamilika, kwa mantiki hii
uislamu,uislamu hauna upungufu na wala
hauhitajii ziada yoyote kutoka popote pale. Haya
yanathibitishwa na kauli tukufu ya Mola Mtukufu:
"LEO NIMEKUKAMILISHIENI DINI YENU, NA
KUKUTIMIZIENI NEEMA YANGU, NA NIMEKUPENDELEENI
UISLAMU UWE DINI YENU…."[5:3]
Aya inaeleza bayana kuwa uislamu ndio mfumo
sahihi na kamili wa maisha, uislamu ni Neema ya
Mwenyezi Mwenyezi Mungu kwa waja wake uislamu
ndio dini TEULE na CHAGUO la Mwenyezi Mwenyezi
Mungu Mtukufu kwa waja wake. Kwa mantiki hii,
leo waislamu kuhukumiana nje ya Qur-ani ,
kufuata mila na tamaduni zinazokhalifiana na
sheria ya Mwenyezi Mwenyezi Mungu ni sawa na
kuibatilisha aya hiyo hapo juu isemayo kuwa
uislamu umekamilika. Matendo yao hayo
yanaonyesha kuwa uislamu umesahau kuyawekea
sheria, kanuni na taratibu baadhi ya maeneo
katika maisha ya mwanadamu. Kwa hivyo, wao
wanayo fursa ya kujipangia sheria, kanuni na
taratibu zitakazokidhi haja zao katika maeneo
husika bila kujali wala kuangalia kuwa kanuni na
taratibu hizo zinapingana na sheria ya Mwenyezi
Mwenyezi Mungu Mtukufu na isitoshe bado watu
hawa waliojiundia mila na tamaduni zao nje ya
uislamu bado wanadai na kujiita kuwa ni
waislamu. Mtu ana khiyari ya ama kuwa au
kutokuwa muislam, kwa ushahidi wa kauli yake
Mwenyezi Mwenyezi Mungu Mtukufu : "HAKUNA
KULAZIMISHWA (mtu kuingia)KATIKA DINI UONGOFU
UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTEFU BASI ANAYEMKATAA
SHETANI NA AKAMWAMINI ALLAH BILA SHAKA YEYE
AMESHIKA KISHIKO CHENYE NGUVU KISICHOKUWA NA
KUVUNJIKA…"[2:256]
Na akasema tena : "NA SEMA : "HUU
NI UKWELI ULOTOKA KWA MOLA WENU BASI ANAYETAKA
NAAMINI NA ANAYETAKA NA AKUFURU
…."[18:29]
Mtu akishautumia uhuru na khiyari aliyopewa
na akauchagua uislamu kama dini na mfumo wa
kuyatawala maisha yake yote, hapo sasa hana
khiyari tena ya kuchagua hukumu/sheria zipi za
uislamu asifuate na zipi asizifuate, bali
analazimishwa kuzifuata shria zote. Mwenyezi
Mungu Mtukufu anaikemea vikali tabia hii ya
kufuata baadhi ya hukumu/sheria na kuacha
nyingine, tusome na kutafakari : "… JE!
MNAAMINI BAADHI YA KITABU NA KUKATAA BAADHI
(yake) ? BASI HAKUNA MALIPO KWA MWENYE KUFANYA
HAYA KATIKA NYINYI ILA FEDHEHA KATIKA MAISHA YA
DUNIA ; NA SIKU YA KIYAMA WATAPELEKWA KATIKA
ADHABU KALI …."[2:85]
Mwenyezi Mungu Mtukufu anazidi kutuambia na
kutuonyesha kuwa Muislamu wa kweli hana khiyari,
uhuru wala uchaguzi katika kufuata ama
kutokufuata sheria/hukumu za kiislamu kama mfumo
sahihi wa maisha, tusome na tuzingatie:
"HAIWI KWA MWANAUME ALIYEAMINI WALA KWA
MWANAMKE ALIYEAMINI, ALLAH NA MTUME WAKE
WANAPOKATA SHAURI, WAWE NA HIARI KATIKA SHAURI
LAO, NA MWENYE KUMUASI ALLAH NA MTUME WAKE,
HAKIKA AMEPOTEA UPOTOFU ULIO WAZI(kabisa)".
[33:36]
Mpaka hapa, tayari tume kwisha thibitisha
kuwa uislamu ni dini iliyokamilika na kwamba
mwislamu hana uchaguzi katika kufuata ama
kutokufuata hukumu/sheria za uislamu.
Muislamu hana fursa hata kidogo ya kujiundia
kanuni, taratibu, mila au desturi na ada zilizo
nje ya uislamu, kitendo hicho ni kosa kubwa
ambalo limeandaliwa adhabu kali iumizayo na
kutia uchungu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Hebu sasa tujaribu kuziangalia baadhi ya mila,
tamaduni, desturi na ada zinazokhalifina na
kupingana na sheria. Desturi na ada hizi
tunazoishi nazo kataka jamii na kurithishana
kizazi hata kizazi zimezoeleka na kuota mizizi
katika jamii zetu kiasi cha kusifanya zionekane
kuwa ni za kawaida na zinakubalika katika dini,
na ukweli ni kwamba hazina nafasi kabisa katika
dini hii iloyokamilika na kujitosheleza.
UNYAGO
Hii ni mila na desturi iliyoenea na kufuatwa
na makabila mengi khusasan hapa kwetu Tanzania.
Unyago ni mila ya kumcheza mtoto wa kike wakati
avunjapo ungo. Wakati huo huandaliwa ngoma
maalum ambayo huwashirikisha akina mama watu
wazima. Hawa kazi yao kubwa ni kile kinachoitwa
"kumfunda" mwanamwali, yaani
kumfahamisha kuwa sasa yeye amekuwa mwanamke na
kumealeza nafasi yake kama mwanamke, majukumu
yake na jinsi ya kuishi na mume. Ngoma hii
huchezwa mahala pa wazi, mahali ambapo hata
mwanamume hupata fursa ya kuwaona wanawake, wake
za watu wakikata viuno. Mahala hapa, mwanamwali
huonyeshwa akiwa kavishwa khanga ya kiuno tu na
baki ya mwili wake kuachwa wazi ikiwa ni pamoja
na matiti yake. Katika ngoma hii wanawake hunywa
pombe ili kutoa aibu na haya wapate kukata viuno
vizuri, na baadhi au wengi washirikio katika
mila hii hujiita kuwa ni waislamu. Waelewe
uislamu hakuna mila kama hizi mbaya na
kushikilia kuzifuata na kuziendeleza desturi
hizi huku wakivaa vazi la uislamu, huko ni
kuudhalilisha na kuutukanisha uislamu. Mila na
desturi hizi huzifai kwa kuwa zinapingana na
sheria kamilifu ya Mwenyezi Mwenyezi Mungu, kwa
hivyo tuziache mara moja pamoja na kuzizoea na
kuzionea ladha kwetu. Mila hizi hazifai kwa
sababu zifuatazo:
- Unyago huwashirikisha mwanaume na
wanawake, kama tushuhudiavyo leo. Katika
uislamu ni kosa kubwa mwanamume
kuchanganyika na wanawake.
- Katika unyago huimbwa nyimbo za matusi,
hili halikubaliki hata kiakili na kimaadili
seuze sheria .
- Katika unyago watu hulewa eti kwa sababu
ya kumsherekea mtoto wao. Uislamu umekataza
ulevu kwa sababu yoyote ile iwayo, hata kama
ni dawa kama wanavyodai hivyo baadhi ya
watu.
- Mwanamwari hudhalilishwa na kunjiwa
heshima yake kama mwanadamu kwa kuanikwa
uchi mbele ya hadhara ya watu wakiwemo
mwamume.
- Katika unyago hupatikana matumizi mabaya
ya mali. Pesa ambazo zingetumika katika
mambo mengiya maendeleo kwa maslahi ya jamii
na familia husika, hutumika kununulia pombe,
kuwalipa wapiga ngoma na kugharimia chakula
cha wanangoma kwa kipind chote cha ngoma.
Hii ndio israafu inakemewa na kukatazwa na
uislamu.
Kwa ujumla, huzalikana na kupatikana katika
desturi na mila hii ya unyago, mambo mengi
ambayo yanakhalifiana na sheria. Kwa mantiki hii
kila aliyekuwa muislamu anpaswa kuziacha mara
moja mila na desturi hizi ili awe muislamu
kamili.Uislamu haupingi wala kulikataa suala la
kumfundisha mtoto wa kike/kiume nafasi yake yeye
kama mwanamume/mwanamke na majukumu yake kama
mke kwa mumewe au mume kwa mkewe. Aishi vipi na
jamii, ailee vipi familia. Uislamu unapinga na
kukataa namna au njia na jinsi itoleavyo elimu
hii. Uislamu umesheheni fani zote za elimu iwe
na elimu ya kijamii, uchumi, afya, ulinzi na
usalama, siasa na kadhalika, zote hizi zimo
ndani ya uislamu, tusome tu tutakutana nazo.
Sasa kama elimu hii tunayo, kwa nini hatujifunzi
na kuitoa kwa misingi yetu ya kiislamu?! Jamani
, tuziache mila, desturi na ada hizi potofu na
badala yake tushikamane na kuifuata mila na
desturi sahihi za uislamu. Uislamu ndio mila
baba yetu Nabii Ibrahimu- Rehema na Amani
zimshukie, tusome: "…..(Nayo dini hii) NI
MILA YA BABA YENU IBRAHIMU…."[22:78]
Hivi ni kweli kuwa leo sisi tunaweza kuwa na
mila na desturi bora kuliko mila ya Nabii
Ibrahimu?! Kuacha kufuata mila ya Baba yetu
Ibrahimu na kujiundia mila zetu wenyewe huo ni
UPUMBAVU, tusome na tukubali: "NA NANI
ATAJITENGA NA MILA YA IBRAHIMU ISPOKUWA
ANAYEITIA NAFSI YAKE KATIKA
UPUMBAVU…"[2:130]
|