|
Mafaqihi
(wanazuoni wa sheria ya Kiislamu) wamekhitilafiana katika kadhia ya
mwanamke kuwa na mimba bila ya mume. Je, anawiwa na ‘hadda’?,
wamekhitilafiana kwa kauli mbili:-
KAULI
YA KWANZA:
Itakapodhihiri mimba kwa mwanamke asiye na mume, mimba hii haimpasishii ‘haddi’.
Lakini ataulizwa, akidai kuwa alibakwa bila ya khiari yake au aliingiliwa
katika mazingira ya ‘shubuha’. Au hakukiri kuzini, katika hali na
mazingira haya hapasiwi na ‘haddi’. Haya ndio madhehebu ya maimamu;
Shaafiy, Abu Haniyfah na Ahmad Ibn Hambal-Allah awarehemu. Rejea kitabu
[AL-MUGHNIY pamoja na SHEREHE yake cha Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy 10/192]
DALILI/USHAHIDI
WA KAULI HII:
Maimamu
walioisimamia kauli hii katika madhehebu ya Hambal, Shaafiy na Hanafiy
wameyafanya kuwa dalili yao majumuisho ya Ibn Qudaamah Al-Maqdisy katika
kadhia hii pale aliposema: “Na kwetu sisi kwa hali ilivyo inamkinika
kuwa mimba hiyo inatokana na kuingiliwa kwa kubakwa au kwa shubuha. Na
hali ilivyo ni kupomoka haddi kwa matendo ya shubuha. Na imekwishasemwa
kwamba mwanamke anaweza kushika mimba bila ya kuingiliwa kimwili. Na hili
hupatikana kwa kuingia mbegu za kiume (manii) ukeni kwake ima kwa kitendo
chake mwenyewe akajiingizia au kwa kitendo cha mtu mwingine kama daktari
na kadhalika. Hii ndio picha inayoweza kuchorwa kwa ujauzito wa mwanamwali;
bikira na hili limewahi kutokea.
Ama maswahaba wa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-riwaya zilizopokewa kwao
zimekhitilafiana. Said amepokea: “Alituhadithia” Khalf Ibn Khaliyfah
“Ametuhadithia” Haashim: “Kwamba mwanamke fulani alipelekwa mbele
ya (Amirul-Muuminina) Umar Ibn Al-Khatwab akiwa na mimba bila ya mume.
Umar akamuuliza (nae) akajibu: Mimi ni mwanamke mwenye kichwa kizito
(obtuse), niliingiliwa na mwanamume fulani nikiwa nimelala. Basi sikuamka
ila baada ya yeye kukidhi matamanio yake, (kwa utetezi wake huu) Umar
akamuondoshea adhabu”.
Na Al-Baraai Ibn Swabrah akapokea kutoka kwa Umar: “Kwamba aliletwa
mwanamke mjamzito, akadai kuwa alibakwa, (Umar) akasema: Muachieni njia
yake (aende huru)”. Na akawaandikia maamirijeshi ya kwamba asiuliwe
mtu ye yote ila kwa idhini yake.
Na imepokewa kutoka kwa Sayyidina Ibn Abbas na Aliy-kwamba wao wamesema: “Yatakapokuwepo
katika (kadhia ya) haddi maneno ‘huenda’ na ‘pengine’, basi (haddi)
ni yenye kuzuiliwa (kutekelezwa)”.
Na imepokewa na Daaruqutwniy kwa isnadi yake kutoka kwa Abdillah Ibn Masoud
na Muaadh Ibn Jabal na Uqbah Ibn Aamir kwamba wao wamesema: “(Suala
la) haddi litakapokutatiza, basi iepushe kiasi uwezacho”. Na
wala hapana makindano kuwa haddi huepushwa au huzuiwa kwa matendo ya
shubuha na hili limethibiti hapa”. Zimekoma dalili za Ibn Qudaamah,
rejea kitabu [AL-MUGHNIY pamoja na SHEREHE yake cha Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy
10/192-194]
KAULI
YA PILI:
Mwanamke
atakapoonekana na ujauzito bila ya kuwa na mume, atalazimikiwa haddi kwa
sababu ya mimba hiyo. Wala madai yake ya kubakwa hayatakubaliwa ikiwa
hayakuambatana na ushahidi wa kulithibitisha hilo. Ama akileta ushahidi
unaozingatiwa mbele ye sheria, basi hatapasiwa na haddi. Ushahidi huu ni
kama vile mwanamke kuja huku akitokwa na damu nae akipiga mayowe ya kuomba
msaada. Au akaja akiwa kamkwida mbakaji wake huyo, haya ndio madhehebu ya
Imamu Maalik-Allah amrehemu. Rejea SHEREHE ya Al-Kharsiy juu ya MUKHTASWAR
KHALIYL-5/333.
DALILI/USHAHIDI
WA KAULI HII YA PILI:
Watu waliosimamia kauli hii ambao ni wafuasi wa madhehebu ya Imamu Maalik
wametoa ushahidi kwa riwaya iliyotolewa na Imamu Bukhaariy kutokana na
kauli ya Sayyidina Umar, pale aliposema: “Na kupopolewa kwa mawe ni
wajibu kwa kila ambaye amezini miongoni mwa wanawake na wanaume
atakapokuwa ni muhswani (mwenye ngome). (Hivyo ni iwapo) utapatikana
ushahidi, au ikadhiri mimba au akakiri”. Angalia rejea iliyotajwa
hapo juu.
|