Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

B/. HEKIMA/FALSAFA YA KUSHURUTIZWA MASHAHIDI WANNE KATIKA KUTHIBITISHA KOSA LA ZINAA

Faida

Ni jambo lisilo na shaka kwamba suala la kutoa ushahidi wa kutendeka kwa kosa/hatia ya zinaa ni suala linalohusu kuthibitisha jinai ya kimaumbile inayomgusa moja kwa moja mtendaji wa jinai hiyo. Jinai inayomfedhehesha muhusika mbele ya macho ya jamii ukiachilia mbali  adhabu kali sana inayoambatana na jinai hiyo. Ni kwa mantiki hii, ndio sheria ikawa makini na kutia mkazo wa haja katika kuweka njia za kuithibitisha jinai hii ambayo inaweza kuyagharimu maisha ya atakayetiwa hatiani. Ni kwa ajili hii jinai/hatia hii ya zinaa ikakhusishwa na mashahidi wanne watakaoshuhudia juu ya dhati ya kitendo cha zinaa, yaani kitendo chenyewe khasa na si vinginevyo. Sheria imelenga katika kuweka mazingira haya magumu ya kupatikana ushahidi wa kuthibitisha kosa la zinaa, kuweka pazia la sitara na kumuondoshea aibu na fedheha mzinifu na jamaa zake. Na Allah Mtukufu anapenda kuwasitiri waja wake na amelipondokesha hilo kwa waja wake pia, kuwa na wao wapende mno kusitiri kuliko kufedhehesha. Na hii ndio mojawapo ya falsafa ya kauli za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayemsitiri muislamu, Allah atamsitiri duniani na akhera”. Rejea kitabu [AT-TARGHIYBU WAT-TARHIYBU].

Kama ambavyo Allah alivyokemea uenezaji wa uchafu/uovu kwa jamii: “KWA YAKINI WALE WANAOPENDA UENEE UOVU KWA WALE WALIOAMINI, WATAPATA ADHABU IUMIZAYO KATIKA DUNIA NA AKHERA, NA ALLAH NDIYE ANAYEJUA (ya maslaha yenu) NA NYINYI HAMJUI”. [24:19]

Kwa hivyo basi, ili kuthibitisha maana ya sitara aliyoipendelea Allah na Mtume wake, ndipo ikashurutizwa ziada ya idadi ya mashahidi kinyume na ushahidi wa makosa mengine. Na katika kushurutizwa ushahidi wa watu wanne ni kuthibitisha maana ya sitara, kwa sababu watu wanne kujua na kushuhudia uchafu huu wa zinaa ukitendeka ni suala la nadra mno kuweza kupatikana. Na kanuni zinasema kwamba kila jambo zinapokithiri sharti zake, jambo hilo huwa kuchache mno kutokea kwake. Kwa sababu kupatikana kwake kutakaposimama juu ya ushahidi wa mashahidi wanne, hakuwezi kuwa kama itakavyokuwa kupatikana kwake kutakaposimama juu ya ushahidi wa mashahidi wawili. Kwa hali na mazingira haya, inathibiti ile maana ya sitara iliyopendekezwa na sheria. Kisha itakapokuwa sitara imependelewa na sheria, basi kushuhudia zinaa itakuwa ni kinyume cha ilivyo bora (khilaful-aula) ambayo marejeo yake ni katika karaha ielekeayo kwenye uharamu (karahatut-tanziyhi). Na vile vile kwa kuwa sitara ndilo jambo lililopendekezwa, basi kueneza khabari ya uovu kunakuwa ni jambo lenye kuchukiza na kulaumiwa.

Ni vema ikaeleweka kwamba sitara hii ni wajibu iwe kwa mtu ambaye hakuzini kwa makusudi na wala hakuifichua dhambi hiyo mbele ya kadamnasi kwa kujinadi na kujinasibu. Ama atakapofikia hatua ya kuivunja mwenyewe sitara aliyositiriwa na Mola wake, akaifichua na kuieneza khabari ya uchafu na uovu wake huo kiasi cha kujigamba na kujifakharisha. Mtu kama huyu kutoa ushahidi dhidi yake kunakuwa ni wajibu na bora zaidi kuliko kuacha kuutoa. Hivi ni kwa sababu matakwa na shabaha ya sheria ni kuisafisha na kuitakasa ardhi kutokana na maasi na maovu, kwani imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Enyi watu, umekwishakufikieni wakati wa kukomeka na mipaka ya Allah (aliyokuwekeeni msiivuke). Basi ye yote atakayekiingia cho chote miongoni mwa taka (madhambi) hizi, basi na ajisitiri kwa sitara ya Allah. Kwani hali ilivyo, ye yote atakayetufunulia dhambi/kosa lake (alilolitenda sirini) tutamsimamishia hukumu ya kitabu cha Allah Mtukufu”. Imamu Maalik (Muwatwaa)-Allah amrehemu.

Na Imamu Shaafiy-Allah amuwiye radhi-akasema: “Nasi tunapenda mtu aliyesibu ‘haddi’ (kosa linalompasishia adhabu kwa mujibu wa sheria) ajisitiri. Na amche Allah Mtukufu na wala asirudie tena kufanya maasia hayo kwani kwa yakini Allah huwakubalia (huwapokelea) toba waja wake”. Rejea kitabu (AL-UMMU).

Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilikuwa kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mara akajiwa na mtu fulani akasema: Ewe Mtume wa Allah, mimi nimetenda kosa linipasishialo adhabu (haddi), basi nisimamishie adhabu. Akasema (Anas): Mtume hakumuuliza juu ya kosa hilo. Akasema: Ukaingia wakati wa swala, (mtu yule) akaswali pamoja na Mtume. Mtume alipomaliza kuswali, mtu yule akamuinukia (akamuendea) na kumwambia: Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi nimetenda kosa linipasishialo adhabu, basi ninakuomba unisimamishie hukumu ya kitabu cha Allah. Mtume akamwambia: “Kwani wewe hukuswali pamoja nasi?” akajibu: Naam, (nimeswali), Mtume akamwambia: Basi bila ya shaka Allah amekwisha kusamehe dhambi yako. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Ibn Hajar-Allah amrehemu-amesema: “Na hakika si vinginevyo, Bwana Mtume hakumtaka ufafanuzi wa kosa. Ima ni kwa sababu hilo linaingia katika mlango wa kupeleleza khabari za watu kulikokatazwa. Na ama ni kwa kupendelea zaidi kusitiri maovu na akaona kwamba kule kutaka kwake kusimamishiwa adhabu tayari ni majuto na kurejea (kwa Mola wake). Na ndio wanazuoni wakapendelea kumfundisha mtu aliyekiri kutenda jambo linalompasishia adhabu kutengua ikrari yake. Afanye hivyo kwa njia ya kuambaambaa au kwa njia ya wazi moja kwa moja ili ajiondolee adhabu (inayomkabili)”. Rejea kitabu (FAT-HUL-BAARIY) cha Ibn Hajar Al-asqalaaniy (12/122) na (AL-BAHRUR-RAAIQ) cha Ibn Najiym Al-hanafiy (5/8)-Allah awarehemu.

 

C/. MAUDHUI YA MANENO YA KUTHIBITISHA USHAHIDI MBELE YA KADHI (TESTIMONY) NA MADHUMUNI YAKE.

Ili kuthibitisha jinai ya zinaa kwa ushahidi unaotolewa mbele ya kadhi (testimony) na ili ushahidi huo ukubaliwe kisheria. Hapana budi washuhudie mashahidi wanne juu ya kuona kwa macho yao dhati ya kitendo cha zinaa baina ya mwanamume na mwanamke. Washuhudie kwamba wao wameiona tupu (ala) ya mwanamume imeingia ndani ya tupu ya mwanamke mithili ya kijiti cha wanja kiingiavyo ndani ya kichupa cha wanja. Tena washuhudie kuona kitendo hicho kwa wakati mmoja na muono mmoja; wote kwa pamoja. Kadhi awadodose mpaka wathibitishe kwamba hakika wao wameiona kwa macho yao ile ya mwanamume ikiingia katika ile ya mwanamke uingiaji wa kijiti cha wanja ndani ya kichupa cha wanja. Kisha kadhi awaulize mashahidi hao:-

ü      Zinaa ni nini.

ü      Zinaa huwaje; yaani zinaa hupatikanaje.

ü      Walishuhudia ikitendeka wapi na wakati gani.

ü      Mwanamume amezini na mwanamke yupi.

Haya yote ni kwa sababu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimuhoji sana swahaba wake Maaiz juu ya hilo na akamwambia: “Mpaka hiyo yako ikaingia ndani ya ile yake?” Akajibu: Naam, (Mtume) akamuuliza (tena): “Kama kizamavyo kijiti cha wanja ndani ya kichupa cha wanja na mithili ya kamba iingiavyo ndani ya kisima?” Akajibu: Naam, (Mtume) akamuuliza (tena): “Je, unatambua zinaa ni nini?” Akajibu: Naam, nimemuendea kwa njia ya haramu (zinaa) kama ambavyo mume amuendeavyo mkewe kwa njia ya halali (ndoa). (Mtume) akamuuliza (tena): “Unataka/unakusudia nini kwa kauli yako hii?” Akasema: (Ninakusudia) unitwaharishe”.

Sasa basi, kama ambavyo kadhi anavyowajibikiwa kumuhoji mtu aliyekiri mwenyewe ili kuithibitisha ikrari yake. Ni hivyo hivyo anao wajibu wa kisheria kuwahoji mashahidi ili kuuthibitisha ushahidi wao.

 

TAFSIRI/UFAFANUZI WA MASWALI YAULIZWAYO.

Ama lengo la kuwauliza zinaa ni nini, ni kwa sababu ya kuwepo imkani ya kumaanisha kitendo kingine kisichohusisha tupu (uchi). Swali liulizalo zinaa ilikuwaje/ilitendeka vipi, ni kwa sababu ya kuwepo imkani ya kutendeka kwa nguvu; bila ya ridhaa au tupu ziligusana pasina dhakari kuingia ndani ya uke. Zinaa ilitendeka wapi, swali hili linakuja kwa sababu yamkinika kitendo alichokishuhudia shahidi huyu sicho alichokishuhudia shahidi yule. Sasa basi wanaulizwa mahala ili kuoanisha ushahidi wao. Swali liulizalo zinaa ilitendeka lini, ni kwa sababu yamkinika kuwa tendo lilitendeka zamani, ujanani mwake au katika hali ya uwendawazimu. Alizini/amezini na nani, kwa sababu yamkinika mwanamke huyo kuwa ni mkewe ambaye mashahidi hawa hawamfahamu. Kwa jumla ni kwamba maswali yote ambayo sheria inamlazimisha kadhi kumuuliza mwenye kukiri/mashahidi yanalenga kupatikana kwa ithibati kabla ya kutolewa kwa hukumu inayoambatana na ikrari/ushahidi huo.

 

TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

“Si halali kumwaga damu ya muislamu anayeshuhudia kwamba hapana muabudiwa wa haki ila Allah na Muhammad ni mjumbe wake, ila kwa mojawapo ya mambo matatu (haya):-

1.       zinaa baada ya ngome, hakika huyo atarujumiwa kwa mawe mpaka kufa.

2.      atakayetoka kumpiga vita Allah na Mtume wake, huyu atauliwa au atasulubiwa au atahamishwa katika nchi.

3.      atakayemuua mtu, naye atauawa kwa sababu ya nafsi aliyoiua”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Abuu Daawoud & Nasaai-Allah awarehemu.


Forum | Guestbook | Tuandikie |