|
Katika macho ya sheria ikrari huzingatiwa kuwa ni hoja dhidi ya
mwenye kukiri; yaani ni hoja inayomtia hatiani na kumpasishia adhabu kwa
mujibu wa sheria. Wala hakusihi kukana/kutengua ikrari baada ya kuthibiti
kwake mbele ya kadhi katika masuala ya haki ila katika masuala ya “haddi”
kama zinaa, wizi, unywaji wa pombe na kadhalika. Masuala haya ya haddi
(adhabu) kunasihi kukana/kutengua ikrari kwa mwenye kukiri. Mathalan, mtu
akikiri uzinifu au kuiba au kunywa pombe, halafu akaitengua ikrari yake,
utenguzi wake huo husihi mbele ya sheria na kwa kusihi kwake huko
humpomoshea adhabu iliyomkabili kutokana na kosa hilo. Mithili ya
kucharazwa bakora au kupopolewa kwa mawe kufuatia hatia ya uzinifu, au
kucharazwa bakora kufuatia hatia ya unywaji pombe na kukatwa mkono
kufuatia hatia ya wizi. Haya ni kwa upande wa haki za Allah Mola Mwenyezi,
ama kwa upande wa haki za waja wa Allah (wanadamu wenziwe), hakusihi
kutengua kwake ikrari baada ya kuthibiti mbele ya kadhi. Hakupomoki
kurudisha kitu kilichoibwa kwa mwenyewe aliyeibiwa baada ya kukiri kuiba
kisha akatengua ikrari yake, kwa sababu hiyo ni haki ya waja na si haki ya
Allah.
Kumependelewa kwa Imamu katika “haddi” ya zinaa kumfundisha mtu
aliyekiri kosa la zinaa kutengua ikrari yake. Angalia, mtu atakapokiri
kutenda kosa la zinaa, halafu akatengua ikrari yake. Linalofuatia utenguzi
huo wa ikrari ni kupomokewa na haddi (adhabu) iliyompasia kutokana kukiri
kwake mara ya kwanza. Bila ya kujali kuwa utenguzi huo ulikuwa ni kabla ya
kuanza kutekelezwa kwa adhabu husika au ni baada ya kuanza kutekelezwa kwa
adhabu hiyo (ndani ya adhabu). Ikiwa ni kabla ya kuanza kutekelezwa kwa
adhabu, kutasimamishwa kucharazwa bakora na kupopolewa kwa mawe. Na ikiwa
ni baada ya kuanza kutekelezwa kwa adhabu husika, yaani baada ya kuanza
kucharazwa bakora kadhaa au kupopolewa kwa mawe. Pale pale baada ya
kutengua ikrari yake, atasikilizwa na adhabu itakoma mara moja na
haitokamilishwa. Ni mamoja ametaja sababu ya utenguzi wake huo au
hakutaja. Hii ni kwa sababu Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alipomdhihirishia Maaiz kutengua ikrari yake kwa kumwambia “Huenda
wewe ulibusu, au ulikonyeza au uliangalia tu”. Lau kauli hii ya
Bwana Mtume ingelikuwa haimpomoshei adhabu husika ingelikuwa haina maana.
Na kwa sababu walipoanza kumpopoa kwa mawe, Maaiz alisema: Nirudisheni
kwa Mtume wa Allah, wala hawakumsikiliza (wakaendelea kumpopoa kwa
mawe mpaka akafa). Walipomtajia hilo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alisema: “Kwa nini hamkumuacha, huenda angelitubia
na Allah akampokelea toba yake”.
Ibn Hajar Al-asqalaaniy-Allah amrehemu-amesema: “Imepokelewa na Abuu
Daawoud na isnadi yake ni HASAN”.
Ibn Abdul-barri amesema: “Na kauli hii (ya Bwana Mtume) ni dalili ya wazi
kabisa inayoonyesha kwamba utenguzi wake unakubaliwa”. Mughnil-Muhtaaj
[4/139]
Na kwamba hukumu ni hii hii iwapo mwenye kukiri atakimbia wakati wa kuanzwa
kutekelezwa kwa adhabu inayoambatana na ikrari yake. Kukimbia huko
kutampomoshea adhabu iliyomuwajibikia, kwa sababu ukimbiaji huo uko katika
maana ya utenguzi wa ikrari. Yote haya ndiyo madhehebu ya maimamu wanne wa
kisunni; Maalik, Shaafiy, Ahmad na Abuu Hanifah.
Na hali kadhalika atakapokiri chini ya mara nne, hakumlazimikii kukamilisha
kiwango cha ikrari kufikia mara nne. Bali kunamuelea Imamu kumuambaa na
kumuelezea kutokukamilisha ikrari. Kama Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alivyompa Maaiz fursa ya kutengua ikrari yake pale alipokiri
zinaa mbele yake mara ya kwanza, ya pili na ya tatu. Hivi ndivyo
ilivyoelezwa katika kitabu (ZAADUL-MAADI).
- KUTHIBITI
ZINAA KWA USHAHIDI WA KUONA:
Ushahidi wa mtu kwa kuona kosa la zinaa likitendeka huzingatiwa mbele ya
sheria kuwa ni njia ya pili ambayo hatia ya zinaa huthibiti kwayo. Na
tafsiri ya “ushahidi” mbele
ya sheria ni: [kutoa khabari au maelezo kuhusiana na jambo fulani kwa
tamko maalum, nalo ni kule kusema “ninashuhudia”]
Sharti
za shahidi:
Ili
ushahidi utolewao uzingatiwe na sheria, kumeshurutizwa huyo shahidi awe:-
- muungwana
(mtu huru); yaani asiwe mtumwa.
- mwenye
akili timamu; yaani asiwe mwendawazimu au amelewa.
- mkubwa;
yaani asiwe mtoto mdogo.
- mwenye
murua; yaani asiwe mtu mpuuzipuuzi.
- si mwenye
kutuhumiwa katika ushahidi wake.
{Rejae kitabu-(MUGHNIL-MUHTAAJ)-4/392 na
NIHAAYATUL-MUHTAAJ (8/125)}.
Ili ushahidi wa kuona hatia/kosa la zinaa ukubaliwe mbele ya sheria, hapana
budi washuhudie mbele ya kadhi mashahidi wanne waadilifu. Washuhudie kuwa
mwanamume na mwanamke wametenda tendo khasa la zinaa na washuhudie kwa
tamko la “zinaa”, waseme katika ushahidi wao: “tumewashuhudia
wakizini”. Na sio kwa tamko jingine lo lote ambalo linabeba maana ya
zinaa likichanganya pamoja na maana nyingine. Limekhusishwa tamko
“zinaa” katika ushahidi kwa sababu hilo ndilo tamko pekee linalobeba
na kumaanisha tendo haramu mbele ya sheria, kinyume na matamko mengine.
Hii ni kwa sababu ya kutumika tamko hilo katika kauli tukufu ya Allah:
“WALA MSIKARIBIE ZINAA. HAKIKA HIYO (zinaa) NI UCHAFU
(mkubwa) NA NI NJIA MBAYA (kabisa)”. [17:32]
- SHERIA
YA KUSHURUTIZWA MASHAHIDI WANNE KATIKA USHAHIDI WA ZINAA:
Tumeeleza
kwamba ili ushahidi wa kuona kosa la zinaa ukubaliwe na uzingatiwe mbele
ya sheria, hapana budi ushuhudiwe (utolewe) na watu wanne juu ya tendo
lenyewe khasa. Hili la kushurutiza mashahidi wanne limethibiti kupitia
kitabu (Qur-ani Tukufu) na sunah (hadithi za Bwana Mtume). Ama kitabu ni
kauli tukufu ya Allah: “NA WALE WANAWAKE WAFANYAO MACHAFU MIONGONI MWA
WANAWAKE WENU; BASI WASHUHUDISHIENI MASHAHIDI WANNE (waliowaona
wanafanya hivyo) MIONGONI MWENU...” [4:15]
Na katika sunah, imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye
radhi-kwamba Sa’ad Ibn Ubaadah alisema: Ewe Mtume wa Allah, unaonaje
nikimkuta mtu na mke wangu, nimpe muda mpaka nilete mashahidi wanne?
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Naam”. Imamu
Shaafiy & Maalik-Allah awarehemu.
Kwa dalili hizi, hapana budi kupatikana mashahidi wanne katika kutoa
ushahidi wa kosa la zinaa. Wakiwa chini ya wanne, sheria itawaona kuwa ni
wasingiziaji wenye lengo la kuvunja heshima ya mtu. Na hili linajulikana
kisheria kwa jina la “qadhfu” ambayo huambatana na adhabu ya
bakora. Kwa mantiki hii basi, kila mmoja wa mashahidi hawa wasiofikia
idadi ya wanne watahukumiwa kucharazwa bakora themanini. Hivi ndivyo
Amirul-Muuminina Umar Ibn Al-khatwaab-Allah amuwiye radhi-alivyowahukumu
mashahidi wasiofikia idadi itambuliwayo na sheria. Akawacharaza bakora kwa
kosa la “qadhfu”, na hukumu hii haikutokana na maoni binafsi ya
Sayyidina Umar, bali alichofanya ni kuitekeleza kivitendo kauli tukufu ya
Allah: “NA WALE WANAOWASINGIZIA WANAWAKE WATWAHARIFU (kuwa wamezini)
KISHA HAWALETI MASHAHIDI WANNE. BASI WAPIGENI MIJELEDI (bakora)
THAMANINI NA MSIWAKUBALIE USHAHIDI WAO TENA NA HAO NDIO MAFASIKI.
ISIPOKUWA WALE WENYE KUTUBU BAADA YA HAYO NA WAKATENGENEZA AMALI NZURI
(hao Allah atawasamehe kwani) BILA SHAKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na)
MWINGI WA KUREHEMU”. [24:4] Na kauli ya Allah: “MBONA HAWAKULETA
MASHAHIDI WANE? NA WALIPOKOSA KULETA MASHAHIDI, BASI HAO MBELE YA
ALLAH NI WAONGO”. [24:13]
|