Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

NJIA ZA KUTHIBITISHA JARIMA YA ZINAA KISHERIA.

Faida

01.  KUTHIBITI ZINAA KWA MUHUSIKA KUKIRI YEYE MWENYEWE.

Kabla hatujaanza kuangalia ni namna gani hatia ya zinaa inavyothibiti kutokana na mtu mwenyewe kukiri kutenda kosa hilo bila ya kulazimishwa na mtu/mamlaka yo yote. Ni vema kwanza tukalibahithi (tafiti) na kulichambua neno hili ‘kukiri’ nini maana ya kukiri katika lugha na sheria.  

A/. KUKIRI KILUGHA: Katika lugha ya Kiarabu neno “kukiri” halimaanishi ila kuthibitisha. Kwa hivyo basi muarabu anaposema: “Fulani amekiri zinaa”, anamaanisha kuwa fulani huyo amethibitisha yeye mwenyewe kuwa amezini. 

B/. KUKIRI KATIKA SHERIA: Sheria inalitafsiri neno kukiri kuwa ni mtu kueleza haki awiwazo nazo bila ya kubagua kuwa ni haki za Allah Muumba wake au ni zile za wanadamu viumbe wenzake. Kwa maana hii basi mtu anapokiri zinaa mbele ya kadhi, sheria humchukulia kuwa anatoa khabari kuwa amepasiwa na haki ya Allah kwa kwenda kinyume na maamrisho au makatazo yake. Kwa hivyo anastahiki adhabu ya kosa hilo kwa mujibu wa sheria. Kwa mantiki hii basi, itakudhihirikia kuwa kisheria kukiri ni kinyume cha kupinga/kukanusha.

 

SHARTI ZA KUSIHI IKRAARI (KUKIRI) YA MTU:

Ili kukiri kuzingatiwe na sheria, kumeshurutizwa huyo mwenye kukiri:-

  1. awe na akili timamu, asiwe mwendawazimu.
  2. awe amebaleghe, yaani awe mtu mzima na wala asiwe mwanamdogo.

Zikikamilika sharti mbili hizi ndipo hatia ya zinaa inaweza kuthibiti kisheria. Itathibiti pale tu muhusika atakapokuja mbele ya kadhi yeye mwenyewe bila ya kushurutishwa na mtu wala bila ya kutenzwa nguvu na mamlaka fulani. Akaja hali ya kuwa ana akili timamu, mtu mzima akakiri yeye mwenyewe kuzini walau mara moja tu. Haya ni kwa mujibu wa ilivyopokewa katika kisa cha “Asiyfu-kibarua/mtumishi”, kama kilivyopokelewa na Abuu Hurayrah na Zaid Ibn Khaalid-Allah awawiye radhi-wamesema: “Tulikuwa (tumekaa) mbele ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasimama mtu mmoja akasema: Ninakuomba kwa haki ya Allah uhukumu baina yetu kwa kitabu cha Allah. Khasimu (mgomvi) wake akasimama na alikuwa ni mjuzi zaidi wa sheria kuliko yeye, akasema: Hukumu kwa (kutumia) kitabu cha Allah na unipe idhini (ya kusema). Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Sema”. Akaanza kusema: Mwanangu wa kiume alikuwa kibarua kwa (bwana) huyu, akazini na mkewe (bwana huyu). Nikampa kutokana na kitendo hicho fidia ya mbuzi mia na mtumishi. Kisha nikawauliza watu wenye elimu,  nao wakanieleza ya kwamba mwanangu anapaswa kupigwa bakora mia moja na kupelekwa uhamishoni kwa kipindi cha mwaka mmoja. Na kwamba mkewe (bwana huyu) apigwe mawe mpaka kufa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:  “Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu i mkononi mwake, nitahukumu baina yenu kwa kitabu cha Allah uliotukuka utajo wake. Wale mbuzi mia moja na mtumishi virudishwe, mwanao amepasiwa bakora mia na kupelekwa uhamishoni kwa kipindi cha mwaka mmoja. Na muendee ewe kiji-Anas (Unaysi) mkewe huyu, akikiri (zinaa) basi mpopoe kwa mawe mpaka kufa”. (Unaysi) akamuendea, akakiri nae akampopoa kwa mawe mpaka akafa”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

WAJIHI WA KUITOLEA DALILI HADITHI HII:

Hadithi hii imefumbuliza kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amekuangika (amekutungika) kupopolewa kwa mawe mpaka kufa kwa utupu wa kukiri bila ya kuongeza kitu. Hivi ndivyo inavyofahamisha kauli yake Bwana Mtume: “Na muendee ewe kiji-Anas mkewe huyu, akikiri (zinaa) basi mpopoe kwa mawe mpaka kufa”.

 

KUTHIBITISHA USAHIHI WA IKRAARI YA MWENYE KUKIRI ZINAA.

Kunatakikana kwa Imamu katika hatia hii ya zinaa, kumuuliza mtu aliyekiri mbele yake kutenda kosa hilo kuhusiana na suala zima la zinaa. Amuulize:-

ü      Zinaa ni nini?

ü      Zinaa huwaje? Hufanyikaje?

ü      Kitendo cha zinaa hufanyika wapi?

Imamu hapaswi kumuuliza mtu aliyekiri zinaa swali kama: umezini lini. Kwani hili ni swali wanaloulizwa mashahidi, haulizwi mwenye kukiri. Usahihi wa ikraari ya zinaa utazingatiwa pale tu mwenye kukiri atakapotaja/atakapoeleza tendo lenyewe khasa ili kuondosha “shub-ha”. [Shub-ha hapa: ni hali ya kutokuwa na uhakika/uyakinifu wa jambo fulani]. Hana budi kufumbuliza (kueleza/kutamka wazi na bayana) kwani “kinaaya”/fumbo haitoshi katika kadhia hii. [Neno “Kinaaya” kilugha: ni kuzungumza/kutamka neno fulani ilhali unakusudia kitu kingine, yaani kuzungumza kwa lugha isiyo wazi; lugha ya fumbo].

 Haya ndiyo maongozi ya kiongozi wa uma-Rehema na Amani zimshukie-kama alivyoyasimulia Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-na kunakiliwa kwetu na Imamu Abuu Daawoud-Allah amrehemu: “Je, ulimnajisi (ulimchafua)?” Akajibu: Naam. (Mtume akaendelea) kumuuliza: “Mpaka ikaingia hiyo iliyoko kwako ndani ya ile iliyoko kwake?” Akajibu: Naam. Akamuuliza (tena): “Unajua zinaa ni nini?”, akajibu: Naam, nimemuendea kwa njia ya haramu namna ambayo mwanamume anavyomuendea mkewe kwa halali. (Mtume) akamuuliza: “Unakusudia nini kwa kauli yako hii?” Akajibu: Unitwaharishe (kutokana na uchafu huu nilioufanya). Mtume akaamrisha apopolewe kwa mawe mpaka kufa, akapopolewa”. Rejea kitabu (FAT-HUL-BAARIY) cha Ibn Hajar Al-Asqalaaniy-Allah amrehemu.

Mwenye kukiri akileta wasifu wa zinaa na kuithibitisha, kumependelewa Imamu amlakinie kuirejea (kuitengua) Ikraari yake, kwa kumwambia: Huenda ulimbusu tu, au ulimgusa tu au ulimuingilia kwa shub-ha. Maneno haya ni mithili ya maneno aliyoyasema Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kumwambia Maaiz alipokiri zinaa: “Huenda ulibusu, au ulikonyeza au  uliangalia tu”. Sahihi-Bukhaariy na sherehe yake Fat-hul-Baariy.

Mwenye kukiri baada ya kuulizwa maswali yote hayo na akajibu: Hapana. Imamu anatakiwa kuichunguza akili yake (huyo mwenye kukiri) na ili kupata ithibati kuwa hana matatizo ya akili awaulize ndugu/jamaa zake. Hivi ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alivyofanya katika kadhia ya Maaiz, pale alipowapelekea jamaa zake mjumbe akiwauliza: “Je, mnajua ubaya wo wote kwa akili yake unaokufanyeni msikubali jambo lo lote kwake?”

Haya yote ni kwa sababu ya kutokuzingatiwa kwa ikraari ya  mwendawazimu wala punguani. Kwa kuzingatia kuwa akili si kitu-dhati (chenye kuonekana), Imamu hana budi kulichunguza hilo kwa makini ili kuepusha hatia ya kumpitishia hukumu mtu asiyezingatiwa na sheria. Akishatambua kuwa hana matatizo yo yote ya akili, sasa ndipo amuulize juu ya “Ihswaani”, yaani iwapo ameoa/ameolewa au aliwahi kuoa/kuolewa. Hii ni kwa sababu ya kukhitalifiana kwa adhabu itolewayo kwa aliye ndani/aliyewahi kuwa ndani ya ndoa na ambaye hajawahi. Amueleweshe kuwa adhabu ya jarima ya zinaa kwa aliye ndani/aliyewahi kuwa ndani ya ndoa ni kupopolewa kwa mawe mpaka kufa. Na bakora mia na kupelekwa uhamishoni kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa aliye nje ya ndoa. Baada ya yote haya ndipo sasa Imamu atampitishia hukumu ya Allah inayompasa, iwapo hakutengua ikraari yake. Kama alikuwa ni mtu aliye ndoani, baada ya kufa kwa kupopolewa kwa mawe, atakoshwa, atakafiniwa (atavikwa sanda) na kuswaliwa na kisha kuzikwa katika makaburi ya waislamu. Atatendewa yote haya kwa kuzingatia kwamba yeye ni mwenye kuuliwa kwa haki, kwa msingi huu atatendewa yote watendewayo maiti wengine waislamu. Maswahaba-Allah awawiye radhi-walimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-juu ya kumkosha, kumkafini na kumswalia Maaiz, akawaambia: “Mfanyieni muwafanyiayo maiti wenu”.

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

“Mtu anapozini imani humtoka na kuwa  juu yake kama mwavuli, akijichopoa imani humrejea tena”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Abuu Daawoud, Al-Baihaqiy & Tirmidhiy-Allah awarehemu


Forum | Guestbook | Tuandikie |