Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

02. MTAZAMO WA SHERIA YA KIISLAMU NA KANUNI ZA KIBINADAMU KUELEKEA JARIMA YA ZINAA.

Faida

Mtazamo wa sheria ya kiislamu katika dhambi/kosa la zinaa unatofautiana mtofautiano wa mbingu na ardhi na ule wa kanuni za kibinadamu zilizopitishwa na mabunge ya nchi mbalimbali ulimwenguni. Sheria ya kiislamu inakizingatia kitendo cha ndoa kinachofanywa nje ya ndoa halali kuwa ni zinaa inayompasishia muhusika adhabu kisheria. Bila ya kuangalia kuwa tendo hilo limetendwa na mtu aliyemo ndani ya ndoa halali, au alipata kuwa ndani ya ndoa au hajapata kuyaonja maisha ya ndoa  aslani. Hivi ndivyo Uislamu unavyoitazama dhambi ya zinaa. Ama kwa upande wa sheria za kimataifa kwa ujumla wake, sheria zilizotungwa na wanadamu kwa ajili ya wanadamu. Huku zinaa yenye kupasisha adhabu inakomea katika tendo la ndoa linalofanywa na mwandoa nje ya ndoa yake. Huyu ataadhibiwa tu na sheria hii kwa sababu tu ya kuvunja ahadi ya uaminifu katika ndoa aliyokula kiapo cha kuilinda wakati wa kufunga ndoa. Hivyo basi, kwa mtazamo wa sheria hii tendo la ndoa linalofanywa na asiye mwanandoa halizingatiwi kuwa ni zinaa ikiwa litatendwa kwa maridhiano binafsi baina ya wenza wawili hao. Ama likiwa si kwa maridhiano litazingatiwa kuwa ni ubakaji (raping/violation), au mwanamke alikuwa chini ya umri wa miaka kumi na nane (18years). Utaona ni namna gani mapungufu ya mwanadamu mpungufu yanavyojidhihirisha katika sheria hii. Sheria moja inakataza kitendo kimoja; kile kile kwa mlango huu na kwa wakati huo huo kukiruhusu kupitia mlango mwingine. Ni wazi kuwa sheria kama hii haiwezi kutekeleza jukumu la kuizuia, kuikomesha na hatimaye kuitokomeza zinaa katika jamii, bali kinyume chake inaweza kuichochea. Isitoshe sheria hii haimuadhibu mwanandoa aliyetenda tendo la ndoa nje ya ndoa mpaka pale mwanandoa mwenza atakaposhitaki mbele ya vyombo vya sheria. Iwapo mwanandoa atatenda tendo hili kwa ridhaa ya mwenza wake kama linavyojitokeza hili katika zile nchi zinazojiita nchi za ulimwengu wa kwanza. Au akatenda katika mazingira ya uficho bila ya mwenza wake kutambua, katika hali mbili hizi hakabiliwi na adhabu yo yote kwa tendo lake hilo. Hali kadhalika ikiwa tendo hili litatendeka baina ya wawili walio nje ya ndoa; mwanamume hajaoa na mwanamke hajaolewa. Tendo hili likatendeka katika mazingira ya ridhaa isiyozingatiwa na ridhaa haizingatiwi iwapo mwanamke ana umri wa chini ya miaka kumi na nane. Hapa sheria hii pungufu haihukumu ila upande mmoja tu, adhabu inamuangukia mwanamume peke yake na kumtakasa mwenza wake huyo. Na hivi hivi ndivyo linavyohukumiwa tendo la liwati (sodomy/homosexuality); kumuingilia mwanamume au mwanamke kinyume na maumbile.

Ama tukija katika sheria ya kiislamu tunaiona ikimuhukumu mzinifu mwanandoa na asiye mwanandoa pindi ikithibiti kwa mujibu wa sheria kuwa katenda tendo hilo chafu. Sheria inamuhukumu bila ya kuangalia kuwa amezini katika mazingira ya maridhiano au nje ya mazingira hayo. Sheria itamuhukumu kwa kuzingatia kuwa anavunja mjengo, usalama na afya ya jamii. Katika sheria ya kiislamu kosa la zinaa ni kosa linaloigusa jamii nzima kwa sababu madhara yake huenea na kuigharimu jamii nzima na wala sio muhusika pekee. Ama katika sheria za kibinadamu zinaa huzingatiwa kuwa ni miongoni mwa masuala binafsi yanayogusa mafungamano na mahusiano baina ya mtu mmoja mmoja. Ni suala lisilogusa kwa namna yo yote maslahi ya jamii. Hili linadhihirika pale ambapo sheria hii haitoi adhabu kwa tendo la zinaa ila tu litakapotendwa na mwanandoa na akapelekwa na mwenza wake katika vyombo vya sheria. Kama hakumshitaki au alimshitaki kisha akamsamehe, hapo sheria haina uwezo wa kumuadhibu mzinifu huyu kwa kuzingatia kuwa hilo ni suala binafsi na wenyewe wameamua kulimaliza kwa ridhaa yao. Kadhalika ukilinganisha kosa na athari ya kosa hilo na adhabu itolewayo havilingani hata kidogo na wala adhabu hiyo haiwazuilii watu kutenda uoza huo. Kutokwenda sambamba kwa adhabu zitolewazo ukilinganisha na uzito na athari mbaya itokanayo na kosa lenyewe. Kumetoa mwanya wa kuongezeka kwa kiwango cha kutisha kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti, kiasi cha mtu mzima kutoona soni wala haya kukibaka kitoto kidogo kisichojua cho chote. Haya yote yanaonyesha ni kwa kiasi gani wanadamu wanahitaji muongozo sahihi na sheria kamili zisizo na mapungufu zitakazo wahakikishia amani, usalama na utulivu wa kweli. Na hili halitapatikana ila tu kwa kujisalimisha katika sheria za Allah Mola Mjuzi wa maslahi na manufaa ya waja wake. Tuufuate kikamilifu muongozo wa Allah ambao anatuambia: “...BASI WATAKAOFUATA MUONGOZO WANGU HUO HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA HAWATAHUZUNIKA”. [2:38]

 

03. AINISHO/MAANA YA ZINAA KILUGHA NA KISHERIA.

Neno ‘ZINAA’ katika mizani na mtazamo wa Uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha, lina maana/tafsiri mbili. Maana mojawapo ya mbili hizo inarejea katika lugha, yaani katika matumizi yasiyo ya kisheria. Na ieleweke tunaposema au kutumia neno ‘lugha’ hapa, huwa hatuilengi ila lugha ya Qur-ani Tukufu (Kiarabu). Wakati ile maana ya pili ya neno zinaa inarejea katika sheria tukufu ya Allah. Sheria aliyowaletea waja wake wote kwa tofauti ya rangi na lugha zao kupitia ulimi wa mja wake ampendaye kuliko wote; Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Hebu sasa na tuzitupie jicho na fikra maana/tafsiri hizo moja baada ya nyingine ili tuende sambamba wakati tutakapokuwa tunalitaja au kulitumia neno  ‘zinaa’.

  1. ZINAA KILUGHA:

Neno ‘zinaa’ katika lugha ya Kiarabu limetumika kwa maana kadhaa kama ifuatavyo:-

                               I.      DHIKI/KUBANWA-Maana hii tunaipata kupitia kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-wakati akiuelekeza uma wake juu ya swala tano: “Asiswali mmoja wenu na ilhali yeye ni ZANAA”.  Yaani akiwa ni mwenye dhiki au kubanwa na mkojo.

                             II.      UFINYU- Waarabu wanaposema (ZANAL-MAUDHWIU), maana: (Mahala/sehemu imezini) wanamaanisha kuwa sehemu/mahala hapo pamekuwa finyu, yaani hapatoshi, hapakidhi haja.

Hivi ndivyo ilivyoelezwa katika kamusi ya lugha inayoitwa (LISAANUL-ARAB), mtunzi: Ibn Mandhuur. Na katika kamusi (TAAJUL-ARUUSI), mtunzi: Zabiydiy.

                          III.      UOVU- Waarabu wanaposema (ZANAR-RAJULU), maana: (Mtu amezini) wanakusudia kuwa amefanya uovu.

Hivi ndivyo lilivyotafsiriwa neno ‘zinaa’ katika kamusi iitwayo (AL-BAHRUL-MUHIYTW). Hizi ni baadhi ya maana za neno ‘zinaa’ kama linavyotumiwa na Waarabu katika mazungumzo (matumizi) yao ya kawaida; yasiyo ya kisheria.

  1. ZINAA KISHERIA:

Mafaqihi wa kiislamu wameiarifisha zinaa kuwa: ni kila maingiliano ya kimwili baina ya mwanamke na mwanamume yaliyofanyika nje ya ama ndoa sahihi, shib-hu ya ndoa au miliki ya kuumeni. Hivi ndivyo mafaqihi walivyoitafsiri zinaa kama tunavyoweza kusoma katika vitabu kadhaa vya fani ya     Fiq-hi mithili ya BIDAAYATUL MUJTAHIDI WA NIHAAYATUL-MUQTASWID.

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI:

 Ø      “Hazini mzinifu wakati azinipo na ilhali yeye ni muumini.

Ø      Wala haibi mwizi wakati aibapo na ilhali ni muumini.

Ø      Na wala hanywi pombe wakati anywapo na ilhali ni muumini”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Riwaya: Abuu Daawoud & Tirmidhiy-Allah awarehemu.


Forum | Guestbook | Tuandikie |