|
I/.
UTANGULIZI:
01: ATHARI YA ZINAA KWA MTU BINAFSI NA KWA JAMII.
Inazingatiwa
jozi ya uwili, uwili utokanao na ujike na udume unaopatikana katika vitu
vyote vilivyomo katika maisha haya (existence). Jozi yenye kupatikana kwa
wanadamu, hayawani, mimea, jamadi (inanimate), katika baki ya maada
nyingine na hata katika chembe (particle/atom) za vitu vyenye mkondo hasi
na chanya. Jozi hii inazingatiwa kuwa ni ajabu (phenomenon) yenye kuvuta
akili na fikra za walimwengu kutafiti na kubahithi. Qur-ani Tukufu
inauvuta mtazamo na akili ya mwanadamu kuielekea ajabu hii kupitia kauli
tukufu ya Allah: “NA KATIKA KILA KITU TUMEUMBA DUME NA JIKE
ILI MPATE KUFAHAMU”. [51:49] Akasema tena: “AMETUKUKA ALLAH
ALIYEUMBA DUME NA JIKE KATIKA (vitu) VYOTE;KATIKA VILE
IVIOTESHAVYO ARDHI (mimea) NA KATIKA NAFSI ZAO (wanadamu) NA KATIKA VILE
WASIVYOVIJUA”. [36:36]
Allah
Mola Muumba ameumba jozi ya udume na ujike katika kila jinsi na aina ya
viumbe vyake. Eneo na dhima ya jozi hiyo hufanya kazi katika ulimwengu
wake makhsusi kwa kulingana na nidhamu (utaratibu) thabiti; isiyo ya
kubahatisha. Katika eneo la wanadamu tunaiona jozi hii baina ya mwanamume
na mwanamke ni chombo/njia ya kuzaana, kuongezeka na kujiimarisha sawasawa
(to balance) katika siha ya mwili na nafsi. Na kwa kupitia ujozi huu ndio
kizazi cha wanadamu huendelea kubakia katika maisha ya sayari hii ya
dunia.
Isitoshe,
mafungamano ya kimaumbile baina ya mwanamume na mwanamke kama
tuyashuhudiavyo katika uhalisia wa maisha. Mafungamano haya ni alama
dhahiri juu ya asili moja inayo wachanganya pamoja mwanamume na mwanamke
tangu mwanzo wa kuwepo kwao. Katika asili yao Allah amewaumba wawili hawa
kutokana na nafsi moja kama tusomavyo: “ENYI WATU! MCHENI MOLA WENU
AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI (asili) MOJA. NA AKAMUUMBA MKEWE
KATIKA NAFSI IE ILE. NA AKAENEZA WANAUME WENGI NA WANAWAKE KUTOKA KATIKA
WAWILI HAO...”. [4:1]
Kwa
kuuzingatia ukweli huu ulio dhahiri kwa kila mmoja wetu, tunalazimika
kukubali kwamba kila mmoja wa wanajozi hawa; mwanamume na mwanamke ni
sehemu isiyotengeka ya mwenzake. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa
kila mmoja wao ni mpungufu anayekamilishwa na mwenziwe pindi waunganapo
kama jozi moja kamili. Wawili hawa kwa pamoja ndio huunda umbile moja
kamili la mwanadamu. Umbile ambalo halipatikani ila kwa wawili hawa
kuungana na kuchanganyika pamoja katika maisha ambayo yatawaunganisha na
kuwa nafsi moja. Na hili la kuwa nafsi na mwili mmoja halipatikani ila kwa
njia na msaada wa ndoa na si vinginevyo. Ni kwa sababu hii ndio mfumo wa
ndoa katika Uislamu ukawa ni mfumo wa kukamilishana
(integration/complementarity) baina ya mwanamume na mwanamke.
Kukamilishana huku katika uhalisia wake ni makutano binafsi
yanayoubadilisha uhusiano baina ya wanandoa kuwa utulivu wa nafsi
(tranquility), mapenzi na huruma (mercy). Hivi ndivyo inavyotubainishia
kauli hii tukufu ya Allah: “NA KATIKA ISHARA ZAKE (za kuonyesha
ihsani zake juu yenu) NI KUWA AMEKUUMBIENI WAKE ZENU KATIKA JINSI YENU ILI
MUPATE UTULIVU KWAO, NAYE AMEJAALIA MAPENZI NA HURUMA
BAINA YENU. BILA SHAKA KATIKA HAYA ZIMO ISHARA KWA WATU WANAOFIKIRI”.
[30:21]
Hii
ndio siri na falsafa ya kuumbwa mwanamume na mwanamke kutokana na asili
moja. Ndoa ndio mfumo bora unaobeba dhamana ya utwaharifu wa tone la manii
(sperm) na ule wa tumbo la uzazi (womb). Ndoa huchukua dhima ya
kuhakikisha kuwa manii yametoka ndipo kuingia ndipo, yaani yametoka
kihalali kuingia mahala pa halali (mke). Ni katika hali na mazingira haya
ya ndoa ndio hudhibitika na kuthibitika ukweli wa
nasabu ya mwanadamu tofauti na ile ya hayawani wengine. Ni chini ya mfumo
huu ndio mzazi huwa hana shaka kuwa mzaliwa ni mwanawe atokanaye na damu
yake. Na kwa janibu ya mwana pia huwa hana shaka juu ya mzazi wake. Nje ya
mfumo huu, mafungamano ya kijinsia baina ya mwanamume na mwanamke kwa njia
ya zinaa hupelekea upotevu na kukatika kwa mlolongo wa nasabu ya
mwanadamu. Katika hali na mazingira haya machafu yanayokhalifiana na
maumbile seuze sheria tukufu. Hakuna baba wa kweli (mume) anayemjua mwana
wa uti wa mgongo wake, wala mwanamke anayemjua mwana wa kifua (mbavu)
chake aliyembeba katika tumbo lake la uzazi (bowels). Wala mtoto hamjui
baba yake aliyemzaa. Kwa sababu hii, bashariya (jamii ya wanadamu wote)
inaporomoka hadi kufikia kiwango cha wanyama katika kuzaliana kwao. Ni kwa
kuyaangalia madhara na udhalili huu ndipo ndoa katika Uislamu ikawa ndio
njia sahihi ya kuigwa na kufuatwa ambayo huwakutanisha pamoja mwanamke na
mwamume. Na ndio njia ya kimaumbile ya kuzaliana inayotakiwa kuyatawala
maisha ya mwanadamu kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda hadhi, utukufu
na heshima ya mwanadamu kama mtu binafsi na kama jamii. Allah Mola
Mtukufu anatuambia: “NA HAKIKA TUMEWATUKUZA WANADAMU...”
[17:70] Sasa ikiwa Allah Mola
aliyetuumba ametutukuza sisi waja wake na akatuwekea utaratibu wa ndoa ili
kuuchunga na kuuendeleza utukufu wetu huu. Kwa nini basi sisi
tuliofadhiliwa na kupendelewa kwa kupewa hiba ya utukufu huu tunaukataa?!
Na badala yake tunautwaa uduni na utwefu kwa kufuata njia chafu na mbaya
ya zinaa inayotuweka na kutulinganisha sawa na wanyama ambao hawakupewa
utukufu mithili ya tuliopewa sisi?!
Tukiwa
wakweli na tukizipa uhuru fikra
na mawazo yetu, tutakongamana na kuwafikiana kwamba zinaa ni chimbuko la
fisadi kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Zinaa ina athari mbaya
zinazomrudia muhusika mwenyewe katika maisha yake na jamii ambazo
zinaihalalisha na kuitungia mifumo maalumu. Chini ya mwavuli wa mifumo hii
michafu inayonuka, mtu anakuwa hana kinga dhidi ya zinaa kwa nafsi,
familia na mke wake. Ukiachilia mbali kwamba zinaa ni mashine yenye jukumu
la kuifisidi siha (afya) ya muendekezaji wa tendo hili lisilo la kiutu.
Zinaa pia ni kiwanda chenye dhima ya kuzalisha na kusambaza maradhi ya
kuambukiza yatokanayo na uoza huu. Maradhi ambayo kwa namna moja au
nyingine huharibu kizazi na asili ya kizazi. Ukimwi ni katika jumla ya
mazao makuu yanayozalishwa na kiwanda hiki zinaa, huu ni ukweli usiokubali
kupingwa wala kukanushwa. Kutokana na kuizingatia fisadi na madhara haya
makubwa, ndipo Uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha ukaikamia
na kuikemea vikali kabisa zinaa. Ukaifanya zinaa kuwa ni miongoni
mwa madhambi makubwa nyuma ya dhambi za kumshirikisha Allah na kumuua mtu.
Kama ulivyofanya kujilinda na kujihifadhi na zinaa kuwa ni miongoni mwa
sifa za waumini waliofaulu na kufuzu, kama tusomavyo: “HAKIKA WAMEFUZU
WAUMINI. AMBAO KATIKA SWALA ZAO HUWA NI WANYENYEKEVU. NA AMBAO HUJIEPUSHA
NA MAMBO YA UPUUZI. NA AMBAO (nguzo ya) ZAKA WANAITEKELEZA. NA AMBAO
TUPU ZAO WANAZILINDA. ISIPOKUWA KWA WAKE ZAO AU KWA (wanawake) WALE
ILIYOWAMILIKI MIKONO YAO YA KUUME (kulia). BASI HAO NDIO WASIOLAUMIWA.
(Lakini) ANAYETAKA KINYUME CHA HAYA, BASI HAO NDIO WARUKAO MIPAKA (ya
Allah)”. [23:1-7]
Na
kwa mantiki hii hii, Uislamu ukamuweka mtu mwenye kuiacha na kujiepusha na
zinaa kuwa ni miongoni mwa aina saba za watu. Watu watakaofunikwa na
kivuli cha arshi ya Allah katika siku nzito ambayo hakutakuwepo na kivuli
kingine ila hicho tu. Haya ni kwa mujibu wa ilivyopokelewa katika hadihti
ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Makundi saba ya watu,
Allah atayapumzisha chini ya jivuli la Arshi yake katika siku ambayo
hakitakuwepo kivuli cho chote ila kivuli chake (hiyo
arshi)...(akamjumuisha miongoni mwao)....na mwanamume aliyeitwa
(katika machafu) na mwanamke mwenye hadhi na uzuri, akasema hakika
mimi ninamkhofu Allah....” Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.
Kwa
kuuangalia ubaya na khatari ya zinaa, Allah Mtukufu akaiharamisha zinaa
kupitia kitabu chake kitukufu na suna ya Mtume wake Mtukufu, akasema: “WALA
MSIIKARIBIE ZINAA. HAKIKA HIYO (zinaa) NI UCHAFU (mkubwa) NA NI
NJIA MBAYA (kabisa)”. [17:32] Allah akaifanya zinaa kuwa ni
miongoni mwa madhambi makubwa, ikizifuatia nyuma dhambi za kumshirikisha
Allah na kuiua nafsi ambayo Allah ameharamisha kuuawa ila kwa haki.
Falsafa na hekima ya kufanywa madhambi haya kuwa ni makubwa ni kwa sababu
kumshirikisha Allah hufisidi dini. Wakati ambapo kuiua nafsi hufisidi
kiwiliwili na kuiachia zinaa kufisidi nasabu za jamii ya wanadamu. Hili
ndilo lililompelekea Imamu Ahmad Ibn Hambal-Allah amuwiye radhi-kusema:
“Siijui baada ya dhambi ya kuua dhambi iliyo kubwa zaidi kuliko
zinaa”. Akaijengea hoja kauli yake hii kwa hadithi ya Abdillah Ibn
Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: Nikasema: Ewe Mtume wa Allah ni dhambi
ipi iliyo kubwa kuliko zote? Akajibu: Ni kumfanya Allah kuwa ana mshirika
(shirki) na ilhali yeye ndiye aliyekuumba”. Akasema: Nikamuuliza (tena):
Kisha ipi? Akajibu: “Ni kumuua mtoto wako kwa kuchelea asije kula pamoja
nawe (njaa)”. Akasema: Nikaendelea kumuuliza: Kisha (inafuatia dhambi)
ipi? Akajibu: Ni kuzini na mke wa jirani yako”. Bukhaariy,
Muslim & Nasaai-Allah awarehemu. Katika kuisadikisha kauli ya Mtume
wake ndipo Allah Mtukufu akaiteremsha kauli yake: “NA WALE
WASIOMUOMBA MUNGU PAMOJA NA ALLAH (shirki), WALA HAWAIUWI NAFSI
ALIYOIHARIMISHA ALLAH ISIPOKUWA KWA HAKI, WALA HAWAZINI. NA
ATAKAYEFANYA HAYO ATAPATA MADHARA (papa hapa ulimwenguni
kabla ya akhera). NA ATAZIDISHIWA ADHABU SIKU YA KIYAMA NA ATAKAA
HUMO KWA KUFEDHEHEKA (muda mrefu kabisa) MILELE. ILA YULE ALIYETUBIA NA
KUAMINI NA KUFANYA VITENDO VIZURI, BASI HAO NDIO ALLAH ATAWABADILISHIA
MAOVU YAO KUWA MEMA. NA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA
KUREHEMU”. [25:68-70]
Uislamu
umeiharamisha zinaa kwa sababu ya madhara adida (mengi) yanayotokana nayo
na ukaweka adhabu kali kwa kila mwenye kujitumbukiza katika uchafu na njia
mbaya hii. Falsafa na hekima ya adhabu kali hii ni kumlinda mtu binafsi na
jamii kwa ujumla dhidi ya madhara na taathira mbaya ya zinaa. Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akatutahadharisha dhidi ya kuacha
kuzitekeleza adhabu hizi kwa
kumuonea huruma muhusika,akatuambia: “Itakayemzuilia huruma yake
kuitekeleza adhabu miongoni mwa adhabu za (makosa zilizowekwa na) Allah. Bila
ya shaka huyo atakuwa amempinga Allah katika amri yake”.
Ahmad-Allah amrehemu.
|