|
Mpenzi
msomaji wetu-Allah akuwafikishe kupenda kujifunza.
Assalaam
Alaykum Warahamatullah! Ama baad, kutokana na ukweli kwamba ulimwengu hivi
sasa umegubikwa na magonjwa mengi ya hatari
yenye kuambukiza. Magonjwa ambayo historia haituonyeshi kuwepo
kwake ulimwenguni katika dunia ile ya wahenga wetu. Magonjwa mithili ya
ukimwi, ebola na mengineyo ambayo wataalamu wa sayansi ya tiba wanakiri
bayana kuwa chanzo chake kikuu cha kuambukiza kutoka mtu mmoja hadi
mwingine ni zinaa. Magonjwa haya ni ushahidi dhahiri wa jinsi ambavyo
wanadamu wa leo hawataki kuishi kulingana na mfumo wa maisha waliofumiwa
na Allah Mola Muumba wao aliye Mjuzi wa lipi limfaalo mwanadamu na lipi
lisilomfaa. Watu wameuvua utu wao na kuuvaa unyama pale walipoacha njia
halali na nzuri ya kukidhi haja zao za kimwili na kuzaliana ndani ya ndoa.
Wakaamua kufanya zinaa na hata kuthubutu ulawiti na usagaji. Matokeo yake
leo serikali mbalimbali duniani badala ya kutenga mabilioni ya pesa katika
nyanja za ustawi wa jamii, mapesa hayo yamekuwa yakipotea bure katika
jitihada za kujaribu kuupiga vita ukimwi na maradhi mengine yasababishwayo
kwa asilimia tisini na tisa kama sio mia na zinaa.
Ni
dhahiri isiyo na kificho wala kukubali kupingwa kwamba vita hii ambayo
tunajasiri kuiita kuwa ni ‘vita pofu’ dhidi ya janga hili hatari la
ukimwi iliyotangazwa na dunia nzima, kamwe haitafanikiwa. Bali janga
na dudu baya hili litaumaliza ulimwengu mzima hata kama bajeti zote
za serikali zote duniani zitatumiwa katika kampeni za kuutokomeza ukimwi.
Kwa nini tunajasiri kusema hivi na sio kusema tu bali kusema kwa kinywa
kipana kabisa. Naam, tunasema hivi kwa sababu ulimwengu hautaki kukiri
kuwa adui tunayepambana nae bila ya mafanikio ni matokeo ya matendo yetu
machafu. Ni natija ya matendo yetu yasiyo na utu, ni zao litokanalo na
kuutupilia mbali mfumo sahihi wa maisha tuliofumiwa na Allah na badala
yake tukajiundia mifumo yetu wenyewe. Hili ni tendo lililopindukia ukomo
wa ubaya na uovu, kwani japokuwa hatutamki kwa ndimi zetu, matendo yetu
haya yanamwambia Allah Muumba wa vyote na yote. Yanamwambia aliyetupa uhai
huu kuwa hajui na wala hafai kutupangia sheria za kutuongoza katika maisha
haya ambayo kila mmoja wetu anakiri kuwa ni mali na milki yake. Ni sawa na
kumwambia kuwa sheria zake zimepitwa na wakati na ilhali hata huo wakati
wenyewe umeembwa nae, kwa maana hiyo hazifai na wala hazihitajiki katika
zama zetu hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Zama za uhuru usio
na mipaka; zama za mtu kuishi kwa mujibu wa matashi na matamanio yake.
Ndugu
zanguni, tukiri na tukubali ili tusalimike sisi wenyewe na tuusalimishe
ulimwengu. Dawa pekee, kinga na tiba sahihi ya maradhi hatari ya ukimwi ni
kuacha zinaa na wala sio kutumia kondom. Ni kuunyenyekea na kuufuata mfumo
sahihi wa maisha tuliochaguliwa na Allah Mola Mtukufu. Ni kwa kufanya hivi
tu ndipo tunapoweza kuokoka na kunusurika na gonjwa hili hatari. Kinyume
na hivi ni kucheza na kujidanganya sisi wenyewe, tutatenga mabilioni ya
mapesa, tutafundisha elimu ya ngono mashuleni. Tutasambaza vijarida,
vipeperushi na matangazo yaelimishayo kuhusu ukimwi, tutakuwa na mpenzi
mmoja, tutavaa kondom na....na.... Lakini bado ukimwi utaendelea
kutuangamiza mithili ya moto uziangamizavyo nyasi kavu nyikani. Turejee
ndugu zanguni kwa Allah, tujisalimisheni katika hukumu na sheria za
Allah, tuishi maisha tuliyopangiwa na Allah aliyetupa bure maisha
haya. Kufanya hivi ndio kusalimika na kuokoka
dhidi ya janga angamizi la ukimwi na majanga mengineyo, tukubali au
tukatae huu ndio ukweli.
Ndugu
msomaji wetu, bila ya chembe ya shaka zinaa ni katika jumla ya madhambi
makubwa. Zinaa ni sababu, chemchem na chanzo cha aina mbalimbali za shari,
uovu na fisadi kubwa katika jamii ya wanadamu. Zinaa husababisha
kudhoofika kwa kizazi, upotevu wa nasabu za wanadamu
na kubomoka kwa familia. Ni kwa ajili ya sababu hizi na nyinginezo,
ndio tunauona Uislamu ukiiharamisha zinaa na kuizuia kwa njia za malezi ya
kiroho na ndoa. Ili kuhakikisha kuwa tendo hili chafu la zinaa haliichafui
na kuifisidi jamii, Uislamu ukaweka adhabu itakayomzuia mzinifu kufanya
tendo hilo baya. Kwa kuweka sheria hizi, Uislamu ukawa umemuhifadhi mtu
binafsi na jamii nzima kutokana na athari mbaya zitokanazo na uchafu huu
wa zinaa. Wakati ambapo Uislamu unayafanya yote haya, kanuni zilizowekwa
na kutungwa na binadamu viumbe dhaifu na wapungufu wa kila hali. Sheria
binadamu hizi zinampa mtu uhuru wa kufanya zinaa katika hali ya maridhiano
na makubaliano baina ya wahusika wa tendo hili. Sote ni mashahidi juu ya
fisadi na uharibifu unaotokana na uhuru huu wa maridhiano machafu
aliyopewa mwanadamu na mwanadamu mwenziwe. Hii yote inaonyesha udhaifu wa
mwanadamu na haja yake ya kuwa na muongozo sahihi wa kumuongoza katika
maisha yake. Muongozo huu hauwezi kutoka kwa mwanadamu aliye sheheni
mapungufu kama yeye, bali ni kwa Muumba wa walimwengu na ulimwengu.
Kwa
kuyazingatia yote haya, Website yako {WEBSITE UISLAMU-MTUMISHI WA UMMA},
inaona fakhri kukutumikia kwa kukuletea mfululizo wa makala zitakazokuwa
chini ya anuani: ADHABU YA ZINAA KATIKA SHERIA YA KIISLAMU kupitia jukwaa
lako hili la NASAHA ZA WIKI. Lengo mama la makala hizi ni kutaka
kukumbusha juu ya maafa ya zinaa na namna ambavyo Uislamu unavyoihifadhi
jamii dhidi ya janga hili. Ni matumaini ya WEBSITE UISLAMU kuwa utanufaika
na makala hizi na zitakusaidia kuliepuka janga hili la ukimwi. Karibu
unufaike kwa msaada na fadhila zake Allah kuanzia wiki kesho.
Wassalaam
Alaykum Warahamatullah!
Daima
ni Website yako; Website Uislamu-Mtumishi wa umma.
|