|
Miongoni
mwa maafa yenye kuogopewa (makubwa) na pingamizi hasi ni kuitupia lawama
dahari na manun’guniko dawama juu ya dhulma ya dahari na ugumu wa siku.
Kiasi cha mtu kufikia kuisawirisha dahari kuwa ni khasimu anayemdhulumu na
kumtesa, au ni adui anayemngojelea misiba. Au ni mtawala dhalimu
anayemuonea mtu asiye na hatia, huku akimkumbatia mtu muovu. Hizi zote ni
nadhari (mitazamo) shurutizi ambazo ama mtu mmoja mmoja au makundi ya watu
hujaribu kuzitoa nafsi zao hatiani kupitia nadharia hizo. Wakakimbia
kubeba mzigo wa matendo/makosa yao na badala yake kujaribu kuwabebesha
wengine au kuibebesha dahari, kadari, bahati mbaya, sadfa na kadhalika.
Wajibu
wao ulikuwa ni kujaribu kuchunguza kwa nini wamefikwa na nakama (adhabu)
na wameondokewa na neema. Kisha watafute ufumbuzi na suluhisho la kina
linaloviunganisha pamoja visababishi
na sababu. Linalojumuisha pamoja natija (matokeo) na vyanzo
(chimbuko) kulingana na suna (taratibu/kawaida/kanuni) ya Allah Mola
Muumba kwa viumbe vyake. Kwani kwa yakini dahari ni chombo tu kinachobeba
matukio yanayoendeshwa na kupitishwa na Allah Muumba dahari, matukio na
watukiwa (viumbe). Huyapitisha matukio hayo kwa mujibu wa sheria na
utaratibu wake aliojipangia Yeye mwenyewe. Hii ndio maana muradi ya
hadithi hii sahihi: “Msiitukane dahari, kwani kwa yakini Allah ndiye
DAHARI”. Muslim-Allah amrehemu
Mapendeleo
na makusudio ya kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“...Allah ndiye DAHARI”, ni kuwa Yeye Allah ndiye muweka
kawaida/kanuni za maumbile na ndiye mpitishaji na muemdeshaji wake.
Tujifunze
kutoka na historia na matukio
ya kweli yaliyowafika wenzetu waliotutangulia katika imani. Waislamu
waliposhindwa katika vita vya Uhud wakiwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-na maswahaba sabini wakafa shahidi. Walikaa chini
wakajiuliza sababu ya donda na balaa lililowasibu baada ya ushindi. Jawabu
ya Qur-ani ikawa: “NYINYI ULIPOKUFIKENI MSIBA AMBAO NYINYI
MMEKWISHAWATIA (maadui) MARA MBILI YA HUO, MNASEMA: UMETOKA WAPI HUU?
SEMA: HUO UMETOKA KWENU WENYEWE. HAKIKA ALLAH NI MWENYE UWEZA JUU
YA KLA KITU”. [3:165] Qur-ani Tukufu inaikariri kanuni/kawaida hii jumla
pale inaposema: “HAYO (ya kuwafika balaa hizi) NI KWA SABAU ALLAH
HABADILISHI KABISA NEEMA ALIZOWANEEMESHA WATU, HATA (mpaka) WABADILISHE
WAO YALIYOMO NYOYONI MWAO (wende nyendo mbaya ndipo Allah awaondoshee
neema yao)...”. [8:53]
Kutokana
na ukweli huu ulio wazi kabisa ni vema wanadamu wakazirushia lawama nafsi
zao huku wakijaribu kusawazisha kombokombo (makosa) zao na kutengeneza
palipofisidika badala ya kuilaumu dahari na kuzikosoa zama. Ni wajibu wa
muumini anaposhukiwa na jambo baya (maafa) kuirejea nafsi yake na
kuangalia sababu ya hayo yaliyomsibu kutokana na ukweli kwamba: “NA
MISIBA INAYOKUPATENI NI KUTOKANA NA VITENDO VYA MIKONO YENU...”
[42:30] Na aseme kama alivyosema nabii Musa; mneni wa Allah-Amani
imshukie-wakati aliporejea kwa kaumu yake akitoka kuzungumza na Mola wake.
Akawakuta watu wake wamekwishapotea, wamejifanyia kigombe kilichokuwa na
sauti (hakina roho) kuwa ndio Mungu wao wakikiabudu. Wakazitupa nyuma ya
migongo yao nasaha za nabii Haarun-Amani imshukie-wakamdharau wasisikilize
maneno yake na hata wakakaribia kumuua. Hapo ndipo nabii Musa akamuelekea
Mola wake kwa unyenyekevu akimuomba: “...MOLA WANGU! NISAMEHE MIMI NA
NDUGU YANGU NA UTUINGIZE KATIKA REHEMA YAKO, MAANA WEWE NDIYE MWENYE
KUREHEMU ZAIDI KULIKO WENYE KUREHEMU (wote)”. [7:151] Na aseme kama
walivyosema watakatifu wa Allah wakati wenzao walipokufa mashahidi:
“...WALA HAWAKUDHOOFIKA WALA HAWAKUDHALILIKA. NA ALLAH ANAWAPENDA
WAFANYAO SUBIRA. WALA HAIKUWA KAULI YAO (watakatifu hao) ILA NI KUSEMA:
MOLA WETU! TUGHUFIRIE MADHAMBI YETU NA KUPITA KWETU KIASI KATIKA MAMBO
YETU NA ITHIBITISHE MIGUU YETU NA UTUSAIDIE JUU YA WATU MAKAFIRI. ALLAH
AKAWAPA MALIPO MAZURI YA DUNIANI NA MALIPO MAZURI YA AKHERA. NA ALLAH
ANAWAPENDA WAFANYAO MEMA”. [3:146-148]
Mpenzi
msomaji wetu, Allah akunufaishe na mfululizo wa makala hizi zilizokuwa
chini ya anuani: WAKATI KATIKA MAISHA YA MUISLAMU. Makala zilizokuwa
zikikujia kupitia jukwaa lako la (NASAHA ZA WIKI). Tunapenda bali
tunalazimika kumshukuru Allah kwa ukamilifu na tunamuomba maghfira kwa
mapungufu yaliyojitokeza katika makala hizi. Mpaka hapa makala hizi
zitakuwa zimetamatia huku tukitaraji kuwa zitakuwa zimekuelimisha na
kukunufaisha kwa namna moja au nyingine. Tunakutakia usomaji mwema na
endelea kunufaika na kufaidika na chakula cha roho kinachotayarishwa na
kupikwa na mtumishi wa uma (WEBSITE UISLAMU), kwani ipo na itaendelea
kuwepo inshallah kwa ajili yako. Tukutane juma lijalo inshaallah.
|