|
Ndugu
waislamu,
Assalaam Alaykum!
Tumo
na tunaishi ndani ya mwezi wa Rabiul–Awwal au Mfungo sita kama
tulivyozoea kuuita. Ni katika siku ya Jumatatu ya usiku wa mwezi kumi na mbili wa
mwezi kama huu wa mwaka 570 A.D. alizaliwa Bwana wa viumbe wote, kipenzi
cha Allah Mtume Muhammad–Rehema na Amani zimshukie. Katika kutukuza mazazi ya Bwana huyu mtukufu, waislamu
wakajiwekea utaratibu usiovunja cho
chote katika misingi ya dini yao; utaratibu wa kusoma MAULID kila
unapofika mwezi huu. Maulid hizi ni sherehe za miaka mingi ambazo
hujirudia kila mwaka. Ni
sherehe za kukumbuka na kuyaenzi mazazi matukufu ya Bwana huyu Mtukufu.
Tunasema kama walivyosema wanazuoni wakubwa wa kutegemewa kwamba si vibaya
kusherehekea mazazi ya Bwana Mtume kwa kusoma maulidi lakini tunasema:
ü
Je, ni wangapi miongoni mwetu tunajua maulidi ni nini?
ü
Je, ni nini natija na athari ya maulidi katika maisha yetu ya kila
siku sisi kama waislamu?
ü
Je, tunajifunza nini kutokana na hizi sherehe za maulidi za kila
mwaka?
Haya
ni maswali ambayo kila mmoja wetu ni lazima ajiulize na ayapatie majibu
yake. Ni kwa kufanya hivi ndipo tutakuwa tumeyasherehekea maulidi haki ya
kuyasherehekea na ndipo lengo la maulidi litakuwa limetimia.
Ni wazi kuwa watu husoma maulidi ili kuonyesha hisia zao katika
kumpenda Mtume wao. Hivi ndivyo anavyoweza kukuambia kila msoma maulidi. Kwa hiyo utaona msingi wa maulidi ni kumpenda Bwana Mtume
na kumpenda Mtume ni dini. Ni jambo aliloliamrisha Allah na Mtume
wake, kwani imani ya mja haikamiliki ila kwa kumpenda Mtume.
Sasa
basi, kutokana na mnasaba huu wa kuingia mwezi huu wa Rabiul-Awwal (Mfungo
sita) ambamo waislamu huadhimisha maulidi ya Mtume wao, Website yako;
WEBSITE UISLAMU inaungana na waislamu wote katika kusherehekea maulidi kwa
kukuletea makala maalumu. Website yako inataraji utafaidika na makala haya
na yatakusaidia kujua namna ya kusheherekea maulidi matukufu ya Mtukufu
Mtume wako. Karibu uwe pamoja nasi katika makala:
TUMPENDEJE
BWANA MTUME?
Miongoni mwa “Qurubaati” (mambo ambayo mja huyafanya ili
kujiweka karibu zaidi na Mola wake) ni kumpenda Mtume wake– Rehema na
Amani zimshukie. Hili ni
jambo lisiloweza kunpigwa wala kukanushwa na ye yote miongoni mwa
waislamu. Na suala hili la
kumpenda Mtume huambatana na alama kadhaa ambazo husadikisha ukweli wa
madai ya wanaodai kumpenda Mtume wa Allah.
Miongoni mwa alama zinazoweza kuwa ni kigezo na kielelezo cha
kumpenda Mtume ni pamoja na:
- Kigezo
Chema:
Katika
jumla ya alama kubwa zinazoonyesha mahaba ya mtu kwa Mtume wake ni
kumfanya Bwana Mtume kuwa ndio kigezo pekee chake chema.
Na kumfanya Bwana Mtume kuwa ni kigezo, maana yake ni kumfuata
katika yote aliyokuja nayo kutoka kwa Mola wake Mtukufu, miongoni mwa
maamrisho na makatazo. Ni
kuushika mwendo wake na kuongozeka na muongozo wake.
Hivi ndivyo anavyotuambia Allah Mola Mwenyezi ndani ya kitabu chake
kitukufu alichomteremshia Mtume wake: “SEMA IKIWA NYINYI MNAMPENDA
ALLAH, BASI NIFUATENI (hapo) ALLAH ATAKUPENDENI NA ATAKUGHUFIRIENI
MADHAMBI YENU NA ALLAH NI MWENYE MAGHUFIRA (na) MWENYE REHEMA (3:31)
Hapa
Allah anafanya kumfuata Mtume wake kuwa ni alama ya mahaba ya mja kwa Mola
wake. Kwa kumfuata Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–hupatikana
mahaba mawili kwa pamoja. Mahaba ya mja kumpenda Mola wake na mahaba ya
Mola kumpenda mja wake, kwani suala si kumpenda Allah tu bali hali ilivyo
ni Allah kukupenda wewe. Allah
anatuambia juu ya hili: “...ATAWAPENDA NAO WATAMPENDA…”
(5:54). Lau Allah hakuwapenda
waja wake, waja wasingeliweza kumpenda yeye na wala Allah hampendi mja
mpaka amfuate Mtume wake kwa dhahiri na siri. Akamsadikisha kwa yale yote
aliyoyaeleza, akamtii katika maamrisho na makatazo na akampenda zaidi
kuliko kiumbe cho chote kiwacho. Hivi ndivyo anavyotuambia Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie: “Haikamiliki imani ya mmoja wenu mpaka (mimi Mtume) niwe
kipenzi zaidi kwake kuliko mzazi wake, mwanawe na watu wote”. Ahmad,
Bukhaariy, Muslim, Nasaai Ibn & Maajah.
Akasema
tena katika kauli nyingine: “Mambo
matatu yatakayokuwa kwake, atapata (mtu huyo) utamu wa imani:
- Allah
na Mtume wake kuwa ni vipenzi mno kwake kuliko wasio wawili hao, na
- Kumpenda
mtu kwa ajili ya Allah tu, na
- Kuchukia
kurudi ukafirini baada ya kuokolewa na Allah kutoka huko, kama
achukiavyo kutupwa motoni”.
Ahmad, Bukhaariy, Muslim, Tirmidhiy, Nasaai & Ibn Maajah.
Mja
atapoonja utamu wa imani na kupata ladha yake, matunda ya imani hiyo
yatadhihiri kupitia viungo na ulimi wake. Hapo ndipo ulimi wake utaiona
tamu dhikri ya Allah kuliko tamu ya vitamu vyote ilivyopata kuvionja na
viungo navyo vitaharakia katika twaa ya Allah. Hapo ndipo penzi la imani
litaugubika moyo kama maji baridi yakiingiavyo kiu katika siku yenye joto
kali kwa mtu mwenye kiu kikali kabisa. Taabu ya twaa humuondokea kwa
kuionea kwake tamu, kwa hivyo basi twaa hubakia kuwa ndio chakula cha moyo
wake. Na huwa ndio furaha ya kifua chake, burudani ya macho yake na neema
ya roho yake. Huiona ladha
mno kuliko ladha za kiwiliwili kiasi cha kutoona taklifu wala kuhisi taabu
katika suala zima la ibada. Na wala hakuna awezaye kupinga kwamba hakuna
daraja tukufu na bora zaidi kuliko daraja ya kumfuata kipenzi Bwana
Mtume–Rehema na Amani zimshukie. Kumfuata katika maamrisho na makatazo
yake, matendo na tabia zake bali mwenendo wake mzima. Wala kamwe
haitomuangazia ye yote nuru ya imani ila kwa kufuata sunah ya Mtume na
kujiepusha na bidaa. Imepokelewa kutoka kwa Anas–Allah amuwiye
radhi–akipokea kutoka kwa Mtume–Rehema na Amani zimshukie-kwamba yeye
Mtume amesema: “...Na atakayeuhisha sunah (mwendo) yangu, kwa yakini
huyo amenipenda”. Tirmidhiy
- Kumfanya
Bwana Mtume kuwa ndio Hakimu:
Hii
pia ni alama ya mahaba ya mtu kwa Mtume wa Allah–Rehema na
Amani
zimshukie. Mwenye kudai kumpenda Bwana Mtume aridhie sheria ya Allah
aliyoiteremsha kupitia ulimi wa Mtume wake iyatawale maisha yake yote.
Bila ya kuwepo mwanya hata mdogo ambamo sheria hiyo ya Allah itakuwa haina
nafasi, airidhie sheria hii kiasi cha kutoona uzito ndani ya nafsi yake
kutokana na hukumu za Allah na Mtume wake.
Hivi ndivyo Allah Bwana Mlezi wetu anavyotuambia: “NAAPA KWA
(haki ya) MOLA WAKO WAO HAWAWI WENYE KUAMINI (kweli kweli) MPAKA
WAKUFANYE (wewe ndiye) HAKIMU (mwamuzi) KATIKA YALE WANAYOKHITALIFIANA,
KISHA WASIONE UZITO NYOYONI MWAO JUU YA HUKUMU ULIYOTOA NA WANYENYEKEE
KABISA”. (4:65)
Hapa
Allah anaikanusha imani kwa mtu atakayeona uzito ndani ya nafsi yake
kutokana na hukumu iliyotolewa na Mtume na akaacha kuinyenyekea na
kusalimu amri kwayo. Kwa hivyo utaona imani ya kweli haipatikani ila kwa
yule atakayemfanya Allah na Mtume wake kuwa ndio mahakimu wake. Hukumu zao
zitawale nafsi na mali yake, kauli na matendo yake, kufuata na kuacha
kwake, kupenda na kuchukia kwake bali maisha yake yote. Kisiwepo kipengele
au nyanja yo yote ya maisha yake isiyotawaliwa na kuongozwa na hukumu
(sheria) za Allah na Mtume wake. Kisha Allah hakutosheka tu na kuikanusha
imani ya asiyemfanya Bwana Mtume kuwa ndio Hakimu wake, bali akaliapia
hilo kwa kauli yake: “NAAPA KWA (haki ya) MOLA WAKO. WAO HAWAWI WENYE
KUAMINI (Kweli kweli) MPAKA WAKUFANYE (wewe ndiye) HAKIMU (mwamuzi) KATIKA
YALE WANAYOKHITALIFIANA…”
Kiapo
hiki cha Allah Mola Muumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ikiwa
kinaashiria jambo, basi haitakuwa ila ni kudhihirisha sharafu ya Mtume na
jinsi Mola wake anavyomjali. Hili linajionyesha wazi pale Allah
alipoifanya hukumu itayotolewa na Mtume wake ndio hukumu yake yeye Allah
na twaa ya Mtume ndio twaa yake yeye.
Kisha akawawajibishia waja wake kusalimu amri kwa hukumu ya Mtume
wake na kuifuata, kwani Mtume ni kama alivyomsifu Mola wake: “WALA
HASEMI KWA MATAMANIO (ya nafsi yake). HAYAKUWA HAYA (anayosema) ILA NI
WAHYI (ufunuo) ULIOFUNULIWA (kwake)”.
(53:3-4)
Kwa
mantiki hii ya aya, hukumu ya Mtume inakuwa ndio hukumu ya Allah. Na huku
kumfanya Mtume kuwa ndio Hakimu wa muumini katika yote na vyote ni katika
zama zote na mahala po pote. Ye
yote ambaye hakumridhia Bwana Mtume kuwa ndio Hakimu wake, huyo bila ya
shaka ye yote ni KAFIRI na amejitoa yeye mwenyewe katika Uislamu. Allah
anatutangazia: “MWENYE KUMTII MTUME AMEMTII ALLAH (kwani
anayoyaamrisha yametoka kwa Allah). NA ANAYEKENGEUKA (anajidhuru
mwenyewe)…” (4:80)
- Kukithirisha
kumtaja Bwana Mtume:
Miongoni
mwa alama zinazoonyesha mahaba ya mtu kwa Mtume wa Allah–Rehema na Amani
zimshukie-ni kukithirisha kumtaja. Kwani mtu akipendapo kitu hukithirisha
kukitaja, yaani hukitaja mara kwa mara. Kumtaja kwake Mtume kuambatane na
taadhima, kudhihirisha unyenyekevu na kujiweka chini yake.
Hii ni kwa sababu kimaumbile mtu akipenda kitu hukinyenyekea na
kukitii. Hivi ndivyo walivyokuwa wengi miongoni mwa maswahaba Allah
awawiye radhi–wanapomtaja Bwana Mtume hunyenyekea,
nyoyo na ngozi zao (miili) husisimka
na wakalia kwa mahaba na shauku. Kwa hivyo basi inamuwajibikia kila
muumini wakati anapomtaja Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–au
anapotajiwa aonyeshe utii na kujiweka chini yake na aione haiba na utukufu
wake kama kwamba huyo hapo Mtume amesimama mbele yake. Hizi ndizo mizani
tatu; kumfuata Mtume, kumfanya Hakimu na kumuadhimisha, mizani za kupimia
mahaba ya mtu kwa Mtume wa Allah. Atakayeyakuta
mambo matatu haya nafsini mwake basi na amuhimidi Allah na kama hana basi
na atake maghfira na atubie kwa Mola wake. Hebu sasa tuangalie ni namna
gani wenzetu walivyompenda kidhati Bwana Mtume–Rehema na Amani
zimshukie:
v
Abdullah Ibn Zubayr–Allah amuwiye radhi-alikuwa anapotajwa Mtume
mbele yake, hulia mpaka akaishiwa na machozi; yakawa hayatoki tena.
v
Ja’afar Ibn Muhammad alikuwa mwingi wa mzaha na tabasamu,
anapotajiwa Bwana Mtume hapo hapo rangi yake hupiga manjano na hali yake
hubadilika.
v
Abdur-rahman Ibn Qaasim, alikuwa anapotajwa Mtume wa Allah,
huangaliwa rangi yake na kuonekana kama mtu aliyetokwa na damu. Ulimi
kinywani umekauka kutokana na haiba ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie.
Hivi
ndivyo waja hawa wa Allah, wanadamu kama sisi walivyomuweka Mtume wa
Allah, unyenyekevu na utii wao huu kwa Mtume hata wawapo mbali nae ukawapa
nafasi ya kuwa karibu na Mtume. Na
ni ukweli usiopingika kwamba ye yote aliye karibu na Mtume huyo ameshafuzu
duniani . Hii ni kwa sababu kuwa karibu na Bwana huyu ni kuwa karibu na
Allah ambaye: “ALIYEMTUMA (aliyemleta) MTUME WAKE KWA UWONGOFU NA DINI
YA HAKI, ILI AISHINDISHE JUU YA DINI ZOTE….”
(48:28)
ALAMA
NYINGINE ZA MAHABA YA MTUME.
I.
Kufurahishwa
na misiba:
Hili
pia ni miongoni mwa vielelezo vya mahaba ya mtu kwa Mtume wa Allah. Mtu
anayedai kumpenda Bwana Mtume utamuona anaposibiwa na misiba/majanga
ambayo ni sehemu ya maisha, hapapatiki wala kubabaika.
Na badala yake huionea furaha misiba hiyo, kwa sababu mpenzi wa
Mtume huona ladha katika kumpenda kwake Bwana huyu kiasi cha kumsahaulisha
na kutompa nafasi ya kukumbuka uzito na uchungu wa misiba iliyomsibu. Huyu
haguswi na misiba kama wanavyoguswa watu, vipi basi iwe hivyo na il-hali
saa zote yu na kipenzi chake Bwana Mtume ambaye tayari ameshamfundisha
akabiliane vipi na misiba. Huyu anakuwa kama kwamba kavikwa tabia na umbile jingine
lisilo la kawaida. Hawa ndio
wale ambao anafiwa na mwanawe, watu wanaenda kuzika yeye anabaki akigawa
mirathi ya kipenzi chake, anasomesha elimu.
II.
Kupenda kukutana nae:
Mtu
mwenye kumpenda kidhati Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-huwa na
shauku kuu ya kukutana nae. Maswahaba Allah awawiye radhi–walipozidiwa
na shauku ya kumuona Bwana Mtume, walimkusudia khasa (walimuendea)
wakahisi raha mno kwa kule kumuona tu na kuponywa shauku yao.
Wakazidi kuona raha na tamu kwa kukaa pamoja nae huku wakimuangalia
na kutabaruku nae. Huku ndiko
kumpenda Mtume wa Allah kweli kweli.
III.
Kuipenda Qur-ani:
Katu
mtu hawezi kudai kumpenda Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-wakati
haipendi Qur-ani aliyomletea kutoka kwa Allah. Ukitaka kuyajua mahaba yako
kwa Bwana Mtume, basi yaangalie kwanza mahaba ya Qur-ani tukufu moyoni
mwako na jinsi unavyoona raha kwa kuisikiliza. Je, unaionea ladha na tamu
Qur-ani kuliko unavyozionea tamu nyimbo na taarabu wakati unapozisikiliza?
Imepokelewa kutoka kwa Sayyidna Uthmaan Ibn Affan–Allah amuwiye
radhi–kwamba yeye amesema: “Lau
nyoyo zetu zingetwaharika zisingeshiba maneno ya Allah”.
IV.
Kupenda Sunah yake:
Mtu
mwenye kudai kumpenda Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ni lazima
aipende sunah yake na kuzisoma hadithi zake sambamba na kuzifanyia kazi.
Kwani mtu ambaye utamu wa imani umepenya moyoni mwake, akilisikia neno
moja tu miongoni mwa maneno matukufu ya Allah au katika hadithi za Mtume
wake, moyo, roho na nafsi yake hulinywa na kulimeza neno hilo hapo hapo.
Yeyote atakayejipamba na kusifika na alama hizi tulizozidhukuru,
basi mtu huyo ni mkamilifu wa mahaba kwa Allah na Mtume wake.
Na huyu ndiye ana kila sababu za kuyasherehekea maulidi. Ama yule
atakayezikhalifu baadhi ya alama, akawa hanazo, basi huyo ni mpungufu wa
mahaba. Lakini yumo mahabani
na wala hatoki, hili linatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie- kwa yule mtu aliyemtia adabu (haddi) kwa sababu ya kunywa
pombe. Baadhi ya maswahaba
walimlaani na kusema: Ee nae kazidi, kila mara kosa hilo hilo tu! Bwana
Mtume akasema: “Msimlaani kwani
hakika yeye anampenda Allah na Mtume wake”.
Kwa
kukhitimisha makala yetu haya, hebu sasa tutazame:-
PICHA
ZA WALIOMPENDA KWELI MTUME WA ALLAH:
q
MWANAMKE WA
KIANSWARI.
Imepokewa
kwamba mwanamke mmoja wa Kianswari aliuliwa baba, kaka na mumewe siku ya
vita vya Uhud, walikokwenda kupigana pamoja na Mtume wa Allah–Rehema na
Amani zimshukie. Watu
walipokuwa wanarudi vitani aliwakimbilia na kuwauliza: Yukoje Mtume wa
Allah? Wakamjibu: Bukheri wa afya kwa himda za Allah kama upendavyo.
Akawaambia: Hebu nionyesheni nimuone, alipomuona akasema: Kila
msiba ni mwepesi kwangu ila msiba wako tu, ewe Mtume wa Allah.
q
THAUBAAN HURU
WA MTUME.
Imamu
Baghawiy–Allah amrehemu–amesema katika tafsiri yake kwamba kauli ya
Allah Mtukufu: “NA WENYE KUMTII ALLAH NA MTUME, BASI HAO WATAKUWA PAMOJA
NA WALE ALIOWANEEMESHA ALLAH: MANABII NA MASADIKI NA MASHAHIDI NA MASALIH
(Watu wema) NA UZURI ULIOJE (kwa mtu) WATU HAO KUWA RAFIKI (zake)”.
(4:69)
Imeshuka
kwa ajili ya Thaubaan, huru wa Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie.
Huyu alimpenda mno Bwana Mtume, alikuwa hajiwezi kabisa kwake.
Siku moja alimuendea Bwana Mtume na il-hali rangi yake imebadilika,
huzuni ikionekana usoni mwake. Mtume wa Allah akamuuliza: “Ni kipi/lipi
lililoibadilisha rangi yako?” Akamjibu: Ewe Mtume wa Allah! Mimi sina
maradhi wala maumivu yo yote, ili tu mimi nisipokuona hujiona mpweke mno
mpaka nikutane nawe. Kisha
ninakumbuka akhera na nikachelea kutokukuona huko kwa sababu wewe
utanyanyuliwa pamoja na mitume wenzio katika daraja za juu peponi.
Nami hata nikiingia peponi nitakuwa katika daraja ya chini yako na
kama sitaingia peponi ndio sitakuona kabisa (na mimi maradhi yangu ni
kukuona wewe) ndipo ikashuka aya hii.
q
ABDULLAH
IBN ZAYD:
Huyu
alikuwa kiungani mwake
akijishughulisha na
kazi za shamba. Mara mwanawe wa
kiume akamjia na kumpa khabari
za kifo cha
Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie. Akasema
baada ya kusikia
khabari hiyo ya huzuni: Ewe
Mola wa haki wee! Nakuomba uniondoshee uoni
wangu ili nisiweze kumuona yeyote
baada ya kufa kipenzi changu Muhammad.
Allah akaikubali dua yake, naam uoni
wake ukaondoshwa–Allah
amuwiye radhi.
q
KAULI YA
ANAS IBN MAALIK :
Imepokelewa
kwamba mtu
mmoja alimuendea Bwana
Mtume–Rehema na Amani
zimshukie-akamuuliza: Ewe Mtume wa Allah! Kiyama kitakuwa
lini? Mtume akamuuliza: “Umekiandalia nini
hicho kiama (unachokiuliza
)?” Yule mtu akamjibu
Mtume: Sikukiandalia wingi wa swala, swaumu
wala sadaka, lakini tu mimi ninampenda Allah
na Mtume wake. Kusikia
kauli yake hii, Bwana Mtume akamwambia:
“ Wewe utakuwa pamoja na
umpendaye”. Kisha Anas; khadimu
wa Mtume nae akasema: “Kwa
yakini mimi ninampenda Mtume wa
Allah, Abuu Bakri na Umar na
ninataraji kuwa pamoja
nao peponi”.
q
MUHABESHI
BILALI :
Huyu
hapa ndiye Bilali muadhini wa Mtume wa
Allah–Rehema na Amani zimshukie. Ameishi
katika kumpenda Bwana Mtume tangu siku
aliposilimu mpaka
anaingia kaburini. Alipokufa aliwasikia
baadhi ya watu wake wakilia na kusema: Ee huzuni iliyoje! Tahamaki kwa mshangao wa
wengi Bilali (maiti) amefungua
macho yake akitabasamu na kusema: Ee furaha iliyoje, kesho
tunakutana na kipenzi
Muhammad na kundi lake. Allah amuwiye
radhi Bilali.
q
UMMU
HUDHAYFAH:
Huyu
ndiye Hudhayfah Ibn Al–Yamaan–Allah
amuwiye radhi–anaulizwa na mama yake: Ewe
mwanangu! Lini ulionana
na Mtume wa Allah- Rehema
na Amani zimshukie? Akamjibu: Siku tatu
zilizopita. Mama yake akamgomba
na kumwambia: Vipi unaweza kusubiri ewe Hudhayfah
kutokumuona Mtume wako
kwa kipindi chote hicho
cha siku tatu? Hudhayfah akamwambia
mama yake: Ewe mama
yangu niache nimuendee Mtume
niswali nae Magharibi kisha nimuombe
anisamehe mimi na wewe. Hudhayfah anasema:
Nikaenda nikaswali
Magharibi pamoja na Mtume, Mtume
akaendelea kuswali (swala zake za Sunah)
mpaka ukaingia wakati
wa swala ya Ishaa. Akaswali Ishaa kisha akaondoka kuingia nyumbani
mwake nami nikamfuatia
nyuma yake. Mtume
akasikia sauti yangu, akauliza: Nani huyo? Ni
Hudhayfah?” Nikasema: Naam (ndiye). Akauliza
tena: “Una haja gani?” Allah ameshakusamehe
wewe na mama yako. Huu
ni muujiza wa dhahiri wa Mtume
wa Allah, anamueleza mtu yaliyomo moyoni
mwake kabla hata hajamueleza–Allah akurehemu ewe Mtume wa Allah .
q
ZAYD
IBN DATHINAH :
Mushrikina
walimteka Zayd na wakamtoa
ili wamuue, wamwambia:
Ewe Zayd tunakuonea huruma
kwa mapenzi ya Allah, je wewe
unapenda Muhammad awe katika
nafasi yako hii, tuipige
upanga shingo yake nawe uwe
kwa watu wako
nyumbani? Zayd akacheka
na kuwaambia: Wallah, mimi sipendi
Muhammad hapo alipo
sasa (wacha hapa) achomwe hata
na mwiba tu, nami
eti niwe nimekaa nyumbani (raha
mustarehe) na wake zangu na
watoto. Abuu Sufyaan wakati
huo akiwa bado kafiri
akasema: Wallah, sijapatapo kumuona ye yote akimpenda mtu
kama maswahaba wa Muhammad
wampendavyo Muhammad.
NENO
KHITAAM:
Tambua na ufahamu ewe
ndugu muislamu-Allah akurehemu– kwamba kumpenda Mtume
wa Allah ni daraja ambayo wenye kushindana
huishindania. Mahaba ya Mtume ni chakula cha nyoyo na
roho na burudani ya macho.
Mahaba ya Mtume ni uhai,
atakayenyimwa uhai huu, basi huyo ni katika
jumla ya wafu. Mahaba ya Mtume
ni nuru, atakayeikosa nuru
hiyo huyo
yumo katika bahari za
viza. Mahaba ya Mtume ni roho ya imani, ni roho ya amali (matendo)
na ni roho ya hali
na makamu yote. Kwa ujumla, moyo
wa mja hauna uhai ila kwa kumpenda
Allah na Mtume wake. Na wala hapana maisha
kama maisha ya wenye kumpenda Bwana Mtume,
macho yao yakatua kwa
kipenzi chao, nafsi zao zikatulizana
kwake na nyoyo zao zikapata utulivu kwake. Wakaliwazika kwa kuwa nae
karibu na wakaneemeka na mahaba yake.
Nyoyoni mwao mna nguvu
ya ajabu isiyoweza kuzuiliwa
ila na mahaba ya Allah na
Mtume wake. Asiyebahatika
kuyapata mahaba haya, huyo
maisha yake yote ni taabu, mashaka,
huzuni, masumbuko, shida, uchungu na majuto.
Naam ndugu muislamu, haya kwa
mukhtasari ndio mahaba ya Mtume. Hebu wakati
ukiyasherehekea maulidi ya
Bwana huyu, jikague:-
ü
Je , kweli wewe una mahaba ya Mtume?
Kama ndivyo kisha jiulize,
ü
Je , inawezekana kweli kwa mwenye kumpenda
Mtume kuacha swala, swaumu, zakah, kusema uongo kutoa na
kupokea rushwa, kufitinisha, kuhusudi, kuwatupa wazazi, ndugu, jamaa,
mayatima na masikini, kuacha kutafuta
elimu na ---- na----?!
Mwisho
kabisa Website yako (WEBSITE UISLAMU)
inakuomba tuombe pamoja: EWE MOLA
WA HAKI WEE! TUNAKUOMBA UTUJAALIE MAHABA
YAKO NA MAHABA YA MTUME WAKO YAPENDEZE
ZAIDI KWETU SISI WAJA WAKO KULIKO
VITU VYOTE. KULIKO HATA MAJI YA
BARIDI YAPENDEZAVYO
KWA KIU – Aaamiyn!
Tunawatakia
waislamu wote popote walipo heri,
fanaka, furaha na baraka ya Maulidi. Maulidi njema kwenu nyote!
Waalaam
Alaykum Warahamatullah
Mtumishi wa umma,
WEBSITE UISLAMU.
|