Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

UMRI WA PILI WA MWANADAMU

Faida

Kunamkinikia mtu aliyeruzukiwa taufiq ya kuutumia vema wakati wake, kuurefusha umri wake na kuupanua mpaka apatakapo Allah hata baada ya kufa kwake. Akaendelea kuwa hai na ilhali amekufa, hili litawezekana tu ikiwa atakuwa ameacha nyuma yake kitakachoendelea kuinufaisha jamii. Akaacha elimu yenye manufaa inayowasaidia watu katika utendaji wa maisha yao ya kila siku. Au akamuacha mtoto mwema atakayemnufaisha yeye na jamii yake kutokana na matendo yake mema. Au akaacha athari njema au mwendo mwema utakaoigwa na kuendelezwa na waliobakia nyuma. Au akaasisi jambo la hisani na ufadhili litakaloendelea kutoa matunda baada ya kufarikiana kwake na ulimwengu huu. Haya yanatokana na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Afapo mwanadamu, thawabu za amali zake zote njema hukatika ila (thawabu za) mambo matatu:

1.     sadaka yenye kuendelea, au

2.    elimu yenye kunufaisha, au

3.     mtoto mwema atakayemuombea Mungu”. Muslim

Na katika hadithi nyingine iliyokusanya mambo mengine zaidi ya mambo matatu haya, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Hakika miongoni mwa amali (matendo)  mema yake yanayomfuata baada ya kufa kwake (ni pamoja na)

1.     elimu aliyoifundisha na kuineza, au

2.    mtoto mwema aliyemuacha, au

3.    msahafu aliourithisha, au

4.    msikiti alioujenga, au

5.    nyumba ya wasafiri (walioharibikiwa), au

6.    kisima alichokichimba, au

7.     sadaka aliyoitoa katika mali yake katika uhai na uzima wake, itakayomfuata baada ya kufa kwake”. Ibn Maajah & Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema tena: “Ye yote atakayeanzisha suna (mwendo) njema, basi utamthibitikia ujira wake na ujira wa watakaomfuata (watakaoifanyia kazi suna hiyo) mpaka siku ya kiyama”. Muslim

Hivi ndivyo Qur-ani Tukufu inavyosema kuhusiana na athari ya amali baada ya mauti: “KWA YAKINI SISI TUTAWAHUISHA WAFU NA TUNAZIANDIKA (amali zao wanazozifanya zisiwache) TAATHIRA NYUMA NA (zile wanazozifanya zikawacha) TAATHIRA ZAO (nyuma)...”. [36:12] Ikasema tena: “SIKU HIYO ATAAMBIWA MWANADAMU ALIYO YATANGULIZA (yasiache athari) NA ALIYOYAAKHIRISHA (yakaacha athari)”. [75:13]

Wanazuoni wanakongamana na kuwafikiana kwamba utajo mwema anaouacha mwanadamu baada ya kufa kwake. Huzingatiwa kuwa ni umri wake mwingine usio na mpaka baada ya umri ule wenye mpaka. Hili ndilo aliloliomba baba wa mitume; nabii Ibrahim-Amani imshukie: “NA UNIJAALIE KUTAJWA KWA WEMA NA WATU WATAKAOKUJA BAADAYE”. [26:84]

Kuna tofauti kubwa ya dhahiri baina ya mtu anayekufa na ilhali nyoyo zinahuzunika juu yake, macho yanabubujika machozi kwa ajili yake na ndimi zote zinamsifia kwa sifa njema na kumuombea rehema. Na yule anayekufa pasipatikane hata jicho la kumtolea machozi, usihuzunike moyo kwa kufarikiana naye na wala ndimi zisimuombee rehema. Hii ndio hali ya watu walioishi katika ulimwengu huu na kujifanya miungu wanaoabudiwa na kutukuzwa, wakiwanyanyasa wanadamu wenziwao na kuwadhulumu. Hii ndio aina ya watu anaowataja mshairi katika ubeti wake:-

     Huyo ndiye ambaye akiishi hana manufaa * Na akifa hawamuhuzunikii zake jamaa (seuze watu kando)!

Hawa ndio walengwa wa kauli tukufu ya Allah: “MABUSTANI MANGAPI NA CHEMCHEM NGAPI WALIZIACHA (baada ya kugharikishwa) NA MIMEA NA MAHALI PAZURI NA NEEMA (kubwa kubwa) WALIZOKUWA WAKIJISTAREHESHA. NAMNA HIVI (tumewafanya) NA TUKAWARITHISHA HAYA WATU WENGINE. MBINGU NA ARDHI HAZIKUWALILIA (walioko ardhini hawakuwalilia wala walioko mbinguni kwani walikuwa watu wabaya). WALA HAWAKUPEWA MUDA (wa kurejea tena ulimwenguni)”. [44:25-29]

Mara nyingi wanapokufa watu waovu wa namna hii, hayafi pamoja nao madhambi na dhuluma zao au ukafiri na upotofu wao. Bali huwarithisha mabaya haya wafuasi wao ambao huzifuata nyayo zao. Ikiwa kwa mujibu wa maneno ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ye yote mwenye kuasisi suna njema, atapata ujira wa suna hiyo na ujira wa watakaoifanya kazi/suna hiyo mpaka siku ya kiyama. Hali kadhalika mwenye kuasisi suna mbaya, yatamthibitikia madhambi yake suna hiyo na madhambi ya watakaomfuata katika kuitenda na kuiendeleza suna/mwenendo huo mbaya ulioasisiwa nae. Na kama ambavyo mtu akiacha nyuma yake elimu yenye manufaa, ujira wa amali yake hiyo njema haukatiki. Basi hali ni kama hiyo kwa mtu atakayeacha athari mbaya na fikra potevu, ujira wa amali yake hiyo mbaya utaendelea kumfuata huko kaburini aliko hadi kule akhera. Hili ndilo lililowafikisha waja wema wa Allah-Allah awarehemu-kusema: (Furaha na raha iliyoje kwa yule anayekufa na yakafa pamoja nae madhambi (maovu) yake. Na adhabu kali (ole wake) yule aliyekufa na ilhali maovu yake yako hai baada yake).

 

TAHADHARI NA MAJANGA YENYE KUANGAMIZA WAKATI WAKO...IX

Baada ya kutambua na kufahamu umuhimu na thamani ya wakati na namna bora ya kuitumia rasilimali hii kuu. Hebu sasa kwa msaada wa Allah Mola Mjuzi wa kila kitu, tujaribu kuyaangalia mambo yanayoweza kuwa ni majanga yanayouangamiza wakati wa mwanadamu. Kwa hakika yako maafa mengi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuwa ni chanzo cha kuuangamiza wakati wa mwanadamu na kumuacha bila ya kunufaika nao. Iwapo mtu hatazinduka mapema atajuta wakati ambapo majuto yake hayo hayatamnufaisha kwa cho chote, kwani umri (wakati) uliopotea hautarudi tena. Miongoni mwa maafa ya wakati ni kama yafuatavyo:-

             I.      MGHAFALA:

Haya ni aina ya maradhi yanayoisibu akili na moyo wa mwanadamu. Maradhi haya humuondoshea mwanadamu nguvu hisia ambazo hufanya kazi ya kuhifadhi, kuchambua na kuzingatia mambo. Kukosekana kwa nguvu hisia hizi humaanisha kukosekana kwa mzinduko angavu wa maana na matokeo mwisho ya vitu/mambo. Kwa mantiki hii basi mkosa nguvu hisia huhusika na vitu/mambo kwa njia ya picha tu ya macho na si kwa njia ya maana inayomfanya aone na kusikia kwa moyo. Huyaangalia mambo kwa dhahiri tu na si kwa hakika ya maumbile yake. Huyaona maganda ya mambo na si kokwa ya ndani na uoni wake hukoma katika kuangalia mwanzo wa mambo na si mwisho wake. Qur-ani Tukufu inawatahadharisha sana waislamu na maradhi haya mabaya ya mghafala. Qur-ani imekwenda kina sana kiasi cha kuwafanya wana mghafala kuwa ni kuni za jahanamu na kuwa ni wapotevu kuliko hata wanyama wasio na akili. Hebu na tuizingatie kwa pamoja aya hii tukufu: “NA BILA YA SHAKA TUMEWAUMBIA MOTO WA JAHANAMU WENGI KATIKA MAJINI NA WANADAMU (kwa sababu hii): NYOYO WANAZO LAKINI HAWAFAHAMU KWAZO, NA MACHO WANAYO LAKINI HAWAONI KWAYO. NA MASIKIO WANAYO LAKINI HAWASIKII KWAYO. HAO NI KAMA WANYAMA, BALI WAO NI WAPOTEVU ZAIDI, HAO NDIO WALIOGHAFILIKA”. [7:179]

Allah anamkhutubu Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “NA MTAJE MOLA WAKO MOYONI MWAKO KWA UNYENYEKEVU NA KHOFU NA BILA YA KUPIGA KELELE KATIKA KAULI (yako hiyo, mkumbuke Mola wako umtaje) ASUBUHI NA JIONI, WALA USIWE MIONGONI MWA WALIOGHAFILIKA”. [7:205] Na katika aya nyingine akamwambia: “...WALA USIWATII WALE AMBAO TUMEZIGHAFILISHA NYOYO ZAO WAKAFUATA MATAMANIO YAO NA MAMBO YAO YAKAWA YAMEPITA MIPAKA (yaani makafiri)”. [18:28]

Ee balaa adhimu iliyoje kwa jamii kupitiwa na matukio yanayoyatetemesha majabali, lakini jamii hiyo haiyazingatii na wala haibadilishwi na matukio hayo. Matukio kwao ni mithili ya mchezo wa kuigiza na si uhalisia wa mambo.

 

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI: Upofu si kupofua macho bali  upofu khasa ni mtu kupofua akili na moyo. Tusome tukipenda: “...KWA HAKIKA MACHO HAYAPOFOKI LAKINI NYOYO AMBAZO ZIMO VIFUANI NDIZO ZINAZOPOFUA (zikadhuru katika dini)”. [22:46]


Forum | Guestbook | Tuandikie |