|
Ni
watu wangapi waliowafikiwa kutenda amali kubwa na nyingi katika umri mdogo
(mchache) mpaka ikadhaniwa kwamba hiyo ni aina ya mambo yasiyo ya kawaida.
Ukweli ulivyo si mambo yasiyo ya kawaida, bali hiyo ni baraka ya umri na
taufiq ya Allah kwa mja wake. Itoshe kuwa ni kigezo na mfano hai kwamba
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Amewafikiwa kuwatoa watu
katika viza vya ushirikina na kuwatia katika nuru ya Uislamu, na akaweza
kuibadilisha kabisa historia nzima ya mwanadamu mpaka leo na mpaka atakapo
Allah. Ameyafanya yote haya katika kipindi kisichopungua miaka ishirini na
tatu. Akasimamisha mfumo mpya na sahihi wa maisha (Uislamu), akakilea
kizazi cha pekee chini ya mfumo huu na kuasisi uma wenye kupigiwa mfano na
dola ya kilimwengu katika kitambo hiki kifupi. Pamoja na vikwazo na magumu
yote aliyokumbana nayo tangu siku ya mwanzo ya kazi yake hii, bado alipata
mafanikio makubwa haya. Na wala usitoe hoja ukasema: Hakika Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliweza kuyafanya yote hayo kwa sababu
alipewa msaada wa miujiza. Nani kama yeye, tu wapi sisi hata
tujilinganishe naye?!
Uhalisia
wa mambo ni kuwa maisha ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika
ulinganiaji na upiganiaji wake wa dini. Yalikuwa yakifuata kanuni na
utaratibu wa Allah wa kawaida (uliozoweleka na kutambuliwa na watu) na
wala haikuwa ni miujiza. Hakika si vinginevyo, muijiza huja mahala
maalumu, mahala ambapo zimetolewa na kufanywa kila sababu zimkinikazo
katika ardhi na haujabakia ila msaada kutoka mbinguni. Ni katika hali na
mazingira kama haya ndipo huja msaada wa miujiza. Kama ambavyo Allah
alivyompa msaada wake katika suala zima la Hijrah wakati alipomteremshia
utulivu wake na kumpa msaada wa majeshi yasiyoonekana. Kadhalika katika
vita vya Badri baada ya kufanya sababu zote, hapo ndipo Allah akampa
msaada wa malaika alfu moja wenye kufuatana mfululizo: “NA ALLAH
HAKUFANYA HAYA ILA IWE BISHARA (khabari ya furaha) NA ILI NYOYO ZENU ZITUE
KWAYO...”. [8:10]
Hebu
waangalie makhalifa waongofu na maswahaba wote wa Bwana Mtume-Allah
awawiye radhi-na wale wote waliowafuatia katika imani. Waangalie namna
gani walivyoufungua ulimwengu, wakaueneza Uislamu, wakayafundisha mataifa,
wakayagurisha kutoka katika dini zao za kijahili na ada zao mbaya katika
kipindi cha miongo kadhaa tu. Kiasi cha kuwaacha wanahistoria
wakiyashangaa mapinduzi haya yaliyofanywa na Uislamu ulimwenguni katika
kipindi kifupi mno kuwahi kutokea katika historia nzima ya mwanadamu.
Mapinduzi ya kidini, kifikra, maisha binafsi na yale ya kijamii sambamba
na mapinduzi ya kisiasa. Hebu muangalie kwa mfano mtu kama Umar Ibn
Abdul-Aziyz-Allah amrehemu. Huyu alifanya kila lililo katika uweza wake
kuhakikisha kuwa ukhalifa unarudi katika uongofu wake kama ulivyokuwa
katika zama za makhalifa waongofu. Aliweka mikakati ya kurejesha haki
zilizodhulumiwa kwa wanaozistahiki na amana kwa wenyewe. Aliyafanya yote
haya ili isije ikampata mbele ya Allah lawama ya mwenye kulaumu. Katika
kipindi kifupi mno cha ukhalifa wake; miaka miwili na nusu tu aliweza
kutokana na nia njema aliyokuwa nayo kuijaza ardhi usawa na uadilifu.
Allah amuwiye radhi amirul-muuminina Umar Ibn Abdul-Aziyz.
Uzito
wa amali huzidi katika mizani ya haki na hurudufika thamani na thawabu
zake mbele ya Allah kila vinapokithiri vikwazo katika njia ya kuitekeleza.
Hapa ndipo unapoonekana ubora wa maswahaba juu ya watu waliokuja baada
yao. Hii ni kwa sababu wao waliamini wakati ambapo watu walikufuru,
wakamsadiki Bwana Mtume katika kipindi ambacho watu wanamkadhibisha na
kumpinga. Kadhalika ndivyo ulivyokuwa ubora wa waliotangulia wakawa wa
kwanza kuingia katika Uislamu miongoni mwa Muhajirina na Answaari, kwa
maswahaba waliowafuatia nyuma yao. Ambao waliosilimu baada ya ‘Fat-hi
Makah’ na kudhihiri nguvu na kitisho cha Uislamu. Katika hili Qur-ani
Tukufu inasema: “...HAWAWI SAWA MIONGONI MWENU WALE WALIOTOA KABLA YA
KUSHINDA (kwa kutekwa Makah) NA WAKAENDELEA KUPIGANA. (Maswahaba) HAO WANA
DARAJA KUBWA ZAIDI KULIKO WALE AMBAO WAMETOA BAADAE NA WAKAPIGANA. NA
ALLAH AMEWAAHIDIA WEMA WOTE HAO...”. [57:10]
Kadhalika
ni kwa mantiki hii amali njema inayotendwa katika zama ambazo jamii za
wanadamu zimefisidika na kufilisika kimaadili. Zama ambazo
viongozi/watawala huwa madhalimu, matajiri huishi maisha ya anasa mno,
wenye nguvu hutakabari na wanazuoni hujipendekeza kwa watu. Zama ambazo
uovu huenea na mambo machafu kufanywa dhahiri shahiri na wema kuadimika.
Amali njema katika zama hizi huwa na ujira mkubwa sana na daraja ya juu
kabisa. Washika dini katika zama hizi na katika hali na mazingira kama
haya ni mithili ya maswahaba wapya, kutokana na kutupwa dini nyuma na
kuwekwa mbele ‘Jahilia”. Imethibiti katika hadithi sahihi kwamba Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ibada katika (zama za
ghasia za) fitna na ikhtilafu ni kama Hijrah ya kunifuata”. Muslim,
Tirmidhiy & Ibn Maajah.
Imepokewa kutoka kwa Abuu Umayyah As-sha’abaaniy amesema:
Nilimuendea Abuu Tha’alabah Al-khashaniy nikamuuliza: Unaifanyaje aya
hii? Akasema: Aya ipi hiyo? Nikamwambia: “ENYI MLIOAMINI! LILILO LAZIMA
JUU YENU NI NAFSI ZENU. HAWAKUDHURUNI WALIOPOTOKA IKIWA MUMEONGOKA...”
[5:105] Akaniambia: Nilimuuliza kuhusiana nayo (aya hiyo) mjuzi wa mambo,
nilimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Bali
jiamrisheni kufanya mema na jikatazeni maovu mpaka utakapoona ubakhili
unatiiwa, matamanio ya nafsi yanafuatwa, dunia inapendwa zaidi (kuliko
akhera) na kila mwenye rai kupendezwa na rai yake. Na utapoona huna uwezo
wa kuamrisha (ukatiiwa, basi wakati huo ndio) jilazimishe na yanayoikhusu
nafsi yako (tu). Hakika mbele yenu kuna siku za subira, kusubiri ndani
ya siku hizo ni mithili ya kukamata kaa la moto. Mwenye kufanya amali
njema ndani ya siku hizo, ana ujira wa mithili ya watu khamsini wanaofanya
mithili ya amali yake hiyo”. Ibn Maajah, Tirmidhiy & Abuu
Daawoud. Abuu Daawoud akazidisha katika riwaya yake: “Pakasemwa
(pakaulizwa) ewe Mtume wa Allah, ujira wa watu khamsini miongoni mwetu
sisi (maswahaba wako) au miongoni mwao (watu wa zama hizo)? Mtume akasema:
Bali ujira wa watu khamsini miongoni mwenu nyinyi”.
Bwana
Mtume ametaja katika baadhi ya riwaya kuelezea sababu ya
urudufu/muongezeko huu wa ujira, akasema: “Hakika nyinyi mnapata
wasaidizi katika kufanya kheri na wao hawatampata wa kuwasaidia katika
(kufanya amali za) kheri”. Kauli hii ya Bwana Mtume inamaanisha kwamba
hadithi hii ilielekezwa kwa baadhi ya maswahaba baada ya kuenea kwa
Uislamu na kuingia watu katika dini makundi kwa makundi na kuwepo
wanaosaidia katika kheri. Kwani waliotangulia wakawa wa mwanzo kuingia
katika dini; miongoni mwa Muhajirina na Answaari, hawakuwa na watu wa
kuwasaidia katika kuutekeleza Uislamu wao, hawa hawalingani na ye yote
katika ubora. Kadhalika hadithi inawajibisha kuendelea kuamrisha mema na
kukataza maovu maadam lipo sikio linalosikia na moyo unaozingatia. Maadam
yapo matumaini japo finyu ya kusikilizwa kwa namna moja au nyingine.
|