Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

TUNAPASWA KUZITUPIA JICHO ZAMA ZA USONI (MUSTAKBALI).

 

     Kama inavyotupasa kuziangalia zama za kisogoni (zilizopita), hali kadhalika imetupasa kuzitupia jicho zama za usoni (zijazo), leo. Ni dhahiri kuwa  maumbile ya mwanadamu yamefungamana zaidi na mustakbali wake kuliko zama zake zilizopita. Mtu mwenye akili timamu hawezi kabisa kughafilika na mustakbali wake.  Kama ambavyo alivyopewa mwanadamu kumbukumbu zinazomsaidia kumuunganishia leo yake na yaliyopita.  Katika mkabala wa hilo akapewa uwezo wa kuwazia mambo asiyoyaona ili umsaidie kusawirisha na kumpa picha ya mustakbali wake na yanayotazamiwa ndani yake.

     Miongoni mwa sifa na tabia za mustakbali ni kuwa kwake ghaibu (Hidden/unseen) na majuhuli (unknown). Hakuna ye yote ajuaye ni lipi litamtokea kwa hakika na ni kheri au shari ipi imjongeleayo.  Hivi ndivyo Allah Mola Muumba wetu anavyotuambia: “….NA NAFSI YO YOTE HAIJUI NI NINI ITACHUMA KESHO, WALA NAFSI HAIJUI ITAFIA ARDHI GANI. BILA SHAKA ALLAH NDIYE MJUZI (ndiye) MWENYE KHABARI (ya mambo yote)” (31:34)

     Sifa nyingine ya mustakbali ni kuwa kila kijacho ndani yake, basi hicho ki karibu ajapodhania mwanadamu kuwa ki mbali au kinachelewa.  Hii ndio sababu pakasemwa na wenye busara waangaliao mambo kwa uhalisia wake (kesho i pamoja na leo na kesho kwa mwenye kuitazamia i karibu) Allah anatuambia ndani ya Qur-ani Tukufu kuhusiana na kiyama ambacho mwanadamu anakiona kuwa ki mbali: “…WALA HALIKUWA HILO JAMBO LA (kufika) SAA (ile ya Kiyama) ILA NI KAMA KUPEPESA JICHO AU NI KARIBU ZAIDI…” (16:77)

     Mwenye akili timamu ni yule anayefanya maandalizi ya mustakbali wake leo na kujitayarisha kwa jambo kabla ya kutokea kwake. Hivi ndivyo Allah anavyotuasa kwa njia ya amri: “ENYI MLIOAMINI! MCHENI ALLAH NA KILA MTU AANGALIE (atazame) ANAYOYATANGULIZA KWA AJILI YA KESHO (Akhera/maisha ya mbeleni)”… (59:18)

     Wale wenye dhana na fikra potofu kwamba dini inamdunisha na kumuweka nyuma mwanadamu kwa sababu inamfungamanisha na yaliyopita na kumalizika.  Hawa ni walemavu wa akili na fikra zao pia ni lemavu kama wao wenyewe.  Wameshindwa kufahamu johari na hakika ya dini ni kumuandaa mwanadamu na maisha ya milele; maisha ya mustakbali wake.  Maisha ya nyumba ambayo hiyo ni bora na yenye kusalikia milele kuliko nyumba aliyomo hivi sasa (dunia).

     Nadharia ya mustakbali ni nadharia ya msingi  katika nguzo/shina la dini.  Imethibiti katika hadithi kwamba: “Hakika mja yu baina ya khofu mbili: Baina ya muda uliopita ambao hajui Allah atamfanya nini katika muda huo na muda uliosalia ambao hajui Allah atamuhukumia nini ndani yake.  Basi na ajitwalie kutokana na nafsi yake kwa manufaa ya nafsi yake. Na achukue duniani kwake kitachomfaa katika akhera yake.  Na achukue cha kumfaa ujanani kabla ya ukongwe. Namuapia yule ambaye nafsi yangu i mikononi mwake, hakuna baada ya mauti wa kumlaumu. Na wala hakuna nyumba nyingine baada ya dunia ila ni pepo au moto.”

     Hii haimaanishi kwamba mwanadamu haushughulikii ila mustakbali wake wa akhera tu basi na aache kuungalia mustakbali wake katika dunia hii aishimo.  La hasha, hayo siyo makusudio na muradi wa Uislamu katika aya na hadithi tulizozitaja.  Hii ni kwa sababu Uislamu umemfundisha muislamu kuizengea kesho yake (mustakabali) kwa kuifanyia maandalizi kwa kupitia sababu (njia) zitakazomsaidia kuithibitisha ndoto yake kuielekea kesho yake.  Hii ni bila ya kuangalia na kuibagua kesho yake hiyo katika matapo mawili; ya kidunia na ile ya kiakhera.  Ikiwa tunakubali kwa mujibu wa imani yetu kwamba Bwana Mtume ndio kigezo kikuu cha kuigwa na waumini wote.  Hebu muangalie anavyoutafuta mustakbali wa ujumbe wake (da’awah) wakati makabila mawili ya Madinah Ausi na Khazraji yalipompa kiapo/ahadi ya uaminifu na utii. Akafikiria suala la Hijrah ambayo ilimgharimu kuuacha mji aliozaliwa na  kuuzoea kwa ajili tu ya kusimamisha sheria na jamii ya Kiislamu. Yote haya hayakuwa ila ni mikakati iliyopangwa barabara ya mustakbali wa Uislamu. Na katika masuala ya kidunia tunamkuta Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie–akiiwekea familia yake akiba ya chakula cha mwaka mzima. Wala hakuona kwamba hili linapingana na kadhia ya kumtegemea Allah.

 

HAJA YA KUJISHUGHULISHA NA LEO (ZAMA AISHIMO MTU).

          Iwapo imemlazimu mwanadamu kusita na kufanya kituo pamoja na zama zilizopita.  Kituo ambamo atautupia jicho wakati uliopita, akayazingatia matukio yaliyopita akafaidika nayo na kuikagua nafsi yake. Kama ilivyompasa kuungalia  mustakbali wake na kuufanyia maandalizi.  Haya yote hufanyka leo, yaani ndani ya zama aishizo mwanadamu. Kwa mantiki hii basi, kumemuwajibikia mwanadamu huyu kuipa umuhimu maalum na wa upendeleo leo yake. Anufaike nayo kabla haijamponyoka na kumpotea asiipate tena kwani tayari itakuwa imeshakuwa jana.

 

JINSI GANI MWANADAMU ANAWEZA KUUREFUSHA UMRI WAKE?

     Si jambo la kutiliwa shaka kwamba kimaumbile mwanadamu ni kiumbe apendaye kuishi na anapenda umri mrefu bali kuishi milele kama  angeliweza. Qur –ani Tukufu inalithibitisha umbile hili kupitia kwa Mayahudi: “NA UTAWAONA (Mayahudi) WANA HAMU KUBWA YA KUISHI KULIKO WATU WENGINE, NA KULIKO WALE WAMSHIRIKISHAO ALLAH (wasioamini Akhera); KILA MMOJA KATIKA WAO ANAPENDA APEWE UMRI WA MIAKA ALFU….”  (2:96)

Mlango huu wa maumbile; maumbile ya kupenda kuishi milele ndio alioingilia Ibilisi kwa baba yetu Adamu. Akamghuri, akala katika matunda ya mti aliokatazwa kuyala: “(Lakini) SHETANI ALIMTIA WASIWASI (alimchokoachokoa) AKAMWAMBIA: EWE ADAMU, JE! NIKUJULISHE MTI WA MILELE NA WA UFALMEUSIOKOMA? BASI WAKAULA WOTE WAWILI (Adamu na Hawa) ….”  (20:120-121)

Dini ya Kiislamu kwa dhati yake inauzingatia umri mrefu kuwa ni neema

utakapotumiwa katika kuinusuru haki na kutenda amali njema.  Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliulizwa ni mtu yupi aliye bora kuliko watu wote? Akajibu kwa kusema: “Mtu uliyekuwa mrefu umri wake na yakawa mema matendo yake”. Tirmidhiy, Twabaraaniy,      Al-Bihaqiy & wengineo.

Kwa upande mwingine ni jambo lisilo na shaka kwamba mauti huja ghafla na kumpokonya mwanadamu matumaini na mapenzi yake haya ya kuwa na umri mrefu. Mauti ndio mwisho wa mizunguko na uhai wa mwanadamu katika ulimwengu huu wa muda mfupi.  Ni jambo lisilopingika kwamba umri ni mfupi sana usiokidhi mipango na matumaini ya mwanadamu.  Kila afaye huwa hajakamilisha mambo na mipango yake aliyojipangia. Hili linatokana na ukweli kwamba uhai ni siku chache tu, ni pumzi kidogo tu zinazokatishwa na mauti bila hata ya kubisha hodi au kutoa taarifa. Bwana-Mtume Rehema na Amani zimshukie-anasema:

  • “Ishi utakavyoishi (lakini tambua) hakika wewe utakufa, na

  • Mpende umpendaye/kipende ukipendacho, hakika utafarikiana (utatengana) nacho (siku moja), na

  • Tenda ulitakalo (lakini tambua) hakika utalipwa kwalo na utaulizwa kuhusiana nalo.” Twabaraaniy

Bado haijaweza na kamwe haitaweza elimu ya sayansi ya utabibu ambayo imefikisha mwanadamu kupandikiza moyo mahala pa moyo mwingine. Wala elimu ya teknolojia iliyomuwezesha mwanadamu kufika mwezini haijaweza na katu haitaweza kupambana na uzee, haijaweza kumrudishia mzee ujana wake. Amesema kweli Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Allah hajapatapo kushusha ugonjwa wo wote ila alishusha pamoja nao dawa yake ila uzee (ukongwe)”. Na katika riwaya nyingine: “….ila mauti.”  Bukhaariy

Sasa ikiwa huu ndio ukweli kuhusiana na uhai/maisha ya mwanadamu vipi basi anaweza kuutumainia kiasi cha kujiwekea mipango mingi? Na il-hali ukweli ni kwamba umri halisi wa mwanadmau ni ile miaka michache anayoipitisha tangu kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake.  Si ajabu ukamkuta mwanadamu kapewa umri wa zaidi ya miaka mia moja lakini katika daftari lake la amali njema ukakuta sifuri.  Hakujinufaisha yeye mwenyewe kutokana na umri huo wala wengine hawakunufaika nao.  Na mtu mwingine huweza kufa angali kijana mbichi, lakini akawa amelijaza daftari lake la amali za kheri na kuwaachia wenzake mema ya kumkumbuka.  Kwa mantiki hii basi, kumbe inawezakana mwanadamu kuurefusha umri wake kwa namna atakavyowafikiwa. Akaurefusha kwa kumuabudu Allah Bwana Mlezi wake, kuwatendea wema viumbe wake. Matendo yake haya yakigubikwa na ikhlaswi (utendaji kwa ajili ya Allah tu) na ukamilifu/ufanisi itakuwa ni bora kwa mtendaji wake. Na kwa kiasi ambacho matendo yake yatakuwa na faida na kuacha athari njema kwa wengine ndio huwa kiasi cha thamani na daraja ya mtendaji.  Matendo haya ni kama vile kuwajulisha watu jambo la uongofu, kuwaokoa katika mambo maovu, kuwatatulia matatizo yao, kuwaondoshea dhulma, au kuwanusuru dhidi ya adui yao na baki ya matendo mengine ambayo manufaa yake huirejea jamii. Hapa ndipo utaona amali kama kulingania kwa Allah  (da’awah) na kuipigania jihadi dini ya Allah zikawa katika kilele cha amali zote kidaraja mbele ya Allah Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie–anasema: “Atakayelingania jambo la uongofu, atakuwa na ujira mithili ya ujira wa watakaomfuata (katika kutenda jambo hilo). Hili (la kupata ujira mithili ya watendaji) halipunguzi cho chote katika ujira wao (watendaji).” Muslim

     Na akasema tena: “Hakika peponi kuna daraja mia moja ambazo Allah amewaandalia mujahidina kaitka njia ya Allah. Umbali ulio baina ya daraja mbili ni kama umbali ulio baina ya mbingu na ardhi.” Bukhaariy

     Mmoja miongoni mwa maswahaba wa Bwana Mtume alipita katika njia za majabalini ambako kuna kijisima cha maji baridi kikamvutia, akajisemea moyoni: Lau ningelijitenga na watu nikakaa katika njia hii na kufanya ibada, lakini sitafanya hivi mpaka nimuombe idhini Mtume wa Allah.  Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie- akamwambia: “Usifanye hivyo, kwani daraja ya mmoja wenu katika njia ya Allah ni bora kuliko swala yake aiswaliyo nyumbani kwake kwa miaka sabini. Je, hampendi Allah akughufirieni na kukuingizeni peponi? Piganeni katika njia ya Allah, ye yote atakayepigana katika njia ya Allah,  (hata) kiasi cha kumkama ngamia (wake) kumemuwajibikia kupata pepo.” Tirmidhiy & Al-Haakim.

     Hivi ndivyo amali zinavyotofautiana na kuzidiana katika daraja na ujira na mwenye mafanikio ni yule mwenye pupa ya kulifanya lililo bora: “….NA KATIKA (kupata) HAYA WASHINDANE WENYE KUSHINDANA.” (83:26)

 

 



Forum | Guestbook | Tuandikie |