|
Mtazamo huu hasi wa mustakbali; msimamo wa kukosa matumaini na
kukata tamaa, unakabiliwa na mtazamo
chanya. Huu si
mwingine zaidi ya msimamo wa kuuelekea mustakbali kwa ndoto tupu zenye
matumaini mema na matamanio bila ya kuwa na elimu inayoenda sambamba na
wakati, kazi wala mikakati ya kimaendeleo. Si hatia kusema kuwa ndoto
zenye matumaini mema na matamanio pekee hazijengi utukufu/heshima na wala
haziyathibitishi matumaini hayo. Sayyidna Aliy Ibn Abuu Twalib–Allah
amuwiye radhi–alimuasa mwanawe: “Tahadhari na kuyategemea matumaini
tupu, kwani kwa yakini (matumaini) hayo ni bidhaa ya mtu mpumbavu (asiye
na akili).”
Na
alisema mshairi mmoja:
Na
wala usiwe mtumwa wa matumaini tupu,
Kwani
matumaini hayo ni rasilimali ya watu muflisi (wa mawazo/fikra).
Qur-ani
Tukufu imeyapinga vikali madai ya Ahlul-Kitaab (Watu wa kitabu) Mayahudi
na manaswara. Madai ya kuingia peponi kwa matumaini/matamanio matupu bila
ya kufanya yale ambayo ndio
sababu ya kuingilia huko peponi: Allah Mola Mtukufu anatuambia: “NA
WALISEMA: HATAINGIA PEPONI ILA ALIYE MYAHUDI AU MNASWARA (mkristo) HAYO NI
MATAMANIO YAO TU (si hukumu ya Allah) SEMA: LETENI DALILI ZENU (juu ya
madai yenu haya) KAMA NYINYI NI WASEMA KWELI. NAAM, WANAOELEKEZA NYUSO ZAO
KWA ALLAH NA WAKAWA NI WATENDAJI MEMA (kwa viumbe wenziwao) BASI WAO
WATAPATA MALIPO YAO KWA MOLA WAO, WALA HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA
HAWATAHUZUNIKA.” (2:111–112)
Qur-ani
haikukomelea tu katika kuyapinga madai na matamanio haya ya Ahlul-Kitaab,
bali imewachanganya pamoja nao waislamu wanaodhania kwamba kujinasibisha
kwao na Uislamu bila ya kuishi kwa mujibu wa Uislamu wao, kutawaokoa mbele
za Allah. Hawa wanaambiwa na Allah: “(Kuingia Peponi) SI KWA MATAMANIO
YENU, WALA SI KWA MATAMANIO YA WATU WALIOPEWA KITABU (kabla yenu lakini
mambo ni haya) ATAKAYEFANYA UBAYA ATALIPWA KWA (ubaya) HUO WALA HATAPATA
MLINZI WALA MSAIDIZI KWA AJILI YAKE MBELE YA ALLAH. NA WATAKAOFANYA
VITENDO VIZURI, WAKIWA WANAUME AU WANAWEKA, HALI WAO NI WENYE KUAMINI,
BASI HAO WATAINGIA PEPONI WALA HAWATADHULUMIWA HATA TUNDU YA KOKWA YA
TENDE.” (4:123–124)
Ni
vema ikaeleweka kwamba inachopinga na kukanusha Qur-ani ni mtu kuyategemea
matamanio tu bila ya kufanya kile kitakachoyathibitisha matamanio hayo.
Lakini Qur-ani haipingi matumaini mema ya siku za usoni na
imetofautisha baina ya mambo mawili haya. Matumaini ni yale yanayokwenda
sambamba na amali (matendo) itakayoyafanikisha, na kama matumaini
hayakukutanishwa na amali yake, basi hicho si kingine bali ni matamanio
matupu. Ni kwa sababu hii ndio hadithi ya Bwana Mtume–Rehema na Amani
zimshukie–ikazingatia kuwa ni ajizi na upumbavu kuyafuata matamanio ya
nafsi kwa kutegemea maghfira (msamaha) ya Allah na ukunjufu wa rehema zake.
Huu ni uwendawazimu, kwani mtu mwenye fikra lemavu hizi haijagonga ngoma
za masikio yake kauli ya Allah: “…BILA SHAKA REHEMA YA ALLAH IKO
KARIBU SANA NA (wale waja wake) WANAOFANYA MEMA.” (7:56)
Na
kauli yake: “...NA REHEMA YANGU INAWEZA KUKIENEA KILA KITU. LAKINI
NITAWAANDIKIA (kweli kweli kabisa) WALE WANAOJIKINGA NA YALE
NILIYOWAKATAZA, NA WANAOTOA ZAKA NA WANAOZIAMINI AYA ZETU.”
(7: 156)
Katika
kuiweka wazi maana hii, imekuja hadithi ya Mtume wa Allah– Rehema na
Amani zimshukie: “Mwenye akili/busara ni yule aliyeihifadhi nafsi yake
na akatenda amali (njema) kwa ajili ya (maisha) baada ya mauti. Na
dhaifu wa akili ni yule aifuatishiaye nafsi yake matamanio yake (maovu) na
akatamani kwa Allah matamanio (matupu bila ya amali).” Tirmidhiy,
Ahmad & Maajah.
Qur-ani
Tukufu inayaenzi matumaini/matarajio na kuwasifia watu watarajiao:
“HAKIKA WALE WALIOAMINI NA WALE WALIOHAJIRI (wakahama kuja Madinah) NA
WAKAPIGANIA NJIA YA ALLAH, HAO NDIO WANAOTUMAI REHEMA YA ALLAH NA ALLAH NI
MWINGI WA KUSAMEHE (na ) MWINGI WA KUREHEMU.”
(2:218)
Baadhi
ya waja wema wa Allah–Allah awarehemu-wanasema:
{Kutaka pepo bila ya amali ni dhambi miongoni mwa dhambi.
Na kutarajia uombezi wa Mtume (shafaa)
bila ya kufuata suna (mwendo wake) ni aina ya ghururi (madanganyo).
Na kutarajia rehema ya Allah pamoja na (kufanya maasi) ni ujinga na
upumbavu}.
c)
WAPENZI WA HADHIRI (ZAMA ZILIZOPO):
Wako watu ambao kamwe hawageuki nyuma kutazama zama zilizopita na
wala hawazielekezei nyuso, nyoyo na akili zama zijazo (mustakbali) Hawa
huishi kwa ajili ya leo yao na ndani ya leo yao (zama zao) tu Haya ni
natija na matokeo ya mtazamo wao kwamba jana (zama zilizopita)
imekwishapita na kwenda zake. Na kipitacho huwa kimekufa, kwa hivyo basi
haiingii akilini kukishughulikia au kukifikiria kilichokufa. Kwa mtazamo
wa kundi hili la watu linaloishi katika jamii yetu, mustakbali (kesho/zama
zijazo) ni kitu ghaibu (hidden/unseen) Na kitu ghaibu ni kitu majuhuli
(unknown), kwa mantiki hii basi haimfalii mtu mhalisia wa mambo
kufungamana na kushikamana na kitu majuhuli. Kwa sababu kufanya hivyo ni
kama kujenga nyumba ya barafu au kuandika angani. Je, nyumba hiyo
itasimama na maandishi hayo yataonekana na mwenye macho akamakinika
kuyasoma?
Hawa
kuzama na kujitoa kwao wazima wazima kwa leo yao kumewapumbaza na
kuwafanya waisahau kesho yao kama kulivyowapumbaza kustafidi na jana yao.
Hawa ni wana wa leo yao na zama zao tu basi, hawajishughulishi na
Akhera kwa sababu hiyo (akhera) ni mustakbali (kitu kijacho). Na wao
itikadi yao ni kutokuuza taslimu (cash) kwa deni la muda mrefu wala
kilichopo kwa kijacho/kisichopo. Na
wala hawajishughulishi na historia wala urithi wa mambo ya kale, kwa
kigezo kuwa hayo yamepita na kumalizika. Tunaposema kwamba watu wenye
fikra hizi ni “wana wa leo yao” tunakusudia kuwa wao ni watu
wasiofikiria wala kujishughulisha ila na zama waishizo tu. Bila ya
kujikumbusha na kuchukua maonyo na mazingatio ya jana (zama zilizopita)
wala kuifikiria na kuipangia mikakati inayoambatana na utekelezaji kesho
yao (zama za usoni). Haya na tukubaliane nao kwamba mtu ajishughulishe tu
na wakati alionao (aishio ndani lyake). Ni kwa nini basi anaupoteza, na ni
kwa nini asiutumie katika maendeleo yake binafsi na jamii kwa ujumla?! Ni
kwa nini aumalizi muda wake wote huo katika kumtii Mola wake, katika
kuinusuru haki (Uislamu) na kutenda mema? Ukweli ulivyo mtu akichunguza na
kutafiti kwa makini atagundua kwamba leo (zama zilizopo) ni fungu lililo
baina ya jana (zama zilizopita) na kesho (mustakbali). Kwa mantiki hii,
hivi ni vitu vyernye uhusiano wa moja kwa moja na mafungamano ya karibu
kabisa. Kwa msingi huu tunaruhusika kusema na si kusema tu, bali kusema
kwa kinywa kipana kabisa.
Kwamba wema na uzuri wa maisha ya leo (sasa) unategemea kabisa msingi
mzuri uliowekwa katika maisha
ya jana (yaliyopita). Na maisha mazuri
ya baadae (mustakbali mwema) unayategemea kwa kiwango kikubwa
kabisa maisha ya sasa (leo). Hivi ni sawa kabisa na kusema kuwa leo
inapangwa na kuandaliwa jana
na kesho inaandaliwa leo. Fikra hizi ndizo zilizomsukuma mshairi mmoja kusema:
[Hazikuwa
zama (ulimwengu )ila ni nyakati mbili (tu);
Uzingatie wakati uliopita na
ufikirie ujao].
Naam,
ni kweli na ni dhahiri kwamba mahala pa kuleta mazingatio ya jana (wakati uliopita)
na fikra za kesho (wakati ujao) ni leo (wakati uliopo).
|