|
Mtazamo sahihi kuelekea wakati ni ule unaozichanganya
pamoja jana,leo na kesho. Huu ndio mtazamo sahihi, mtazamo unaozitazama
zama zilizopita ukaziunganisha na za sasa, ukazitazama zama zilizopo
ukaziunganisha na zile zijazo.
HATUNA BUDI KUZITUPIA JICHO ZAMA ZILIZOPITA:
-
Tunalazimika kuzitupia jicho zama zilizopita ili:-
-
Tuchukue mazingatio kupitia matukio yaliyopita.
-
Tuwaidhike na miisho ya nyumati zilizopita, vipi
ulikuwa mwisho wao.
-
Tuangalie namna Allah alivyowatendea
(alivyowaadabisha).
Kwa hivyo basi utaona kwamba zama zilizopita ni chombo cha
matukio na ni khazina ya mazingatio na mafunzo. Hebu tuzitafakari pamoja
kauli hizi za Allah Mola Muumba wetu:
“ZIMEPITA ADABU NAMNA KWA NAMNA WALIZOTIWA WALIOKUWA
KABLA YENU. BASI SAFIRINI KATIKA NCHI NA MUONE ULIKUWAJE
MWISHO WA WALE WALIOKADHIBISHA (amri zetu). HAYA NI
MAELEZO YALIYO WAZI KWA WATU (wote wa zama zote) NA UWONGOZI NA MAUIDHA
KWA WAMCHAO.” (3:137-138)
Aya inawaelezea watu wa nyumati zilizoishi ulimwenguni
hapa kabla yetu na kututaka tujionee wenyewe namna Allah alivyowaadhibu
kutokana na kuzikhalifu amri zake. Tukishaona maangamivu ya watu shupavu,
wakukutavu wa nyoyo, ndipo tukae chini tutafakari na kujiuliza kwa nini
yaliwasibu yaliyowasibu? Tukishayajua tujiepushe nayo ili kuepuka
yasijetufika mithili yaliyowafika wao. Hivi ndivyo tunavyoweza kujifunza
kutoka katika zama zilizopita mafunzo yanayotufaa leo katika zama hai.
Tuzidi kutafakari:- “KAMA YAMEKUPATENI MAJARAHA, BASI NA WATU HAO
YAMEWAPATA MAJARAHA KAMA HAYA. NA SIKU ZA NAMNA HII TUNAWALETEA WATU KWA
ZAMU…” (3:140)
Tukipata machungu katika kuipigania dini ya Allah, basi
tutambue kwamba sisi sio wa kwanza kufikwa na hayo. Wenzetu waliotu
tangulia katika imani pia yaliwapata machungu tena pengine makali kuliko
yetu, wakasubiri na Allah akawapa ushindi. Kwa hivyo ni juu yetu nasi
kuipigania dini ya Allah huku tukiwa tumeshika silaha kali subira, tuone
Allah atakavyotunusuru: “ENYI MLIOAMINI! MKIINUSURU DINI YA ALLAH, NAYE
ATAKUNUSURUNI NA ATAITHUBUTISHA MIGUU YENU.” (47:7)
Tuzidi kuwaidhika na yaliyopita na tuchukue mazingatio
yatakayotufaa leo: “NA MANABII WANGAPI WALIPIGANA NA MAADUI NA PAMOJA
NAO KULIKUWA NA WATAKATIFU WENGI. HAWAKULEGEA KWA YALE YALIYOWASIBU KATIKA
NJIA YA ALLAH, WALA HAWAKUDHOOFIKA WALA HAWAKUDHALILIKA NA ALLAH
ANAWAPENDA WAFANYAO SUBIRA.” (3: 146)
Kuzitazama zama zilizopita na kujifunza kutokana na
matukio yake ni amri ya Allah iliyokuja ndani ya Qur-ani Tukufu: “JE,
HAWATEMBEI KATIKA ARDHI ILI WAPATE NYOYO (akili) ZA KUFAHAMIA, AU MASIKIO
YA KUSIKILIA? KWA HAKIKA MACHO HAYAPOFOKI (yakadhuru katika dini) LAKINI
NYOYO AMBAZO ZIMO VIFUANI NDIZO ZINAZOPOFOKA (zikadhuru katika dini).”
(22: 46)
Kingine wanachoweza kufaidika nacho watu wa zama za leo
kutokana na urithi wa waliowatangulia ni pamoja na elimu zao za fani
mbalimbali, ustaarabu na utamaduni wao. Lakini kufaidika huku ni baada ya
kuchekecha na kuchuja, tukayachukua yale mazuri yanayoenda sambamba na
zama pamoja na hali zetu. Ni haki yetu kuwarithi waliotutangulia, kwani
Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie –anatuambia: “Neno lenye
hekima (busara/elimu) ni kipotewa cha muumini, po pote atapokikuta basi
yeye ana haki nacho zaidi (kuliko mtu mwingine).” Tirmidhiy & Ibn
Maajah
Si sawa kukiacha cha kale/zamani eti kwa sababu tu ni cha
kale. Hii ni kwa sababu viko vitu vingi vinavyozingatiwa kuwa ni vya kale
na ambavyo kimaumbile/kiasili havikubali upya vina faida na ubora hadi hii
leo. Hebu tuifanye Qur-ani Tukufu kama kigezo, kisha tujiulize: Je,
haukuwa ubora wa Qur-ani ni kwa sababu hiyo Qur-ani ni maneno makongwe ya
Allah ambayo upya wake hauchakai na wala haipitwi na wakati? Je, ubora wa
Al-Ka’abah hautokani na kuwa kwake “nyumba kongwe ya ibada” yenye
kukusudiwa na watu zama baada ya zama? Bila ya shaka Qur-ani haifanyiwi
upya, ikaonekana hii iliyopo ni ya siku nyingi kwa hivyo imechoka/haifai
iondolewe na iletwe mpya. Haya si maumbile ya Qur-ani kwani yenyewe
kimaumbile haichakai, ilifaa jana, inafaa leo na itaendelea kufaa kesho na
upya wake kuzidi siku hata siku. Hali kadhalika Al-Ka’abah haihitajii
kufanyiwa upya, ikaondolewa kwa kuwa ni kongwe na kuletwa nyingine. Kama
ambavyo hakika ya hali na mambo isivyo na haja ya kufanyiwa upya.
Wamechupa mipaka watetezi wa upya pale walipokipa kisogo
kila cha kale na kukipigia makofi kila kipya kiingiacho. Wamefanya hivi
pamoja na ukweli kwamba miongoni mwa vya kale kuna ambavyo vina manufaa
makubwa sana mpaka leo. Na katika vipya kuna ambavyo vina madhara tupu na
havifai kabisa pamoja na upya wake. Wamesahau na kughafilika kwamba ukale
na upya ni masuala mawili yenye kunasibikiana kwa karibu sana. Uhalisia wa
mambo ulivyo cha kale/zamani kwa watu fulani hicho ni kipya kwa watu
wengine, hivi ni sawa na kusema: (cha kale chako ni kipya cha mwenzio) na
kinyume chake (kipya chako ni cha kale cha mwenzio). Kadhalika ieleweke
kwamba kipya hakitasalikia kipya milele, hili linatokana na ukweli kwamba
cha kale cha leo ndicho kilichokuwa kipya cha jana. Na hivyo hivyo kipya
cha leo ndicho kitachokuwa cha kale kesho, huu ndio ukweli tumekubali au
tumekataa. Kila mwanadamu hana budi kuwa na kituo cha kuitazama kila siku
inayompitia. Katika kituo hicho aikague nafsi yake na kujiuliza:
-Amefanya nini katika siku yake hiyo iliyopita?
- Kwa nini amefanya hivyo? Au
-Kwa nini ameacha kufanya? Na kadhalika.
Ni bora zaidi kama atakuwa na mazoea ya kulifanya zoezi
hili kila siku kabla ya kulala. Kwa yakini kipindi hiki cha mwanadamu
kuikagua nafsi yake kinachukuliwa kuwa ni kipindi chake cha kupiga hatua
mbele. Kipindi cha kujikosoa na kujisahihisha, kipindi cha kukiri udhaifu
wake na kujirekebisha. Hiki ni kipindi ambamo mwanadamu huwa ni hakimu wa
matamanio yake, hakimu wa dhamira yake. Ni kipindi ambacho muumini
huiwekea imani yake askari wa kuilinda na mkaguzi wa kuikagua, sambamba na
jaji wa kuihukumu nafsi yake. Kwa mtindo na tabia hii, muislamu hupiga
hatua kutoka katika hali ya “Nafsi yenye kuamrisha sana maovu” na
kuingia katika hali ya “nafsi inayojilaumu sana katika kutenda maovu”.
Katika kuhimiza juu ya zoezi zima la mtu kuikagua nafsi yake,
Amirul-Muuminina Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi–anatuambia:
“Zihesabuni/zikagueni nafsi zenu kabla ya kukaguliwa (mbele ya Allah) na
zipimeni amali zenu kabla hamjapimiwa.”
Sayyidna Umar mwenyewe alikuwa unapoingia usiku akiipiga
bakora miguu yake na kujiambia: Leo nimefanya nini?
Ni muhimu kila mmoja wetu awe na tabia na mazoea ya
kuangalia ametenda nini katika ulimwengu na akhera yake kila siku.
Akishindwa basi na ajitahidi kulifanya zoezi hili japo mara moja kwa juma
ili kujua:
-Ni lipi lilimpasa kulitenda na je, alilitenda?
-Ni lipi halikumpasa kulitenda, je, aliliacha?
Kisha awe na kituo kirefu cha kutafakari na kujikagua
mwishoni mwa kila mwezi. Na si vibaya kuwa na kitabu cha rekodi za matukio
ya kila siku, kwani kina msaada mkubwa katika kukumbuka yaliyopita. Halafu
tena awe na kituo kirefu zaidi wakati wa kuuaga mwaka unaomalizika na
kuupokea mwaka mpya. Hiki ndio kipindi kizuri cha kuyarejea na kuyafanyia
uchunguzi wa kina yote yaliyopita katika kipindi cha mwaka mzima.
Yaliyopita ni pamoja na mafanikio na matatizo, aangalie ameyafikia vipi
mafanikio na kwa nini amepatwa na matatizo. Kadhalika hiki ni kipindi cha
kupanga mikakati na mipango ya mwaka uliokabili (mpya) sambamba na
kuyatafutia ufumbuzi muafaka na munasibu matatizo yote ya mwaka
unaomalizika. Hii ndio hesabu ya kufunga mwaka ya muislamu.
Miongoni mwa bidaa ngeni zilizozushwa na watu wa
magharibi, na kwa bahati mbaya zikaigwa na baadhi ya waislamu. Ni mtu
kufanya halfa ya furaha na kuandaa vitamu na vinono miongoni mwa vyakula
na vinywaji. Hafla hii hufanywa kila unapopita mwaka mmoja katika umri wa
muhusika, hiki ndicho kile kinachoitwa “Birthday”. Waislamu
wamejiingiza katika mambo ambayo Allah hakuyateremshia dalili, mithili ya
kuwasha mishumaa kwa idadi ya umri wa muhusika (mwenye birthday yake) na
kisha kuizima kwa mtindo wa kimaigizoigizo. Na watu wakapelekeana zawadi
kuonyesha hisia zao za upendo kwa muhusika kutokana na sherehe yake hii.
Hivi ndugu zanguni, tuliyoamrishwa na Mola wetu kuyatenda, tumeyatenda
yote yamemalizika mpaka tena tukaamua kujibebesha mzigo wa
tusiyoamrishwa?! Linalotakikana kufanywa na mtu mwenye akili na busara.
Badala ya huku kuiga kiupofu upofu mambo ambayo hayana maana wala faida,
angeitumia fursa hii ya kumponyoka mwaka mmoja katika uhai wake kama kituo
cha kutafakari na kuzingatia. Akafanya kama afanyavyo mfanyabiashara kila
mwisho wa mwaka; huyarejea upya madaftari yake ya kumbukumbu za fedha,
hesabu ya mali iliyopo sambamba na madeni awiwayo na awiyayo.
Mfanyabiashara hufanya hivi ili kujua khasara na faida. Na muislamu ni
mfanyabiashara anayefanya biashara na Mola ambapo rasilimali yake ni uhai
wake: “ENYI MLIOAMINI! JE, NIKUJULISHENI BIASHARA ITAKAYOKUOKOENI NA
ADHABU IUMIZAYO? (Basi biashara yenyewe ni hii): MUAMININI ALLAH NA MTUME
WAKE, NA IPIGANIENI DINI YA ALLAH KWA MALI ZENU NA NAFSI ZENU, HAYA NI
BORA KWENU IKIWA MNAJUA. (Mkifanya haya) ATAKUSAMEHENI DHAMBI ZENU NA
ATAKUINGIZENI KATIKA MABUSTANI YAPITAYO MITO MBELE YAKE NA (atakupeni)
MASKANI MAZURI MAZURI KATIKA BUSTANI ZA MILELE, HUKU NDIKO KUFUZU
KUKUBWA.” (61: 10 – 12)
Badala ya kufanya “Birthday” inayoambatana na mambo
yasiyo mridhi Allah kila mtu anapotimiza umri wa mwaka mmoja zaidi.
Muislamu alipaswa kuitumia fursa hii kuitafakari biashara yake hiyo
iliyoelezwa katika aya hizo za Qur-ani. Akapima ufanisi na tija,
akaangalia matatizo na mafanikio sambamba na faida (twaa) na hasara
(uasi). Na akamuomba Mola wake amtakabalie mema yote aliyoyatenda katika
mwaka uliopita na amsamehe madhambi aliyoyatenda. Bila ya kusahau kumuomba
ambubujishie kheri, furaha na fanaka katika mwaka wake mpya na amkinge
dhidi ya majanga na maafa mbalimbali. Huku akiamini kuwa Allah atamuuliza
juu ya mwaka wake huo uliomalizika.
|