|
b) WENYE KUFUNGAMANA (MAKHADIMU) NA MUSTAKBALI (WAKATI
UJAO/KESHO):
Tukiwaweka kando watu wa kundi hili la jana ambao daima
huangalia nyuma kwa sura moja au nyingine. Tunakutana na kundi jingine
lenye kufungamana na kuamini katika mustakbali (zama za usoni/zijazo mbele
yao). Kundi hili ni la watu ambao huzipa mgongo wa kwa heri ya kuonana
zama zilizopita. Watu wa kundi hili daima huangalia mbele hawageuki nyuma,
msimamo wao huu huwafanya waitupilie mbali historia (tarekh) na hivyo
kujidhulumu wenyewe fursa ya kujifunza kutokana na historia. Hawana haja
kabisa na historia ya watu/nyumati zilizokuwa kabla yao na wala hawataki
kabisa urithi wa kitamaduni, kidini wala ule wa kiustaarabu. Bila ya
kuangalia mazuri yatokanayo na urithi huu wakayaenzi kwa kuyaendeleza na
kuyaboresha na kuyatupilia mbali yaliyo mabaya na ya upotofu. Hawa ni wale
ambao aghlabu husikika wakinena: (Hebu tuondokeeni na hadithi za mababu
waliokufa na kushiba mauti na tuacheni tutafiti vijana watakaokuwa
viongozi wa kesho). Na pengine hunena: (Kwa yakini macho yetu hayakuumbwa
visogoni mwetu hata tuweze kutazama nyuma. Bali yameumbwa nyusoni mwetu
ili tuweze kuangalia mbele). Hunena maneno haya na mithili yake, maneno
haya huwa ni haki iliyokusudiwa batili iwapo mtu atalenga kuzisahau kabisa
zama zilizopita na yake yote. Na kukataa urithi na yote yaliyomo ndani
yake na kuimwagia mchanga (kuizika) historia na yote iliyoyasheheneza
miongini mwa darsa, mazingatio, maongozi na mashauri yanayoongoza akili na
nyoyo. Ee uzuri ulioje wa kauli ya Allah iliyomo ndani ya kitabu chake
kitukufu ikizindua kustafidi na kuwaidhika na yaliyopita: “JE,
HAWATEMBEI KATIKA ARDHI (wakaona athari za mambo ya kale) ILI WAPATE NYOYO
(akili) ZA KUFAHAMU AU MASIKIO YA KUSIKILIA? KWA HAKIKA MACHO HAYAPOFOKI
(yakadhuru katika dini) LAKINI NYOYO AMBAZO ZIMO VIFUANI NDIZO
ZINAZOPOFOKA (zikadhuru katika dini)”. (17:46)
MTAZAMO HASI/LEMAVU KUELEKEA MUSTAKBALI (MTAZAMO WA KUKATA
TAMAA):
Wako miongoni mwa watu ambao huitazama kesho na kuifikiria
kwa mtazamo wa mtu aliyekata tamaa. Mtu aliyevaa mawani meusi tii (mno)
anautazama uhai, viumbe hai, zama na mahala kwa nyuma ya mawani hayo. Mara
tahamaki mtu huyu hukata tamaa na kesho na kupoteza kabisa matumaini na
kufaulu kutokana na kuyatazama kwake mambo/vitu kwa kutumia zana isiyo
sahihi wala muafaka. Imekita ndani ya nafsi yake dhana ya kwamba kamwe
mambo hayabadiliki kutoka katika hali mbaya ila kwenda katika hali mbaya
zaidi kuliko ya sasa/iliyopita. Na kwamba maisha ni mithili ya usiku wa
kiza totoro usiochomozewa na alfajiri wala kiza chake hakiondoshwi na
mwangaza mkali wa jua. Huu bila ya shaka yo yote ni mtazamo bomoa;
unaombomoa yeye binafsi, maisha yake na jamii yake. Maisha ya mtu yasiyo
na mionzi ya matumaini ya mustakbali ni ya dhiki zaidi kuliko dhiki ya
ngamia kuingia katika tundu ya sindano. Maisha ya jamii iliyokosa
matumaini na mipango ya baadae ni maisha mafu yasiyo na roho wala harakati
Lau si matumaini na mipango ya mustakbali, asingelijenga aliyejenga akakaa
na tukakaa, asingelima aliyelima akavuna akala na tukala na wala
elimu/sayansi na teknoloja isingelipiga hatua mbele na kufika hapa ilipo
leo. Natija ya haya yote ni kwamba dini, historia na uhalisia wa mambo,
vyote hivi vinatufundisha kwamba:-
-
Maisha hayana maana ikiwa yanasuhubiana na kukata
tamaa.
-
Hakika pamoja na dhiki huja faraja au faraja
husuhubiana na dhiki au faraja imo ndani ya dhiki.
-
Baada ya usiku kuondoka hatimaye huchomoza alfajiri.
-
Kudumu kwa hali moja milele ni muhali, yaani ni jambo
lisilowezekana kwani mambo huenda na kubadilika.
Allah Mola Mjuzi wa yote anatuambia ndani ya kitabu chake
kitukufu: “…HAWAKATI TAMAA NA REHEMA YA ALLAH ISIPOKUWA WATU
MAKAFIRI”. (12:87)
Na katika aya nyingine anasema: “….NA NANI ANAYEKATA
TAMAA YA REHEMA YA MOLA WAKE ISIPOKUWA WALE WALIOPOTEA?” (15:56)
Miongoni mwa sura za kukata tamaa na kukosa matumaini ni
ile itikadi iliyoenea miongoni mwa watu wengi kwamba hivi sasa tunaishi na
tumo katika zama za mwisho. Umri wa dunia umekwisha na kwamba alama za
kiyama zilizotajwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-zimeshadhihiri
dhahiri shahiri. Na kwamba kheri katika zama hizi za mwisho ni mtu
kujiweka nyuma na shari iko katika kujiweka mbele kimaendeleo. Na kwamba
taa ya dini inazimika siku baada ya siku mpaka itazimika kabisa na
kumaanisha kufutika kwa kitu dini katika uso wa ardhi hii. Na hivyo kutoa
fursa ya kuenea kwa ukafiri dunia nzima mpaka kiyama hakitasimama ila kwa
kafiri mwana wa kafiri. Kwa hivyo basi kwa kuyazingatia yote hayo kunakuwa
hakuna mantiki ya mtu kuwa na mipango ya baadae ya kmaendeleo. Hii ni
kwasababu hakuna matumaini wala tamaa ya kuirekebisha au kuibadilisha hali
hii iliyokabili usoni mwetu. Dalili na ushahidi wanaoutoa juu ya nadharia
yao hii ya kukata tamaa ni hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Bwana
Mtume– Rehema na Amani zimshukie–zikitaja khabari za fitna na alama za
kiyama.
Lakini uhalisia na ukweli wa mambo na hali si kama
walivyofahamu watu hawa kwa nadharia yao hii inayotazama mambo kwa ujuu
juu tu bila ya kuzama ndani. Huu ni ufahamu mfupi kwani aya na hadithi
zilizokuja katika kutaja ukaribu wa kusimama kwa kiyama na kudhihiri kwa
alama zake. Aya na hadithi hizi hazimaanishi kwamba kiyama hicho ki
mlangoni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukaribu na umbali wa kitu ni
dhana ya ulinganifu wa kitu kimoja baina ya kingine. Ni nani ajuaye,
huenda baina yetu na hicho kiyama kuna maalfu ya miaka. Hajui kusimama kwa
kiyama ila Allah pekee ambaye yeye ndiye Msimamishaji wa hicho kiyama. Na
nani ajuaye huenda hicho kiyama ki karibu yetu zaidi kuliko tunavyofikiria
na kusawirisha! Na kuhusiana na hicho kiyama Qur-ani Tukufu
haikuzidisha zaidi ya kusema:
“….PENGINE KIAMA KIKO KARIBU”. (33:63)
“...LABDA KIAMA KIMEKARIBIA”. (42:17)
“...HAITAKUFIKIENI (saa hiyo–yaani kiama) ILA KWA
GHAFLA (tu
hivi)…” (7:187)
Kuletwa kwa Mtume wetu-Rehema na Amani zimshukie–peke
yake ni miongoni mwa alama za kiyama, kwani Mtume ndiye aliyesema:
“Nimetumilizwa (nimepewa utume) mimi na kiyama kama
viwili hivi….na akapacha baina ya dole gumba na kidole cha kati.”
Buhkaariy & Muslim
Kwa hivyo basi kuacha kufanya amali za kimaendeleo kwa
lengo la kuustawisha na kuuamirisha uliwengu. Kwa madai ya kuhuisha sheria
ya Kiislamu, uma wa Kiislamu na dola ya Kiislamu kwa kungojea kusimama kwa
kiyama. Na kwa kutegemea kwamba sisi tuko katika zama za mwisho, hili ni
suala lipingwalo na kukanushwa na dini kwa nguvu zote. Kwani ni dini hii
ndio iliyomuamrisha muislamu kujitahidi kufanya amali maadam yu hai. Na
waislamu kwa kulizingatia hili ni uma wenye kuamrishwa kufanya amali mpaka
ufungwe mlango wa toba. Na hili la kufungwa mlango wa toba litapatikana
katika siku za mwisho za umri wa duniani, ambapo jua litachomoza kutokea
upande wa magharibi: “…SIKU ZITAKAPOFIKA BAADHI YA ISHARA ZA MOLA
WAKO, BASI MTU (kafiri) HAITAMFAA IMANI YAKE, AMBAYE ALIKUWA HAKUAMINI
ZAMANI, AU (muislamu) HAKUCHUMA KHERI KATIKA UISLAMU WAKE….” (6:158)
Na kwa yakini imekuja kutoka kwa Mtume wa Allah amri ya
kuendelea kufanya amali za kidunia (za maendeleo), dunia ambayo si cho
chote katika mtazamo wa dini. Amri hii ni pale aliposema:
“Kitakaposimama kiyama na ilhali mkononi mwa mmoja wenu kuna mche, basi
akiweza kisisimame mpaka aupande basi na aupande”. Ahmad & Bukhaariy
Basi ikiwa muislamu ameamrishwa asiuache mche wake hata
kama kasikia mpulizo wa parapanda mpaka aikamilishe kazi yake hiyo kiasi
ya uwezo wake. Anaamrishwa hivyo hata kama yeye hatanufaika na mche huo
wala ye yote baada yake. Iweje basi baina yetu na kiyama ambacho ki masafa
yasiyojulikana ila na Muumba wa ulimwengu pekee?! Kwa yakini kufanya kazi
ni suala linalotakiwa hata kama kazi hiyo haikumpa matunda muhusika.
Ikimpa matunda mbele atakuwa amefuzu kwa kupata vizuri viwili; dunia na
akhera. Na kama haikumpa matunda mbele (hapa duniani), basi inatosha
kwamba yeye amejitahidi, ametekeleza wajibu wake na amepata udhuru wa
kumsemea mbele ya Allah.
|