|
Nabii Muhammad – Rehema na Amani
zimshukie – alipotumwa na Mwenyezi Mungu
Mtukufu kuja ulimwenguni kuuhusisha Uislamu
ulioasisiwa na Mitume waliomtangulia, alimkuta
mwanamke akiishi chini ya mazingira na kivuli
cha ukandamizaji. Katika ulimwengu ule, mwanamke
hakuwa na haki yeyote ile katika jamii yake bali
alionekana kama ni bidhaa inayoweza kuuzwa
wakati wowote. Mwanamke alichukuliwa kama ni
chombo cha kumstarehesha na kukidhi matamanio ya
kimwili ya mwanamume. Mwanamke alihesabika kuwa
ni chombo cha uzalishaji na hakuwa na
uchaguzi/uhuru wa kupanga na kuamua. Haya kwa
mukhtasari ndiyo mazingira ambayo Uislamu
ulimkuta mwanamke akiishi chini ya anga lake.
Mwenyezi Mungu kupitia mfumo sahihi wa maisha
(Uislamu) ambao dhamana ya uongozi wake alimpa
Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie –
akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhulma,
uonevu na unyanyasaji ule. Uislamu ukamjengea
mwanamke mazingira bora, kanuni na sheria ambazo
zitamuhakikishia uhuru, usalama, amani, haki na
usawa katika jamii yake. Uislamu ukamtayarishia
mwanamke anga zuri, chini ya anga hilo ataishi
huku akijihisi kuwa ni binadamu kamili, mwenye
haki sawa kama mwanamume na ukamdhaminia kupata
haki zote kama binadamu bila ya kuhitajia
upendeleo maalum kama tusikiavyo istilahi hii
ikipigiwa kelele ulimwenguni kote bila ya
utekelezaji wowote. Uislamu ukamuondoshea
mwanamke tuhuma ya kumpotosha Baba yetu Adam –
amani iwashukie wote – peponi na kuwa yeye
(mwanamke) ndiye asili na chanzo cha uovu wote
huu utendekao ulimwenguni. Uislamu ukabainisha
kwamba ni shetani mlaaniwa ndiye aliyewapoteza
Nabii Adam na mama yetu Hawaa, kama tunavyosoma
katika kitabu cha Uislamu "(Lakini) SHETANI
(yule Iblis adui yao) ALIWATELEZESHA WOTE WAWILI
(wakakhalifu amri ile, wakala katika mti huo
waliokatazwa) NA AKAWATOA KATIKA ILE (hali)
WALIYOKUWA NAYO …[2:36].
Uislamu unakiri na kutangaza wazi kuwa watu
wote bila ya kujali rangi au hali zao kimaisha
wameumbwa kutokana na nafsi moja tu. Tusome,
tuzingatie na tukubali : "ENYI WATU !
MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI
(asili) MOJA …." [4:1]
Huu ni usawa wa binadamu katika mfumo adilifu
wa maisha (Uislamu). Chini ya kivuli cha mfumo
huu, mwanamke na mwanamume wanaogelea pamoja
katika bahari moja ya usawa wa haki zote za
msingi za binadamu bila ya kubaliwa. Isitoshe
ule utukufu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu aliompa
mwanadamu katika kauli yake : "NA HAKIKA
TUMEWATUKUZA WANADAMU …" [17:70]. Huu ni
utukufu aliozawadiwa mwanadamu yoyote bila ya
kuangalia ni mwanamume au mwanamke, wote
wanashirikiana kwa usawa katika utukufu huu.
Qur-ani Tukufu inapomzungumzia mtu au wanadamu,
basi huwa inamkusudia mwanamume pamoja na
mwanamke. Ama inapotaka kumtaja mwanamume au
mwanamke peke yake bila ya kumhusisha mwenzake
basi hutumia istilahi "wanamume" au
"wanawake".
Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
anazidi kuudhihirisha ulimwengu nafasi aliyonayo
mwanamke katika mfumo huu sahihi wa maisha
(Uislamu). Anatuonyesha uhusiano uliopo baina ya
mwanamume na mwanamke katika kauli yake:
"Wanawake ni ndugu baba mmoja, mama mmoja
na wanamume, wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa
na wanamume) kama ile haki iliyo juu yao
kuwafanyia wanamume" Abu Dawoud. Istilahi
ya ndugu baba mmoja, mama mmoja aliyoitumia
Bwana Mtume inatoa sura kamili ya usawa baina ya
mwanamke na mwanamume.
Kwa jicho la mfumo kamili huu wa maisha
(Uislamu) wanamume na wanawake kiasili ni sawa
sawa bila tofauti yeyote mbele ya Mola wao. Ila
tofauti na ubora utajitokeza katika amali njema
anazozifanya kila mmoja wao, ni dhahiri kuwa
mzuri na mwingi wa amali njema hawezi kulingana
sawa na mchache wa amali njema bila ya kuangalia
ni mwanamume au mwanamke, hii ndio mojawapo wa
misingi na kanuni za Uislamu. Tusome kwa
mazingatio na kutafakari : "WAFANYAJI MEMA,
WANAMUME AU WANAWAKE, HALI YA KUWA NI WAISLAMU,
TUTAWAHUISHA MAISHA MEMA NA TUTAWAPA UJIRA WAO
(Akhera) MKUBWA KABISA KWA SABABU YA YALE MEMA
WALIYOKUWA WAKIYATENDA" [16:97]. Uislamu
unazidi kumthibitishia na kumuhakikishia
mwanamke nafasi ya usawa kwa kumpa fursa sawa ya
kukubaliwa na kujibiwa dua sawa sawa/sambamba na
mwanamume bila ya kupoteza amali zake njema.
Hili linathibitishwa na Qur-ani Tukufu :
"MOLA WAO AKAWAKUBALIA (maombi yao kwa
kusema) HAKIKA MIMI SITAPOTEZA JUHUDI (amali) YA
MWANAMUME AU MWANAMKE (kwani nyinyi) NI NYINYI
KWA NYINYI …" [3:195].Muundo wa maelezo
ya Qur-ani Tukufu NI NYINYI KWA NYINYI
unatufahamisha kuwa kuna hali ya kutegemeana
baina ya mwanamume na mwanamke na kwamba maisha
ya kila mmoja wao hayakamiliki bila ya
kushirikiana na mwenziwe.
Uislamu unauthamini mchango wa mwanamke
katika jamii, ndio maana ukampa nafasi na haki
sawa ya kushiriki katika vitakatifu vya kidini
"Jihadi" sambamba na mwanamume. Katika
medani ya vita kuna watakaokufa mashahidi, kuna
majeruhi, wapiganaji ni wanadamu wanahitaji
huduma ya maji na chakula. Nani atakayetoa
huduma hizi ili kuipa ushindi dini ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu ? Hapo ndipo unapoonekana umuhimu
wa mchango wa mwanamke katika kuipigania dini ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni kutokana na sababu
hii na nyinginezo ndio tunamkuta Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – alikuwa haendi
katika vita vyovyote ila ataambatana na
wanawake. Bibi Umayyah bint Qays ni mwanamke
anayetajwa sana katika vitabu vya historia ya
Uislamu kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa
katika vita vya Khaybar. Kwa kuuona na
kuuthamini mchango wa bibi huyu, baada ya
kumalizika vita hivi Bwana Mtume – Rehema na
Amani zimshukie – alimtunukia kidani
alichokivaa maisha yake. Alipokurubia kufa
aliusia azikwe pamoja na kidani chake – Allah
amuwie radhi -. Mwanamke huyu na wale wote
watakaomuiga wanaingia katika kauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu : "LAKINI MTUME NA WALE
WALIOAMINI PAMOJA WALIIPIGANIA (dini) KWA MALI
ZAO NA NAFSI ZAO; NA HAO NDIO WATAKAOPATA KHERI;
NA HAO NDIO WENYE KUFUZU (kufaulu) . ALLAH
AMEWATENGENEZEA MABUSTANI YAPITAYO MITO MBELE
YAKE, WAKAE HUMO. HUKO NDIKO KUFUZU
KUKUBWA" [9:88-89]
Kadhalika Uislamu haukumuacha nyuma mwanamke
katika uwanja wa elimu bali umemshirikisha
kikamilifu sambamba na mwanamke. Hili
linathibitishwa na kauli/agizo la Bwana Mtume
– Rehema na Amani zimshukie - :
"Utafutaji/Kutafuta elimu ni fardhi ya
lazima kabisa kwa kila muislamu mwanamume na
muislamu mwanamke". Utaona kupitia
agizo/kauli hii ya Bwana Mtume, Uislamu
umewajibisha mwanamke apate elimu.
Hivi baada ya haki hizi za msingi alizopewa
mwanamke wa Uislamu, haki ambazo zinalindwa na
kusimamiwa na sheria madhubuti, kuna mtu
muadilifu atakayefunua kinywa kipana na kudai
kuwa eti Uislamu unamdhulumu na kumkandamiza
mwanamke ?! Ndugu zanguni, ni lazima tukubali
kuwa hapa kuna mambo mawili; Uislamu kama dini
na mfumo sahihi wa maisha unaotawaliwa na sheria
ya Allah na upande wa pili kuna wanaoitwa
waislamu wanaitawaliwa na desturi/ada na
mwenendo mbaya dhidi ya mwanamke. Kwa hivyo ni
lazima tutofautishe baina ya vitu viwili hivi
kama kweli tu waadilifu.
Kelele hizi na wimbo huu wa kunyanyaswa,
kudhulumiwa na kunyimwa haki mwanamke zilizoenea
leo ulimwenguni kote ni kelele zipigwazo na
kambi za magharibi na mashariki. Hawa hawana
ushahidi wa kuyathibitisha madai yao haya bali
kwa makusudi mazima wanataka kuipaka matope dini
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; hawa ndio Mwenyezi
Mungu anataumbia : "WANATAKA KUZIMA NURU YA
ALLAH (Uislamu) KWA VINYWA VYAO; NA ALLAH
ATAKAMILISHA NURU YAKE IJAPOKUWA WASHIRIKINA
WATACHUKUWA" [61:8].
Tukifanya uchunguzi wa kiadilifu tutagundua
kuwa ustaarabu wa kimagharibi ndio unaomnyima
haki na kumdhulumu mwanamke. Ikiwa mwanamke
anapoolewa huko katika ulimwengu wa kwanza
(Ulaya) kwa watu walioendelea kama wanavyodai
ananyimwa hata haki ya kuitwa kwa jina la baba
yake mzazi bali ananasibishwa na familia ya mume
aliyemuoa. Kwa mfano mwanamke anayeitwa Vicky
James akiolewa na Michael Brown anaitwa Mrs
Vicky Brown. Ikiwa mwanamke huyu hapati haki ya
kuitwa kwa jina la baba yake aliyemzaa vipi
unamtazamia kupata haki nyingine katika jamii
hiyo ?! Katika Uislamu, mambo ni kinyume kabisa
na hivyo. Wakeze Mtume, ambaye kwa mujibu wa
imani ya kiislamu ndiye kiumbe bora kuliko wote
hawakupata kuitwa mathalan Bibi Muhammad bin
Abdillahi, bali waliitwa kwa majina ya baba zao,
kama Bibi Aysha binti AbuBakri, Hafsa binti
Umar, Zaynab binti Jahshi na kadhalika. Katika
hali kama hii utawasikia na kuwaona watu wenye
fikra lemavu waliorogwa na ukoloni mamboleo
wakisema : Tunataka kuwa kama watu wa Magharibi.
Huu ni udumavu wa fikra na mawazo. Hivi kumvua
nguo mwanamke na kumuacha uchi mbele ya
kadamnasi ya watu katika kile kinachoitwa
mashindano ya urembo, ndiko kumpa haki na uhuru
mwanamke ? Huu ndio ustaarabu na maendeleo
tunayotaka kuyaiga kutoka Magharibi ?! Je, kuja
nyumbani kijana wa kiume na kumpiga busu mtoto
wa kike mbele ya wazazi wake na kisha kumchukua
kokote atakako na kumrudisha wakati autakao kwa
madai ya uchumba na hili likapewa baraka zote za
wazazi wa binti. Kijana akishamtia binti mimba
amkimbie na kumuacha aubebe mzigo huo peke yake
na kwenda kwenda kumtafuta kimwana mwingine na
kustarehe naye na kuendeleza uchafu wake. Je,
huu ndio usawa, haki na uhuru anaopewa mwanamke
na ulimwengu wa magharibi na sisi tukataga
kuuiga kibubusabubusa ? Haya si maendeleo bali
maondoleo ya utu na maadili mema, na hizi ni
tabia na silka za kinyama si za kibinadamu hata
kidogo. Huu ndio ukweli, tukikubali au kukataa.
Uislamu haukuja kumdhulumu, kumuonea na
kumkandamiza mwanamke, bali umekuja kumkomboa
kutoka katika jahilia na kumpa haki zote
anazostahiki kuzipata kama binadamu. Hebu
tuhitimishe makala yetu haya kwa kuangalia mfano
hai huu ambao unatoa sura/picha ya uhuru kamili
ya kujieleza na kuchangia fikra aliopewa
mwanamke chini ya mfumo sahihi wa maisha
(Uislamu). Zama za ukhalifa(utawala) wa Sayyidna
Umar – Allah amuwie radhi – wanawake
walikuwa wakiwatoza wanamume mahari kubwa sana.
Hali iliyopelekea baadhi ya wanamume wenye
kipato duni kushindwa kuoa. Sayyidna Umar kama
kiongozi mkuu wa dola ile ya kiislamu aliliona
tatizo hili na kujiona kuwa anawajibika
kulitafutia ufumbuzi wa haraka. Akaamua kuitisha
mkutano wa hadhara na kupiga marufuku utozaji
mkubwa wa mahari na badala yake akaweka kiwango
maalum cha mahari. Hapo ndipo aliposimama
mwanamke mmoja na kusema : " Ewe Umar,
ikiwa Mwenyezi Mungu mwenyewe ameturuhusu
kuchukua mrundi wa mali (mali nyingi isiyo na
idadi) vipi leo wewe unatuzuia na kutupiga
marufuku kuchukua mali kidogo tu ? Hebu jaribu
kufikiri huyu ni kiongozi wa dola, anaambiwa
maneno hayo mbele ya watu na anayemwambia ni
mwanamke, unafikiri alichukua hatua gani ?
Sayyidna Umar aliuheshimu uhuru wa kujieleza na
haki ya kusikilizwa ya mwanamke huyu. Akasalimu
amri na kusema : Umar amekosea na mwanamke
amepatia. Je, ni haki gani zaidi ya hizi
tunataka apewe mwanamke ?! Hebu mchukue mwanamke
huyu na umlete katika jamii yetu ya leo. Je,
atathubutu kufungua kinywa chake na kumwambia
kiongozi/mtawala maneno hayo ya kumkosoa mbele
ya hadhira tena bila ya kuanza kwa kumuita
mtukufu/mheshimiwa raisi, akamuita kwa jina lake
tu, na kiongozi huyo akakiri mbele ya watu kuwa
kweli kakosea ?! Hebu tuache chuki zetu na
tujaribu kuwa waadilifu na wakweli ili tuweze
kuiona haki kuwa ni haki na kuifuata na kuiona
batili kuwa ni batili na tuiepuke.
|