Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

WAKATI WA MWANADAMU BAINA YA JANA, LEO NA KESHO ..... VI

 

Kimsingi wakati ambao mwanadamu anaishi ndani yake unagawanyika katika vigawanyo vikuu vitatu:-

  • wakati uliopita (jana),

  • wakati hadhiri/uliopo (leo), na

  • wakati mustakbali/ujao (kesho).

Watu katika mahusiano/mafungamano yao na wakati kupitia vigawanyo vyake hivi, wako katika makundi kadhaa. Kidesturi na kiuzoefu makundi haya husimama baina ya ncha mbili; ubadhirifu (utumiaji mbaya) na upotezaji wa wakati. Kwa mizani hii tunakutana na makundi yafuatayo:-

Makhadimu (watumwa) wa wakati uliopita.

Makhadimu wa hadhiri,

Makhadimu wa mustakbali, na

Wakatikati ambao hukipa kila kigawanyo cha wakati haki yake.

 

A: WENYE KUFUNGAMANA (MAKHADIMU) NA ZAMA ZILIZOPITA (JANA):

Ni ukweli usiopingika kwamba katika jamii zetu liko kundi la watu ambao hawajui katika zama (wakati) ila jana iliyopita tayari. Hawa kutokana na ufahamu wao huu wa wakati, huendelea kuishi katika wakati uliopita (jana) na hali ya kuwa tayari wamo katika hadhiri (wakati uliopo/leo). Hawashughuliki kabisa na leo yenye kushuhudiwa na viumbe wote, wala hawana khabari kabisa na kesho yenye kuwaita. Ni mamoja ikiwa ujana/ukale wao ni natija ya nafsi zao, au wameurithi kwa wahenga wao au unatokana na kaumu zao zilizopita. Kundi hili la makhadimu wa ukale/jana lina sura kadhaa:-

Hujifakharisha kwa yaliyopita wakiamini kufanya hivyo ni kuwaenzi wahenga wao. Lakini hufanya hivyo bila ya wao kuongeza jipya katika yale yaliyopita au wao kuleta ziada itakayoiunganisha jana ya wahenga wao na leo yao wao. Hawa ni watu ambao daima husikika wakisema: Tulikuwa bwana..., baba zetu na mababu zetu ndio walikuwa.... Wala huwasikii wakisema: Sisi tumefanya kadha au tumeanzisha kadha au tunasimamia kadha. Allah amrehemu yule aliyesema: “Kwa yakini kijana ni yule asemaye: Mimi ndiye. Wala kijana si yule asemaye: Baba yangu alikuwa”.

Hakuna anayekanusha wala kupinga kwamba mtu kujifakharisha na kujitukuza na wahenga wetu wema na kuyaenzi mambo yao mema ni jambo jema linalofaa kutendwa na kila mmoja wetu. Lakini swali linalojitokeza ni kuwa tujifakharishe na kuyaenzi vipi mema hayo? Je, kunatosha tu kusema babu zetu walikuwa au haya ni urithi wa babu zetu? Bila ya shaka fakhri na maenzi mazuri ni kuyakamilisha/kuyaendeleza yote mema waliyoyaanza na kutuachia. Na kuwaiga katika mambo ya kheri waliyokuwa wakiyafanya.

Huamini katika urithi wa wahenga. Watu hawa hudai utakatifu katika kila kilichoachwa na wahenga na kuona kuwa ni kosa kuufanyia uchunganuzi wenye kulenga kuyaendeleza yote yaliyo ya sawa na kuyaacha yasiyo ya sawa. Haya hutokana na kuamini kwamba daima zama zilizopita ni bora kuliko zama tulizomo leo. Na kwamba watu wa leo hawana kipya wanachoweza kukifanya ambacho hakikufanywa na waliopita. Hapa ni wajibu wetu kujua maana na eleweko la urithi/mirathi na kisha kuifanyia tathmini. Wako watu wanaoenda sambamba na eleweko la urithi kama lilivyo ndani ya Qur-ani Tukufu na Sunah. Waislamu hawana khiari katika kulazimikiana na kushikamana na eleweko hilo kwa mujibu wa imani yao: “HAIWI KWA MWANAMUME ALIYEAMINI WALA KWA MWANAMKE ALIYEAMINI, ALLAH NA MTUME WAKE WANAPOKATA SHAURI, WAWE NA KHIARI KATIKA SHAURI LAO...” [33:36]

Urithi kwa janibu ya ki-Mungu hauna nafasi ya kuwekwa katika mizani ya kupimwa au kusita katika ama kufuata au kutokufuata. Bali ni wajibu wa kila muislamu kulifuata kila lililoachwa na wahenga wetu wema (salafu) ambalo imethibiti kuwa latoka kwa Allah na Mtume wake. Ama janibu ya kibinadamu, hii ni wajibu kuiweka katika chekeche litakalochekecha na kuchuja baina ya likubaliwalo na Allah na Mtume wake na lisilokubaliwa. Katika mirathi hii ya kibinadamu yako mambo yanachukua sifa ya kitaifa na si ya kimataifa. Haya yatabeba chapa ya mahala husika na wala hayafai mahala pengine. Kadhalika yako ambayo yanayochukua chapa ya zama za zake na hayafai katika zama nyingine.

Huyafuata ya kale kwa kuiga tu bila ya kuwa na hoja za msingi ila kusema tu hivi ndivyo walivyokuwa/walivyofanya wazee wetu waliotangulia. Hawataki kabisa kuyatahini na kuyahoji ya wazee ili kujua haki na batili, uongofu na upotofu wake. Hawa msimamo wao ni msimamo wa mtu mwenye kupokea na kutekeleza/kufuata kama alivyopokea bila ya kuhoji usahihi au ubatili wake. Hawa ndio watu ambao Qur-ani Tukufu inasema juu yao: “NA WANAPOAMBIWA: FUATENI ALIYOYATEREMSHA ALLAH, HUSEMA: BALI TUTAFUATA YALE TULIYOWAKUTA NAYO BABA ZETU. JE, HATA KAMA BABA ZAO WALIKUWA HAWAFAHAMU CHO CHOTE WALA HAWAKUONGOKA (watawafuata tu)?” [2:170] Huu ndio msimamo/hoja walizokabiliana nazo Mitume wa Allah wakati wa kufikisha ujumbe wa Mola wao kwa waja wake. Hii ndio kaumu ya Nabii Huud-Amani ya Allah imshukie-inamuambia Mtume wao: “...JE, UMETUJIA ILI TUMUABUDU ALLAH PEKE YAKE NA TUYAACHE WALIYOKUWA WAKIYAABUDU BABA ZETU?...” [7:70] Na hivi ndivyo Thamudi walivyomwambia mtume wao Nabii Swaleh-Amani ya Allah imshukie: “ ...EWE SWALEH! BILA YA SHAKA ULIKUWA UNAYETARAJIWA (kheri) KWETU KABLA YA HAYA (sasa umeharibika). OH! UNATUKATAZA KUABUDU WALIOWAABUDU BABA ZETU?...” [11:62]

Na Nabii Ibrahimu-Amani ya Allah imshukie-alipoiambia kaumu yake: “...NI NINI MASANAMU HAYA MNAYAKALIA WAKATI WOTE (kuyaabudu)? WAKASEMA: TULIWAKUTA BABA ZETU WAKIYAABUDU (basi na sisi tunayaabudu)”. [21:52-53]

Na hivyi hivyo ndivyo kaumu ya Nabii Shuaib ilivyomwambia Mtume wao: “...EWE SHUAIB! SWALA ZAKO (zinakuzuzua sana)! ZINAKUAMRISHA (utuamrishe) TUYAACHE WALIYOKUWA WAKIYAABUDU BABA ZETU...” [11:87]

Hivi ndivyo Qur-ani Tukufu ilivyoikariri suna (mwenendo) hii na kuisajili: “NA KADHALIKA HATUKUPELEKA MUONYAJI KATIKA MJI WO WOTE ILA MATAJIRI WAKE WALISEMA: KWA YAKINI TULIWAKUTA BABA ZETU JUU YA DASTURI (zao makhsusi) NA HAKIKA SISI TUTAFUATA NYAYO ZAO”. [43:23]

Qur-ani Tukufu imeupinga uchovu na ugumu huu wa kiakili wa kundi hili la watu wa kufuata waliyoyarithi kutoka kwa baba (wazee) zao ufuataji mpofu. Qur-ani ikawarudi kama ifuatavyo: “...JE, HATA KAMA BABA ZAO WALIKUWA HAWAFAHAMU CHO CHOTE WALA HAWAKUONGOKA (watawafuata tu)? [2:170]

“...JE, HATA KAMA BABA ZAO WALIKUWA HAWAJUI KITU WALA HAWAKUONGOKA (watawafuata tu)?” [5:104]

“AKASEMA (huyo Mtume wao): HATA KAMA NAKULETEENI (dasturi) YENYE UWONGOFU BORA KULIKO MLIYOWAKUTA NAYO BABA ZENU (mtaendelea na dasturi ya wazee wenu)?...” [43:24]

Kadhalika waliomo katika zama za leo lakini wao wanaishi katika zama zilizopita. Hawa ni wale wanaouonea majonzi na majuto wakati uliokwishawapita tayari, daima husikika wakisema: Laiti ningefanya/nisingefanya kadha, lau ningelifanya kadha ingelikuwa kadha. Aina hii ya fikra/hisia humtia mtu katika utumwa wa huzuni kuu na kumfanya aishi katika uchungu unaomkosesha raha na furaha. Aishi katika masumbuko ya moyo yasiyo na sababu, masumbuko ambayo pengine yakamsababishia maradhi ambayo yakawa ndio sababu ya mauti yake. Ni kwa kuyazingatia na kuyajua haya ndio wenye hekima wakasema: “Kuyashughulikia yaliyofutu katika wakati uliopita ni kupoteza wakati wa sasa”. Si ajabu wala jambo la kushangaza Qur-ani Tukufu na Sunah kuupinga mwenedno na tabia hii. Allah Mola Mwenyezi anawaambia waislamu baada ya kusibiwa na yaliyowasibu katika vita vya Uhud: “ENYI MLIOAMINI! MSIWE KAMA WALE WALIOKUFURU NA WAKASEMA JUU YA NDUGU ZAO WALIPOSAFIRI KATIKA NCHI AU WALIPOPIGANA (wakafa): WANGALIKUWA KWETU WASINGALIKUFA WALA WASIMGALIUAWA. (Allah amewatia dhana hii) ILI AFANYE HAYO KUWA MAJUTO KATIKA NYOYO ZAO...” [3:156]

Nae Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Muumini mwenye nguvu ni mbora na anapendeza zaidi mbele za Allah kuliko muumini dhaifu. Na kila mmoja yuna kheri (yake), pupia (kufanya) yatakayokunufaisha na umtake msaada Allah. Na (kamwe) usiwe na ajizi na wala usiseme: Lau mimi ningelifanya kadha ingelikuwa kadha. Lakini (wewe) sema: (Hivi ndivyo) alivyokadiria Allah na alitakalo (Yeye) huwa/hulitenda. Kwani (neno) ‘LAU’ hufungua amali ya shetani”. Muslim



Forum | Guestbook | Tuandikie |