Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

UTARATIBU WA MAISHA YA KILA SIKU YA MUISLAMU...V.     Inaendelea

 

ALASIRI (JIONI):

Unapoingia wakati wa Alasiri na muadhini akalingana na kunadi: Haya njooni kuswali. Hapo muislamu huamka kutoka katika mapumziko ya mchana kama alikuwa amelala. Au ataacha kazi yake kama alikuwa kazini, akichapukia msikitini kuswali swala ambayo huzingatiwa kuwa ni ‘Swala ya kati na kati’ ya siku. Hakujuzu kwa muislamu kuipuuzia swala hii bali na swala nyingine zote kwa kisingizio cha kubanwa na kazi. Akajipa uhalali na kibali cha kuendelea na kazi/biashara na kuacha kuuitikia wito wa swala uliogonga ngoma za masikio yake na kupenya mvunguni mwa moyo wake. Wasifu wa waumini wa kwelikweli ni kama alivyoueleza Allah Mola Mtukufu ndani ya kitabu chake kitukufu kwamba ni: “WATU AMBAO BIASHARA WALA KUUZA HAKUWASHUGHULISHI (hakuwasahaulishi) KUMKUMBUKA ALLAH, NA KUSIMAMISHA SWALA NA KUTOA ZAKA. WANAIOGOPA SIKU AMBAYO NYOYO ZITADAHADARI NA MACHO (pia yatadahadari)” [24:37]

Haifai kabisa kwa muislamu kuiakhirisha swala ya Alasiri kwa uzembe tu mpaka jua likapiga umanjano na kuelekea kuzama. Hiyo ni swala ya wanafiki kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hiyo ni swala ya mnafiki, hiyo ni swala ya mnafiki achungae (afuatiliaye) mionzi ya jua hata linapokuwa (jua) baina ya pembe mbili za shetani. (Hapo ndipo) huinuka na kuidonoa swala (rakaa) nne, hamdhukuru Allah ndani yake ila kidogo tu”. Muslim

 

MAGHRIBI:

Jua linapotua na kuzama, muislamu huharakia kwenda kuswali swala ya maghribi katika wakati wake wa mwanzo. Muislamu hufanya hivi kwa kuzingatia udhiki wa wakati wa swala hii ya maghribi. Akimaliza kuiswali swala hii ya fardhi sambamba na suna zake andamizi, husoma kiasi kimkinikacho cha nyiradi na dhikri za jioni zilizopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah. Kisha muislamu hula chakula chake cha usiku bila ya israfu wala kujidhili. Halafu tena huswali swala ya Ishaa pamoja na suna zake zote na huiakhirisha suna ya Witri kama ana mazoea ya kuamka usiku kuswali. Na iwapo hana mazoea hayo huiswali kabisa kabla ya kulala. Na pengine muislamu anaweza kuakhirisha kula chakula chake cha usiku mpaka baada ya kuswali swala ya Ishaa. Ni sawa kufanya hivyo ila tu kama kitawekwa chakula sambamba na kuingia wakati wa swala, hapo atatakiwa kula kwanza kisha ndio aswali kama ilivyokuja katika hadithi ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Itakapokimiwa swala na ikahudhuria ‘Ashaa’-(chakula cha usiku), basi anzeni na hiyo Ashaa”. Bukhaariy & Muslim.

Falsafa na hekima ya kauli hii ya Mtume inayotupa fursa ya kukitanguliza chakula juu ya swala ni kumfanya muislamu aswali bila ya moyo wake kushughulishwa na kitu kingine zaidi ya kunong’ona na Allah Bwana Mlezi wake. Kabla ya kulala muislamu anaweza kukidhi baadhi ya haki, mithili ya ziara fupi kwa ndugu, jamaa na marafiki bila ya kuwasahau majirani. Kadhalika kunampasa muislamu kujipangia utaratibu wa kujisomea kila siku kwa lengo la kujiongezea maarifa yake kama Allah alivyomwambia Mtume wake: “...NA (uombe) USEME: MOLA WANGU NIZIDISHIE ELIMU” [20:114]

Kauli hii ya Allah kwa Mtume wake kama inaashiria jambo, basi jambo hili halitakuwa jingine bali ni kumtaka muislamu awe na njia na utaratibu ambao utamuhakikishia kuzidi kielimu siku hata siku. Na ni vema kwake yeye ikiwa atateua kujisomea vitabu na magazeti/majarida yatakayomnufaisha katika dini na dunia yake.

Si dhambi na wala si hatia kwa muislamu kuistarehesha nafsi yake kwa burudani, michezo na pumbao za halali katika sehemu ya kipindi cha mchana au usiku. Kwa sharti kwamba burudani yake hiyo isichupe mipaka kiasi cha kumfanya kuipoteza:-

Haki ya Mola wake katika ibada, au

Haki ya jicho lake kaitka kulala, au

Haki ya mwili wake katika kupumzika, au

Haki ya familia yake katika uangalizi na usimamizi, au

Haki ya kazi yake katika tija na ufanisi, au

Haki miongoni mwa haki za watu wengine.

 

Kadhalika si wema na wala si uwalii na Ucha-Mungu kwa muislamu kukesha sehemu kubwa ya usiku au kila usiku mpaka akakosa nishati (nguvu) ya kutekeleza baadhi ya haki zinazompasa na kumuwajibikia. Muislamu hatakiwi kukesha usiku kucha kuswali, halafu asubuhi akawa anasinzia kazini na kushindwa kuyatekeleza vema majukumu yake. Bali anatakiwa kuwa na mizani sawa baina ya amali zake, asipunje au kuzidisha upande mmoja. Hili linatokana na falsafa ya mizani kwamba kuzidisha upande mmoja wa kitanga cha mizani kunamaanisha kupunja upande wa pili wa mizani hiyo hiyo. Na kufanya hivyo ni kuikhalifu amri ya Mwingi wa rehema (Allah) iliyomo ndani ya kitabu chake kitukufu: “ILI MSIDHULUMU KATIKA KUPIMA (na mengineyo). BASI PIMENI KIPIMO KWA HAKI WALA MSIPUNGUZE MIZANI”. [55:8-9]

Na katika jumla ya mambo ambayo muislamu ni wajibu wake kuyakumbuka na wala asiyasahau katika kila siku inayompitia, ni haki ya jamii. Hii ni haki ambayo Allah Mola Mwenyezi ameiamrisha katika kitabu chake aliposema: “MUABUDUNI ALLAH NA WALA MSIMSHIRIKISHE NA KITU CHO CHOTE. NA WAFANYIENI IHSANI WAZAZI WAWILI, NA JAMAA NA MAYATIMA NA MASIKINI NA JIRANI WALIO KARIBU NA JIRANI WALIO MBALI, NA RAFIKI WALIO UBAVUNI (mwenu) NA MSAFIRI ALIYEHARIBIKIWA NA WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YENU YA KULIA. BILA SHAKA ALLAH HAWAPENDI WENYE KIBURI WAJIVUNAO”. [4:36] Ya mwanzo na kubwa ya haki zote ni haki ya Allah Mola Mtukufu, Muumba viumbe, Mmiliki wa vyote, Mtoa bure uhai na Mwenye neema zote: “NA NEEMA YO YOTE MLIYONAYO, BASI IMETOKA KWA ALLAH...” [16:53] Basi hakumuhalalikii muislamu ye yote awaye kughafilika na kuzembea katika kuitekeleza haki ya Allah. Na ya mbele katika haki za kila siku za Allah ni swala, swala ambayo Allah ameufanya wasifu wa mwanzo wa waumini ni kunyenyekea ndani yake: “HAKIKA WAMEFUZU WAUMINI. AMBAO KATIKA SWALA ZAO HUWA WANYENYEKEVU”. [23:1-2] Na wasifu wao wa mwisho ni kuihifadhi swala: “NA AMBAO SWALA ZAO WANAZIHIFADHI” [23:9]

Na akawafaradhishia jangwa la moto/adhabu kali wale wote ambao huipuuza swala mpaka ukawafutu wakati wake maalumu uliowekwa na sheria: “BASI ADHABU KALI ITAWATHIBITIKIA WANAOSWALI. AMBAO WANAZIAKHIRISHA SWALA ZAO (wakaziswali nje ya wakati wake)”. [108:4-5]

Baada ya haki ya Allah na ya Mtume wake, haki inayofuatia ni haki ya wazazi wawili; baba na mama. Haki hii ya kuwatendea wema wazazi katika kitabu cha Allah imekuja ikiiandamia ‘Tauheed’-(kumpwekesha Allah) na mahala pengine ikiiandamia ‘Ikhlaaswi’-(kufanya ibada kwa ajili ya Allah tu). Ikiwa kuja kwa haki hii kwa mtiririko huu kunaashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa ila ni kuonyesha uzito wa haki ya wazazi wawili. Kwamba hakuna haki iliyo juu ya haki ya wazazi baada ya haki ya Allah na Mtume wake. Na kati ya haki za wazazi wawili, Qur-ani Tukufu na suna toharifu zinampa mama umuhimu na upendeleo wa pekee kuliko baba. Hili linatokana na majukumu mazito anayoyabeba yeye kama mama kwa watoto na mke kwa mume. Majukumu ambayo hayawezwi kubebwa na mwingine ye yote ila yeye pekee. Sehemu ya majukumu hayo mazito ni pamoja na taabu na adha zinazomsibu tangu kutunga kwa mimba, kujifungua na kulea: “...MAMA YAKE AMECHUKUA MIMBA YAKE KWA TAABU NA AKAMZAA KWA TAABU. NA KUBEBA MIMBA YAKE HATA KUMUACHISHA ZIWA (uchache wake) NI MIEZI THALATHINI...” [46:15]

Baada ya haki ya wazazi, inayofuatia ni haki ya jamaa. Jamaa zako kiislamu ni pamoja na nduguzo wa kiume na wale wa kike (kaka na dada zako), maami (baba wakubwa na wadogo), mashangazi, wajomba, makhalaati (mama wakubwa na wadogo). Na watoto wa wote hawa tuliowataja na baki ya ndugu wengine wa nasabu (damu). Kisha zinaandamia haki za wanyonge na wasiojiweza katika jamii, hawa ni pamoja na mayatima, masikini na wasafiri walioharibikiwa safarini. Halafu tena ndio zinafuatia haki za jirani wa karibu na yule wa mbali na rafiki wa ubavuni. Huyu ni yule unayesuhubiana naye pamoja ama mjini ama safarini kwa wasifu wa kudumu au wa muda maalumu. Na anaingia chini ya tafsiri hii ya ‘rafiki wa ubavuni’, mke kwa mumewe na mume kwa mkewe. Ya mwisho ya haki hizi ni haki ya ‘milki ya kuumeni’ : “...NA WALE ILIYOWAMILIKI MIKONO YENU YA KULIA (kuume)...” Haki hii katika aya hii ijapokuwa inamuelekea moja kwa moja mtumwa na uwajibu wa kumtendea wema katika zama zile za utumwa. Lakini aya hii kwa kuzingatia ‘ueneaji wa tamko lake’ inakikusanya na kukichanganya kila kilicho chini ya milki ya mtu. Hapo ndipo wanapoingia watumishi wa majumbani, waajiriwa wa maofisini na mashambani, na zana na vitendea kazi vyote. Wote na vyote hivi anaamrishwa kuvitendea wema kwa kuvihifadhi, kuvichunga dhidi ya madhara au uharibifu wo wote ule.

KULALA:

Sasa ni wakati wa kulala baada ya kuikamilisha ratiba hiyo ya kutwa nzima. Muislamu anapotaka kulala, ni suna atie udhu na kuswali rakaa mbili. Kisha ndipo apande kitandani kwake akilalia ubavu wake wa kulia, ilhali anamdhukuru Allah kwa dhikri zilizopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mithili ya kauli yake Bwana Mtume: “BISMIKA RABBIY WADHWA’ATU JANBIY, WABIKA ARFA’UHU, IN AMSAKTA NAFSIY FAGHFIR LAHAA, WA IN ARSALTAHAA FAHFADHW-HAA BIMAA TAHFADHWU BIHII ‘IBAADAKAS-SWAALIHIYN” Na nyinginezo nyingi mithili ya hii. Ni muhimu muislamu akavisoma vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni wetu katika uwanja wa kauli na amali za kidini anazotakiwa kuzifanya asubuhi, jioni na usiku. Tunamshauri pamoja na vitabu vinginevyo, kusoma vitabu vifuatavyo:-

‘Amalul-yaumi wal-laylah : Imamu Nasaai

Al-adhkaar : Imamu Nawawiy

Al-hiswnul-haswiyn : Ibn Al-jazariy.

 

Ndugu mpenzi msomaji wetu, kwa faida yako ili uzijue vema ‘haki jamii’, rejea darsa zetu za HAKI NA WAJIBU katika somo la AKHLAAQ. Kadhalika kwa ufafanuzi wa taratibu za kulala, tunakushauri urejee somo la ‘ADABU ZA KULALA’ katika mada ya Akhlaaq.



Forum | Guestbook | Tuandikie |