|
Muislamu akitaka
kubarikiwa katika umri wake, basi hana budi kuishi kwa kuufuata utaratibu
wa maisha ya kila siku kama ulivyo katika mfumo safi na sahihi wa maisha
(Uislamu). Utaratibu huu chini ya mfumo huu, unamtaka muislamu kuamka na
kulala mapema kama hana la muhimu la kumshughulisha wakati huo. Siku kwa
muislamu huanza mapema tangu kuchomoza kwa alfajiri au kwa uchache kabla
ya kuchomoza kwa jua. Kwa utaratibu huu wa kuamka mapema, muislamu
huipokea asubuhi yake hali ya kuwa ni twahara safi kabla haijachafuliwa na
pumzi za wenye dhambi, ambao hawaviachi vitanda vyao ila jua la saa nne
saa sita. Utaratibu huu humpa muislamu fursa ya kuipokea siku yake na
‘umapema’ ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliuombea
umati wake baraka ndani yake: “Ewe Mola wa haki wee! Ubarikie umati
wangu katika mapema yao”. Ahmad, Ibn Hibbaan, Al-Haakim, Ibn Maajah
& wengineo.
Miongoni mwa
maafa/mabalaa waliyotahiniwa nayo waislamu wa leo ni pamoja na kubadilisha
kwao utaratibu wa siku yao. Leo utawashuhudia waislamu wakikesha katika
luninga (televisheni) zao mpaka usiku mwingi. Kisha ndipo hupanda
vitandani wakakoroma mpaka swala yenye fadhila kubwa (Sub-hi) ikawapita.
Swala ambayo Allah anaielezea: “...NA (msiache) QUR-ANI YA (swala ya)
ALFAJIRI. HAKIKA (kusoma) QUR-ANI KATIKA (kuswali swala ya) ALFAJIRI
KUNAHUDHURIWA (na Malaika)”. [17:78]
Mmojawapo wa wahenga
wetu wema (salafu)-Allah awarehemu-alipata kusema: “Ninamstaajabia mtu
mwenye kuswali (swala ya) Sub-hi baada ya kuchomoza jua, vipi
ataruzukiwa!” Imepokewa na Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa
Mutme wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Shetani hufunga
kichogoni kwa mmoja wenu anapolala mafundo matatu, hupiga chapa katika
kila fundo: Uwe juu yako usiku mrefu, lala. Akiamka akamdhukuru Allah,
hufunguka fundo moja na akitawadha (kwa ajili ya swala) hufunguka fundo la
pili. Na akiswali, hufunguka mafundo yote matatu, basi akaamka akiwa
mchangamfu mwenye nguvu na mwema wa nafsi. Na kama hakufanya hivyo
atapambaukiwa akiwa mbaya wa nafsi na mvivu”. Bukhaariy
Huu ndio muongozo wa
kufuatwa na kila muislamu kwa maslahi na manufaa yake. Muislamu huianza
siku yake kwa kumtii Allah kwa kuswali swala ya fardhi na suna. Kwa kusoma
nyiradi za asubuhi zilizopokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-mithili ya nyiradi hizi: ASW-BAHANAA WA ASW-BAHAL-MULKU LILLAAH,
WAL-HAMDULILLAAH, LAA SHARIYKA LAHUU, LAA ILAAHA ILLAA HUWA, WA
ILAYHIN-NUSHUUR” . “ALLAAHUMMA MAA ASW-BAHA BIY MIN-NI’IMATIN AU
BIAHADIN MIN KHALQIKA FAMINKA WAHDAKA LAA SHARIYKA LAKA, FALAKAL-HAMDU
WALAKAS-SHUKRU”. “ALLAAHUMMA INNIY ASW-BAHATU MINKA FIY NI’IMATIN WA
‘AAFIYATIN WASITRI, FAATIM NI’IMATAKA ‘ALAYYA WA ‘AAFIYATAKA
WASITRAKA FID-DUNIYAA WAL-AAKHIRAH”. Kisha asome Qur-ani Tukufu kiasi
cha uwezo wake, ayasome maneno matukufu ya Mola wake kwa unyenyekevu
mkubwa, ufahamu wa maana na huku akileta mazingatio: “(Na hiki) KITABU;
TUMEKITEREMSHA KWAKO, CHENYE BARAKA NYINGI, ILI WAPATE KUZIFIKIRI
(kuzizingatia) AYA ZAKE NA WENYE AKILI WAWAIDHIKE”. [38:29] Halafu tena
ndipo apate kifungua kinywa chake kwa wastani bila ya kushiba kupita
kiasi. Akimaliza ndipo aelekee kazini kwake kwa ajili ya ibada ya kutafuta
riziki yake ya halali, kwani muislamu hali bila ya kufanya kazi. Muislamu
anatakiwa kuizingatia kazi yake kuwa ni sehemu ya ibada aliyoumbiwa au kwa
maneno mengine ni sehemu isiyotengeka ya dini yake. Ibada hii ya kutafuta
riziki yake ya halali isimsahaulishe kumdhukuru Allah Mola Mtoa riziki
anayoitafuta kila unapoingia wakati wa swala. Kazi hii muda wa kuambiwa
kuwa ni ibada na ni ibada kweli inayompatia thawabu ikiwa ni ya halali na
kinyume chake pia kinafanya kazi, isiwe ni kisingizio cha kuacha swala
kama ibada mama, bali kwa muumini mkamilifu wa imani ni kazi na swala. Na
katika huko kufanya kazi, muislamu anatakiwa kuifanya kazi yake kwa
ukamilifu na uaminifu utakaoleta tija ili kufikia ufanisi na kupata
matunda halali ya jasho lake. Ukamilifu na ufanisi kazini ni fardhi kwa
muislamu kama alivyoambiwa na Mtume wake-Rehema Amani zimshukie: “Kwa
yakini Allah anapenda anapofanya kazi mmoja wenu, (aifanye kwa) ukamilifu
(ufanisi na ustadi)”. Al-Baihaqiy, Abuu Ya’alaa & Ibn ‘Asaakir.
Katika jumla ya
wajibu na majukumu ya kila siku ya muislamu ambayo hakumjuzii kuyasahau au
kuzembea kuyatekeleza ni wajibu wa utumishi wake kwa jamii yake. Na
kuisaidia kwa namna moja au nyingine kufikia malengo na haja zao.
Autekeleze wajibu wake huu kwa moyo mkunjufu huku akiamini kuwa hiyo ni
sadaka. Imepokelewa na Abuu Muusa-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Kunamlazimu kila muislamu (kutoa)
sadaka, (maswahaba) wakamuuliza: Ewe Mtume wa Allah je, kama hana (cha
kutoa sadaka)? Akajibu: “Afanye kazi kwa mkono wake ili ajinufaishe yeye
mwenyewe na atoe sadaka. Wakamuuliza (tena): Je, kama hakuweza (kufanya
kazi)? Akasema: “Amsaidie mwenye haja aombaye msaada. Wakauliza (tena):
Je, kama hakufanya hivyo? Akajibu: “Basi na aamrishe mema (huku
akiyatenda). Wakauliza (tena): Je, kama hakufanya hivyo? Akawajibu:
“Basi na ajizuie na shari (uovu), kwani hakika (kufanya hivyo) ni
sadaka”. Bukhaariy & Muslim
Sadaka hii au tuseme
kodi hii ya kijamii ni fardhi ya kila siku kwa kila muislamu. Kwa
kuitekeleza sadaka hii iliyofaradhishwa na Mtume wake, anakuwa ni chemchem
inayobubujisha kheri, manufaa na salama kwa jamii inayomzunguka.
Kadhalika
imepokelewa katika hadithi iliyotajwa na Abuu Hurayrah-Allah amuwiye
radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “ Kila
mfupa/maungio/kiungo cha watu kinalazimikiwa na sadaka katika kila siku
ichomozewayo na jua:
Kufanya uadilifu
baina ya wawili ni sadaka, na
Kumsaidia mtu katika
kipando chake (mnyama/gari n.k.) ukampandisha au ukampakilia mzigo wake
juu ya mnyama huyo ni sadaka, na
Neno jema (zuri) ni
sadaka, na
Kila khatua
unayopiga kwenda kuswali ni sadaka, na
Kuondosha adha
(chupa, jiwe, kinyesi n.k.) njiani ni sadaka”. Bukhaariy & Muslim
Kwa kuyafanyia kazi
maneno haya matukufu ya Mtukufu Mtume wetu kunampasa kila muislamu
kumshukuru Allah kwa neema hii ya mifupa na viungo alivyopewa. Aishukuru
neema hii kwa kuvitumia viungo na mifupa yake hiyo katika kumtii Mola wake
na kuwanufaisha waja wake kwa kuwatendea wema ulio ndani ya uweza wake.
MCHANA:
Sasa tayari ni
mchana na adhana ya adhuhuri inasikika na masikio ya kila muumini.
Muislamu anasimamisha kazi, anatika mbio kwenda kuitekeleza fardhi ya
swala kwani kaambiwa katika adhana (ALLAAHU AKBAR) yaani Allah ni Mkubwa
kuliko kila kitu, ikiwa ni pamoja kazi yake hiyo. Anajitahidi upeo wa
juhudi yake kuitekeleza fardhi ya swala kwa wakati wake uliowekwa na
sheria tena kwa jamaa. Muislamu anatakiwa kutambua kuwa wakati wa mwanzo
wa swala ni radhi za Allah na Allah ametuamrisha kushindana katika mambo
ya kheri. Ili kuusisitiza umuhimu wa swala ya jamaa, Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie-alikusudia kuzichoma moto nyumba za watu wanaochelewa
kuhudhuria swala za jamaa pamoja nae msikitini. Na katika kuonyesha ubora
na fadhila za swala ya jamaa, Bwana Mtume akasema kwamba swala ya jamaa ni
bora kuishinda swala ya mtu pweke kwa daraja ishirini na saba. Baada ya
swala, muislamu huenda kupata chakula chake cha mchana kabla ya kurejea
tena kazini. Chakula kitokanacho na vizuri vizuri alivyoruzukiwa na Allah
Mola Mwenye kuruzuku wema na waovu bila ya kubagua. Hula bila ya israfu
kiasi cha kuvimbiwa na kumfanya ashindwe kufanya kazi na badala yake alale
na kukoroma. Pia katika ulaji wake huu, muislamu hajidhiki kwa kula
chakula kidogo mno kisichokidhi mahitaji ya mwili wake na hivyo kumfanya
kukosa nguvu na nishati itakayomuwezesha kufanya kazi. Au akajidhiki kwa
kula chakula cha aina moja tu siku hata siku na kumfanya akose viinilishe
muhimu vinavyohitajiwa na mwili wake. Muislamu anatakiwa kufanya kazi kwa
juhudi, maarifa na ufanisi na ale, anywe, avae na aishi mahala pazuri
maadam tu hafanyi israfu na ubadhirifu anaouchukia Allah. Hebu na tuitegee
sikio la uzingativu kauli hii tukufu ya Allah: “ENYI WANADAMU! CHUKUENI
MAPAMBO YENU (vaeni nguo zenu nzuri mzipendazo) WAKATI WA KILA SWALA, NA
KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri). LAKINI MSIPITE KIASI TU, HAKIKA YEYE
(Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI (wabadhirifu). SEMA: NI NANI
ALIYEHARIMISHA MAPAMBO YA ALLAH AMBAYO AMEWATOLEA WAJA WAKE. NA (nani
aliyeharimisha) VITU VIZURI KATIKA VYAKULA? SEMA: VITU HIVYO
VIMEWAHALALIKIA WAISLAMU (hapa) KATIKA MAISHA YA DUNIA (na) VITAKUWA VYAO
PEKE YAO SIKU YA KIYAMA...” [7: 31-32]
Katika nchi za joto
au katika majira ya joto, watu huweza kuhitajia mapumziko kidogo ya
mchana. Mapumziko haya yanajulikana katika Uislamu kama
‘Qailuulah’-(siesta). Mapumziko haya yana msaada mkubwa katika
kusimama usiku kuswali na katika kuamka mapema. Qur-ani Tukufu
imeyaashiria mapumziko haya katika kauli tukufu ya Allah: “...NA
MNAPOVUA NGO ZENU ADHUHURI...” [24:58]
|