Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

WAKATI KATIKA MAISHA YA MUISLAMU

 

WAJIBU WA MUISLAMU KUELEKEA WAKATI….IV

vi) KILA WAKATI NA AMALI YAKE.

Inampasa muumini kujua linalotakiwa kutendwa katika wakati alionao; aliomo hivi sasa ndani yake. Je, ni wakati wa amali ya moyo, ulimi au viungo? Akishajua ni wakati wa amali gani kati ya hizo tulizozitaja, aipanie na kujitahidi kuitenda kiasi cha kuoana na makusudi yake na hivyo kuipa nafasi kubwa ya kuweza kukubaliwa mbele ya Allah.

Imekuja katika wasia wa Amirul-Muumini Abuu Bakri kwa Sayyidna Umar-Allah awawiye radhi-wakati anamuachia ukhalifa: “Tambua kwamba Allah anazo amali (anazotaka zitendwe) wakati wa mchana, hakubali (zitendwe) wakati wa usiku.”

Itakuwazikia basi, kwamba suala si mtu kufanya cho chote wakati wo wote, bali muhimu ni mtu kufanya amali munasibu katika wakati muafaka. Ni kutokana na ukweli huu kwamba kila wakati una amali yake inayonasibu kufanywa ndani yake. Tunamuona Allah ameziwekea nyakati maalum ibada nyingi, haijuzu kwa muumini kuzitenda kabla au baada ya nyakati hizo. Mathalan haisihi kufunga swaumu ya Ramadhani katika mwezi wa Dhul-Hijah kama ambavyo isivyosihi kufanya ibada ya Hijah katika mwezi wa Ramadhani, kwa sababu sio wakati wake uliowekwa na sheria. Allah ameyafanya haya kwa hekima na busara, miongoni mwa hekima za kuziwekea nyakati maalum kathiri (nyingi) ya ibada. Ni pamoja na kutufahamisha kwamba kitu/jambo/amali haikubaliwi kabla ya kuingia wakati wake wala baada ya kupita wakati wake. Allah Mola Mwenyezi amesema kuhusiana na suala la swala: “KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI.” (4:103)

Na akasema katika swaumu: “…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhan) NA AFUNGE…” (2:185)

Na katika Hijah akasema: “HIJA NI MIEZI MAALUM….” (2: 197)

Na katika zakah akasema: “…NA TOENI HAKI YAKE SIKU YA KUVUNWA KWAKE….” (6: 141)

Anasema mmoja miongoni mwa waja wa Allah wenye kuzijua neema na ihsani zake – Allah awarehemu: “Nyakati za mja ni nne hazina wa tano wake:

-Wakati wa neema,

-Wakati wa balaa (mitihani ya maisha),

-Wakati wa twaa, na

-Wakati wa maasi.

 

Na ana Allah juu yako katika kila wakati miongoni mwa nyakati hizi sehemu (hisa) ya uja/utumwa ambao ni haki yake kwako kwa mujibu wa hukumu ya ubwana/ulezi na uungu wake. Basi utakayekuwa wakati wake ni twaa, basi njia yake ni kushuhudia neema kutoka kwa Allah kumshukia yeye kwa kumuongozea katika twaa na kumuwafikisha kuitenda. Na utakayekuwa wakati wake ni neema, basi njia yake (ya kuidumisha neema hiyo) ni shukrani, nayo ni furaha ya moyo

kwa Allah. Na utakayekuwa wakati wake ni maasia, basi njia yake (ya kujinasua nayo) ni toba na Istighfaari. Na utakayekuwa wakati wake ni balaa (majanga) basi njia yake (ya kuyashinda) ni kuridhia (kuwa yanatoka kwa Allah) na kusubiri (faraja kutoka kwake).”

 

Maneno haya yenye thamani aliyoyasema mja huyu wa Allah aliyewafikiwa kuzijua neema na ihsani za Mola wake. Yanayaeleza na kuyatafsiri yaliyotamkwa na Qur-ani na Sunah katika safu (makamu) ya twaa, Allah Mola Mwenyezi

anasema: “SEMA:KWA FADHILA ZA ALLAH NA KWA REHEMA YAKE (ndiyo mumepata haya) BASI NA WAFURAHI KWA HAYO. HAYA NI BORA KULIKO HIVYO WANAVYOVIKUSANYA.” (10:58)

Na katika safu ya maasia anasema: “SEMA: ENYI WAJA WANGU MLIOJIDHULUMU NAFSI ZENU (kwa kutenda maasi)! MSIKATE TAMAA NA REHEMA YA ALLAH, BILA SHAKA ALLAH HUSAMEHE DHAMBI ZOTE (kwa mwenye kutubia na kutubu na kuleta Istighfaari ) HAKIKA YEYE NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU.” (39:53)

Na anasema katika safu ya balaa (majanga/misiba): “NA TUTAKUTIENI KATIKA MSUKOSUKO WA (baadhi ya mambo haya); KHOFU NA NJAA NA UPUNGUFU WA MALI NA WA WATU NA WA MATUNDA NA WAPASHE KHABARI NJEMA WANAOSUBIRI AMBAO UWAPATAPO MSIBA HUSEMA: HAKIKA SISI NI WAJAWA ALLAH NA KWAKE YEYE TUTAREJEA (atatupa jaza yake).” (2:155-156)

Ama katika Sunah, imepokelewa kwamba Mtume wa Allah– Rehema na Amani zimshukie–amesema: “Ajabu iliyoje kwa jambo la muumini, hakika jambo lake lote ni kheri na hilo halipatikani kwa ye yote ila kwa muumini tu. Ikimpata raha (la kufurahisha) hushukuru na ikawa ni kheri kwake na ikimpata taabu (la kuhuzunisha) husubiri na ikawa ni kheri kwake.” Muslim

 

vii). KUZENGEA NYAKATI BORA; ZENYE FADHILA.

Linalotakikana kufanywa na muislamu mwenye pupa ya kushindana katika mambo ya kheri ni kuzizengea nyakati bora. Nyakati ambazo Allah amezipendelea kuliko nyakati nyingine kwa kuzipa hadhi na heshima ya pekee ya

kiroho. Heshima na hadhi inayoainisha ubora na fadhila zake, kama ilivyopokewa katika hadithi: “Hakika yuna Mola wenu katika zama zenu vipawa, basi vizengeeni (vipawa hivyo)” Twabaraaniy

Ukhusishaji huu wa nyakati fulani kwa ubora na fadhila ni suala la kimungu, kwani Allah humkhusu (humtemshia) kwa rehema zake amtakaye na kwa akitakacho. Kama ambavyo Allah alivyowaboresha (alivyowafanya bora) baadhi ya waja wake zaidi kuliko wengine: “MITUME HAO TUME WAFADHILISHA (tumewaboresha) BAADHI YAO ZAIDI KULIKO WENGINE MIONGONI MWAO WAKO AMBAO ALLAH

ALISEMA NAO NA WENGINE AKAWAPANDISHA KATIKA VYEO

VIKUBWA KABISA…” (2:253)

Na akaziboresha baadhi ya sehemu katika ardhi yake zaidi kuliko sehemu nyingine. Kadhalika ameziboresha na kuzifadhilisha zaidi baadhi ya nyakati kuliko nyingine: “NA MOLA WAKO HUUMBA ATAKAVYO NA HUCHAGUA (atakavyo) HAWANA (viumbe) KHIYARI…..” (28:68)

Allah Mola Mwenyezi ameyafadhilisha katika usiku masaa (nyakati) ya maladaku (nyakati za kabla ya alfajiri). Haya ni masaa ya theluthi ya mwisho ya usiku, ambamo Allah hujidhihirisha kwa waja wake kila usiku kwa kuwashukia ushukaji unaolingana na dhati yake tukufu. Basi hunadi (hulingana): “Je, yuko mwenye kutaka maghfira (msamaha) nimghufirie? Je, yuko mwenye kutubu nimpokelee toba yake? Je, yuko mwenye kuomba (nimpe ambacho). Je, yuko mwenye haja (nimkidhie)? (Huendelea kunadi hivyo) mpaka

kuchimbuka (kuchomoza) kwa alfajiri”. Ahmad & Muslim

Kwa ajili hiyo Allah amewasifia waja wake wema wamchao kwa kusema: “KWA YAKINI WAMCHAO ALLAH WATAKUWA KATIKA MABUSTANI NA CHEMCHEM WANAPOKEA ALIYOWAPA MOLA WAO KWA HAKIKA WAO WALIKUWA WAKIFANYA WEMA KABLA YA HAYA. WALIKUWA WAKILALA KIDOGO TU USKU NA WAKIOMBA MAGHUFIRA (msamaha)

NYAKATI ZA KABLA YA ALFAJIRI.” (51:15-18) Nae Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie–anasema: “Wakati ambao Bwana Mlezi anakuwa karibu mno na mja wake ni ndani ya sehemu ya mwisho ya usiku. Basi ukiweza kuwa miongoni mwa wanaomdhukuru Allah katika nyakati hizo, basi kuwa (miongoni mwao).”

Tirmidhiy, Nasaai, Al-Haakim & wengineo

Na Allah ameichagua na kuifadhilisha zaidi siku ya Ijumaa miongoni mwa siku saba za juma. Siku hii ya Ijumaa ni Idi (siku kuu) ya juma kwa waislamu na ndani ya siku hii kuna fardhi ya swala ya Ijumaa. Swala ambayo kuwakusanya pamoja waislamu wa kitongoji fulani mahala pamoja. Ndani ya siku hii kuna muda maalumu (wa upendeleo) ambao hujibiwa maombi ya waombaji. Muislamu hausadifu muda huo akimuomba Mola wake jambo la kheri ila humpa. Imekuja katika hadithi: “Bora ya siku iliyochomozewa na jua ni siku ya Ijumaa…” Na ndani yake kuna muda ambao hausadifu mja muumini na il-hali yu ndani ya swala akimuomba Allah cho chote ila humpa kitu hicho.” Ahmad

Na katika siku za mwaka mzima, Allah ameyafadhilisha masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijah (Mfunguo tatu) kiasi cha kuyaapia: “NAAPA KWA ALFAJIRI. NA MASIKU KUMI (ya mwanzo ya Dhul-Hijah)”. [89:1-2]. Na bora ya masiku kumi haya ni ile siku ya Arafah (mwezi tisaa-Dhul-Hijah). Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas–Allah awawiye radhi: “Hapana miongoni mwa masiku (ya mwaka mzima) yapendezayo zaidi kwa Allah kufanya amali ndani yake kuliko masiku haya (kumi).” Maswahaba wakauliza: Ewe Mtume wa Allah wala kuliko kupigana jihadi katika dini ya Allah? Mtume akawajibu: “Wala jihadi katika dini ya Allah (hailingani na amali inayotendwa katika masiku haya kumi). Ila mtu atoke (katika njia ya Allah) kwa nafsi na mali yake (mwenyewe), na kisirejee cho chote katika hivyo (yaani afe shahidi)”. Bukhaariy.

Na katika miezi kumi na mbili inayofanya mwaka mmoja, Allah ameukhitari na kuufadhilisha mwezi wa Ramadhan. Huu ni mwezi ambao imeteremshwa Qur-ani Tukufu ndani yake ili iwe ni muongozo kwa watu wote na upambanuzi wa baina ya haki na batili. Mwezi ambao Allah amewafaradishia waja wake ibada ya funga (swaumu) na Mtume wake akawasunishia kisimamo cha usiku (tarawehe). Ndani ya mwezi huu kumependekezwa kukithirisha amali njema, za kheri. Kwa hivyo, basi mwezi huu ambao ni chaguo la Allah kwa waja wake waumini ni musimu wa kushindana katika mambo ya kheri kwa ajili tu ya kutaraji radhi za Allah. Imepokelewa kutoka kwa Ubaadah Ibn As-swaamit–Allah amuwiye radhi–kwamba Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie siku moja alisema wakati ulipoingia mwezi wa Ramadhani: “Imekujieni Ramadhan, mwezi wa baraka, Allah anakufunikeni ndani yake na kwa sababu hiyo rehema yake hukushushieni na madhambi huyapomosha (huyafuta). Huyajibu maombi yenu, Allah huyaangalia mashindano yenu (katika kheri na wema) ndani yake (mwezi huu) na hujifakharisha nanyi kwa malaika wake. Basi muonesheni Allah kheri katika nafsi zenu (kwa kutenda amali njema), kwani kwa yakini mtu muovu ni yule aliyenyimwa rehema za Allah Mtukufu ndani yake (mwezi huu).” Imani Suyuutw (Al-Jaamiul-Kabiyr). Mwezi mzima wa Ramadhan ni mwezi muhimu kwa muislamu, lakini sehemu yenye umuhimu zaidi kwa muislamu, kuliko nyingine ni ile theluthi yake ya mwisho, yaani kumi lake la mwisho. Umuhimu mkubwa wa kumi hili unatokana na mambo mawili ya msingi:-

-Kumi hili ndio mwisho wa mwezi huu mtukufu na kwa yakini amali zote huzingatiwa mwishoni na sio mwanzoni. Hili linatokana na imkani ya kuanza vema na kumaliza vibaya, kwa mantiki hii ndio ikawa mazingatio ya mambo/amali ni mwisho wake. Ni kwa kulizingatia na kulijua hili ndio ikawa katika jumla ya dua za Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-ni kauli yake: “Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba ujaalie bora (kheri) ya umri wangu mwisho wake, na bora ya amali zangu mwisho wake na bora ya siku zangu siku ya kukutana nawe.”

Kumi hili ndilo linalodhaniwa kuwemo ndani yake “Laylatul-Qadri.” Huu ni usiku ambao Allah Mola Mwenyezi ameufadhilisha zaidi kuliko miezi alfu moja na kutokana na ubora wake ukapewa sura kamili ndani ya Qur-ani Tukufu: “HAKIKA TUMEITEREMSHA (Qur-ani) KATIKA LAYLATUL– QADRI (usiku wenye heshima kubwa, usiku mwa mwezi wa Ramadhan). NA JAMBO GANI LITAKALOKUJULISHA (hata ukajua) NI NINI HUO USIKU WA LAYLATUL-QADRI? HUO USIKU WA HISHIMA (huo) NI BORA KULIKO MIEZI ELFU. HUTEREMKA MALAIKA NA ROHO (za viumbe watakatifu) KATIKA (usiku) HUO KWA IDHINI YA MOLA WAO KWA KILA JAMBO. NI AMANI (usiku) HUO MPAKA MAPAMBAZUKO YA ALFAJIRI.” (97:1-5)

Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akifunga kibwewe linapoingia kumi la mwisho (la Ramadhan) na kuuhuisha usiku wake. Na akiwaamsha wakeze (kufanya ibada) na alilikhusisha (kumi hili) na ibada ya Itikafu.

Na katika miezi kumi na mbili ya mwaka, Allah ameifadhilisha miezi mine mitukufu baada ya Ramadhan. Miezi minne hiyo ni Rajab, Dhul Qa’adah, Dhul-Hijah na Muharam. Tusome: “IDADI YA MEZI (ya mwaka mmoja) MBELE YA ALLAH NI MIEZI KUMI NA MBILI KATIKA ILIMU YA ALLAH (mwenyewe tangu) SIKU ALIPOUMBA MBINGU NA ARDHI KATIKA HIYO IMO MINNE ILIYO MITUKUFU KABISA (nayo ni Rajabu, Mfunguo pili, Mfunguo tatu na Mfunguo nne)…” (9:36)



Forum | Guestbook | Tuandikie |