Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

WAKATI KATIKA MAISHA YA MUISLAMU

 

WAJIBU WA MUISLAMU KUELEKEA WAKATI….IV

III/. KUYAENDEA HARAKA MAMBO YA KHERI.

Linalofaa na kunasibu kutendwa na muumini baada ya kujua thamani na umuhimu wa wakati ni pamoja na kuutumia wakati wake katika kufanya mambo mbali mbali ya kheri (mema). Ahakikishe kuwa wakati wake unatumika katika mambo yote ambayo manufaa na maslahi yake yatamrejea yeye binafsi kama mtendaji. Bila ya kuinyima manufaa hayo familia na jamii yake kwa ujmla leo ulimwenguni na kesho mbele ya Allah Mola Mwenye khabari za yote tuyatendayo ya dhahiri na siri. Muislamu ayatende mambo ya kheri bila ya kuhitaji msukumo utokao nje yake bali ajitume yeye mwenyewe kutokana na manufaa ya mambo hayo. Autupilie mbali uvivu na ajizi ya kuakhirisha jambo la leo ili alifanye kesho au kufanya mambo nusunusu bila ya ukamilifu. Miongoni mwa dua na dhikri ambazo Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ameufundisha umati wake kuzisoma asubuhi na jioni ni pamoja na: “Ewe Mola wa haki wee! Hakika mimi ninakuomba unikinge na wasiwasi wa moyo (hammu) na huzuni na unikinge na ajizi na uvivu”. Kuyaendea haraka mambo ya kheri ni amri ya Allah kama ilivyokuja ndani aya Qur-ani Tukufu: “NA KILA UMA ULIKUWA NA QIBLAH WALICHOKIELEKEA. BASI JITAHIDINI KUFANYA MEMA...” [2:148]

Kadhalika Allah anawaambia watu wa kitabu: “...NA KAMA ALLAH ANGALITAKA ANGEKUFANYENI KUNDI MOJA (la kufuata sharia moja), LAKINI ANATAKA KUKUJARIBUNI KWA HAYO ALIYOKUPENI. BASI SHINDANENI KATIKA KUYAFIKILIA MAMBO YA KHERI. NYINYI NYOTE MARUDIO YENU NI KWA ALLAH...” [5:48]

Allah Mola mwenye shani akaendelea kusema katika kuraghibisha pepo na neema zake zilizomo humo: “NA YAENDEENI UPESI UPESI MAGHUFIRA YA MOLA WENU NA PEPO (yake) AMBAYO UPANA WAKE (tu) NI (sawa na) MBINGU NA ARDHI. (Pepo) ILIYOWEKEWA WAMCHAO ALLAH”. [3:133]

Katika aya hizi na zenye kushabihiana nazo, Allah anawaamrisha waja wake kuyashindania na kuyaendea haraka maghufira (msamaha wa dhambi) yake na pepo yake. Yaani washindane na kuharakia kuziendea sababu zitakazowadhaminia kupata maghufira na pepo ya Mola wao. Na sababu hizi si nyingine bali ni imani thabiti, ucha-Mungu na amali njema, na kushindana katika mambo haya ni jambo jema linalotakiwa kuazimiwa na kila muislamu: “...NA KATIKA (kupata) HAYA WASHINDANE WENYE KUSHINDANA”. [83:26]

Katika ushindani huu wa kheri, Allah amewasifia baadhi ya mitume wake kwa kauli yake: “...BILA SHAKA WAO WALIKUWA WEPESI WA KUFANYA MEMA NA KUTUOMBA KWA SHAUKU NA KHOFU NAO WALIKUWA WAKITUNYENYEKEA”. [21:90]

Na akawasifia watu wema katika Ahlul-Kitaab kwamba wao: “WANAMUAMINI ALLAH NA SIKU YA MWISHO NA WANAAMRISHA MEMA NA WANAKATAZA MAOVU NA WANAYAENDEA MBIO MAMBO MEMA. NA HAO NDIO MIONGONI MWA HAO WATENDAO MEMA (kweli kweli)”. [3:114]

Kwa janibu yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakuacha kuuamrisha umati wake kutenda amali njema haraka haraka kabla ya kukosa nafasi kutokana na kushughulika mno, akasema: “Hamngojei nyinyi ila utajiri unaomfanya mtu kuwa jeuri, au ufakiri unaomsahaulisha mtu, au maradhi yenye kumfisidi au ukongwe unaomaliza. Au mauti yenye kuandalia au Dajjaal basi (huyo) ni shari ghaibu yenye kungojewa au kiyama basi (hicho) ni kizito sana na kichungu kabisa”. Tirmidhiy

 

IV/. KUCHUKUA MAZINGATIO KUTOKANA NA KUJA NA KUPITA KWA SIKU.

Kunampasa muumini kuchukua mazingatio kutokana na siku zinazomjia na kupita, kwani usiku na mchana hukichakaza kila kilicho kipya na vinakisogeza karibu kila kilicho mbali. Kama ambavyo vinavyoupunguza umri wa kila kilicho hai na vinamzeesha kila aliye kijana/mdogo. Hakika kupita kwa zama, na kuandamizana kwa usiku na mchana bila ya kuwa na mazingatio sio sifa ya muumini. Kwani katika kila siku inayopita, bali kila saa inayomalizika na kila kipindi (kitambo) kinachopita hutokea ulimwenguni na katika mwili wa binadamu mabadiliko na matukio mbali mbali. Yako miongoni mwa mabadiliko hayo yanayoonekana kwa macho na yasiyoonekana ila kwa hisia tu kadhalika yako yanayojulikana na yasiyojulikana. Katika mabadiliko na matukio yote hayo kuna dalili na uwezo wa Allah kwa kila mwenye akili. Kama ambavyo kuna ukumbusho kwa kila mwenye moyo na mazingatio kwa kila mwenye busara. Hivi ndivyo Allah anavyotuambia ndani ya Qur-ani Tukufu: “BILA SHAKA KATIKA KUUMBWA MBINGU NA ARDHI NA MFUATANO WA USIKU NA MCHANA, ZIKO HOJA (za kuonyesha kuwepo kwa Allah) KWA WENYE AKILI”. [3:190]

Na akasema tena: “ALLAH HUBADILISHA USIKU NA MCHANA (baada ya mchana ukaja usiku na baada ya usiku ukaja mchana). BILA SHAKA KATIKA HAYO IMO DALILI KWA WENYE BUSARA”. [24:44]

 

V/. KUUPANGIA RATIBA WAKATI.

Kunamuwajibikia muumini wa kweli kuupangia ratiba wakati wake na kuhakikisha kuwa anaifuata na kuiheshimu ratiba yake hiyo. Apange katika ratiba hiyo nini cha kufanya, kifanyweje na wakati gani na kwa muda gani. Ratiba hiyo iyachanganye pamoja mambo yote yenye sura ya dini na yale yenye sura ya dunia. Ayapange kulingana na umuhimu, akianzia na lile lenye umuhimu mkubwa na kushuka chini. Alitangulize lenye kuhitaji haraka na alicheleweshe lisilo la haraka na lenye wakati maalumu litendwe ndani ya wakati wake huo. Miongoni mwa aliyoyapokea Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kutoka katika vitabu (mbao) vya Nabii Ibrahimu ni pamoja na: “Yatakikana kwa mwenye akili kama hakushindwa na akili yake awe na mida minne (nyakati nne):-

Muda wa kumnong’oneza Mola wake,

Muda wa kuikagua nafsi yake,

Muda wa kutafakari sanaa (uumbaji) ya Allah, na

Muda wa kutafuta haja zake (kazi) za kimaisha (chakula, maji, nguo n.k.)” Ibn Hibbaan na Al-Haakim

Ratiba hii ya muislamu isisahau kuweka na kutenga muda wa kupumzika, hili linatokana na ukweli kwamba binadamu ni kiumbe anayechoka. Na hivyo kuhitajia mapumziko yatakayomrejeshea nguvu mpya ya mwili na akili. Imamu Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi-anayaelezea maumbile na udhaifu huu wa mwanadamu, anasema: “Zipumzisheni nyoyo muda baada ya muda kwani hakika moyo ukilazimishwa hupofua (huingia upofu ukatenda bila ya mazingatio na kufikiria)”.

Si vema kwa muislamu kuisonga na kuitaabisha mno nafsi yake kwa amali kiasi cha kumdhoofisha na kumfanya kutoendelea tena na amali hiyo. Hata kama kusonga na kutaabisha huku kutakuwa ni kwa ajili ya ibada kama swaumu za suna, kuswali usiku na kadhalika. Siku zote muislamu anatakiwa kuwa mkatikati wa mambo, ni kwa sababu hii ndio Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipowaona maswahaba wake wamekithiri kuswali suna nyuma yake usiku, akawaambia: “Chukueni (fanyeni) katika amali hizi (za kheri) kiasi mkiwezacho, kwani Allah hachoki (kulipa) mpaka mchoke nyinyi (kutenda amali). Na kwa hakika amali ipendezayo zaidi mbele ya Allah ni ile yenye kudumu hata kama ni chache”. Bukhaariy & Muslim

Na mahala pengine Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema: “Hakika dini hii ni nyepesi, hataitilia mikazo dini hii ye yote ila itamshinda. Basi fanyeni amali kwa ukatikati, na (kama hamuwezi kufanya kwa ukamilifu) basi fanyeni kiasi cha kuukaribia (huo ukamilifu). Na zifurahieni thawabu (za amali yenye kudumu hata kama ni chache)”. Bukhaariy & Nasaai

Na katika kauli yake nyingine, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anampa ushauri nasaha mtu anayebalighisha (anayezidisha kupita kiasi) kusoma Qur-ani, kuamka usiku kuswali, na kufunga swaumu za suna. Anamnasihi kufanya amali hizo kwa ukatikati, anasema: “Hakika mwili wako una haki juu yako, familia (mkeo) yako ina haki juu yako na mgeni wako pia anayo haki juu yako”. Bukhaariy

Na mahala pengine Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliwaasa maswahaba wake waliosema kuwa wao sasa watazama katika twaa ya Allah na kuipa mgongo dunia. Kwa hivyo basi hawatalala usiku bali watakesha kufanya ibada, hawatakula mchana na kamwe hawataoa, akawaambia: “Hakika si vinginevyo, mimi ninamchelea zaidi Allah na kumcha kuliko nyinyi. Lakini (pamoja na hivyo) ninasimama usiku kuswali na ninalala, ninafunga na kufuturu (kula) na ninaoa wanawake. Basi ye yote yule atakayejitenga na mwendo wangu huu si katika mimi”. Bukhaariy

Hii ndio suna ya Mtume wa Allah na huu ndio utaratibu wake, utaratibu na njia ya ukatikati katika ufanyaji wa amali. Utaratibu unaoweka mizani baina ya haki ya nafsi na haki ya Allah Mola wa nafsi. Si katika sehemu ya mafundisho ya Uislamu muislamu kuutumia muda wake wote katika kazi, anatoka nyumbani alfajiri na mapema na kurudi usiku wa manane. Kwa utaratibu wake huu unaoukhalifu Uislamu anaidhulumu familia yake usimamizi, ushauri na nasaha zake na kuwaacha watoto kulelewa na mama pekee. Kadhalika si Uislamu mume kukesha usiku kucha kuswali kila siku, kwani kufanya hivyo ni kumnyima mke haki yake ya kimaumbile na ni kuidhoofisha afya yake. Uislamu haujamkataza muumini wake kujitengea muda wa kujipumzisha na kujiburudisha kwa burudani na michezo halali itakayomjenga kiafya.



Forum | Guestbook | Tuandikie |