Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

WAKATI KATIKA MAISHA YA MUISLAMU

 

WAJIBU WA MUISLAMU KUELEKEA WAKATI….IV

Ikiwa wakati una thamani na umuhimu mkubwa sana kama tulivyokwishaona, kiasi cha kuchukuliwa/kuhesabiwa kuwa ndio uhai au maisha yenyewe kabisa. Basi ni lazima muislamu atakuwa anao wajibu mkubwa kuelekea wakati ambao ndio rasilimali yake kuu anayoitegemea katika maisha haya na hata yale yajayo pia. Inatakikana mno kwa muislamu huyu kuichunga, kuitunza, kuihifadhi na kuiweka mbele ya macho yake rasilimali yake hii yenye thamani isiyolinganishika na cho chote. Kinachompasa muislamu baada ya kuifahamu thamani na kuutambua umuhimu huu wa wakati. Ni kuihamisha thamani hii kutoka katika daira (mzunguko) ya maarifa na utambuzi kuitia katika daira ya imani na matashi/matakwa. Kisha kutoka katika daira hiyo mpaka katika daira ya amali na utendaji/utekelezaji.

 

  1. PUPA YA KUSTAFIDI (KUFAIDIKA) NA WAKATI.
  2. Wajibu wa kwanza wa muislamu kuelekea wakati ni kuuhifadhi mithili ya anavyoihifadhi mali yake bali zaidi kuliko hivyo. Awe na pupa ya kutaka kustafidi na wakati wake wote kwa ajili ya manufaa yake katika dini yake na dunia yake. Kadhalika ahakikishe kuwa jamii yake nayo inafaidika kutokana na wakati wake katika ustawi wa kiroho na kimaada. Kwa janibu (upande) hii ya kuujali na kuuhifadhi wakati, wahenga wetu wema (salafu)-Allah awawiye radhi-walikuwa na pupa kubwa sana na wakati wao. Hili lilitokana na kuijua kwao thamani na umuhimu wa wakati. Mwanachuoni Al-Hassan Al-Biswriy-Allah amrehemu-anauelezea ukweli huu, anasema: “Niliwadiriki watu walioupupia wakati wao kuliko mnavyozipupia nyinyi dirham na dinari (pesa) zenu leo!”

    Kwa utambuzi wao huu wa thamani na umuhimu wa wakati, salafu waliuratibia wakati wao, nini cha kufanya na kifanywe wakati gani na waliiheshimu ratiba yao hiyo. Hivyo amali zao zikafanywa kama zilivyopangwa na kwa wakati ziliopangiwa bila ya kupunguza au kuongeza. Kwa utaratibu wao huu mzuri wakawa hawana wakati unaopotea bure bila ya kufaidika nao. Umar Ibn Abdul-Aziz-Allah amuwiye radhi-anatuasa juu ya wakati, anasema: “Hakika usiku na mchana (wakati) vinafanya kazi ndani yako, basi nawe fanya kazi ndani yake (viwili hivyo)”.

    Ufafanuzi wa maneno haya ni kwamba kila mchana na usiku vinapopita na kwenda zao huwa vimepunguza sehemu ya umri wako. Na kuondoka na fursa yako ya kufanya amali ndani yake. Kwa hivyo basi utumie mchana na usiku wa leo kwa kufanya amali itakayokunufaisha katika mchana na usiku wa kesho. Kwani mchana na usiku wa leo ni shamba litakalokupa mavuno katika mchana na usiku wa kesho sambamba na maisha ya milele ya akhera.

    Katika kuielezea thamani ya wakati, salafu walikuwa na msemo: Wakati ni upanga, kama hukuutumia kukatia, utakukata wewe (kwa sababu kazi yake ni kukata na haustahamili kukaa bila ya kukata). Na siku zote waliufanya wakati kuwa ni chombo chao cha kusafiria kutoka katika hali duni kwenda katika hali iliyo bora. Kwa mtindo huu waliifanya leo kuwa ni bora kuliko jana na kesho kuwa ni bora kuliko leo. Hata mmoja wao akafikia kusema: Mtu itakayekuwa leo yake ni kama jana yake (hakuna tofauti), basi mtu huyo amepunjika (amekula khasara). Na mtu ambaye leo yake itakuwa mbaya kuliko jana yake, basi mtu huyo amelaaniwa.

    Salafu walipupia kwa pupa kuu kuona kuwa siku, sehemu ya siku au hata kitambo kidogo cha wakati hakipiti bila ya kufaidika nacho ama kwa kutafuta elimu yenye manufaa. Au kwa kutenda amali njema au kwa kuisaidia jamii na kadhalika. Walifanya hivi ili kuhakikisha kuwa umri wao haupotei bure. Swahaba Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi-alikuwa akisema: “Sikupata kukijutia kitu cho chote mithili ya nilivyoijutia siku iliyozama jua lake ukapungua umri wangu na isizidi amali yangu ndani yake (siku hiyo)”. Naye swahaba mwingine alisema: Kila siku inayonipitia nikawa sizidishi ndani yake elimu itakayoni kurubisha kwa Allah Mtukufu, basi nisibarikiwe katika uchomozaji wa jua la siku hiyo.

     

  3. KUUFANYA NGAWIRA (NYARA) WAKATI WA FARAGHA.

Miongoni mwa neema ambazo watu wameghafilika nazo na kujingikiwa thamani yake na wala hawaishukuru ni neema ya wakati wa faragha. Wakati ambao mtu huwa amepumzika na hana la kumshughulisha wakati huo katika mambo ya lazima ya kila siku. Imepokelewa na Ibn Abas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Neema mbili miongoni mwa neema za Allah wamepunjwa katika neema mbili hizo wengi miongoni mwa watu (neema hizo ni neema ya) siha (afya) na (neema ya) wakati wa faragha”.

Bukhaariy

Wakati wa faragha alioukusudia Bwana mtume ni ule wakati ambao mtu hana shughuli za kimaisha ambazo kwa namna moja au nyingine humnyima fursa ya kutenda amali njema zenye sura ya kiakhera. Kauli hii ya Bwana Mtume haigongani na hadithi nyingine nyingi zinazohimiza kuchuma na kutafuta maisha. Maadam hili la kutafuta maisha halimtumbukizi na kumzamisha mtu katika bahari kina ya maisha kiasi cha kumfanya ashindwe kuitekeleza haki ya Allah. Asili ya neno alilolitumia Bwana Mtume “kupunja” na mahala linapotumika ni katika sekta ya biashara na uchuuzi. Na hapa katika hadithi hii kama anavyosema mwanachuoni mkubwa Al-Manaawiy-Allah amrehemu-anamshabihisha mtu mkalafu na mfanya biashara. Na anaishabihisha siha (afya njema) na faragha na rasilimali ya mkalafu huyo. Hii ni kwa sababu siha na faragha ni katika jumla ya sababu za kupatia faida na ni zana za mafanikio. Basi ye yote atakayeamiliana na Allah kwa kutekeleza maamrisho yake atapata faida. Na atakayeamiliana na shetani kwa kufuata nyayo zake, huyo ataipoteza rasilimali yake hii na kupata khasara kubwa. Katika hadithi nyingine Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Itumie fursa ya mambo matano kabla hayajakufika mambo matano...(katika jumla ya hayo): “Itumie faragha yako kabla ya kushughulika kwako”.

Fursa hii ya faragha haisalikii daima kuwa ni faragha isiyo na jambo la kutendwa ndani yake. Uzoefu na hali ilivyo inaonyesha kuwa ni lazima faragha iwe na jambo ama la kheri au la shari linalotendeka ndani yake. Ukweli wa hili unaonekana katika maisha yetu ya kila siku, hebu waangalie watu wanapotoka kazini na katika shughuli zao mbali mbali za mchana kutwa, wanaitumiaje fursa yao ya faragha? Utaona wako wanaorudi nyumbani na kujipumzisha na familia zao. Na pia wako ambao huunganisha wakaenda katika mabaa na vilabu vya usiku mpaka usiku wa manane. Kwa hivyo basi utagundua kwamba mtu ambaye hakuishughulisha nafsi yake na mambo ya haki na kheri. Hapana shaka nafsi hiyo itamuendesha yeye na kumshughulisha na mambo ya batili na upotofu. Anasema mmoja wa watu wema: “Kufaraghika wakati (ukawa huna) shughuli (ya kufanya wakati huo), hiyo ni neema adhimu (kubwa sana). Mja atakapoikufuru neema hii kwa kuifungulia nafsi yake mlango wa matamanio na akavutwa nayo. Allah atampindulia neema ya moyo wake na atampokonya usafi wa moyo aliokuwa nao (na hapo ndipo hukosa haya/soni na akatenda lo lote bila ya kubali (kujali)”.

Salafu wetu wema-Allah awarehemu-walikuwa hawapendezwi mtu kuwa amefaraghika hana la kumshughulisha si katika dini yake wala dunia yake, akawa yupo tu hana alitendalo. Kwani hapo ndio hugeuka neema hiyo ya faragha na kuwa nakama (adhabu/mateso/maangamivu). Ndipo pakasemwa: “Faragha kwa wanamume ni mghafala (kujisahau) na kwa wanawake ni kiamshi/kichocheo cha matamanio/ashki”. Ukweli wa hili unajidhihirisha katika kisa cha Nabii Yusuf na Bi. Zuleikhah mke wa waziri kama kilivyotajwa ndani ya Qur-ani Tukufu. Bibi Zuleikhah asingegubikwa na kufunikwa na penzi zito la Nabii Yusuf kiasi cha kupanga vitimbi vitakavyomtia mtegoni Nabii Yusuf. Haya yote ni natija ya faragha kubwa aliyokuwa nayo bibi huyu katika maisha yake. Na khatari hii ya faragha ikazidi pale ilipochanganyika na kijana mwenye uzuri uliopindukia na uwezo wa mali unaomuwezesha mtu kupata anachokihitaji.

Yatakikana kwa kila muislamu; mwanamume au mwanamke kuiona fursa ya faragha aliyonayo kuwa ni neema aliyopewa na Allah. Kwani muono huu ndio utakaompelekea kuitumia vema fursa hiyo katika mambo yenye maslahi na manufaa naye katika ulimwengu huu wa leo na ule wa kesho. Mola wetu Mtukufu tunamuomba atuwafikishe kuitumia vema fursa ya faragha tunayoipata.



Forum | Guestbook | Tuandikie |