1.
KUONDOKA/KUMALIZIKA HARAKA:
Hii ni sifa kuu
ya wakati. Wakati unapita/unakwenda mwendo wa mawingu na unakimbia mbio
za upepo. Hivi ndivyo unavyoweza kuimithilisha kasi ya mpito wa wakati
bila ya kujali ni wakati wa furaha na raha au wakati wa huzuni na shida.
Kimtazamo siku za furaha hupita haraka sana kuliko siku za huzuni na
shida ambazo huonekana zikijikongoja taratibu sana. Hizi ni hisia na
mtazamo wa mtu anayepita katika kipindi hicho kigumu, na si ukweli na
hakika ya mambo ilivyo. Hakika itaendelea kubakia ilivyo kuwa wakati
unapita haraka.
Umri wo wote
atakaopewa mtu kuishi ulimwenguni hapa, urefuke utakavyorefuka hata
ukapindukia miaka alfu, bado utakuwa ni mfupi. Ufupi huu unatokana na
ukweli kuwa mauti/kifo ndio mwisho wa kila kilicho hai, katika ulimwengu
huu. Allah amrehemu mshairi aliyenena: (Ikiwa kufa ndio mwisho wa umri
basi ni sawasawa ufupi na urefu wa umri).
Siku mauti
yatakapo muhudhuria mtu, miaka aliyoishi itajikunja na kuonekana kama ni
vipindi vifupi vilivyopita kama umeta wa radi. Imepokelewa hekaya kwamba
malaika wa mauti- Allah amshushie Amani – alipomjia Nabii Nuhu –
Amani imshukie – ili amfishe baada ya kuishi zaidi ya miaka alfu moja.
Alimuuliza akisema: Ewe mrefu wa umri kuliko Mitume wote, umeionaje
dunia? Akajibu (Nuhu): Mithili ya nyumba yenye milango miwili, nimeingia
(nyumbani humo) kupitia mmojawapo wa milango na kutoka kupitia mlango
mwingine.
Mazingatio si
usahihi wa kisa/hekaya hii bali mazingatio yako kwenye ukweli na hakika
inayoelezwa na kisa chenyewe ambao ni ufupi wa umri wakati wa kufa.
Anavyouona mwanadamu umri (wakati) wakati wa kufa ndivyo atavyouona
wakati wa kusimama kiyama. Hivi ndivyo Allah Muumba wa wakati
anavyolielezea hilo: “SIKU WATAKAPO KIOANA WATAKUWA KAMA KWAMBA
HAWAKUKAA (ulimwenguni) ILA JIONI MOJA AU MCHANA WAKE (kutokana na
kishindo kitakachowafika)”. (79:46)
“NA
(wakumbushe) SIKU ATAKAYOWAKUSANYA (waone)KAMA KWAMBA HAWAKUKAA (akili
zimewaruka hata hawajui kiasi cha wakati)….” (10:45)
2. KILICHOPITA
KATIKA WAKATI KIMEPITA, HAKIRUDI NA WALA HAKINA BADALI.
Hii ni sifa na
tabia nyingine ya wakati kwamba kila siku iliyopita, saa iliyomalizika
na kila kipindi kinachopita ni muhali kujirudia tena kama ambavyo ni
muhali kupata badala yake. Hii ndio maana na muradi wa kauli ya Sheykh
Al-Hassan Al-Biswriy- Allah amrehemu: “Hapana siku yo yote
inayochomoza alfajiri yake ila hulingana (hunadi) siku hiyo (na kusema):
Ewe mwanadamu wee! Mimi ni kiumbe mpya, na ni shahidi juu ya amali zako
(za leo, mbaya na njema). Basi jichukulie masurufu (ya akhera) kwangu
kwani mimi nikiondoka sirudi tena mpaka siku ya Kiyama.”
Huu ndio ukweli
usiopingika kuhusiana na wakati. Baada ya kutunga mimba, mwanadamu hukua
kadri siku (wakati) zinavyopita kutoka hali moja kwenda nyingine, mpaka
akawa kiumbe kamili akazaliwa. Baada ya kuzaliwa na kuanza kuvuta hewa
ya ulimwengu huu akiwa katika kipindi cha uchanga. Kuja na kuondoka kwa
siku (wakati) humchukua kutoka katika kipindi hiki cha uchanga na
kumfikisha katika kipindi cha utoto. Kisha kutoka utotoni hadi ujanani,
safari hii ya ujana humfikisha katika kituo cha utu-uzima. Kutokea hapo
mpaka uzeeni na ukogweni, halafu hapo ndipo siku (wakati) huikhitimishia
safari yake hii kaburini. Kwa mlolongo huu ni muhali kwa mzee kutamani
kurudi ujanani na akaweza kuurufia ujana. Umuhali huu unatokna na ukweli
kwamba siku (wakati) za ujana zimekwishakwenda na kupita na kwa tabia ya
wakati, haziwezi kurudi tena. Kwa mantiki utafahamikiwa kuwa wakati una
sifa na kanuni ya mbele kwa mbele, yaani kuja na kuondoka haraka bila ya
kurudi tena. Sifa hii ya wakati inakhalifiana na maumbile ya mwanadamu
ya kutamani kurudia yaliyopita. Kuhusiana na maumbile haya ya mwanadamu,
tunasoma: “HATA YANAPOMFIKIA MMOJA WAO MAUTI, HUSEMA MOLA WANGU!
NIRUDISHE (Ulimwenguni) ILI NIFANYE MEMA SASA BADALA YA YALE
NILIYOYAACHA….” (23: 99-100)
Ukweli huu pia
unadhihirishwa na kauli ya mshahiri:-
Ee laiti ujana
ungerudi siku moja, Nikapata kuueleza yaliyofanywa na uzee.
3. WAKATI NDIO
KITU CHA THAMANI KULIKO VYOTE ANAVYOVIMILIKI MWANADAMU (WAKATI NDIO
RASILIMALI KUU YA MWANADAMU).
Kwa kuwa
imekuwa ni tabia ya wakati kuondoka haraka na kwamba kilichopita katika
wakati ndio kimepita, hakirudi na wala hakina badali. Kwa tabia na sifa
hii ya wakati, inaufanya wakati kuwa ndio kitu ghali na cha thamani
kuliko vyote vinavyomilikiwa na mwanadamu. Ughali na thamani hii ya
wakati unatokana na ukweli kwamba wakati ndio chombo na mahala pa kazi
na uzalishaji wote uanompatia milki mwanadamu. Kwa mantiki hii sote
tutakubaliana kwamba wakati ndio rasilimali ya kweli ya mtu/jamii.
Rasilimali hii haimilikiwi na mwanadamu na wala haimfuati mwanadamu
anavyotaka. Bali mwanadamu ndio analazimika kuifuata na kuichunga ili
aweze kuchuma na kumiliki kupitia rasilimali hii kuu. Kwa hivyo thamani
ya wakati haiwezi kumithilishwa na dhahabu wala jiwe lo lote la thamani
ulijualo, kwa sababu wakati ndio uhai/umri wa mtu. Hivi ndivyo
alivyouona wakati Hassan Al-Bana – Allah amrehemu: “Huo (wakati)
ndio uhai (wenyewe)! Haukuwa uhai wa mwanadamu ila ni ule wakati ambao
anaoupitisha tangu saa ya kuzaliwa mpaka ya kufa.”
Kauli hii ya
Hassan Al-Banaa inashabihiana na ile ya Al-Hassan Al-Biswriy- Allah
awarehemu wote: “Ewe mwanadamu wee! Hakika wewe si chochote ila ni
siku zilizojumuishwa pamoja, kila inapokwenda zake siku moja huwa
imeondoka baadhi yako.”
Mtu asiyeiona
thamani ya wakati leo, hapana shaka kuwa ataiona na kuijua thamani hiyo
kesho wakati ambapo tayari wakati huo utakuwa umepita na hautarudi tena.
Kuhusiana na hili la kutokuiona thamani ya wakati ila bada ya kupita.
Kisha tena ndipo mwanadamu ajute majuto yasiyomfalia kitu ila uchungu.
Qur-ani inatukumbusha sehemu mbili ambazo mwanadamu ataujutia wakati
alioupoteza
WAKATI WA
KUTOKA ROHO:
Wakati
mwanadamu anapoipa mgongo dunia bila ya khiyari yake na
kuikabili
akhera, atatamani apewe muda kidogo tu. Ajali (mauti) yake iakhirishwe
kidogo ili apate fursa ya kutengeneza aliyoyaharibu na kuyadiriki
yaliyomfutu/yaliyompita. Tuitegee sikio Qur-ani tukufu: “ENYI
MLIOAMINI! YASIKUSAHAULISHENI MALI YENU WALA WATOTO WENU KUMKUMBUKA
ALLAH, NA WAFANYAO HAYO, HAO NDIO WENYE KUKHASIRIKA. NA TOENI KATIKA
YALE TULIYOKUPENI, KABLA MMOJA WENU HAYAJAMTIA MAUTI, KISHA AKASEMA:
MOLA WANGU! HUNIAKHIRISHI MUDA KIDOGO (tu) NIKATOA SADAKA NA NIKAWA
MIONGONI MWA WATENDA MEMA?” (63: 9-10)
Na jawabu la
matamanio haya matupu litakuwa ni la kukatisha tamaa kabisa kuonyesha
kuwa kilichopita kimepita na wala hakidirikiwi: “LAKINI ALLAH
HATAIAKHIRISHA NAFSI YOYOTE INAPOKUJA AJALI YAKE NA ALLAH ANAZO KHABARI
ZA MNAYOYATENDA (yote).” (63:11)
AKHERA:
Hapa ndipo
mahala ambapo kila nafsi italipwa kwa ukamilifu kila iliyochuma na kisha
watu wa peponi waingie pepini na wale wa motoni waingie motoni. Hapo
ndipo watakapotamani watu wa motoni kurudi kwa mara nyingine tena katika
maisha haya ya majukumu (taklifu). Warudi duniani ili waanze upya
kutenda amali njema zitakazowanufaisha akhera. Haiyawi, hayawi ng’o
hayo wayatakayo, kwani kipindi cha kufanya amali tayari kimepita na sasa
ni wakati wa kipindi cha jazaa/malipo ya amali zilizotendwa katika
kipindi kilichomalizika. Kuhusiana na hili Qur-ani Tukufu inatuambia:
“NA WALE WALIOKUFURU WATAKUWA NA MOTO WA JAHANAMU, HAWATAHUKUMIWA
KUFA, WALA HAWATAPUNGUZIWA ADHABU YAKE HIVI NDIVYO TUNAVYOMLIPA KILA
ASIYE NA SHUKRANI. NAO HUMO WATAPIGA MAKELELE (watalia wanasema): MOLA
WETU! TUTOE (motoni uturejeze duniani) TUTAFANYA VITENDO VIZURI
VISIVYOKUWA VILE TULIVYOKUWA TUKIFANYA (Allah awaambie) HATUKUKUPENI
UMRI WA (kuweza) KUKUMBUKA MWENYE KUKUMBUKA? NA AKAKUJIENI MUONYAJI,
BASI ONJENI (adhabu) MADHALIMU HAWANA WA KUWANUSURU.” (35: 36-37)
Hoja yao hiyo
ya kutaka kurudisha nyuma kilichopita mbali ya kuwa inapingana na kanuni
ya wakati itakatiliwa mbali na swali kemeo/karipio: “HATUKUKUPENI UMRI
WA (kuweza) KUKUMBUKA MWENYE KUKUMBUKA NA AKAKUJIENI MUONYAJI?……”
Hawatapata
jawabu ya swali hili, kwa sababu Allah tayari alishaukata mzizi mkuu wa
mti wa udhuru pale alipompa kila mwenye dhima (mukalafu) umri (wakati)
unaotosha kutenda kila alilokalifishwa nalo. Na akamuwekea ada ya
kumkumbusha kila anapoghafilika na kujisahau khasa kwa mtu aliyebahatika
kuishi miaka sitini. Umri huu unatosha kabisa kumzindua aliyeghafilika
na kumpa fursa ya kutubu. Hili ndilo eleweko la kauli ya Bwana Mtume –
Rehema na Amani zimshukie – “Allah amemuondoshea udhuru mtu
aliyemngojea (asimfishe) mpaka akafikia umri wa miaka sitini.”