|
NEMBO (MAMBO MATUKUFU) NA DESTURI
ZA UISLAMU ZINASISITIZA
THAMANI YA WAKATI...II
Fardhi za kiislamu na desturi za Uislamu zimekuja kuthibitisha
thamani ya wakati na kuijali kila hatua na sehemu ya wakati. Fardhi na
desturi hizi zinaamsha aina fulani ya mwamko uanomzindua muislamu juu ya
umuhimu wa wakati na mwenendo mzima wa ulimwengu sambamba na mzunguko wa
sayari, nyota, jua na mpishano wa mchana na usiku. Usiku unapotoa mkono wa
kwaheri na kuiachia alfajiri kubisha hodi, huinuka mlinganiaji wa Allah na
kuijaza anga kwa sauti ya wito wa Allah
(adhana.) Sauti hii iliyosheheni maneno matukufu kabisa huwazindua
walioghafilika na kuwaamsha waliolala waamke na kuipokea asubuhi toharifu
kutoka mikononi mwa Allah. Sauti hii husema: (Haya njooni kwenye swala,
haya njooni kwenye kunadi sada “kufaulu”), huzidi na kuongeza: (Swala
ni bora kuliko usingizi). Nyoyo na ndimi za waumini huipokea sauti hii ya
wito wa Allah kwa utii na unyenyekevu mkubwa na haraka watu kawa huamka
kujitayarisha kwa ajili ya swala. Swala
hii ya alfajiri huashiria kuanza kwa siku mpya na harakati zake.
Jua linapotenguka na vichwa na watu wakiwa wamezama katika shughuli
za kimaisha, hurejea mlinganiaji (muadhini) kulingana kwa mara ya pili
tena. Mlinganiaji huyu hushuhudia upweke/umoja wa Allah na ujumbe/risala
ya nabii wake Muhammad na kisha kutoa wito wa swala, wito wa kufaulu.
Waumini wakiusikia wito huu, haraka na kwa utii uliojaa unyenyekevu
huziacha shughuli zao za kimaisha. Wakaenda
kusimama mbele ya Mola wao; awapaye riziki yao na Mpangaji na Msimamizi wa
kweli wa mambo yao yote. Huwa mbele yake kwa dakika kadhaa wakiitupa dunia
nyuma ya migongo yao. Haya
yote hufanyika katika swala ya katikati ya mchana; swala
ya Adhuhuri. Swala ambayo huwakumbusha kumalizika kwa asubuhi; nusu
ya kwanza ya mchana na kuingia kwa nusu ya pili.
Na wakati urefu wa kivuli cha kitu unapolingana sawa na urefu wa
kitu husika na taratibu jua likaanza kuelekea mazamioni hapo ndipo
mlinganiaji wa Allah hulingania tena kwa mara ya tatu akiwaita waja wa
Allah kuja katika nyumba ya Allah kutekeleza fardhi ya Allah, fardhi ya
Alasiri. Kuingia kwa swala hii kama kunaashiria jambo mbali na kupata
radhi za allah, basi ni kumalizika kwa mchana na kuanza kwa jioni ambayo
ni nembo ya makomeleo ya shughuli za mchana kutwa.
Wengi miongoni mwa waja wa Allah huanza kuelekea katika maskani zao
kwa ajili ya kupumzika kutokana na uchovu wa shughuli za kutafuta maisha
za mchana kutwa.
Na wakati mionzi ya jua inapotoweka na kutoonekana kabisa katika
pambizo za mbingu na kutoa nafasi kwa kiza cha usiku kuanza kutawala. Wakati huu kwa mara ya nne, mlinganiaji wa Allah hulingania
tena, akiwaita waja wa Allah kuitekeleza swala inayoashiria kumalizika kwa
mchana na kuanza kwa usiku. Hii
si nyingine bali ni swala ya Maghribi ambayo huwakuta watu walio wengi
wakiwa tayari wamesharejea majumbani mwao.
Na wakati yanapozama na kupotea kabisa makungu mekundu (the red of
sunset) hapo ndipo husikika adhana ya mwisho.
Hii ndiyo adhana ya swala ya mwisho, inayofunga siku ya muislamu,
hii si nyingine bali ni adhana ya swala ya Ishaa.
Wakati huu muislamu huonyesha shukrani na asante zake kwa Allah
Mola Muweza wa yote na vyote. Anamshukuru kwa kumjalia kuamka salama,
kwenda na kurudi salama salimini kazini sambamba na kumuomba ulinzi na
salama katika kiza cha usiku kilichomfunika.
Kwa utaratibu huu wa ibada uliowekwa na Allah kwa hekima na busara
zake tukufu kupitia mfumo sahihi wa maisha (Uislamu). Muilamu hupata fursa
ya kuianza siku yake kwa swala; akayaunga mawasiliano yake na Mola wake
kabla ya kitu kingine cho chote, eh bakhti na saada iliyoje kuishi chini
ya mfumo huu! Kadhalika muislamu huzidi kuyaendeleza mawasiliano haya kila
baada ya muda fulani na hatimaye huikhitimisha siku yake hii kwa swala
kama alivyoianza. Huu ndio
utaratibu wa kila siku wa maisha ya muislamu, kwa kuishi na utaratibu huu
muislamu anakuwa anakumbushwa na fardhi hizi ama kuanza au kumalizika kwa
kipindi fulani cha siku na kumkumbusha wajibu wake kwa kipindi hicho.
Na katika kila juma, muislamu hujiwa na siku ya Ijumaa.
Ndani ya siku hii, waislamu huuitikia wito wa Allah, wito wa swala
ya juma. Hii ni swala ambayo
huwapa fursa ya kukutana pamoja, mahala pamoja na kupata ujumbe mmoja.
Hii ni swala inayoashiria kumalizika kwa siku saba zinazoitwa juma
na kuanza kwa juma jipya. Swala nne za Ijumaa humaanisha kukamilikwa kwa mwezi mmoja
ambapo muislamu hungojea kwa hamu na shauku kuu kuandama kwa mwezi
mwandamo (Hilaal/Crescent.) Muislamu huupokea mwezi mpya kwa Tahlili, Takbiyr na dua, ambapo husikika akisema:
“ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR, AL-HAMDULILLAAHIL-LADHIY
KHALAQAKA, WAQADDARAKA MANAAZIL, WAJA’ALAKA AAYATAN LIL-‘AALAMIYNA.
ALLAAHUMMA AHIL-HU ALAYNAA BIL-AMNI WAL-IYMAAN, WASSALAAMATI WAL-ISLAAM,
WA TAUFIYQ LIMAA TUHIBBU WATARDHWAA. HILAAL KHAYRUN WARUSHDI, RABBIY
WARABBUKAL-LAAHU”.
Kumalizika na kuanza kwa mwezi mwingine, hatimaye humkutanisha
muislamu na fursa adhimu fursa ya mwaka hata mwaka.
Hii si nyingine bali ni mwezi mtukufu wa Ramadhan, mwezi ambao
hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kuachwa wazi kwa wale wote
watakao jikurubisha kwa Mola wao kwa kufanya amali njema ndani ya mwezi
huu. Milango ya moto pia hufugwa sambamba na kutiwa pingu
mashetani kwa baraka ya mwezi huu mtukufu. Ili wasizichafue na
kuziharibu ibada za waja wa Allah ndani ya mwezi huu mtukufu.
Ni ndani ya mwezi huu ambamo hulingania mlinganiaji mwingine, huyu
hulingania kutokea mbinguni na si ardhini kama ilivyo ada kwa swala tano
za kila siku. Mlinganiaji huyu hupaaza sauti kuwaambia waumini: (Jongea
ewe mtaka kheri na mbalika (kuwa mbali) ewe mtaka shari) Wito huu
hupatikanao ndani ya mlingano huu wa mbinguni humfanya aliyeasi kutubia
upesi. Na kumzindua
aliyeghafilika na kumuabudu Mola wake na kuwarejesha wote hawa kwenye
uwanja wa Allah. Katika
uwanja huu huzitafuta radhi na maghfirah yake kwa wasila wa ibada tukufu
na kongwe, ibada ya swaumu na ibada ya kisimamo cha usiku. Ibada hii ya
swaumu humkumbusha muislamu kumalizika kwa zaidi ya theluthi mbili za
mwaka na kwamba kasalikiwa na theluthi moja tu ili kuukamilisha mwaka.
Baada ya muislamu kuimaliza safari hii ya roho ndani ya mwezi wa
Ramadhani, hupata fursa nyingine ya safari.
Hii ni safari inayohusisha roho na mwili pamoja, hii si nyingine
bali ni safari ya kwenda kuitimiza na kuitekeleza nguzo ya tano ya
Uislamu; nguzo ya Hijah. Maandalizi
ya safari hii huanza mara tu baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa
Ramadhani. Ibada hii ya Hijah huashiria kumalizika kwa mwaka wa Kiisalmu
na hivyo kumfanya muislamu awe katika matayarisho ya kuupokea mwaka wake
mpya. Ambayo hii ni fursa
pekee ya kutathmini mafanikio na matatizo yake ya kimwili na kiroho
sambamba na kuyapatia ufumbuzi/suluhisho muafaka.
Wahenga wetu wema – Allah awarehemu – walikuwa wakiziita swala
tano kuwa ni “Mizani/kipimo cha siku”, Ijumaa waliita: “Mizani ya
mwaka,” na waliita Hijah
kuwa ni: “Mizani ya umri.” Majina haya hawakuyaleta kwa njia ya mchezo
na burudani, bali yalitokana na pupa yao juu ya umuhimu na thamani ya
wakati . Ndio wakazifanya ibada hizi kuwa ni kipimo chao cha kupima
utendaji wao wa kila siku, kila juma, kila mwaka na hatimaye umri wa mtu.
Vipimo hivi viliwasukuma kufikiri na kuwaza kabla ya kuamua ama kutenda na
kusema au kutokutenda na kutokusema jambo fulani. Walisukumwa kufanya
hivyo na muongozo kutoka kwa Mtume wao – Rehema na Amani zimshukie –
alipowaasa: “Unapotaka kufanya jambo lo lote lile basi (kwanza)
uzingatie mwisho wake (jambo hilo). Ikiwa una kheri (yaani lina mwisho
mwema jambo hilo) basi endelea (nalo) litende na ikiwa una shari (yaani
lina mwisho mbaya, basi liache (usilitende).”
Ibn Al-Mubaarak
Ukiayaachilia mbali yote haya, utaikuta fardhi ya Zakah ambayo
katika hali nyingi hupasa mara moja kwa mwaka. Kwa kuzitekeleza ibada
hizi, muislamu hubaki kuwa macho na mwenendo mzima wa wakati.
Hivi ndivvyo ambavyo fardhi na ibada hizi za uislamu zinavyomsaidia
muislamu kwenda sambamba na kuujali wakati wake ambao ndio rasilimali yake
kuu.
|