|
Haukuwa Uislamu ndiyo dini ya
kwanza kuruhusu kuoa wake wengi na wala Uislamu
haukuzua utaratibu huu. Bali Uislamu umekuwa
ndiyo dini ya kwanza kuratibisha na kuyawekea
utaratibu mzuri masuala ya ndoa. Isitoshe
Uislamu ukaliwekea suala la kuoa wake wengi
masharti madhubuti na magumu, ambayo Mume
analazimika kuyazingatia kabla ya kuongeza
mke/wake.
Suala la kuoa wake wengi halikuwa tu ni ada
na desturi za waarabu zama za jahiliya, bali pia
ilikuwa ni desturi ya mataifa mbalimbali kwa
namna moja au nyengine, kama historia inavyokiri
ukweli huu. Historia inaonyesha kuwa hata hapa
kwetu Tanzania, watemi (machifu) wa makabila
mbali mbali bali watu wa kawaida wenye mali
walikuwa na wake wengi, huu ni ukweli
usiopingika. Utaratibu huu wa kuoa wake wengi
ulikuwemo pia katika vitabu vilivyotangulia
Qur-ani Tukufu. Mna ndani ya Taurati maandiko na
matukio yanayouthibitisha ukweli huu na wala
hamna ndani ya Injili aya/maandiko
yanayoharimisha kuoa wake wengi. Bali kuoa wake
wengi kulizuiliwa na kanisa katika karne ya kati
{karne ya 10-15 AD} na wakati mwingine
waliruhusiwa na kanisa baadhi ya wafalme wakubwa
kuoa wake wengi. Rejea vitabu vya historia ya
kanisa.
Uislamu umeruhusu kuoa wake wengi kwa sharti
- isizidi idadi yao wake wanne
- Kufanya uadilifu baina yao.
Tunasoma ndani ya Qur-ani Tukufu juu ya
ruhusa hii : "…. BASI OENI MNAOWAPENDA
KATIKA WANAWAKE (maadam mtafanya uadilifu)
WAWILI AU WATATU AU WANNE (tu). NA MKIOGOPA KUWA
HAMWEZI KUFANYA UADILIFU, BASI (oeni) MMOJA TU,
AU (wawekeni masuria) WALE AMBAO MIKONO YENU YA
KUUME IMEWAMILIKI. KUFANYA HIVYO NDIKO
KUTAPELEKEA KUTOFANYA UJEURI." [4:3]
Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
alimwambia Ghaylan At-thaqafiy, ambaye alisilimu
akiwa na wake kumi "Kaa na wanne (tu)
miongoni mwao na waache (wataliki)
waliosalia" At-tirmidhiy, An-nisaai na Ibn
Maajah. Ni vema ikafahamika kwamba huyu Ghaylan
alikuwa ndiye mtemi (mfalme) wa Twaif.
Suala hili la kuoa wake wengi ni suala
lililofanywa na mwenyewe Bwana Mtume, maswahaba
na waliokuja baada yao na ni suala ambalo umma
mzima wa kiislamu umekongamana juu yake. Sheria
hii inayomruhusu mwanamume kuoa zaidi ya mke
mmoja ina maslahi na manufaa kwa wote wawili;
mwanamume na mwanamke. Kwa upande wa mwanamume :
- Inawezekana kabisa mkewe akawa
hamtoshelezei haja yake ya maumbile. Hili
husababishwa na uwezo mkubwa wa mume katika
tendo la ndoa na udhaifu wa mke. Mume hataki
kumuacha mkewe, sasa ataitosheleza wapi kiu
yake ? Hapo ndipo uislamu ukamruhusu kuoa
mke mwingine na yule wa mwanzo kubakia pale
pale. Lau uislamu usingemruhusu mume huyu
kuongeza mke mwingine ni dhahiri kuwa ili
kukidhi haja yake angefanya moja kati ya
mawili. Ima angemtaliki huyu aliye naye,
asiyekidhi haja na kuoa mwingine au angekuwa
na nyumba ndogo (mwanamke wa pembeni/kimada)
- Kadhalika mwanamke anaweza kuwa tasa;
hazai na mume anatamani kupata watoto,
ambalo hili la kupata watoto ni mojawapo ya
malengo na madhumuni ya ndoa. Lakini mume
anampenda mkewe na kwa sababu moja au
nyingine hataki kumuacha. Sasa huyu mume
afanyeje ili aweze kupata watoto kuendeleza
kizazi cha binadamu ? Akazae nje ya ndoa ?
Hapana, hilo ni kosa. Hapa ndipo sheria
ikaizingatia haki ya huyu mume kupata watoto
na ikamruhusu kuoa mke mwingine ajaribu
bahati yake. Huenda Mola wake akamruzuku
watoto kwa mke huyu.
Haya ni baadhi tu ya maslahi ya sheria hii ya
kuoa zaidi ya mke mmoja kwa upande wa mume. Hebu
tuangalie mwanamke naye, ananufaika vipi na
sheria hii :
- Inawezekana kabisa mke akapatwa na
maradhi; yakamsababishia kushindwa kabisa
kuitekeleza haki ya unyumba kwa mumewe.
Maskini mke huyu mgonjwa, aende wapi na
il-hali sasa katika kipindi kigumu cha
ugonjwa ndio anahitajia zaidi huruma,
mapenzi na liwazo la mumewe. Mumewe amtaliki
? La, hapana, sheria inambana mume kuwa
katika mkataba wa ndoa alichukua ahadi
kuishi naye katika raha/shida,
uzima/ugonjwa, basi amuuguze mkewe na ili
kukidhi haja zake za kimaumbile basi na aoe
mke mwingine, Je hapo mwanamke hajanufaika?
- Kadhalika kama ambavyo binadamu
anavyotofautiana katika sura, akili, tabia
na kadhalika. Ni kama hivyo pia
tunatofautiana katika uwezo/nguvu ya
kujamiiana. Inaweza uwezo wa mume ukawa ni
mkubwa sana kuliko mkewe, mume ni tembo na
mke ni kondoo, vipi kondoo atahimili
vishindo vya tembo ? Sasa, ili mke huyu
asiichukie ndoa na hatimaye kukimbia,
uislamu ukamruhusu mume kuongeza mke
mwingine. Siku za zamu ya mke mwingine, huyu
asiyehimili vishindo atapata kupumzika. Hebu
tuwe wakweli, mwanamke huyu kanufaika au la?
Vile vile sheria hii ina maslahi makubwa kwa
jamii. Hakuna jamii isiyokuwa na wajane na
mayatima; ambao hawa wanataka wapate uangalizi
na malezi. Nani basi atawalea wajane hawa
waliofiwa na waume zao na hawa walioachwa na
baba zao ? Hapo ndipo Uislamu ukampa ruhusa
mwanaume ambaye tayari ana mke, kuongeza mke
mwingine. Pengine huyu atakayemuoa ni huyo
mjane, mwenye mayatima. Je hapo mwanamke huyu
hajasitirika na wanawe ? Kwani huyu mume atakuwa
anawajibika kumhudumia yeye na wanawe. Waswahili
husema ukipenda boga penda na maua yake. Je,
hapa jamii imenufaika au haikunufaika ?
Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake
duniani ni kubwa kuliko idadi ya wanaume,
kadhalika idadi ya wanyama jike ni kubwa kuliko
ya wanyama dume. Haya ni matokeo ya utafiti
uliofanywa na taasisi mbali mbali ulimwenguni
kote. Sasa itakuwa tunakubaliana na takwimu hizi
na leo vita vimetapakaa duniani kote na wahanga
(victims) wa vita hivi, wengi wao ni wanaume kwa
kuwa wao ndio askari wanaopigana vita. Hebu
tuchukulie/tukadirie kuwa uwiano wa wanaume na
wanawake duniani 1:5 yaani mwanaume mmoja kwa
wanawake watano. Sasa ikiwa kila mmoja akioa mke
mmoja hawa waliobaki waende wapi, wakaolewe na
nani ? Hawa pia ni binadamu, wanayo haki yao ya
msingi ya kupenda na kupendwa katika jamii.
Wanayo matakwa yao ya kimaumbile, wakakidhi wapi
haja na hamu zao za kimaumbile ? Ni kwa
kuzingatia hili ndio uislamu ukamruhusu mwanaume
kuoa mke zaidi ya mke mmoja kwa sharti ya kuwa
awe muadilifu baina yao.
Ni lazima tukubali kuwa kila sheria
aliyotuwekea Mola wetu mtukufu ina faida,maslahi
na manufaa kwetu sisi waja wake. Akiamrisha au
kukataza ni kwa maslahi na faida yetu sisi
wenyewe. Ni mamoja tumeyajua na kuyaona maslahi
na faida za amri au katazo hilo au hapana.
Kushindwa kwetu kuyajua maslahi na kuziona
faida, hakuziondoshi faida na maslahi hayo na
kuyafanya yasiwepo, bali yatabakia pale pale.
Huu ndio ukweli usiopingika. Waislamu tumekuwa
tukiwacha mafundisho ya dini yetu na kufuata
mafundisho ya shetani yaliyopitia kwa wanaojiita
wanamaendeleo. Leo matatizo yanayotukuta
yanatokana na kuacha mafundisho ya Uislamu.
Tukodolee macho wakati wa Mtume na masahaba na
tuone nia zao katika kuoa wake wengi, jinsi
mwanamke wa kiislamu alivyohifadhika, wajane wa
vita pia nao hawakutupwa mkono, na Mtume
–Rehema na Amani zimshukie – ndiye aliyeanza
kuonyesha mfano. Je, tuna mfano mkubwa kuliko wa
Mtume wakati Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuamrisha
tumfuate ? Tunafuata mkumbo wa maadui wa
kiislamu unaodai haki za wanawake na kushikilia
kuoa mke mmoja, pamoja na kuweka vimada,
kumvunjia mwanamke heshima yake kwa kumvua nguo
na kumtumia kwenye matangazo ya biashara,
madansa, miss world na kadhalika. Leo mwanamke
akiolewa ananyang’anywa hata jina la mzazi
wake na kujulikana kwa jina la mumewe, Mrs
fulani, sasa ni nani anayemtakia mema mwanamke,
Mwenyezi Mungu aliyemuumba au wakazi wa dunia
hii wakiongozwa na mwanaume ambaye yuko tayari
kufanya lolote kutekeleza matashi ya nafsi yake
???
|