|
VITA VYA
BADRI-IJUMAA, RAMADHANI 17/02 A.H. {13th MARCH/624 A.D.}
Allah Mtukufu
anasema: “NA ALLAH ALIKUNUSURUNI KATIKA (vita vya) BADRI, HALI NYINYI
MLIKUWA DHAIFU. BASI MCHENI ALLAH ILI MPATE KUSHUKURU (kila wakati kwa
neema zinazokujieni)”. [3:123]
Katika mwezi mtukufu
wa Ramadhani vilipiganwa vita vya kwanza tangu kuasisiwa kwa dola ya
kiislamu Madinah. Hivi ndivyo vita vya Badri, vita vilivyotoa taswira ya
ushindi wa Uislamu. Imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alisikia kwamba Abuu Sufyaan anarudi na msafara wa biashara wa
Makurayshi akitokea Shamu. Msafara huo ulikuwa umesheheni mali nyingi,
Bwana Mtume akawatolea wito maswahaba wake kuutokea msafara huu, akasema:
“Huo msafara wa Makurayshi una mali zao, utokeeni huenda Allah akaufanya
ngawira kwenu”. Baadhi ya maswahaba wakawa wepesi wakaitika wito na
kutoka na wengine wakawiwa uzito kutoka kwa sababu hawakujuwa kuwa
kutakuwa na vita. Na kwa kutambua kwao kwamba lengo la kutoka ni kuteka
msafara na sio kupigana au kuua watu.
Abuu Sufyaan
alipokaribia kufika Hijazi, akaanza kupeleleza khabari za Mtume kwa
kuuliza kila msafara aliokutana nao njiani. Mpaka akapata khabari kutoka
kwa msafara mmoja ya kwamba Mtume amemtokea na maswahaba wake ili kuuteka
msafara wake na kupora mali yote. Hapo ndipo alipoanza kuchukua hatua za
makusudi na za haraka za tahadhari. Akapeleka khabari Makah akiwajuliasha
juu ya khatari inayoukabili msafara uliosheheni mali zao. Kwa kawaida
Makurayshi walikuwa wakifanya biashara za msimu mara mbili kwa mwaka.
Biashara ya majira ya Kaskazi kuelekea nchi ya Shamu na ile ya majira ya
Kusi kulekea Yemen. Hii ndio misafara ya baishara inayotajwa na kauli
tukufu ya Allah: “ILI KUWAFANYA MAKURESHI WAENDELEE. WAENDELEE NA SAFARA
ZAO ZA WAKATI WA KUSI (kwenda Yaman) NA WAKATI WA KASKAZI (kwenda Shamu).
BASI NA WAMUABUDU BWANA WA NYUMBA HII (Al-Kaaba). AMBAYE ANAWALISHA KATIKA
NJAA NA ANAWAPA AMANI KATIKA KHOFU”. [106:1-4]
Khabari zilipofika
Makkah, watu wakajiandaa haraka haraka kwenda kuuhami msafara wao usitekwe
na Bwana Mtume. Hawakubakia nyuma katika watukufu wa kikurayshi ila
wachache tu ambao walituma wawakilishi wao. Walipokamilisha maandalizi yao
na kukubaliana kuanza safari ya kwenda kupambana na waislamu ili kuulinda
msafara wao. Wanawake wao wakaanza kuimba na kupiga dufu wakiwaponda na
kuwabeza waislamu ili kulihamasisha na kulishajiisha jeshi lao. Abuu Jahli
ndiye aliyekuwa kiongozi wa makafiri aliyetwaa sukani ya kuliongoza jeshi
hili dhidi ya waislamu. Kisha Ibilisi akajitokeza katika sura ya mtu
mshauri mtoa nasaha na kuwapambia amali yao hii kwa kuwaambia: “…LEO
HAKUNA WATU WA KUKUSHINDENI, NA MIMI NI MLINZI WENU…” [8:48]
Yaani nitakuwa
pamoja nanyi katika dhiki na faraja na sitokutupeni mkono mpaka nione
mwisho wa kadhia hii.
JESHI LA
WAISLAMU.
Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-akatoka siku kadhaa baada ya kuanza kwa mfungo mtukufu
wa mwezi wa Ramadhani. Akatoka huku akiongozwa na bendera mbili; moja
ikichukuliwa na Sayyidna Aliy Ibn Abiy Twaalib na nyingine ikibebwa na
Answaari. Walipokaribia kufika Badri ikawajia khabari kwamba tayari
Makurayshi wamekwishatoka kuja kuuhami msafara wao kwa gharama yo yote
iwayo. Wametoka wakiwa na chakula cha kutosha na zana kamili za vita. Ni
vema ikakumbukwa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakutoka kwa
ajili ya vita, kwa hiyo hakuwa amejiandaa kivita. Waislamu wakashitushwa
sana na khabari hii, lakini imani yao isiyotetereka ikawafanya wathibiti
na kusimama imara kukabiliana na lo lote litakalojitokeza. Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawakusanya watu wazima miongoni mwa
maswahaba wake. Akawataka ushauri wa nini kifanyike ili kukabiliana na
hatari inayowajongelea. Akawaelezea khabari iliyomfikia kuhusiana na
Makurayshi na maandalizi yao kabambe katika kupigana na waislamu.
Bwana Mtume
alipomaliza kuwasilisha ripoti ya hali ya mambo ilivyo, ndipo aliposimama
Sayyidna Abuu Bakri-Allah amuwiye radhi-kuelezea msimamo wake kuelekea
hali hiyo. Akazungumza maneno mazuri, akidhihirisha nguvu na ushujaa wake.
Akabainisha kwamba yeye yu thabiti mithili ya jabali kubwa. Alipomaliza
kuelezea msimamo wake huo na kuketi chini, ndipo ikawa sasa ni zamu ya
Sayyidna Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi. Naye kama ilivyokuwa
kwa mtangulizi wake akazungumza maneno mazuri. Maneno yenye kumathilisha
ushujaa wa kweli na nia thabiti katika kupambana na adui kwa gharama yo
yote iwayo. Akaonyesha shauku yake ya kutaka kukutana na Mola wake kupitia
njia ya kuipigania dini yake. Na pepo ambayo upana wake ni mithili ya
mbingu na ardhi kuwa ndio jazaa yake. Sayyidna Umar akaketi chini ili
kutoa fursa kwa Al-Miqdaad-Allah amuwiye radhi-kuelezea msimamo wake.
Akasimama na kusema neno lake lenye kusalikia na kukumbukwa daima: “Ewe
Mtume wa Allah! Tekeleza alilokuamrisha Allah, sisi tu pamoja nawe kwa lo
lote. Wallaah, sisi hatukuambii wewe kama Bani Israaili walivyomwambia
Musa: Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa kungojea
nini litakalokuwa. Lakini tunachosema sisi: Nenda wewe na Mola wako
mkapigane, na sisi tutapigana pamoja nanyi. Tunamuapia yule aliyekutuma
kwa haki, lau ungelitupeleka Barkil-Ghimaadi (sehemu iliyo mbali na
Makkah), bila ya shaka tungelikufuata. Na wala asingelibakia nyuma ye yote
miongoni mwetu mpaka tulituze jicho lako na tukikunjue kifua chako kwa
furaha”. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamjazi dua njema kwa
maneno yake hayo mazuri yaliyosheheni ukweli na nia ya dhati. Kisha
akasema: Nipeni ushauri enyi watu, akiwalenga Answaari kwani wazungumzaji
wote waliopita walikuwa wanawawakilisha Muhajirina. Hapo ndipo aliposimama
Sa’ad Ibn Muaadh na kusema: Wallah kama kwamba unatukusudia sisi ewe
Mtume wa Allah! Mtume akajibu: Ndio. Sa’ad akaanza kusema: Hakika sisi
tumekuamini, tumekusadiki na tumeshuhudia kwamba dini uliyokuja nayo ndio
dini ya haki. Na tumekupa ahadi na dhamana ya utii juu ya dini hii, basi
tekeleza ulitakalo ewe Mtume wa Allah, nasi tu pamoja nawe. Tunamuapia
yule aliyekutuma kwa haki, lau ungelituonyesha bahari hii na ukaiingia,
bila ya shaka tungeliingia pamoja nawe. Na wala asingelisalia nyuma hata
mtu mmoja katika sisi na wala sisi hatuoni vibaya kukutana na adui yetu
kesho. Hakika sisi ni wastahamilivu vitani, wakweli katika mapambano,
huenda Allah akakuonyesha kwetu litakalolituza jicho lako, basi tupeleke
kwa baraka za Allah.
Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-akafurahishwa mno na kauli hii ya Sa’ad, kauli
ilyowakilisha msimamo wa Answaari, kisha akasema: “Enendeni na ikupateni
bishara njema, kwani hakika Allah ameniahidi mojawapo ya mapote mawili.
Wallah, kama kwamba mimi hivi sasa ninayaona maanguko ya watu wale”. Kwa
kauli hii ya Bwana Mtume, maswahaba wakatambua kwamba sasa ni vita tu
hakuna njia ya kuviepuka. Jua lilipokuchwa Bwana Mtume akawatuma Sayyidna
Aliy, Sa’ad Ibn Abiy Waqaaswi na Zubeir kupeleleza khabari za
Makurayshi. Njiani wakakwaana na waajiriwa wawili wa Makurayshi,
wakawakamata na kuwaleta mbele ya Mtume. Mtume akaanza kuwasaili:
Makurayshi wako kiasi gani? Wakajibu: Hatujui, akazidi kuwasaili:
Wanachinja ngamia wangapi kwa siku? Wakajibu: Siku moja ngamia tisa na
siku nyingine ngamia kumi. Bwana Mtume akasema: Idadi ya adui ni kati ya
mia tisa na alfu moja, halafu akawauliza: Ni nani katika watukufu wa
Makurayshi aliyemo msafarani? Wakamtajia majina kumi na tano, Mtume
akawageukia maswahaba wake na kuwaambia: “Haya Makkah ndio hiyo
imekutupieni maini yake (wanawe vipenzi) na kuwatanguliza wanamume wake
bila ya kubakisha kijana au ye yote mwenye kuweza kubeba silaha ila
wamekuja naye!”
Idadi ya maswahaba
wa Mtume ilikuwa ni mia tatu na kumi na tatu tu. Tukirejea kwa Abuu
Sufyaan tunamkuta amefanikiwa kuwakwepa waislamu na kuuokoa msafara na
kufika Makkah salama. Alipofika Makkah akawaandikia barua watu wake
akiwataka warejee, kwani hakuna tena sababu ya kupigana. Akawaambia katika
ujumbe wake huo:Enyi jamaa zangu! Bila ya shaka nyinyi mlitoka kwa ajili
ya kuuhami msafara wenu, na tayari Allah amekwishauokoa basi rejeeni. Na
fikra hii ya kurudi ikawa ndio fikra ya wengi miongoni mwa washirikina
wale. Abuu Sufyaan pamoja na ushirikina wake, bado alikuwa ni mtu mwenye
busara na uoni wa mbali. Lakini hali haikuwa hivyo kwa Abuu Jahli, kwani
yeye aliipinga kwa nguvu zote fikra hiyo, akasema: Wallah, kamwe
hatutarudi nyuma mpaka tukae Badri siku tatu, tukichinja ngamia, tukilisha
chakula na kunywa pombe. Waarabu watusike na kutujua sisi ni nani na
waendelee kutuogopa. Wallah hapana, haturudi mpaka Allah ahukumu baina
yetu na Muhammad. Huyu Abuu Jahli alikuwa ni mtu mjinga, mpenda fakhri
asiyeangalia natija ya mambo kabla ya kuyaingia.
MPAMBANO WAANZA.
Majeshi mawili haya
yalipokutana, wa mwanzo kutimua mbio alikuwa ni Ibilisi ambaye alitoa
mchango mkubwa katika kuchochea vita hivi. Yeye alirudi kisengerenyuma
mpaka safu ya mwisho kabisa, akijitenga kabisa na mushirikina aliowatia
hamasa na kuwapandisha mori wa vita,huku akiahidi kuwa pamoja nao mpaka
mwisho wa kadhia hii. Akijitetea kwa kujitenga huku kwa kusema kuwa yeye
anayaona wasioyaona wenziwe (Makurayshi). Huu ndio msimamo wa Ibilisi
katika mambo yote, hulipamba na kuliremba jambo kisha akawapendezeshea
watu hata wakaliingia kichwa kichwa. Wakishaliingia ndio huwatupa mkono,
huyoo akenda zake na kuwacheka kwa upumbavu wao wa kuyaingia mambo bila ya
kutafakari.
Kamanda Mkuu wa
waislamu; Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwaamuru maswahaba
wake wasishambulie ila kwa amri yake. Akapanga safu na namna ya kuelekeza
mashambulizi, kisha akarejea hemani kwake akiwa pamoja na Abuu Bakri.
Mtume akawa anamuomba humo Mola wake ampe nusra na ushindi, akisema:
“Ewe Mola wangu wa haki wee! Ukikiacha kipote hiki cha waumini kuangamia
leo, hutoabudiwa kamwe. Ewe mwenye uhai wa maisha, msimamia kila jambo
tunaomba msaada kwa rehema zako”. Yakawa mafungamano ya Mtume na
kumtegemea kwake Mola wake ni kwa kiwango cha juu sana kuliko wakati
mwingine wo wote. Baada ya kuomba sana, Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alirejea tena kwa maswahaba wake na kuwakhutubia. Katika khutuba
yake hiyo aliwahimiza kupigana kwa nia safi (Ikhlaaswi), akawaamrisha
kusubiri na kuwa na ujasiri mbele ya adui. Na akawabashiria ushindi na
nusra ya Allah, akasema: “Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi
mwake, leo mtu hatapigana nao akauawa hali ya kuwa ni mwenye kusubiri na
kutarajia jazaa ya Allah. Akisonga mbele bila ya kurudi nyuma, ila Allah
atamuingiza peponi”. Bwana Mtume akawaraghibisha na kuwatia shauku ya
pepo maswahaba wake. Hili likamjaza mori wa vita Umeir Ibn Al-Humaam,
akasema huku akiwa na tende mkononi akizila: Shabaash, hivi kumbe hapana
kizuizi kati yangu na pepo ila ni kuuliwa na watu hawa! Akazitupilia mbali
tende alizokuwa nazo mkononi, akachukua upanga wake na kujitoma katikati
ya maadui. Akazivuna shingo kadhaa za adui kwa ushujaa na nguvu ya ajabu.
Kisha naye akauawa-Allah amuwiye radhi yeye na wenzake wote na kila
aipiganiaye dini hii mpaka siku ya Kiyama.
Kisha Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akachota mchanga kwa kiganja chake,
akawaelekezea Makurayshi na kusema: “Nyuso zimejaa ubaya”. Halafu
akawapulizia na kuwaamrisha maswahaba wake kuanza mashambulizi kama mtu
mmoja. Wakawaendesha mbio makafiri wale, Allah akautambua ukweli wa
waumini na kuiona ikhlaaswi yao. Hapo ndipo ukawajia msaada kutoka
mbinguni, likashuka jeshi la malaika chini ya uongozi wa Jibrili. Hapo
ukawa unasikika mgongo na mchakacho wa silaha tu bila ya kuonekana
wapiganaji. Mtu haoni ila kupukutika kwa vichwa tu bila ya kumuona
mpigaji. Waislamu hawakuupata msaada huu ila ni kutokana na ukweli wao na
imani yao thabiti. Ndipo Allah naye akawatekelezea ahadi yake ya
kuwanusuru. Kutokana na ukweli kwamba nguvu ya mbinguni (ya Muumba)
haiwezi kupambanishwa na nguvu ya ardhini (ya viumbe), ushindi ukawa ni wa
waislamu.
VITA VYAMALIZIKA.
Vita vikamalizika
baada ya kuuawa viongozi na mamwinyi wa kikurayshi, hapo wakakimbia
waliokimbia na wengine wakakamatwa mateka. Mwisho mwema ukawa ni wa
wacha-Mungu, nusra na ushindi ukawa ni wa waumini. Na makafiri fungu lao
likawa ni fedheha na kushindwa, Allah Taala anasema: “(Kumbukeni) MOLA
WAKO ALIPOWAFUNULIA MALAIKA (akawaambia): HAKIKA MIMI NI PAMOJA NANYI,
BASI WATIENI NGUVU WALE WALIOAMINI, NITATIA WOGA KATIKA NYOYO ZA MAKAFIRI.
BASI WAPIGENI JUU YA SHINGO (zao) NA KATENI KILA NCHA ZA VIDOLE VYAO. HAYO
NI KWA SABABU WAMEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE. NA MWENYE KUMUASI ALLAH NA
MTUME WAKE (atamuadhibisha) KWANI ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU”. [8:12-13]
NENO KHITAMI:
DARSA NA MAZINGATIO.
Tukiwa tunaishi na
tukio hili kongwe la vita vya Badri, inatupasa kuinamisha vichwa vyetu ili
kuonyesha heshima zetu kwa kikundi hiki kidogo cha waumini. Maswahaba wa
Mtume Mtukufu ambao wamezisadikisha kiamalia ahadi walizozichukua mbele ya
Allah Mola Muumba wao. Kipi tuwezacho kukisema kwa watu waliotoka
majumbani mwao wakiamini kuwa wanakwenda matembezini tu kusikokuwa na
taabu wala matata yo yote. Hakuna vita wala mapambano, tahamaki wako ana
kwa ana na kundi kubwa linalotisha, lenye uchu wa kuangamiza. Lakini
pamoja na yote hayo hawakubabaika wala kutetereka kama ambavyo ingeweza
kutokea kwetu. Katika hali hiyo ngumu na kitatange hicho kisichotazamiwa,
wote kwa pamoja wanamzunguka Bwana Mtume na kuonyesha utayarifu wao katika
kukabiliana na hali hiyo. Wakaonyesha kupevuka kwao kiimani na kiwango cha
juu cha subira wawamo katika hali ya vita. Wakawa tayari kupambana na adui
kwa gharama yo yote iwayo na kwa hali yo yote ile. Mbele yao kulikuwa na
ama ushindi (nusra) au kaburi, lakini hakuna kitu kusalimu amri mbele ya
adui wa Allah na Mtume wake.
Tunaweza kusema nini
juu ya watu ambao katika usiku wa kuamkia mpambano wa makundi mawili yale.
Pamoja na kuitambua nguvu kubwa ya adui yao na maandalizi kabambe ya vita,
bado walilala usingizi mwanana usio na mang’amung’amu. Usingizi wao
huu katika kipindi hiki cha hatari, kama unaashiria jambo basi ni
kuonyesha namna gani walivyopevuka kiimani. Hili ndilo analoliashiria
Allah kwa kauli yake: “(Kumbukeni) ALIPOKULETEENI USINGIZI ULIOKUWA
(alama ya) SALAMA ITOKAYO KWAKE…” [8:11]
Naam, walilala
usingizi wa amani uliowaondolea kila aina ya khofu. Wote walilala na
ilhali vita vi tayari mbele ya macho yao, na adui akingojea kwa uchu mkuu
fursa ya kuwasagasaga. Wote walilala kama anavyolala mtu nyumbani kwake.
Wote walilala ila mtu mmoja tu, huyo hakufunika jicho lake na wala
hakuuweka ubavu wake chini. Huyu alikesha katika usiku ule wa usingizi wa
amani na salama. Alikesha kama mlinzi wao, akiwaombea nusra ya Allah na
kuswali kwa ajili yao. Huyu hakuwa mwingine bali ni Mtume wa Allah,
akionyesha namna gani anavyowajali watu wake na jinsi kiongozi atakiwavyo
kuwa kwa watu wake. Huyu ndiye Mtume ambaye Allah anatuambia juu yake:
“AMEKUFIKIENI MTUME ALIYE JINSI MOJA NA NYINYI, YANAMUHUZUNISHA
YANAYOKUTAABISHENI, ANAKUHANGAIKIENI. (Na) KWA WALIOAMINI NI MPOLE NA
MWENYE HURUMA”. [9:128]
Imepokelewa kutoka
kwa Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Tulijikuta siku ya Badri
hakuna ye yote miongoni mwetu ila alilala isipokuwa Mtume wa Allah pekee.
Yeye alisimama chini ya mti akiswali na kulia mpaka kulipopambazuka”.
Je, umepata kumuona
au hata kumsikia tu kamanda mithili ya kamanda huyu mtukufu? Au umewahi
kumshuhudia kiongozi kama huyu; Mtume aliye Mtumishi wa watu?!
Tunaweza kusema nini
kwa watu ambao waliyaonea tamu mauti na dunia ikawa si kitu mbele yao pale
waliposikia wito wa Mtume: “Iinukieni pepo ambayo upana wake ni sawa na
upana wa mbingu na ardhi”. Hapo kila mmoja wao akatambua kuwa hapana
kinachomzuia kuingia peponi ila ni kupigana na adui mpaka auawe. Hapo
ndipo akajitoma katikati ya kundi la maadui mithili ya mshale, akifyeka
vichwa kwa nguvu zake zote kuliani na kushotoni. Mpaka anapozidiwa na
kuanguka chini maiti, akiwa tayari amekwisha jihakikishia nishani ya
ushahidi. Kwa hali hii, nusra ikawa jirani mno na wao mithili ya nyama na
mfupa na msaada wa Allah ukawa pamoja nao. Kwa kitendo chao hiki wakawa
wametoa na kuacha darsa lenye mazingatio makubwa kwa vizazi vijavyo baada
yao. Darsa ambazo historia ya Uislamu haikamiliki bila ya kutajwa na sio
kutajwa tu bali kutumika katika kuyapatia ufumbuzi na tiba sahihi matatizo
yanayowazunguka waislamu leo ulimwenguni kote. Wakati tukiwa ndani ya
kumbukizi za tukio hili kongwe lililosheheni suluhisho la magumu
yanayowafika waislamu leo, bado
-
Uislamu ni mgeni
katika ardhi za kiislamu.
-
Waislamu hawajui
utukufu na thamani ya Uislamu wao.
-
Sheria na adabu
za kiislamu hazijatawala ulimwengu hata katika ardhi za kiislamu.
-
Maeneo
matakatifu ya waislamu yako chini ya mikono najisi ya Mayahudi
waliowauwa mitume wa Allah pasi na haki.
-
Hakuna umoja
wala mshikamano na udugu wa kiislamu baina ya waislamu.
-
Waislamu pamoja
na wingi wao na utajiri wao, ndio jamii nyonge na dhalili duniani
kote.
-
Waislamu
wanamkumbatia na kumfanya kafiri kuwa ndiye mwandani wao kinyume cha
waumini wenzao!
-
Waislamu
wanapigana wao kwa wao kwa sababu ya fitina wanazopandikiziwa na adui.
-
Waislamu
wanategemea nguvu za mashariki au magharibi kuwalinda. Wamesahau
kwamba nusra haiwi na wala haitoki ila kwa Allah tu pekee.
Ndugu waislamu po
pote pale mlipo katika ardhi hii ya Allah, tukiwa katika kumbukumbu ya
vita hivi vya Badri ni wajibu wetu:-
Kuamini kuwa jihadi
ni FARDHI YA LAZIMA. Ni ibada iliyofaradhishwa juu yetu kama
ilivyofaradhishwa swaumu. Kama alivyosema Allah: “ENYI MLIOAMINI!
MMELAZIMISHWA (mmefaradhishiwa) KUFUNGA (swaumu)…” [2:183] Akasema
katika sura hiyo hiyo: “MMELAZIMISHWA KUPIGANA VITA (kwa ajili ya
dini)…” [2:216] Na tuamini kuwa jihadi haikomelei tu kwa maswahaba wa
Mtume, bali inaendelea muda wa kusalikia Uislamu katika ardhi hii. Kwani
imekuja katika hadithi tukufu: “Piganeni jihadi na mushirikina kwa mali
zenu, nafsi zenu na ndimi zenu”.
Katika kipindi hiki
kigumu ambacho tumezungukwa na adui kila upande kiasi cha kutokuwa na
kimbilio. Ni wajibu wetu tujiunganishe na Allah Mola Mshindi
asiyeshindika. Na tukumbuke kuwa Uislamu ni imani/itikadi na mfumo mzima
wa maisha kabla ya kuwa kwake ni nguvu na silaha iliyo mikononi mwetu
tayari kumzima adui ye yote. Nyoyo zetu zitakapotwaharika na ghururi za
shetani na dunia na imani yetu ikaimarika kwa kutenda mambo ya twaa. Hapo
tutakuwa tumekwisha jihakikishia sababu za ushindi na nusra dhidi ya kila
adui yetu. Na hapo ndipo Allah atakapotutimizia ahadi yake kongwe:
“…NA NI WAJIBU JUU YETU KUWANUSURU WALIOAMINI…” [30:47]
Mtumishi wa Umma
{WEBSITE UISLAMU} inawatakia waislamu wote ulimwenguni kote kumbukizi
njema na tafakari za kina zenye suluhisho za magumu yao za vita vya Badri.
Allah awaridhie mashahidi wa Badri na wote walioupigania, wanaoupigania na
watakaoupigania Uislamu mpaka siku ya Kiyama. Ewe Mola wa haki! Unusuru
Uislamu na waislamu po pote pale walipo katika mashariki na magharibi ya
ardhi yako, Aaamiiyn!
Wassalaamu Alaykum
Warahmatullah Wabarakaatuh.
|