|
IBADA YA ITIKAFU.
MAANA YA ITIKAFU:
Kilugha neno “Itikafu” lina maana kuu mbili, kama
zifuatazo:
Kuzuia, na
Kukaa.
Kisheria “Itikafu” ni: Kitendo cha kukaa msikitini kwa
mfumo maalumu uambatanao na nia ya kujikurubisha kwa Allah, kwa kutekeleza
ibada mbali mbali.
HUKUMU YA ITIKAFU:
Itikafu ni ibada ya SUNAH katika wakati wo wote na
imekokotezwa sana katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Na itikafu
kwa upande mwingine inaweza kuchukua hukumu ya UWAJIBU, hii ni iwapo mtu
atajiwajibishia mwenyewe. Mtu atakaposema nimenuia kukaa itikafu siku moja
au mbili iwapo nitapata mtoto mathalan. Katika mazingira haya itikafu
itakuwa imekwisha kuwa wajibu juu yake. Kwa sababu ya msingi
usemao:(Kutekeleza nadhiri ni wajibu). Imepokelewa kwamba Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mwenye kutia nadhiri ya kumtii
Allah, basi na amtii”. Bukhaariy
DALILI YA ITIKAFU:
Ibada hii ya itikafu imethibiti ndani ya Qur-ani Tukufu,
suna ya Mtume na Ijmaa ya wanazuoni. Allah Mtukufu anasema: “…WALA
MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU MISIKITINI. HIYO NI MIPAKA YA
ALLAH, BASI MSIIKARIBIE…” [2:187]
Yaani Allah Mtukufu anawaamrisha waja wake waumini
kutokuwaingilia wake zao katika kipindi chote cha kukaa kwao itikafu
msikitini. Na katika sunah, imepokewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye
radhi-amesema: “Mtume-Rehema na amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu
katika kumi la mwisho la Ramadhani…” Bukhaariy & Muslim
SHARTI ZA KUSIHI ITIKAFU:
Ili itikafu ya mja isihi kisheria ni wajibu zipatikane
sharti zifuatazo:-
Nia, kwa sababu amali zote hufungama na nia kama
ilivyothibiti katika hadithi sahihi.
Twahara ya hadathi kubwa. Itikafu haisihi kwa mtu mwenye
janaba, mwenye hedhi na mwenye nifasi.
Itikafu ifanyike msikitini kwa ushahidi wa kauli tukufu ya
Allah: “…WALA MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU
MSIKITINI…”
TANBIHI:
Mwanamke ana haki ya kukaa itikafu msikitini kama aliyo
nayo mwanamume. Ila tu haki yake hii ni lazima ipate idhini ya mumewe
akiwa ni mke wa mtu. Au walii wake kama si mwanandoa. Na sharti akae
itikafu katika mahala palipotengwa kwa ajili ya wanawake msikitini humo.
Hii ni kwa sababu wakeze Mtume-Allah awawiye radhi-walikuwa wakikaa
itikafu msikitini na katika mahala palipotengwa kwa ajili yao.
YENYE KUBATILISHA ITIKAFU:
Ibada ya itikafu huwa ni batili mbele ya sheria, iwapo
muhusika wa ibada hii atafanya mojawapo ya mambo haya:-
Kumuingilia mkewe.
Kutoka msikitini bila ya dharura ya msingi.
Kuondokewa na akili kwa kupatwa na wazimu, kulewa na baki
ya mambo mengine.
Kupatwa na hedhi au nifasi.
TANBIHI:
Kutoka msikitini kwa ajili ya kwenda kukidhi haja ya
kimaumbile kama kukidhi haja ndogo/kubwa. Kukoga na kununua mahitaji yake
ya lazima mithili ya chakula, kinywaji na mengineyo. Haya yote
hayabatilishi ibada ya itikafu, kwani imepokelewa kutoka kwa Bibi
Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alikuwa anapokaa itikafu haingii nyumbani ila kwa haja ya
mwanadamu”. Bukhaairy & Muslim
YALIYOSUNIWA KUTENDWA NA MKAA ITIKAFU:
Mwenye kukaa itikafu ni suna kwake kukithirisha:-
Ibada mbali mbali za suna.
Kusoma Qur-ani Tukufu.
Kuleta nyiradi mbali mbali (kumdhukuru Allah kwa wingi)
Kuleta istighfaari (kumuomba Allah msamaha wa dhambi).
Kumswalia Bwana Mtume.
Kuomba dua.
Na baki ya mambo mengine ya twaa ambayo yanamkurubisha mja
na kumuunga na Mola wake.
USIKU WA CHEO/MTUKUFU (LAYLATUL-QADRI).
Kama ambavyo Allah Mtukufu amemkirimu Mtume wake katika
mwezi wa Rajabu kwa kumpeleka safari tukufu ya Israa na Miiraji. Na kama
ambavyo amemkirimu katika mwezi wa Shaabani kwa kumbadilishia Qiblah
kutoka msikiti wa Baytul-Maqdis kwenda msikiti mtukufu wa Makah. Ndivyo
hivyo amemkirimu katika mwezi wa Ramadhani kwa kumpa usiku mtukufu.
Uliotukuzwa na kupewa hishima ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake.
Kuhusiana na hili Allah Mtukufu anasema: “ HAKIKA TUMEITEREMSHA
(Qur-ani) KATIKA LAYLATUL-QADRI (usiku wenye hishima kubwa). NA JAMBO GANI
LITAKALOKUJULISHA (hata ukaujua) NI NINI HUO USIKU WA LAYLATUL-QADRI? HUO
USIKU WA HISHIMA (huo) NI BORA KULIKO MIEZI ELFU. HUTEREMKA MALAIKA NA
ROHO MUAMINIFU (JibriIi) KATIKA (usiku) HUO KWA IDHINI YA MOLA WAO KWA
KILA JAMBO. NI AMANI (usiku) HUO MPAKA MAPAMBAZUKO YA ALFAJIRI”.
[97:1-5]
WAKATI WAKE:
Laylatul-Qadri inatarajiwa sana kuwa inapatikana katika
kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Ni kwa ajili hii ndio kukasuniwa
kukaa itikafu ndani ya kumi hili la mwisho ili kuuzengea usiku huu
mtukufu. Usiku ambao ibada ifanywayo humo ni bora zaidi kiujira kuliko
ibada ya miezi alfu moja isiyo na Laylatul-Qadri.
Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye
radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikaa
itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani na akisema: “Izengeeni
(itafuteni) Laylatul-Qadri katika kumi la mwisho la Ramadhani”.
Na katika riwaya yake nyingine, Bibi Aysha amesema:
“Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-linapoingia hilo kumi
(la mwisho) uhuhisha usiku. Na akawaamsha wakeze na akajipinda na
kujifunga kibwebwe (katika kufanya ibada) mpaka Allah alipomfisha. Kisha
wakeze wakakaa itikafu baada yake”.
KUUHUHISHA USIKU HUU KWA IBADA:
Kuuhuhisha usiku huu kwa kufanya aina kwa aina za ibada ni
suna. Kwa sababu hivyo ndivyo alivyofanya Bwana Mtume, wakeze na maswahaba
wake. Na hekima ya kuuhuhisha usiku huu kwa ibada ni kuikumbuka neema ya
Allah kwa waja wake. Neema ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake,
muongozo wa watu uliosheheni kheri za ulimwengu na akhera yao. Ikiwa Allah
Mtukufu ameutukuza usiku huu wa cheo hata akashusha sura nzima ndani ya
Qur-ani kwa jina la usiku huu. Basi ni wajibu wetu sisi kama waislamu
kuujua utukufu, cheo, hishima, umuhimu na thamani ya usiku huu kwetu.
Tulionyeshe hili kwa kupupia kuuhuhisha usiku huu kwa kila aina za ibada
na kujikurubisha kwa Allah. Muislamu mwenye akili, mkamilifu wa imani ni
yule anayeuzengea usiku huu na kuuhuhisha kwa ibada.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Atakayesimama (kufanya ibada) usiku wa Laylatul-Qadri kwa imani na
kutaraji malipo ya Allah, atafutiwa dhambi zake zilizotangulia”.
Bukhaariy & Muslim
ZAKAATUL-FITRI.
ZAKAATUL-FITRI NI NINI?
Zakaatul-fitri ni kile chakula au thamani ya chakula hicho
anachokitoa mtu ndani ya mwezi wa Ramadhani na kuwapa mafakiri na wenye
shida kabla ya Eidil-Fitri.
NINI HUKUMU YAKE?
Zakaatul-Fitri ni FARDHI mbele ya kundi kubwa la wanazuoni
(jopo la wataalamu wa fani ya Fiq-hi). Ufaradhi huu unatokana na hadithi
iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-AMEFARADHISHA Zakaatul-Fitri
ya Ramadhani. Pishi ya tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana,
mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika waislamu. Na ameamrisha
itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid)”.
Bukhaariy & Muslim
Bwana Mtume ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha
itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani. Yaani
katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.
NINI FALSAFA/HEKIMA YAKE?
Zakaatul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni
mwake ni:-
Kuwasaidia wenye shida katika siku ya sikukuu ili furaha
ienee kwa watu wote.
Kuunga mapungufu na kuziba makosa yanayoweza kuwa
yamemtokea mtu katika swaumu yake.
Haya tunayafahamu kupitia hadithi ya Ibn Abbas-Allah
awawiye radhi-kwamba yeye amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana
na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa
kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada
ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo”. Abuu Daawoud
INAMUWAJIBIKIA NANI?
Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila muislamu, mwenye uwezo
wa kutoa hata kama hamiliki kiwango cha zaka ya fardhi. Mwenye kumiliki
chakula chake na familia yake cha siku ya Eid, kinachozidi hapo ni wajibu
akitoe kama Zakaatul-Fitri. Atajitolea yeye mwenyewe na watu wote ambao
chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye. Hawa ni pamoja na wanawe
ambao bado wanamtegemea yeye, wazazi wake, mkewe na wale wote walio chini
ya ulezi wake kwa njia ya wajibu na wala sio kwa njia ya ihsaani/ khiari.
NINI KITOLEWACHO?
Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi
alichowaamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-maswahaba wake
kukitoa kwa ajili ya Zakaatul-Fitri. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile
iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye
radhi-amesema: “Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukimtolea Zakaatul-Fitri kila mkubwa na
mdogo. Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au
kibaba cha maziwa ya unga”. Bukhaariy & Muslim
Na imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah
amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikhutubu siku moja au mbili kabla ya Eid akasema: Toeni kibaba
cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana
au mtumwa, mkubwa au mtoto”. Abuu Daawoud
Mafaqihi wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia
chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na
shughuli zao mbali mbali. Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾
ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila
kichwa kimoja.
ITOLEWE LINI?
Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa
kuamkia siku ya Eid. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Eid.
Na wajibu wa kutoa haupomoki/hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa. Bali
itakuwa ni deni iliyo katika dhima ya aliyewajibikiwa kutoa. Na itamlazimu
kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na
akafanya uzembe kutoa. Na haisihi kuchelewa kutoa bila ya dharura na ni
haramu kisheria. Kwa sababu ucheleweshaji huu unapelekea kupotea kwa lengo
la utoaji wake ambalo ni kuondosha uhitaji wa masikini katika siku ile ya
furaha. Ambao Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amelizungumzia suala
lao kwa kusema: “Watosheeni na udhalili wa kuomba katika siku hii”.
Yaani siku ya Edil-Fitri.
APEWE NANI?
Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni wale wale wenye sifa
ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah:
“SADAKA HUPEWA (watu hawa): MAFAKIRI NA MASIKINI NA WANAOZITUMIKIA NA
WANAOTIWA NGUVU NYOYO ZAO (juu ya Uislamu) NA KATIKA KUWAPA UUNGWANA
WATUMWA NA KATIKA KUWASAIDIA WENYE DENI NA KATIKA (kutengeneza) MAMBO
ALIYOAMRISHA ALLAH NA KATIKA (kupewa) WASAFIRI (walioharibikiwa) NI FARDHI
INAYOTOKA KWA ALLAH, NA ALLAH NI MJUZI (na) MWENYE HEKIMA”. [9:60]
Lakini masikini na mafakiri ndio walengwa khasa wa
Zaakatul-Fitri kuliko mafungu mengine yaliyotajwa.
|