Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

TA'QIYM - KUONDOSHA UZAZI KWA KUJITIA UTASA

Faida

Allah mola mtukufu ametukuza na kumfadhilisha mwanadamu kuliko viumbe vingine alivyoumba:"NA HAKIKA TUMEWATUKUZA WANADAMU NA TUMEWAPA VYA KUPANDA BARANI NA BAHARINI, NA TUMEWARUZUKU VITU VIZURI NA TUMEWAFANYA BORA KULIKO WENGI KATIKA WALE TILIOWAUMBA KWA UTUKUFU ULIO MKUBWA (kabisa)" (17:70)

Tena Allah amemuhalalishia mwanadamu huyu vyote vilivyo vizuri vizuri na venye manufaa kwake na akamuharamishia vyote vilivyo vibaya vibaya na vyenye madhara kwake. Na akampa mwanadamu mwanaume mke wa jinsi yake, yaani mwanadamu mwenzie na akamruzuku kutokana na mke huyu kizazi (watoto):"NA ALLAH AMEKUUMBIENI WAKE KATIKA JINSI YENU, NA AKAKUJALIENI KUTOKA KWA WAKE ZENU WATOTO NA WAJUKUU, NA AKAKURUZUKUNI VITU VIZURI. BASI JE, WANAAMINI YASIYOKUWA YA HAKI NA KUZIKATAA NEEMA ZA ALLAH ?" (16:72)

hii ndiyo suna (kawaida/dasturi) ya Allah mola mwenye hekima aliyoiweka katika umbile la mwanadamu. kuiheshimu kawaida hii ya kimaumbile, bila ya kuichezea kwa kuizuia kutekeleza jukumu iliyoumbiwa ni kuiheshimu haki ya Allah mola mmiliki wa ulimwengu na vyote vilivyomo ni pamoja na viungo vyako vya uzazi "HIYO NDIYO KAWAIDA (suna) YA ALLAH ILIYOTANGULIA ZAMANI; WALA HUTAPATA MABADILIKO KATIKA KAWAIDA YA ALLAH" (48:23)

Hebu sasa tujaribu kuangalia neno "TA’AQIYM"- (sterilization). "ta'aqiym" hali ni neno la kiarabu lenya kumaanisha tendo cha kufanya mwanamke au mwanamume kuwa tasa. Kitendo hiki kina lengo la kumfanya muhusika (mwanamume/mwanammke) asiweze kuzaa ili kupunguza ongezeko la kasi ya idadi ya watu kama wanavyodai waasisi wa mpango huu. Tendo hili la kumtia mtu utasa ambao hakuumbwa nao hutekelezwa kwa kutumia njia mbali mbali (vasectomies) miongoni mwa njia zilizokuwa zikitumika zamani ni kuvunja na kupasua pumbu (testicles) za mwanamume sawa na ifanyikavyo kwa ngo'mbe (maksai) leo hutumika njia kwa kukata nrija unaosafisha mbegu za uzazi (manii) kadhalika hutumika njia za kumeza dawa au kudunga sindano ambayo huwa au kudhoofisha nguvu za vihayawani vya manii (spermatozoon) ama kwa upande wa mwanamke hufungwa mfereji wa mayai (fallopian tube) ili usiweze kusafisha na kuyapeleka mayai pahala ambapo yatarutubisha na kukuzwa kutokana na kukutana na mbegu za mwanamume. Kadhalika hutumika pia njia ya kuling'olea mbali fuko la uzazi (hysterectomy). Wakati mwingine hutumika njia ya kumeza vidonge kadunga sindano na kadhalika. Kumtia utasa mwanamume ni kitendo haramu kwa mtazamo wa uislamu, uharamu huu unatokana na kuzuia kazi yake maalumu (function) aliyoumbiwa na kumfanya ashabiane na mwanmke katika baadhi ya tabia (properties) zake. na tendo hili linapingana na hekima (wisdom) ya Allah katika kuumba jozi mbili; ya kiume na ya kike:"ENYI WATU! MCHENI MOLA WENU AMBAYE AMEKUUMBENI KATIKA NAFSI (asili) MOJA. NA AKAMUUMBA MKWE KATIKA NAFSI ILE ILE. NA AKAENEZA WANAUME WENGI NA WANAWAKE KUTOKA KATIKA WAWILI HAO.....". (4:1)

Hali kadhalika utaona kuwa ni haramu kumfanya tasa mwanamke kwa hekima hii. Utasa ni haramu kwa sababu unamaanisha kukata sababu ya kuzaliana, kuongezeka na kujaza ulimwengu kama alivyokusudia Allah mola muumba wa ulimwengu. Ni kutokana na sababu hii na nyinginezo ndio tinamuona Bwana Mtume rehema na amani zimshukie akilikemea na kuharamisha tendo hili la kujitia utasa.

Imepokelewa katika sahihi al Bukhariy kwamba Abu Hurayrah Allah amuwie radhi alimuomba Mtume rehma na amani zimshukie ruhusa ya kujihasi (awe tasa) kwa sababu ya kukosa gharama za kuolea naye (Abu Hurayrah) alikuwa kijana anachelea kutumbukia katika zinaa. Mtume akampa mgongo bila ya kumjibu mpaka (Abu Hurayrah) akayakiri maneno yake haya mara tatu, ndipo akamuambia:" ewe Abu Hurayrah kalamu imekwisha kauka kwa hayo yanayokukuta, basi ishi mpweke (bachelor) au acha (kuishi mpweke, yani oa)".

Imekuja katika riwaya nyingi zilizopokewa na Imam Ahmad kwamba baadhi ya masahaba walimuomba Bwana Mtume awape idhini ya kujihasi, akawakataza na kawambia: kujihasi kwa umati wangu ni kwa kufunga na kusimama usiku(kuswali). Imam Nawawiy pia ametaja katika sherehe ya Muslim (juzuu ya 9 sahifa77) kwamba kujihasi ni haramu kwa mwanadamu awe ni mkubwa au mtoto.

kwa hiyo basi suala la mtu kujifanya tasa, awe ni mwanamume au mwnamke ni haramu kisheria ikiwa anakusudia kuondosha uzazi moja kwa moja. Hii ni kwa sababu tendo hili linatishia kumaliza uzazi cha jamii ya mwanadamu ambacho ndicho lengo kluu la ndoa na kuumba kwa jinsi ya kike au kiume.

Ama ikiwa utasa huo ni wa muda maalum, kwa sababu maalumu inayokubalika kisheria. Tunakusudia kwa neno "utasa wa muda" kuzuia uzazi kwa kipindi fulani bila ya kuuathiri mfumo mzima wa uzazi yaani mtu anabakia na uwezo wake wa kuzaa pindi akitaka kufanya hivyo. Aina hii ya utasa inajuzu kisheria ikiwa iko sababu inayohitajika kifanya hivyo inazingatia/inakubalika katika msingi wa sheria. Udhuru/sababu hiyo inaweza kuwa kama ni kuondoa/kuzuia madhara yanayoweza kuhatarisha maisha ya muhusika iwapo atashika mimba. Au utasa huu wa muda utakusudiwa kuwa ni njia ya kutoa nafsi baina ya mimba na mimba ila kumpa mama fursa ya kuinyonyesha na kuijenga upya afya ya mama na mtoto.

Amenukuu Imam Bujayramiy kwamba ni haramu kutumia kitu/njia inayoweza kuzuia mimba kabisa (milele) ama njia inayochelewesha tu, ujauzito kwa muda fulani bila ya kuathiri uwezo wa mtu kuzaa si haramu. Na isitoshe ikawa ni udhuru/sababu inayozingatia kama vile ulezi wa mtoto si haramu na kama ikiwa bila ya udhuru, inakuwa ni haramu. (Hashiyatul-Khatwib, juzuu 4 sahifa 40)

 


TUJIFUNZE NA TUKUBALI: kuondosha kizazi ili mtu awe tasa kwa njia na sababu yeyote ile iwayo ni HARAMU maadam sababu hiyo haikufungamana na afya ya muhusika. na hata kama ipo sababu hiyo ya kiafya ni lazima hatua hiyo ichukuliwe kwa maafikiano na makubaliano baina ya mume na mke.


Forum | Guestbook | Tuandikie |