|
Utoaji mimba ni
kitendo cha kuikatisha bila ya ridha wala khiyari yake safari ya mwanadamu
mtarajiwa kuja katika ulimwengu huu kuishi kama alivyotaka
mola wake. Kitendo hiki humfanya katika kituo cha mwanzo cha safari
hii, ambacho ni tumbo la mama, na huweza kufanya kabla ya mwanadamu huyu
kuviviziwa/kupuliziwa roho yaani kabla ya mimba kutimiza umri wa miezi
minne na kuendelea.
Kuhusiana na
swala la umri wa kuviviziwa roho, huyu hapa mwanasayansi mahiri, Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: "Hakika
mmoja wenu hukusanywa umbo/umbile lake tumboni mwa mama yake hali
ya kuwa ni tone la manii kwa muda wa siku 40.kisha huwa pande la damu kwa
mfano wa muda huo (yaani siku 40) kisha huwa pande la nyama kwa mfano wa
muda huo, kisha (hapo ndipo) hupelekewa malaika akamviviza roho (katika
umri huo wa siku 120 ambazo ni sawa na miezi minne).........Bukhariy na
Muslim.
Utoaji wa mimba
ni swala lililoenea ulimwenguni kote hivi sasa na kujaribu kukemewa na
taasisi na madhehebu mbalimbali za kidini na hata baadhi ya wanasiasa.
hili ni suala ambalo linashughulisha akili ya wanawake wengi wajawazito.
hasa pale wanapojikuta njia pande, ama waendelee kubeba mimba mpaka
kujifungua au waitoe. Kwa kuwa tunaamini kuwa uislamu ni dini na mfumo wa
maisha unaokwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu : "BASI UELEKEZE
USO WAKO KATIKA DINI ILIYO SAWASAWA, NDILO UMBILE LA ALLAH ALILOWAUMBIA
WATU (yaani hii dini ya kiislamu inafikiana barabara na umbo la binadamu).
HAKUNA MABADILIKO KATIKA MAUMBILE YA VIUMBE VYA ALLAH. HIYO NDIYO DINI
ILIYO HAKI, LAKINI WATU WENGI HAWAJUII". (30:30)
Ni nini mtazamo
wa dini hii ya maumbile kuhusiana na suala zima la utoaji wa mimba?
Uislamu kama
dini au mfumo sahihi wa maisha unalitazama swala hili kwa mitazamo miwili
tofauti. uislamu unaliangalia suala la
utoaji wa mimba :
1) Baada ya
kiumbe kuviviziwa roho na
2) Kabla ya
kiumbe kuviviziwa roho
Mitazamo hii
miwili iliyosimama kwa kigezo cha kuviviziwa ama kutokuviviziwa roho
iniatufikisha katika hukumu mbili tofauti kama zifuatavyo:-
1)
HUUMU ZA KUTOA MIMBA BAADA YA KIUMBE KUVIVIZIWA\KUPULIZWA ROHO:
Uislamu
unakitizama kitendo cha kutoa mimba baada ya mimba kufikishwa umri wa
kuviviziwa roho, yaani miezi minne kama tulivyo kwishwa bainisha kuwa ni
kitendo cha haramu na ni jarima (crime/offence). Kwa mtazamo huu sii
halali kwa muislamu yoyote kushiriki ama kukifanya kitendo hiki dhalimu
kinachomnyima mwanadamu na mtarajiwa haki ya kuishi na kufurahia maisha.
Hili ni kosa la jinai dhidi
ya kiumbe hai aliyekamilika inalompelekea mtendaji wake diyah (Indemnity)
ikiwa mimba itatoka na kiumbe akawa hai au adhabu nyingine inayohusika
mali chini ya kiwango cha diyah
ikiwa mimba itatoka na kiumbe akawa tayari ashakufa tangu tumboni. Utoaji
mimba katika hali na mazingira haya utakua ni kosa la jinai hata kama
utafanywa na mama wa mwanamimba huyo au baba yake. Wote hawa watakuwa na
hatia mbele ya sheria na watastahiki kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Ama akithibiti
kutokana na kauli ya matatibu bingwa katika fanii hii ya uzazi kutokana na
uzoefu, elimu na utafiti wao kwamba mama kuendelea kubeba husika katika
kipindi hiki ni kuhatarisha maisha yake.
Hali ilivyo
inaonyesha lazima tu mama atakufa aidha katika kipindi hiki cha ujazito,
au wakati wa kujifungua au mara tu baada ya kujifungua kutokana na sababu
mbalimbali.
Katika hali na
mazingira kama haya uislamu unatoa nafasi itumike kanuni ya kuiondosha
lenye madhara kidogo kati ya mambo mawili yenye madhara. Itaangalia ikiwa
matabibu watasema kuwa kuendelea kuishi kwa mimba hiyo hakumaanishi
kingine zaidi ya kifo kwa mama mjazito na ikawa hakuna njia nyingine ya
kuyaokowa maisha yake ila ni kuitoa mimba hiyo. Utoaji mimba katika hali
hii na mazingira haya utakua ni jambo la lazima lisiloepukika. Kufa mama
ni madhara na hali kadhalika kufa mwanamimba pia ni madhara . Lakini
madhara haya ya kufa mwanamimba si makubwa sana ukilinganisha na madhara
ya kufa mama. Kwa mantiki hii mama huyu hatokuwa muhanga kwa sababu ya
kutoa maisha tya mwanamimba, kwani mama ndiye asili na shina halingolewi
kwa sababu ya tawi. Mama huyu tayari ana sehemu ya wajibu ya kuitekeleza
katika maisha haya, ambayo mwanamimba huyu hana, na isistoshe yeye mama
ndiyo msingi na nguzo kuu ya familia.
Ni jambo
lisiloingia akilini kuutoa muhanga uhai wake kwa ajili ya huyu mwanamimba
ambaye uhai ake haujathibiti bado; atazaliwa hai au atafia
tumboni:".... MAMA ASITIWE TAABUNI KWA AJILI YA MTOTO WAKE
....(2:233)
2. HUKUMU YA
KUTOA MIMBA KABLA YA KIUMBE KUVIVIZIWA ROHO.
Utoaji mimba
kabla ya mimba hajatimiza umri wa siku 120- yaani miezi minne ambayo ndio
umri wa kuviviziwa roho kiumbe. Ni halali kuitoa mimba iliyo chini ya
miezi minne kama kuna haja/sababu ya kupelekea kufanya hivyo. Na kama
hakuna haja ipelekeayo kutoa, basi itakua haramu kisheria kuitoa kauli
jumla, wanazuoni wa fiqhi wamekongamana na kuwafikiana kwamba utoaji mimba
ni kitendo haramu kisichokubalika katika umri wowote wa mimba/uajzito ila
kwa dharura iliyithibitisha na matabibu bingwa wa masuala ya uzazi.
NYONGEZA/FAIDA:
JE, AIBU/KASORO
(Defect/Blemish) YA JANINI/MWANAMIMBA (Embroy/Foetus) NI UDHURU (Excuse)
UNAOHALALISHA KUTOA MIMBA?
Ni jambo lililo
wazi kwa kila mmoja wetu kwamba baadhi ya mimba huwa na mapungufu ya
kimaumbile (ulemavu-deformities). Kutokana na hatua ya maendeleo
iliyofikia katika elimu ya sayansi na teknologia. Mapungufu/ulemavu huu
huweza kuonekana kupitia vyombo vya kisasa na il-hali mtoto angali
tumboni. Pia utaalamu huu huweza kuonyesha uwezekano wa mtoto mtarajiwa
kurithi aibu/ulemavu au maradhi aliyo nayo baba au mama yake. Na suala la
mtoto kurithi tabia, maumbile au maradhi kutoka kwa mmaja wa wazazi wake
ni suala linalozingatia na sheria, yaani uislamu unalikubali sasa
tujiulize:-
- Je
inajuzu kutoa mimba pindipo itakapokundulika mapungufu/aibu/ulemavu
mabaya utakaomfanya mtoto mtarajiwa kushindwa kuishi maisha ya
kawaida?
- Je
inajuzu kuitoa mimba hayo hata kama anaweza kuishi maisha ya kawaida
baada ya kuzaliwa pamoja na ulemavu/mapungufu hayo?
Inabainika
kutokana na kauli za mafaqihi kwamba mimba ikishakaa katika fuko/tumbo la
uzazi kwa muda wa siku 120 au miezi minne. Imethibiti kwa ushahidi wa
Quran na sunnah kuviviziwa roho kwa kiumbe hicho katika kipindi hicho.
Kutokana na kuviviziwa roho
huku, kiumbe huyu anatambulika na sheria kuwa ni mwanadanmu mwenye
kustahiki kapata haki zote za kimsingi kama wanadamu wengine. Ni kwa
sababu ya kuzotambua na kuzikubali haki za mtoto huyu aliye tumboni ndio
sheria ikajuzisha kumuekea wasiyah (Bequests), waqfu (Endowment) na
kustahiki kurithi (Inheritance). Kwa mantiki hii, mwanamimba huyu
anazingatia kisheria kuwa ni miongoni mwa nafsi ambazo Allah ameharamisha
kuuliwa ila kwa haki :...." WALA MSIMUUE MTU AMBAYE ALLAH
AMEHARAMISHA (kuuawa) ILA IKIWA (Imetokea) HAKI(ya
kuuawa)...."(6:151)
Kwa
hali hii ni haramu kuitoa mimba hiyo ila kama sababu ya msingi
inayohitajisha jambo hilo. Hata ulemavu/mapungufu ya kimwili yawe
yatakavyokua hayawezi kuwa ni sababu ya msingi ya kuhalalisha tendo hili
ovu. Hii ni kutokana na kuwa maendeleo ya elimu ya tiba yameonyesha kwamba
baadhi ya maradhi/ulelemavu huwa hautibiki kwa kipindi fulani na baadae
ukapatikana ufumbuzi wake yakatibika.Utakasifu ni milki yake Allah ambae
aliyefundisha mwanadamu chungu ya mambo aliyokua hayajui
NANYI HAMKUOEWA
KATIKA ILIMU (ujuzi) ILA KIDOGO KABISA (17:85)
Kwa hivyo suala
la kusema kuwa mimba hii ikizaliwa mtoto huyu atashindwa kiishi maisha ya
kawaida, kwa sababu hii ni bora kuitoa mimba , halikubaliki.
Ama ikiwa
kasoro/mapungufu haya ni ya kurithi kutoka kwa mmoja wa wazazi, inamkiniki
kuyazuia yasienee kwa kizazi chao kwa kuizuia mimba kwa muda. Na jambo
hili linajuzu kama dawa/tiba ambayo imeamrisha na sheria. Kama
haikumkinika kuzuia mimba baina ya mke na mume ambao imedhihirika kuwa
wote wawili au mmoja wao ana maradhi hatari ya kuambukiza ambayo mtoto
hawezi kusalimika nayo kama vile ukimwi (AIDS) na ikathibiti kwa vipimo
kwamba mtoto ameathirika na hatoweza kuishi, inajuzu kisheria kuitoa mimba
hii mida wa kuwa hajatimiza umri wa siku 120 yaani miezi minee tumboni.
Ama wanamimba
ambao wana kasoro/mapungufu ambayo inamkinika kutibika tumboni kwa dawa
atakazotumia mama yake au kwa njia ya operesheni (upasuaji) baada ya
kuzaliwa. Na wale wenye ulemavu ambao haiwazuilii kuishi maisha ya
kawaida. hata zote hizi hazizingatii na sheria kuwa ni udhuru
unaohalalisha kutolewa kwa mimba hizo. Kipimo kinachozingatia katika
kujuzisha utoaji wa mimba hizi ni kuthibiti kielimu kwa hatari ya
kasoro/mapungufu hayo na kwamba hayana tiba. Ama kasoro za kimaumbile kama
vile, upungufu wa mkono au mguu mmoja, hizi hazizingatiwi kuwa ni
mapungufu (udhuru) unaohalalisha utoaji wa mimba husika.Kwani maendeleo ya
kielimu yameonyesha uwezekano wa mtu kuwekewa viungo bandia na vikafanya
kazi bila ya tofauti kubwa na viungo halisi.
Haya ndiyo
tunayoweza kuyaelezea kuhusiana na suala zima la utoaji wa mimba.
USHAURI WA
BURE:
Ewe daktari
muisalmu wee, unayeshughulika na utoaji mimba. Elewa sheria haikuruhusu
kufanya kitendo hiki kiovu ila kwa dharura ambazo tumezibainisha humu.
Kinyume na hivi utakua umejitumbukiza katika hatia na midhambi ya kuwa
nafsi ambayo Allah kaharamisha kuuliwa. Tena usifikie uamuzi wa haraka
kabla ya kuthibitisha na vipimo na kashauriana na jopo la madaktari
wenzio.
|