Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MTIZAMO WA UISLAMU KUHUSIANA NA SUALA LA WINGI WA WATU.

 

Ni suala lisilo na shaka kwamba Uislamu umemfanya mtoto kuwa ni  haki ya shirika baina ya wazazi, baba na mama. Baba  kama mkuu wa familia ana sehemu ya haki na wajibu kwa mtoto kama ambavyo mama mlezi wa familia pia ana haki na wajibu kwa mwanawe. Mtoto katika Uislamu si wa baba pekee au wa mama pekee bali ni haki shirika baina yao na pia jamii. Kwa hivyo ni jukumu la baba kuhakikisha kuwa anampa mtoto katika utaratibu utaratibu ulionekana na sheria. Pia atambue kwamba baada ya kumpata mtoto ana dhima kuu ya kumlea kwa maana ya malezi kama atakiwanavyo na sheria. Ahakikishe anampa malezi  ambayo yatamfanya awe ni tunu kwake yeye kama mzazi (baba/mama) na kwa jamii yake.

 Jamii ifaidike nae na yeye afaidike nayo. Mtoto akiwa ni utaji/nembo ya mazazi wake, pia haachi kuwa ni tofali linaloungana na matofali mengine katika kuujenga ukuta imara (jamii). Ni suala lisilopingika kwamba uhai/uimara wa jamii/umma unategemea kwa kiazi kikubwa nguvu kazi ya jamii/taifa hilo na nguvu kazi hii kwa asilimia nyingi inategemea  ongezeko la watu na uwezo wao wa kufanya kazi.

 Uislamu umehimiza sana suala la uwekaji wa misingi imara ya nguzu kazi, heshima ya mtu binafsi na umma/taifa, upanuzi wa makazi (mipango endelevu ya miji), mgawanyiko wa madaraka na taifa kwa  ujumla. Misingi na malengo haya hayawezi kufikiwa kama khakuna ongezeko la watu ambao litamaanisha ongezeko la nguvu kazi ya jamii/taifa husika. Uislamu unaamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumba wanadamu na kuwaleta ulimwenguni wazaane na kuijaza  ulimwengu sambamba na kuustawisha. Kwa mantiki hiyo Qur-ani tukufu imeraghibisha na hadithi zimehimiza sana suala la ndoa pamoja na ukweli kwamba ndoa  ni suala la kiamumbile lisiloepukika. Hebu tuitupie jicho na fikra za kuangalia neema ya Allah aya hii: ‘NA ALLAH AMEKUUMBENI WAKE KATIKA JINSI YENU, NA AKAKUJAALIENI KUTOKA KWA WAKE ZENU WATOTO NA WAJUKUU. NA AKAKURUZUKUNI VITU VIZURI VIZURI. BASI JE, WANAAMINI YASIYOKUWA YA HAKI  NA KUZIKATAA NEEMA ZA ALLAH? (16: 72)

Ukitaka kuijua hadhi, daraja na nafasi ya watoto katika maisha haya, isome kwa mazingatio kauli hi ya Mola Wako:” MALI NA WATOTO NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA………” (18: 46)

Na huyu hapa Mtume wako Rehema na Amani zimshukie akilizungumzia suala la ndoa na kuzaana, hebu tumsikilize na tumuelewe :“Oaneni, mzaane, mtaongezeka, kwani hakika mimi nitajifakharisha nanyi kwa nyumati zingine siku ya Qiyama.

Kuna mazingatio/sababu kuu mbili za msingi ambazo zinapeleka kuwepo na ulazima wa jamii ya wanadamu kuoana na kuzaana kwa msingi ya sheria.

1.      Sababu ya kwanza ni ile haki ya jamii kwa mtoto kutokana na mchango wake katika kuiendeleza jamii kama mwanajamii. Hili linatokana na ukweli kwamba “ Mjenga nchi ni mwananchi, kwa hivyo ni dhahiri kwamba jamii/taifa lolote haliwezi kupiga hatua yoyote ya kimaendeleo ila kwa mchango wa nguvu kazi za wanajamii/wananchi wenyewe na khasa vijana ikiwa sote tunakubaliana hivi, basi hatutashindwa kuiona flasafa ya Uislamu katika kuhimiza suala la ndoa, na kuzaana.

2.      Sababu ya pili ni kutopingana na utaratibu wa maumbile aliotupangia na kutuimbia Mola wetu kwa kuvizuia viungo vyetu kutekeleza jukumu/kazi vilivyoumbwa kwa ajili hiyo tu. Sisi kama  viumbe hatumiliki maumbile yetu na utendaji kazi wake na hivyo basi hatuna haki ya kuuzuia au kuubadilisha utendaji kazi wake. Kwani kufanya hivyo hakutamaanisha kingine zaidi ya kupingana na maumbile ya Allah:…..”MOLA WETU NI YULE ALIYEKUPA KILA KITU UMBO LAKE KISHA AKAKIONGOZA (kufuata kinachowafiki umbo lake hilo).” (20: 50)

“………..AMEUMBA KILA KITU NA AKAKIKADIRIA KIPIMO (chake)” (25: 2)

“ ALIYEUMBA (kila kitu na) AKAKITENGENEZA. NA AKAKIKADIRIA (kila kimoja jambo lake) NA AKAKIONGOZA (kufanya jambo hilo)” (87: 2-3).

UISLAMU HAURIDHI WINGI USIOKUWA NA NGUVU.

Yanapokutana pamoja mazingatio/sababu kwa mbili hizi tulizozitaja ambazo ni:

1.                  Haki ya umma (jamii) na

2.                  Haki ya maumbile

Zinazokutana katika dharura/umuhimu wa kupatikana kizazi pia huungana pamoja tena katika janibu (Upande) nyingine muhimu ambayo ni “uwajibu wa kuondoa madhara”ambayo humfika mke au jamii. Madhara haya humsibu mama khasa bali na jamii kwa ujumla kutokana na matumizi, mabaya ya uhuru wa kuoa na kuzaa uliotolewa na Uislamu kama ambavyo maumbile yakiunga mkono na sayansi ya tiba yasivyoukiri ujauzito wenye madhara kwa mama  au mtoto na kuwafikiwa na Uislamu, dini inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu:”……DINI ILIYO SAWA SAWA NDIO UMBILE ALLAH ALILOWAUMBIA WATU (yaani dini  hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu)…………” (30:30.)

Kadhalika ni kama hivyo, Uislamu hawakubali wala kuridhia wingi usiokuwa na nguvukazi ya kuweza kujikimu wenyewe na kujilinda dhidi ya umma dhalimu. Wingi huu hauwezi kumpa Mtume fursa ya kujifakharisha siku ya kiyama mbele ya nyumati nyingine. Hivi ndivyo yanavyoashiria na kufahamisha maneneo haya ya Bwnaa Mtume Rehema na Amani zimshukie:  “Mataifa yanakurubia kuitana pamoja dhidi yenu kama sisimizi wanavyoitana kwenye sahani yao. Basi (hapo) akauliza mwenye kuuliza: Hivi ni kutokana na uchache wetu wakati huo? (Mtume) akamjibu: Hapana, bali nyinyi mtakuwa wengi, lakini wingi wenu huo utakuwa ni mithili lya takataka zinazosombwa na maji na Allah ataondosha ataondosha utisho wenu mioyoni mwa maadui zenu (mtakuwa hamtishi tena). Na atazionyesha nyoyo zenu udhaifu. Akauliza muulizaji: Ni upi udhaifu huo, ewe Mtume wa Allah? (Mtume) akajibu: Kuipenda dunia na kuchukia kufa: Abuu Daawoud.

Bila ya shaka tukiielewa vema hadithi hi tutaona na kujua kwamba inaashiria kuwa wingi usiokuwa na nguvu za kujihami uliotawaliwa na maradhi, ukagubikwa na umasikini na kukumbatiwa na ujinga hauna kheri wala manufaa. Jamii/uma  uliosheheni wajinga, masikini na wagonjwa, siku zote utakuwa ni uma ombaomba na tegemezi. Hali hii ya kutegemea misaada itauodolea uma huuhaiba mbele ya nyumati (mataifa) nyingine. Hautakuwa na sauti wala uhuru wa kujiamulia mambo yake wenyewe bali ni sharti ufuate  mapenzi na matakwa ya bwana mtoa misaada. Uislamu sambamba na kuhimiza watu kuzaana kwa lengo la kuisitawisha jamii ya wanadamu, pia umesisitiza na kuulinda  wingi huo na udhaifu na kila lipelekealo udhaifu na kuufanya kama wingi wa sisimizi unaoweza kusambaratishwa na kishindo kidogo tu. Uislamu ukaulinda na kuuhifadhi wingi huu kwa kuweka vigezo/kinga zifuatazo:

a./ Kuhimiza afya njema  ya mwili, akili na itikadi dhidi ya maradhi mbalimbali. Hili linaweza kuonekana kupitia mafundisho  sahihi ya Uislamu. Ndipo unaukuta Uislamu unampa ruhusa ya kula mchana wa mwezi wa Ramadhani mgonjwa ili kumuepusha na kuzidiwa na maradhi. Unamtaka ale ili kuiimarisha na kuijenga afya yake. Si hivyo tu bali umemruhusu hata msafiri nae ale ili kuonyesha kuwa Uislamu unaithamini na kuipa umuhimu wa kwanza afya yake na pia unatambua mashaka ya safari. Isitoshe ukamuhalalisha mtu kutayamamu kwa kutumia udongo/mchanga badala ya kutumia maji katika twahara ya udhu au josho, iwapo matumizi ya maji yatauzidisha ugonjwa au kupelekea kuchelewa kupona au kupata kovu/dosari yoyote mwilini.

Bila ya shaka mtu mwenye kufuatilia  kwa makini vifungu vya sheria ya kiislamu atagundua kuwa  uzingatiaji wa siha njema (afya) na maradhi ndio msingi mkuu wa hukumu nyingi kama sio zote. Zaidi ya yote hayo imekuja amri ya kuwataka waislamu kufanya dawa na kujitibia katika kauli nyingi za Mtume wa Allah - Rehema na Amani zimshukie. Bali yeye mwenyewe Bwana Mtume ameelekeza dawa kadhaa za kutibu maradhi mbalimbali. Hii ni miongoni mwa kauli zake hizo zenye  kuitakia mema jamii/umati wake: “Fanyeni dawa enyi waja wa MwenyeziMungu, kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hajaleta ugonjwa ila ameuwekea na dawa yake isipokuwa ugonjwa mmoja tu Uzee”, Imam Ahmad.

Pia ametahadhairhsa dhidi ya maradhi ya kuambukiza na hatua za kujikinga dhidi ya maradhi hayo yanapoingia katika kitongoji/mji, akasema: “Mtakapoisikia tauni iko mahala basi msitoke  kwa ajili ya kuikimbia (kwani kukimbia ni kuitoa hapo na kuieneza huko mkimbiliako)” Bukhaariy

b./  Kumpa mmojawapo wa wanandoa haki ya kuvunja mkataba wa ndoa iwapo:

  1. Itadhihirka kwamba mmoja wao ana maradhi yanayojilikwamisha lengo la ndoa kutimia

  2. Au ana maradhi yanayoweza kumuambukiza mwenzi wake au kizazi chao.

 Ikiwa kama Uislamu unajifakharisha kwa wingi na unataka nguvukazi katika usitawi wa jamii, basi unautaka uma/jamii uwe na wingi wenye nguvu, afya njema, elimu na jhali bora ya kimaisha ili kulinda hadi, heshima na itikadi yao sambamba na kuwa huru katika kuchagua.



Forum | Guestbook | Tuandikie |