Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

AZLU (COITUS INTERRUPTUS)

Faida

Nini Azlu?

Azlu katika Istilahi ya sheria ni kitendo cha mume kumwaga manii (mbegu za uzazi) nje ya uke wakati wa kufikia kilele cha tendo la ndoa. Kwa maana hii kitendo cha ndoa (jimaa) katika sura hii kinakamilika bila ya manii ya mume kukutana na yale ya mkewe. Nini lengo/madhumuni ya Azlu?

Mume na mke huitumia njia hii ya “Azlu” kwa maridhiano baina yao kwa lengo la kuzuia kushika mimba kwa sababu maalum inayozingatiwa na sheria. Sababu hiyo inaweza kuwa ni ulezi wa mtoto ambaye bado anahitaji malezi ya karibu zaidi ya mama yake. Kushika mimba wakati huo kutapelekea kumpokonya baadhi ya haki zake za malezi na hivyo kumsababishia udhaifu wa mwili na akili ambao unaweza kuendelea katika maisha yake yote.

Dalili/Ushahidi wa Azlu.

Zimepokelewa hadithi nyingi katika kuhalalisha na kujuzisha “Azlu” kwa ufumbulizo (uwazi) kabis pia ni vema ikafahamika kwamba “Azlu” ni tendo kongwe lililokuwepo hata katika zama za Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie. Baadhi ya masahaba wa Mtume waliitumia azlu kama njia ya kuzuia mimba na Mtume alikuwa akijua lakini hakuna kauli ya ufumbulizo iliyopokea kutoka kwa Mtume kwamba aliwakataza jambo hilo. Mas-ala haya ya “Azlu” ni mas-ala ambayo mafaqihi (wataalamu wa sheria ya Kiislamu) wameyashughukia sana kwa kuyatafiti na kuyajadili na kuyatolea maoni mbalimbali. Ukipenda kuziona rai na kauli za mafaqihi kuhusiana na mas-ala haya, unashauriwa kurejea vitabu kama:-

1.    Ihyaau uhumid diyn Imam Ghazaal

2.    Al-jaamii Liahkaamil Quraan Alqurtubiy

Zifuatazo ni baadhi ya “Nasi” na nukuu zinazoithibitisha “Azlu”

1.     Imepokelewa kutoka kwa Jaabiri Ibn Abdillah Allah amuwiye radhi kwamba mtu mmoja alimuendea Mtume Rehema na Amani zimshukie akamwambia: Hakika mimi ninaye mjakazi (suria) ambaye ni mtumishi na mnyweshelezaji wetu wa mitende. Mimi humzungukia (humuingilia) na sipendi ashike mimba! Mtume Rehema na Amani zimshukie akamwambia: “ Mfanyie  “Azlu” ukitaka, kwani hakika ya hali atapata tu alichokadiriwwa (akipate)”. Muslim.

Maelezo:    Kauli ya Mtume (kwani hakika ya hali atapata tu alichokadiriwa), inamaanisha kuwa ikiwa Allah amemuandikia kushika mimba, basi atashika tu, huyo mimba kwa muda uliokadiriwa ashike bila ya kizuizi.

2.     Imepokelewa (tena) na Jaabir Ibn Abdillah Allah amuwiye radhi amesema: “Tulikuwa tukifanya Azlu” katika zama za Mtume Rehema na Amani zimshukie na il-hali Qur-aan ikishuka.”

Maelezo:    Kauli ya Jaabir: … na il-hali Qur-aan ikishuka) inaonyesha uhalali wa suala zima la “Azlu”. Kwani kama ingelikuwa ni haramu, basi Qur-aan ingelikataza na kukemea kwani ilikuwa bado inaendelea kushuka. Kwa kuwa haikushuka aya kuharamisha, basi hii ni dalili na ushahidi wa wazi kwamba “Azlu” inajuzu ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo.

3.     Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbaas Allah awawiye radhi amesema: “Amekataza Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kumfanyia “Azlu” mwanamke muungwana ila kwa idhini yake”. Abdul-rasaaq na Al-baihaqiy

Maelezo:    Kauli ya Mtume “--- ila kwa idhini yake” inashiria kuwa “Azlu” inajuzu kwa ridhaa na idhini ya mke.

4.     Imepokelewa kutoka wa Abuu Said, amesema: Mayahudi walisema: “Azlu” ni uuaji mdogo, Mtume Rehema na Amani zimshukie akasema “Wameongopa Mayahudu, hakika Allah Mtukufu lau atataka kuumba cho chote, hawezi yeyote kumzuia”.Ahmad na Abuu Daawaoud.

Maelezo:    Kwa mujibu wa hadithi; “Azlu” si jinai “Azlu” haimzuii Allah kuumba anachokitaka na alichokikadiria ifuatayo inaliweka wazi hilo.

5.     Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik Allah amuwiye radhi amesema: mtu mmoja alikuja kumuuliza Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuhusiana na (suala la) Azlu’ Mtume akamjiibu: “Lau maji (manii) ambayo mtoto huwa kutokana nayo (maji hayo) utayamwaga juu ya mwamba, basi bila ya shaka Allah atamtoa mtoto katika mwamba huo. Au yatatoka (hayo maji) humo mwambani na Allah ataumba ataumba  tu nafsi atakayo yeye kuiumba.” Ahmad na Al-bazaar.

MADAKTARI (MATABIBU) WA KIISLAMU NA NJIA ZA KUZUIA MIMBA.

Kumbukumbu sahihi za kihistoria zinathibitisha kwamba matabibu wa kiislamu walitafiti njia mbalimbali za kuzuia mimba kwa misingi inayokubalika na uislamu. Kisha tafiti hizi na matokeo yake zikahamishwa  na kupelekewa ulaya na baada ya muda, ulimwengu ukafanywa uamini kwamba ziliasisiwa na matabibu wazungu wakristo mwenye kuangalia kwa uchunguzi katika vitabu vya utabibu vya zama za ustawi wa uislamu atagundua vimekusanya milango maalum inayoelezea njia mbalimbali za kuzuia mimba. Vitabu hivi vimeendelea kutumiwa na kusomeshwa katika vyuo vikuu vya ulaya mpaka katika karne ya kumi na saba Miladia. Vifuatavyo ni baadhi tu ya vitabu hivyo:-

1.    Al-qaanun cha Ibn Siynaa

2.    Al-haawiy Fiy Twibbi cha Ismail Al-jirjaaniy

3.    Al-kitaabul Malakiy cha Aliy Ibn Abbaas

4.    Al Irshaad cha Ibn Al-jaamii

5.    Tadhkirah Daawoud Al-antwakiy

Kwa mfano tatibu bingwa muislamu; Ibn Siynaa amesajili katika kiabu chake Al-qaanuun njia ishirini (20) za kuzuia mimba bila ya kuidhuru afya ya mama au mfumo mzima wa uzazi na kumsababishia ugumba. Njia zote hizi zilijaribiwa na kuonyesha mafanikio makubwa. Ziliendelea kuwa ni msingi usioepukika wa kuanzia kwa matabibu wa leo. Njia hizo zilikusanya kwa pamoja matumizi ya vyakula na madawa kama asali, siki (vinegar), tindikali (acid), chumvi na zeti ya hardali (mustard) na kadhalika.

HITIMISHO.

Nasi na nukuu za hadithi tulizozitaja katika kujuzu kwa “azlu” na kushughulika kwa mafaqihi na matabibu wa Kiislamu katika suala hili. Huu ni ushahidi dhahiri kwamba watu tangi enzi hizo kwa sababu mbalimbali za kimazingira (kijamii) na kisiha walihisi kuwa kuna haja ya kuwa na mpango wa familia (uzazi wa mpango). Kadhalika inaonyesha kwamba walilipatia ufumbuzi sahihi tatizo la uongezekaji wa idadi ya watu ilinaloupigisha ulimwengu kelele hivi sasa. Ufumbuzi wao huu ulifanywa kwa akili na werevu mkubwa chini ya misingi ya sheria za Allah. Isitoshe inadhihirisha ni jinsi gani ulivyokuwa mtazamo wao katika jukumu lao kwa familia zao. Kwa kuujua uzito na ukubwa wa dhima hii ndio waktafuta njia za kupanga familia ili ziwe ni wasila (njia ya kusaidia) wa kuwasaidia kuyatekeleza majukumu yao haya kama wanavyopaswa na walivyoamrishwa na sheria.


TUJIFUNZE NA TUKUBALI KUWA: Kushindwa kuwahudumia, kuwapa malezi bora watoto ikiwa ni pamoja na elimu ni kuwadhulumu. Na dhulma ni dhambi.

Allah ndiye Mjuzi mno.


Forum | Guestbook | Tuandikie |