|
Njia pekee
ya kutuwezesha kulifikia lengo hili ni kuwa na mpango wa familia. Mipango
huu utakuwa na dhima ya kuilinda nguvu na uwezo wa familia katika
kusimamia na kutekeleza wajibu wake. Kwa janibu (upande) wa kizazi
kinachopatikana, dhima ya mpango huu itakuwa ni kuzalisha kizazi chenye
afya njema kitakachopata haki zake zote za malezi. Ama kwa upande wa
jamii, mpango huu utakuwa na dhama ya kuhakikisha ustawi wa ukuaji wake na
kujitegemea kwa mahitaji yake. Kwa kuzingatia kanuni na misingi ya sheria,
lengo la mpango huu lifikiwe kupita njia zifuatazo:-
1.
Kuzuia kushika mimba kwa muda ili kumpa fursa mama kumnyonyesha
mwanawe kwa kipindi kamili. Qur-ani tukufu imeufanya muda wa kunyonyesha
kuwa ni miaka miwili kamili, tusome:- NA WANAWAKE WALIOZAA
WAWANYONYESHE WATOTO WAO MIAKA MIWILI KAMILI, KWA ANAYETAKA KUKAMILISHA
KUNYONYESHA; NA NI JUU YA BABA (yake) CHAKULA CHAO (hao watoto na mama) NA
NGUO ZAO KWA SHARIA WALA HAIKALIFISHWI NAFSI YOYOTE ILA KWA KADRI YA WASAA
WAKE. MAMA ASITIWE TAABUNI KWA AJILI YA MTOTO WAKE, WALA BABA (asitiwe
taabuni) KWA AJILI YA MTOTO WAKE NA JUU YA MRITHI (inapokuwa baba kafa) NI
KAMA HIVYO - - - [2 : 233]
Katika
aya hii tukufu kuna mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia, miongoni mwake ni
kama ifuatavyo:-
i.
Muda timilifu wa kunyonyesha.
Aya
inataja muda timilifu wa kumnyonyesha mtoto kuwa ni miaka miwili kamili.
Huu ndio muda uliowekwa na sheria wa kumnyonyesha mtoto kwa kuizingatia
afya yake na ya mama yake. Muda huu wa kumnyonyesha ukichanganywa pamoja
na ule muda ujauzito mpaka kujifungua, utakuta takriban kuna kipindi cha
miaka mitatu baina ya mimba na mimba nyingine. Hiki ni kipindi
kinachotosha kumfanya mtoto awe na siha njema na kukua vizuri.
ii.
Kutoikalifisha nafsi kuliko uweza (wasaa) wake.
MWENYE
WASAA AGHARIMU KADIRI YA WASAA WAKE; NA YULE AMBAYE AMEPUNGUKIWA RIZIKI
YAKE, ATOE KATIKA KILE ALICHOPEWA NA ALLAH, ALLAH HAMKALIFISHI MTU YE YOTE
ILA KWA KADIRI YA ALICHOMPA ---. [65 : 7]
Aya
hii inaashiria upande wa uchumi na umuhimu wake katika uwanja wa familia,
kwani ni upande huu wa uchumi ndio unaoipa familia uwezo wa kuihudumia
familia.
iii.
Taathira ya mimba, unyonyeshaji na malezi kwa afya ya mama.
Kipindi
cha ujauzito ni kipindi amacho mama hupitia katika hali ngumu sana
kimaumbile na kiakili (mawazo) NA TUMEMUUSIA MWANAADAMU AFANYE WEMA KWA
WAZAZI WAKE MAMA YAKE AMECHUKUA MIMBA YAKE KWA TAABU NA KAMZAA KWA TAABU
NA KUBEBA MIMBA YAKE HATA KUMWACHISHA ZIWA (uchache wake) NI MIEZI
THELATHINI. (46: 15).
Lishe
ya mama, kinga dhidi ya maradhi hulazimika kushirikiana na mwanawe
(mimba), unyonyeshaji na suala zima la ulezi huiathiri kwa kiasi kikubwa
afya ya mama kimwili, kiakili na kitabia. Kwa mantiki hii mama anahitaji
kupewa fursa ya kutosha kuweza kuijenga upya afya
yake, hivyo ndivyo inavyoashiriwa na aya:
..MAMA ASITIWE
TAABUNI KWA AJILI YA MTOTO WAKE
..
2.
Kufunga uzazi kabisa.
Iwapo
mke na mume, wote wawili au mmoja wao ana gonjwa sugu la kuambukiza.
Gonjwa ambalo mtoto atakayezaliwa hatasalimika nalo, ni lazima tu
litamkumba. Katika hali kama hii ni vema kwa wanandoa hawa wakakubaliana
kufunga uzazi kabisa ili kumuepusha mtoto atakayezaliwa na maambukizo
yatakayowagharimu wao na kumnyima furaha mtoto. Kwa ufafanuzi wa kina
kuhusiana na mas-ala haya unaweza
kurejea kitabu (NIHAYATUL MUHTAAJ) Juzuu ya nane (8) ukurasa 240, cha
Imam Ramliy.
Njia
mbili hizi ndizo tiba ya mpango wa uzazi inayomkinga na kumuepusha mtoto
na udhaifu unaoweza kumpata kutokana na kunyonyeshwa katika kipindi cha
ujauzito. Pia ndio kinga ya
maradhi ya kuambukiza kama ukimwi, ukoma (Leprosy) na kifua kikuu
(tuberculosis) ambayo anaweza kuambukizwa na wazazi wake. Kadhalika hizi
ndizo njia salama zitakazomuepusha mama na udhaifu wa mwili kutokana na
kushika mimba zito baada ya mwimba bila ya kupata muda wa kutosha
kupumzika na kujenga afya yake.
3.
Uwezo wa familia.
Uwezo
wa familia katika kuwakimu na kuwahudumia watoto wao na kuwalea ni kigezo
kingine kinachoweza kuhalalisha mpango wa uzazi ikiwa familia itachelea
kujitia hatiani kwa kushindwa kuwapa watoto wao watakaowazaa haki yao ya
malezi na hivyo kusababisha kuharibika kwa maisha ya watoto
hao baadaye. Baasi ni bora na inajuzu kwa familia hiyo kujihusisha
na mpango nwa uzazi kwa kutumia njia zinazokubalika kisheria. Uislam
hauzui mpango huu wa uzazi bali unauhimiza kwa ajili tu ya kuondosha
madhara yanayoweza kumpata mtu katika maisha yake. Ruhusa hii iantokana na
kanuni ya Uislamu isemayo. Madhara huondoshwa/huzuiwa kwa kiasi
imkinikavyo
..
TANBIHI:
Uislamu haukuruhusu kufunga/kuzuia uzazi kwa kile kinachoitwa
Mripuko/ongezeko la watu duniani. Naam, wachumi wanasema kuna ongezeko
kubwa la watu duniani, ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wa dunia. Ni
kweli, kutokana na sensa zinazofanywa kwa kuzingatia idadi ya watoto
watakaozaliwa baada ya miaka kadhaa. Lakini sensa na tafiti hizi
hazikukadiria eneo la ardhi litakalokaliwa na idadi hiyo na chakula
kitakachokidhi haja yake!. Tumefanya juhudi zipi za makusudi za kiuchumi
na kijamii sisi tuliokadiria idadi hiyo ya watu katika kukabiliana na
ongezeko hilo? Unaposema tupunguze idadi ya watu tu bila ya kusema tukuze
uchumi maradufu ili kukabiliana na idadi hiyo, utakuwa na mtazamo hasi
mtazamo dhaifu/lemavu. Uislamu unakutaka uwe na mtazamo chanya/mtazamo hai
utuambie mathalan, kufikia mwaka 2010 idadi ya watu itakuwa imeongezeka
kwa asilimia kumi (10%) ongezeko hili litahitaji eneo la ardhi za mita
mraba kadhaa, chakula tani kadhaa na huduma za kijamii (shule, hospitali)
kiasi kadhaa. Kisha uhimize kufanyakazi ili kufikia makadirio hayo ili
kulingana na ongezeko kadirio
hilo. Ni lazima tuwe na mitazamo yote miwili, hasi na chanya ili tuwe na
mizani na kusimama sawa bila ya kuyumba huku au kule. Kwa nini tukimbilie
dhana ya upunguzaji wa watu na hatuikimbilii dhana ya kuongeza uzalishaji
na kuboresha huduma za kijamii?? Kwa kuikimbilia dhana hii hasi ya
upunguzaji idadi ya watu kwa kuzuia mimba, utakuwa umeelekea upande kiasi
ambao unakusaidia kuwa mvivu na kuridhika na hatua ya maendeleo
uliyofikia. Kwa nini tusiikimbilie dhana chanya ya uongezaji wa
uzalishaji, dhana ambayo itatusukuma kuongeza nguvu kazi za makusudi ili
kukuza hali ya uchumi? Tuukiri kukweli huu:
NA AKABARIKIA HUMO NA
AKAKADIRIA HUMO CHAKULA CHAKE (cha kuwatosha watakaokaa humo, ameyafanya
haya) KATIKA SIKU NNE (mida minne). HAYA NI SAWA
KABISA KWA HAO WANAOULIZA (mambo wakataka kuyajua). (41:10)
Rasilimali
ya kututosha sisi leo na hao watakaokuja kesho tayari ipo, kinachohitajika
tu ni nguvu kazi iambatanayo na juhudi, maarifa na
matumizi sahihi ya rasilimali hiyo, sambamba na kuilinda kwa faida
yetu na faida ya vizazi vijavyo.
|