|
Leo ulimwenguni kote kutokana na
kile kinachojulikana kama wimbi la kwenda na
wakati, uhuru na haki ya mtu kufanya/kuishi
atakavyo; si jambo la kushangaza wala
kustaajabisha kuwaona vijana wa kiume wakiwa
wamejipamba kwa kuvaa mikufu, pete na hata
hereni za dhahabu. Hili leo si geni tena bali ni
jambo la kawaida na fakhari hata katika miji ya
mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi, ambako
asilimia kubwa ya wakazi wake ni wafuasi wa dini
ya Kiislamu kwa miongo ya miaka. Uvaaji huu wa
dhahabu kwa vijana wa kiume umeingizwa pande
zetu hizi za Afrika ya Mashariki na vijana
waliotoka huku kwenda nchi za Ulaya kutafuta
ajira hasa ya ubaharia. Hawa waliporejea wakiwa
wameuiga utamaduni huo wa kigeni na kuwaathiri
vijana wengine, limbukeni wenye kuiga kila
kiingiacho mjini.
Utamaduni huu wa vijana wa kiume
kujipamba kwa kuvaa dhahabu unakwenda kinyume na
utamaduni wa mila ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu
amemuumba mwanamume na Mwanamke na kumpa kila
mmoja maumbile na tabia zinazotofautiana na
mwenzake. Ikiwa hili linaashiria kitu, basi si
kingine bali ni kutofautiana pia katika nafasi
na majukumu ya kila mmoja wao. Nadharia
inaonyesha kuwa tabia na maumbile ya mwanaume ni
ukakamavu na ugumu, wakati ambapo tabia na
maumbile ya kike ni ulaini na ulegevu. Uislamu
unamtaka mwanaume alelekee katika mazingira
yaliyo mbali na udhaifu,unyonge na anasa
zinazoweza kunlegeza ili aweze kuwa imara na
mwenye nguvu katika kupambana na harakati za
maisha ya kila siku, ambapo sehemu kubwa ya
jukumu hilo amebebeshwa yeye na sheria . Sasa
kwa kuzingatia kuwa madini ya dhahabu na hariri
ni vitu vya anasa ambavyo humfanya mvaaji
aonekane amependeza machoni mwake yeye mwenyewe
kwanza na machoni mwa wengine na natija yake ni
kuvaana na maumbile ya kupendeza ambayo ni
ulaini na ulegevu. Pengine kwa njia moja au
nyingine hii ndio inaweza kuwa hekima/falsafa ya
kuharamishwa dhahabu na hariri kwa wanaume kwa
kuwa inakubaliana na tabia na maumbile yao.
Hebu tujaribu kuwa wakweli,
tuwatie katika mizani ya haki na uadilifu
wanaume wenye kuvaa dhahabu na wasiovaa dhahabu,
tutagundua nini? Bila ya shaka mtakubaliana na
mimi kuwa ipo tofauti ya dhahiri baina yao,
wavaao dhahabu watakuwa wameathirika na tabia na
maumbile ya kike. Taathira hii utaiona katika
mwendo wao, uzungumzaji wao, uvaaji wao na
wakati mwingine huiga hasa tabia za kike kama
vile kusuka nywele na kutumia vipodozi.
Ni kweli usiopingika kwamba
kujua hekima/falsafa ya kuharamishwa dhahabu na
hariri kwa wanaume, hii ni elimu isiyo na
manufaa na ni ujinga usiodhuru. Usiulize hekima
kwa kuwa kumeshurutishwa katika kuulizia hekima
ya amri au makatazo, awe huyo
muamrishaji/mkatazaji analingana sawa na
kufanana na huyo muamrishaji/mkatazwaji na hapa
ni suala la Mungu Muumba Muamrishaji na
mwanadamu kiumbe muamrishwa. Kwa mantiki hii
mwanadamu hana budi kuikubali na kuipokea amri
kwa kuwa Mola wake ameamrisha/amekataza,kisha
baada ya kutekeleza aliloamrishwa ndipo anaweza
kutafuata kujua hekima/falsafa ya amri ile.
Lakini kule kujua hekima/falsafa iliyomo katika
amri au katazoisiwe ni sharti ambalo kwanza ni
lazima litimizwe kabla ya kuamrika au
kukatazika. Muislamu wa kweli anaambiwa na Mola
wake:
“HAIWI KWA MWANAUME ALIYEAMINI
WALA KWA MWANAMKE ALIYEAMINI, ALLAH NA MTUME
WAKE WANAPOKATA SHAURI,WAWE NA HIARI KATIKA
SHAURI LAO. NA MWENYE KAMUASI ALLAH NA MTUME
WAKE, HAKIKA AMEPOTEA UPOTOFU ULIO WAZI (kabisa)
[33:36]
Kuharamishwa uvaaji wa dhahabu
kwa wanaume kumethibiti katika hadithi nyingi
sahihi zilizopokelewa kutika kwa Mtume wa
Mwenyezi Mungu –Rehema na Amani zimshukie.
- Amepokea (riwaya) Imamu Bukhaariy, Muislam
na Ahmad kwamba Mtume wa Allah “Amekataza
(kuvaa) pete ya dhahabu”.
- Imepokelewa kutoka kawa Ibn Abbaas-Allah
awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah aliiona
pete ya dhahabu kidoleni mwa mtu, akamvua na
kuitupa (huku) akisema “ Mmoja wenu
analikusudia kaa la moto na kulivaa mkononi?”
Mtu yule akaambiwa baada ya kwenda zake
mtume “ Itwae pete yako unufaike nayo.
Akawajibu Wallah hapana, kamwe sitaichukua
ikiwa aliyeitupa ni Mtume wa Allah –Rehema
na Amani zimshukie.” Muislam
- Na katika jumla ya riwaya zilizopokelewa
kwamba Mtume wa Allah –Rehema na Amani
zimshukie amesema : “ Ye yote mwenye
kumuamini Allah na siku ya mwisho basi
asivae hariri wala dhahabu.”
Al-musnad {Musnadul–Imam Ahmad}
|