Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

UISLAMU NA SUALA LA UTASA

 

Allah Sub-haana wa taala – kwa hekima zake tukufu zisizohojiwa: “HAULIZWI (Allah) ANAYOYAFANYA (kwani yote ni ya haki) LAKINI WAO (Viumbe) WATAULIZWA” (21:23). Humfanya huyu tajiri na yule fukara, humpa nguvu huyu na yule kumfanya mnyonge/dhaifu. Humfanya huyu kuwa mwerevu na yule kuwa mpumbavu, huyu humfanya mweupe na yule mweusi. “NA KAMA MOLA WAKO ANGALIPENDA, ANGALIWAFANYA WATU WOTE KUWA UMATI MMOJA. KWA HIVYO WATAENDELEA TU KUHITILAFIANA.” (11:118).

Lakini kumbe kuhitilafiana kwa viumbe katika lugha rangi, maumbile, hali za kiafya na kimaisha…….na…….ni alama/ishara ionyeshayo uweza wa Allah: “NA KATIKA ISHARA ZAKE (za kuonyesha uweza wake) NI KUUMBA MBINGU NA ARDHI, NA KUHITILAFIANA LUGHA ZENU NA RANGI ZENU NA (mengine yenu, na il-hali Muumbaji ndiye huyo huyo mmoja). KWA YAKINI KATIKA HAYA ZIMO ISHARA KWA WENYE UJUZI” (30:22).

Ni kutokana na  na hekima hizi hizi, Allah humfanya huyu kuwa ni mzai na yule kuwa ni tasa, huyu humpa watoto wa kike tu. Hivyo ndivyo  tunavyosoma ndani ya kitabu kisicho na shaka na kilicho muongozo kwa watu wote” UFALME WA MBINGU NA ARDHI NI WA ALLAH, ANAUMBA APENDAYO, ANAMPA AMTAKAYE WATOTO WA KIKE NA ANAMPA AMTAKAYE WATOTO WA KIUME, AU HUWACHANGAYA (watoto) WA KIUME NA WA KIKE (Kwa mtu mmoja)  NA HUMFANYA TASA AMTAKAYE, HAKIKA YEYE NI MJUZI, MUWEZA” (42:49-50)

Aya zinabainisha bayana kwamba anayetoa uzazi au utasa ni Allah pekee. Suala linajitokeza. Je, ni halali kwa wawili  (mke na mume) waliopewa mtihani wa utasa na Allah kutafuta mtoto kwa kutumia njia za kitaalamu kamavile “Upandikizaji wa mbegu za uzazi katika tumbo la uzazi”?!.

Tunasema hali ya kuwa tunalitarajia sana msaada wa Allah aliye Mjuzi mno: Upandikizaji tunaoukusudia hapa ni ule ukutanaji wa mbegu za uzazi za mwanamume na yai la mwanamke bila ya maingiliano ya moja kwa moja ya kimwili kwa lengo la kupata mtoto. Huu ndio upandikizaji tunaouzungumzia hapa. Tafadhali elewa hivyo.

Suala hili la upandikizaji wa mimba si muuujiza wala suala geni ulimwenguni hapa. Asili ya mwanadamu iligundua uwezekano wa jambo hili miongo kadhaa ya miaka iliyopita. Historia iantuonyesha kwamba Waarabu waliitumia njia hii ya upandikizaji katika kupandikiza mitende katika karne ya kumi na nne (14thC A.D). Nazo nchi za Magharibi zikaigundua  njia hii katika karne ya kumi na nane (18thC AD) karne nne baada ya Waarabu. Mtu wa kwanza kufanya jaribio hilila upandikizaji kwa binadamu alikuwa ni daktari wa Kiingereza, John  Hunter mnamo mwaka 1899 miladia, na jaribio hili lilihusisha mbegu za mwanamume (manii) kwa mkewe. Ama huu upandikizaji wa mimba kwa mwanamke bila ya kutumia bmegu za mumewe bali kwa kutumia mbegu za mtu mwingine, huu ulifanywa kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa mnamo mwaka 1918 Miladia. Kutoka hapo ndipo ulipoenea katika pande mbalimbali za ulimwengu ulioendelea kisayansi na teknolojia mpaka wakafikia kuanzisha benki ya mbegu za kiume (manii) kwa lengo hili la upandikizaji. Utaalamu huu ukaendelea mpaka ukafikia hatua ya kupandikiza mbegu nje ya tumbo la uzazi, zikapandikizwa ndani ya chupa iliyoandaliwa maalumu kwa kazi  hiyo. Chupa hii huwa mithili ya kitaru cha miche ambapo ikikua huenda kupandikizwa shambani. Hivyo ndivyo ilivyo kwa chupa hii, baada ya muda fulani kupita tangu kupandikizwa kwa yai, yai hilo hurejeshwa tena katika tumbo la mwanamke lililotwaliwa kwake yai hilo au kwa mwanamke mwingine yeyote. Na pengine  huwekwa katika tumbo la hayawani mwingine asiye mwanadamu ili aibebe mimba hiyo aliyopandikizwa badala ya binadamu (mwanamke). Hapa ndipo ulipofumuka upinzani dhidi ya upandikizaji huu wa mimba kutoka katika majukwaa ya kidini na ya kisiasa. Khasa khasa pale upandikizaji unapowahusisha watu wasiokuwa mke na mume, au ulezi wa mimba anapopewa mwanamke mwingine au mnyama.

Mafaqihi (Wataalamu mabingwa wa sheria ya Kiislamu wamesema kwa sura ya jumla kwama.

·        Utapokuwa upandikizaji wa mimba ni kwa manii ya mume kwa mkewe, hapana kizuizi iwapo kutakuwa na uhakika na uthibitifu wa hilo.

·        Ama upandikizaji utakapohusisha manii ya mtu mwingine asiye mume, hapa itakuwa hairuhusiwi kisheria.

Baada ya kutolewa fatua hii, maswali mengi yakachimbuka kutokana nayo, yakaelekezwa katika Baraza la Fatwa, la Misri. Baraza likayajibu maswali hayo mwezi 6 mfunguo 8, mwaka 1400 Hijiria sawa na tarehe 23 Machi, mwaka 1980 Miladia, chini ya Mufthi Shaykh Jaadul –haq Aliy jaadul-Haq.

Ufuatao ni mukhtasari wa fatwa hiyo kwa utaratibu wa swali na jawabu:

SWALI 1:    Kuna hukumu gani iwapo yatatwaliwa manii ya mume na kupandikizwa mkewe aliye tasa (asiyeshika mimba) wakiwepo wote wawili (mume na mke)?

JAWABU:   kwa kuwa lengo kuu la mafungamano na mahusiano ya kimaumbile baina ya mume na mke ni kupata watoto ili kuendeleza jamii ya wanadamu. Na kukawa kuna matatizo ya kimaumbile au maradhi baina ya mke na mume au mmoja wao. Matatizo yanayopelekea kushindikana kutunga mimba katika njia ya kawaida ya kimaumbile kama alivyotaka Allah. hapo anaruhusiwa  kisheria kutumia njia hii ya upandikizaji iwapo wawili hao (mke na Mume) wataona kuna haja ya kufanya hivyo. Kwa sharti kwamba upandikizaji  mimba huu uwe ni kwa dhati ya mani ya mume kwa mkewe, bila ya kubadilishwa au kuchanganywa na manii ya mwanamume mwingine au mnyama.

SWALI 2:    Vipi, iwapo manii ya mume hayana uwezo katika upandikizaji, yakatwaliwa manii ya mwanamume mwingine na kupandikizwa kwa mkwe.

JAWABU:   Kupandikizwa mke manii ya mwanamume mwingine asiye mumewe kwa kigezo cha kutokufaa manii ya mumewe katika suala zima la upandikizaji mimba ni jambo lililohalalishwa kisheria. Uharamu huu unatokana na kuchanganyika kwa nasabu na kumnasibisha mtoto na baba ambaye hatokani na manii yake manii ya mtu mwingine, kisha mtoto awe wa mtu mwingine?

SWALI 3:    Vipi, ikiwa yatachukuliwa manii  ya mume na kupandikizwa na yai la mwanamke asiye mkewe. Kisha yai hili lilopandikizwa   likahamishwa na kwenda kuwekwa katika tumbo la uzazi la mwanamke ambaye mumewe ndiye mwenye manii yale.

JAWABU:   Sura hii hatofautiani sana na ile  sura ya kwanza, inaingia chini ya maana ya zinaa. Mtoto atakayeumbwa na kuzaliwa kupitia utaratibu huu atahesabika kisheria kuwa ni mtoto wa haramu (wa nje ya ndoa) kwa yakini. Hata kama manii haya ni ya mume lakini kama ijulikanavyo ni kwamba mimba haitungi ila kwa idhini na mapenzi ya Allah wakati manii ya mume yanapokutana na yai la mkewe. Katika sura hii yai la mke linakosekana na badala yake linatumika yai la  mke linakosekana na badala yake linatumika yai la mwanamke mwingine asiye mke wa mwanamume mwenye  manii husika. Hili linamfanya mke asiwe konde kama alivyokusudia Allah iwe:” WAKE ZENU NI KAMA KONDE ZENU. BASI ZIENDENI KONDE ZENU MPENDAVYO……..” (2:223).

Katika sura hii mke hakuwa konde kwa sababu zao (mtoto) limezalishwa na konde nyingine (mwanamke asiye mke). Mimba anayoibeba mwanamke ni lazima iwe ni natija ya maingiliano ya kisheria ya kimaumbile baina ya mke na mume. Iwe ni kwa njia ya kawaida ya kukutana katika tendo la ndoa au kwa upandikizaji wa yai na kisha kurudishwa katika tumbo la uzazi ili likue na kisha kuzaliwa  mtoto kama alivyosema Allah: “….HUKUUMBENI MATUMBONI MWA MAMA ZENU – UMBO BAADA YA UMBO – KATIKA VIZA VITATU……..” (39:6)

Fatwa hii ni ndefu lakini sisi tumeifupisha kwa kiasi ambacho kitakusaidia kukupa mwangaza katika suala zima la upandikizaji wa mimba ambao leo umeenea ulimwenguni kote khasa ulimwengu wa Magharibi. Kwa ufahamu zaidi juu ya suala hili ikiwa hukutoshelezwa na maelezo yetu, unaweza kuwauliza masheikh waliokuzunguka hapo ulipo.


 


Forum | Guestbook | Tuandikie |