Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

UISLAMU NA SUALA LA HIJABU-III

 

Naam, ni kweli kuwa Uislamu umempa ruhusa mwanamke atoke nyumbani kwake kwenda kufanya kazi. Lakini ni vema tukakiri kuwa hakuna ruhusa/uhuru usio na mipaka, je, aende kufanya kazi katika mazingira gani? Tufuatane pamoja, hatua kwa hatua:-

1.  Apewe idhini na mumewe au walii wake, yaani babu, baba, kaka, ami na kadhalika. Tumeona katika somo lililopita kwamba wanawake wanatakiwa wawaombe waume zao idhini/ruhusa ya kwenda msikitini kwa mujibu wa hadithi ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie. Sasa iwapo kwenda msikitini kunahitaji idhini ya mume, basi ni aula (bora) zaidi kutoka kwenda kufanya kazi kupate idhini na baraka zote za mume. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anasema katika kubainisha haki za mume kwa mkewe: “…….Na wala (mwanamke) asitoke nyumbani kwake ila kwa idhini yake (mume). Ikiwa atafanya hivyo (atatoka bila ya ruhusa ya mumewe) watamlaani malaika wa mbingu na malaika wa adhabu mpaka atakaporejea (nyumbani kwake) Twabaraany.

2.  Aende kazini na afanye kazi il-hali akiwa amevaa mavazi ya heshima na sitara kama sheria inavyomtaka. Nguo zisiwe.

-      Nyepesi zinazoonesha rangi ya mwili.

-      Zenye kubana kiasi cha kuliacha finyango la mwili kuonekana na aonaye.

-     Na mapambo ya kuvutia mno kiasi cha kuwashawishi wanamume kumkazia macho.

3.  Asikae faraghani, peke yake na mtu ambae si maharimu yake hata kama ndie bosi wake kazini. Lazima awe katika mazingira ya watu wengine ambapo farahga mazingira ya watu wengine ambapo faragha haina nafasi.

4.  Usiwepo msongamano utakaopeleka kugusana wanamume na wanawake kama inavyokuwa masokoni, katika vyombo vya usafiri na kadhalika.

5.  Kazini kuwepo na mazingira ya amani ambayo yatamdhamini kutokufikwa na matendo yote mabaya, ya fedheha na yenye kuudhalilisha utu wake. Kama vile kufanya kazi mahala pa uchafu, katika vilabu vya pombe, nyumba za kulala wageni, mahoteli ya kitalu, mahala panapochezwa kamari, humu mote ni mahala ambapo mwanamke anaweza kudhalilishwa kijinsia kwa kubakwa au kudhalilishwa kisaikolojia kwa kutukanwa na mambo mengine machafu yenye kufanana na hayo.

6.  Kazi isimzuie kutekeleza wajibu wake kwa Mola wake, mumewe na wananwe, kwani kutokutekeleza wajibu ni haramu. Kwa mantiki  hiyo kila linalopelekea kutokutekeleza wajibu nalo litakuwa ni haramu.

Haya ndiyo mazingira ambamo mwanamke wa Kiislamu anaruhusiwa kufanya kazi .

Naam ni ukweli, ndiyo ni ukweli uliodhahiri na usiopingika kwamba kila uma duniani una nembo yake rasmi ambayo inautambulisha uma huo mbele ya nyumati nyingine, nambo  hiyo huundwa na mila, desturi na utamaduni wao. Vyote hivi huonekana kupitia namna yao ya kula, kunywa, mavazi maskani na sanaa zao mbalimbali. Mambo yote haya ndio huonesha na kutoa picha ya ustaarabu na itikadi za uma husika.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumba watu wakiwa wanatofautiana katika mambo mengi, na tofauti hii itaendelea kuwepo mpaka mwisho wa dunia. Ukweli huu usio na shaka unajidhihirisha kupitia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “ NA KAMA MOLA WAKO ANGALIPENDA, ANGALIWAFANYA WATU WOTE KUWA UMATI MMOJA. ( Angaliwafanya wote kufuata kitu kimoja. Lakini amewapa akili na nguvu ya kutumia akili zao hizo watakavyo, ikiwa kwa wema au ubaya.)  KWA HIVYO WATAENDELEA TU KUHITILAFIANA. ISIPOKUWA WALE AMBAO MOLA WAKO AMEWAREHEMU. NA KWA (rehema) HIYO MUNGU AMEWAUMBA (ila wenyewe tu hao wengine wamekhitari mabaya) NA LITATIMIA NENO LA MOLA WAKO (la kuwa): KWELI KWELI NITAIJAZA JAHANAMU KWA MAJINI A BINADAMU WOTE (walio wabaya). (11:118-119).

Uzuri au ubaya wa utamaduni wa jamii Fulani ya watu unategemea kwa kiasi kikubwa mtizamo wa jamii nyingine ya nje. Ni wazi kuwa utamaduni unaoonekana mzuri tu kwa jamii Fulani ukawa ni mbaya machoni mwa jamii nyingine. Mwanamke wa kihindi mathalan ana vazi lake rasmi lijulikanalo kama “Saari” vazi hili ndilo humtambulisha mbele ya jamii nyingine kuwa yeye ni nani. Mwanamke huyu hulionea fakhri vazi lake hili na hulivaa popote pale ulimwenguni hata kama anashiriki katika vikao vikuu vya jumuia za kimataifa. Kwa kuwa ni utamaduni wake, yeye binafsi haoni haya kulivaa vazi lake hilo na hakuna yeyote aliyethubutu kumkosoa au kumlaumu kwa uvaaji wake huo, hata, wale watu wa nchi za magharibi wanaojidai kuwa ni mabingwa wa kukosoa na mahodari wa kusema. Pengine linaweza likawa si vazi la kikazi, lakini ndio vazi linalovaliwa na mwanamke muhindi mlalahoi na hata aliyekuwa Waziri Mkuu bibi Indra Ghandi. Bado hakuna aliyethubutu kusema kuwa vazi hili la “Saari” linamzuia mwanamke huyu wa kihindi kufanya kazi mbalimbali za uzalishaji.

 Mwanamke wa Ulaya mpaka mwanzoni mwa karne ya ushirini (20thC) alikuwa akifunika kichwa chake na kuvaa mavazi marefu na hakukuwepo na wa kumlaumu au kumkosoa. Lakini taratibu kwa kigezo cha kile kinachodaiwa maendeleo na kwenda na wakati akaanza kulibadili vazi lake hili mpaka kufikia hapa lilipo leo, likimuacha bila ya sitara na kuifanya bishara ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie  “itimie” Makundi mawili ya watu wa motoni sijayaona (bado katika uhai wangu) watu wenye fimbo kama mikia ya ng’ombe wanawapiga watu, na wanawake waliovaa na il-hali wako uchi, watembeao kwa maringo……………………” Muslim.

Ama mwanamke muislamu anayemuamini Allah, Mtume wake na  siku ya kiyama, Uislamu unamtaka avae mavazi ya sitara. Mavazi ambayo kumsababishia  usumbufu na uchokozi kutoka kwa wanaume na natija yake ikawa ni kudhalilishwa kijinsia. Na si sahihi kusema kuwa vazi hili la kiislamu linamnyima uhuru mwanamke kushiriki vema katika kazi mbalimbali za kimaendeleo. Kwani tumewashuhudia wanawake wengi katika nchi zenye Waislamu wengi wakifanya kazi katika taasisi na mashirika mbalimbali ya kibinafsi na hata yale ya kiserikali, yakiwemo mashirika ya ndege wakifanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa kabisa. Mavazi yao hayakuwa na wala hayajawa na kikwazo katika utendaji wao wa kazi na majukumu yao kama sehemu muhimu ya jamii. Kwa hivyo tuhuma hizi hazina msingi wala hoja itokanayo na utafiti wa kielimu. Hizi ni kelele za watu wa magharibi wanaotaka kuona mila, desturi na utamaduni wao unaitawala dunia na hili ni kinyume kabisa na maumbile waliyoumbiwa wanadamu.

Kutokana na wepesi wa dini hii inayokubaliana na maumbile ya mwanadamu, imemruhusu mwanamke kutoka kwenda kufanya kazi na wala haikumfungia ndani tu kama inavyodaiwa. Kulichofanywa na dini hii ni kumuandalia mazingira bora ambamo humo ataweza kufanya kazi kwa amani na utulivu bila ya kudhallishwa wla kubughudhiwa na yeyote awaye. Ikamjengea ukuta wa kumkinga na madhara, kero na maudhi yanayoweza kumpata kutoka kwa wanajamii wengine. Ni wajibu wake na yeye pia ajizuie kuwaudhi au kuwasababishia wengine kero/madhara kwani mwanamke, mwenyewe ndiye chanzo cha madhara mengi yanayomsibu hivi sasa. Lau angelishikamana barabara na dini yake na akatambua kwamba Hijabu ni haki yake na ipo kwa maslahi yake asingefikia hapa alipo leo ambapo anaonekana kama ni chombo cha kutangazia matangazo ya biashara na kumstarehesha mwanaume, akinunuliwa kama bidhaa dukani/sokoni. Angelibakia na utu na heshima yake kama mwanamke na mama wa jamii.

Mtu anaweza kuthubutu kusema kuwa, baadhi ya kazi zinahitaji vazi rasmi. Tunasema kuwa kazi haiwezi kuwa ni sababu/ruhusa ya kuvunja sheria ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambae ndiye aliyemuamrisha mwanamke kuvaa vazi la sitara. Aliyeweka sheria ya kuvaa vazi fulani mahala fulani ni jamii, swali ni je, tuitii sheria ya Allah isiyo na upungufu au utitii kanuni iliyowekwa na mwanadamu mpungufu? Tusome: “KISHA TUMEKUWEKA JUU YA SHARIA YA AMRI YETU, BASI IFUATE, WALA USIFUATE MATAMANIO YA WALE WASIOJUA (kitu) KWA YAKINI HAO HAWATAKUFAA CHOCHOTE  MBELE YA ALLAH…………..” ( 45:18-19]


 

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |