|
ZIJUE
NASAHA ZA WIKI
Nasaha za wiki
ni ukumbi wa kunasihiana, kubadilishana,kukosoana,kushauriana,
na kuelimishana katika nyanja mbalimbali.
Tutakumbushana
kupitia nasaha za wiki juu ya yale yatupasayo
kutenda ama kutotenda kwa mujibu wa amri na
maelekezo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kadhalika
nasaha za wiki itakuwa ikikuletea msimamo na
kauli ya Uislamu juu ya kadhia/masuala
mbalimbali yanayojitokeza ulimwenguni hivi leo
kutokana na kupanuka na kukua kwa elimu ya
sayansi na technolojia. Masuala kama vile
upandikizaji na viungo, watoto wa chupa., uzazi
wa mpango, utoaji wa mimba na kadhalika.
CHIMBUKO
NA MSINGI WA NASAHA ZA WIKI
Nasaha za wiki
ni natija na zao la kauli tukufu ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu: "NA WANAOAMINI WANAMUME NA
WANAOAMINI WANAWAKE, NI MARAFIKI WAO KWA WAO .
HUYAAMRISHA YALIYO MEMA NA HUYAKATAZA YALIYO
MABAYA, NA HUSIMAMISHA SWALA NA HUTOA ZAKA NA
HUMTII ALLAH NA MTUME WAKE. HAO NDIO AMBAO ALLAH
ATAWAREHEMU. HAKIKA ALLAH NI MWENYE NGUVU NA
MWENYE HEKIMA" [ 9:71]
Kadhalika nasaha
za wiki zimejiegemeza katika kauli ya Bwana
Mtume –Rehema na Amani za Allah zimshukie
"Yeyote miongoni mwenu atakayeuona
uovu,basi auondoshe kwa mkono wake, kama
hakuweza (kuuondosha kwa mkono) basi (auondoshe)
kwa ulimi wake na kama hakuweza basi (achukie)
kwa moyo wake na huko (kuchukia) ni imani dhaifu
zaidi" Muslim.
Hizi ndizo hatua
za kufuata katika kuuondosha uovu katika jamii
kama alivyotuelekeza Bwana Mtume. Uzoefu
umethibitisha kuwa ugonjwa ukipuuzwa na kuachwa
mwilini bila ya kupatiwa matibabu muafaka na
katika wakati muafaka, maradhi hayo husambaa na
kuenea mwilini na hatimaye husababisha madhara
makubwa na pengine kifo. Hali ni hiyo hiyo pia
kwa maasi, uovu ukiachwa bila kukemewa na mtu
akawa huru kutenda uovu bila kuulizwa wala
kukatazwa, matokeo yake ni kufa kwa jamii
kimaadili. Matokeo ni kuzaliwa jamii isiyo na
chembe ya utu, jamii ya waenda uchi, jamii ya
walevi, wavuta bangi na kadhalika.
Sasa ili
kuepusha kujenga ukuta mzima kwa sababu ya
kutokuziba ufa pale pale tu ujikokezapo. Website
yako WEBSITE UISLAMU ikaonelea ni vema
ikakuletea fursa hii ya Nasaha za wiki ili uweze
kujikumbusha na kujielimisha juu ya lipi utende
upate radhi za Mola wako Muumba na lipi usitende
ili uziepuke ghadhabu na adhabu kali za Mola
wako aliye mkali mno wa kuadhibu. Mola wetu
Mtukufu tunakuomba ututie chini ya kauli yako
tukufu:
"……BASI
WAPE HABARI NJEMA WAJA WANGU HAWA AMBAO
HUSIKILIZA KAULI ( nyingi zinazosemwa),
WAKAFUATA ZILE ZILIZO NJEMA, HAO NDIO
ALIOWAONGOA ALLAH NA HAO NDIO WENYE AKILI"
[39:17-18]
MADA
YA KWANZA:
RUSHWA:HATARI
NA ATHARI ZAKE
Msemo
"Rushwa ni adui wa haki", kelele
zinapopigwa ulimwenguni kote na wanasiasa,
viongozi na serikali na wale wa dini dhidi ya
rushwa. Haya yote ni ishara na dalili wazi juu
na namna jamii inavyoathirika na kukerwa na
mdudu mbaya huyu, rushwa. Rushwa ni mdudu mwenye
athari mbaya sana kwa jamii, mdudu anayeua bila
huruma haki za kimsingi na za kijamii.
Mwenyezi Mungu
Mtukufu anatuasa:
"WALA MSILIANE MALI ZENU KWA BATILI NA
KUZIPELEKA KWA MAHAKIMU ILI MPATE KULA SEHEMU YA
MALI YA WATU KWA DHAMBI NA HALI MNAJUA"
[2:188]. Amesema swahaba wa Mtume-Ibn
Abbas-Allah amuwiye radhi-katika kuitafasiri aya
hii: Katazo hili linamuhusu mtu mwenye kumiliki
mali bila ya uhalali wowote, kisha akamuendea
hakimu kutaka kupata uhalali wa kumiliki na
ilhali anajua fika kuwa haki si yake. Huyo
aelewe kuwa anapata dhambi na anachokila ni
haramu.
Aya inafahamisha
kuwa hukumu ya huyu hakimu kumuhalalishia
dhalimu na kumpa haki asiyoistahiki haibadilishi
chochote hakika na ukweli. Hakika itabakia pale
pale mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa mali ile si
haki yake na ukweli ni kuwa mali itabakia kuwa
ni haramu inayompatia dhambi za uovu wake huo.
Kwa mantiki hii, hakimu muhalalishaji wa haramu
hali anajua na dhalimu muhalalishiwa haramu hali
nafsi yake inakiri kuwa haramu wawili hawa
watashirikiana katika dhambi za uovu huu.
Mwenyezi Mungu
anatukataza na kutuonya katika aya hii kula au
kuchukua mali ya mtu kwa njia ya batili yaani
kwa njia isiyo ya halali. Kula mali ya mtu katika
njia ya batili ni pamoja na kupokonya,
kupora,kudhulumu,kupokea rushwa na kadhalika.
Kwa nini Mwenyezi Mungu amesema:" WALA
MSILIANE MALI ZENU", akatumia neno KULA
badala ya KUCHUKUA. Neno KULA limetumika kwa
kuwa ndio makusudi na lengo kuu la
kuchukua/kupata mali. Mporaji anapopora ili ale,
dhalimu anadhulumu apate kula, mpokea rushwa
anapokea pia kwa ajili ya Tumbo. Hili ndilo
lengo la kwanza, kisha ndio hufuatia mengine
kama vile kuvaa,kujenga,kununua gari,shamba na
kadhalika. Ndio maana watu husikika wakisema
(Fulani anakula mali za watu) wakiimanisha:
Anachukua mali za watu bila ya uhalali,kwa njia
batili.
Mwenyezi Mungu
amewaumba wanadamu na akawapangia na kuwawekea
sheria zitakazoyatawala maisha yao katika
ulimwengu huu wa muda,ili waishi kwa
amani,salama na utulivu. Mwenye nguvu
asimdhulumu mnyonge wala mkubwa asimuonee mdogo.
Basi mfanyakazi anayepokea rushwa kwa ajili ya
kutoa huduma,huyu anaivunja misingi ya amani
katika jamii, anavuruga nidhamu/utaratibu wa
sheria. Huyu mbali ya kuwa ana hatia mbele ya
mahakama adilifu ya Mwenyezi Mungu pia anaikosea
jamii nzima kwa kuwa anapokea ujira kwa kuivunja
amani. Mtoaji wa rushwa pia haiepuki hatia kwa
kuwa kutoa anatoa ujira kufisidi/kuharibu
uadilifu. Mali anayoipokea mlaji rushwa ni moto
na ataadhibiwa kwa uchukuaji wa mali hiyo adhabu
kali kabisa, kwa sababu ya kuvunja kwake sheria
ambayo misingi yake mikuu ni uadilifu na amani.
Hebu uone ubaya na athari ya rushwa kwa jamii
kupitia mifano hali ifuatayo:
Serikali/Shirika
la umma limetangaza nafasi za kazi.
Wananchi wenye sifa zinazotakiwa wakajitokeza
kujaza nafasi hizo. Mtu aliyekabidhiwa na umma
dhamana ya kuhoji watu hawa na hatimaye
kuwaajiri wanaostahiki. Huyu anayapiga teke
maadili na muongozo wa kazi yake,badala ya
kuwachagua watu kwa sifa husika, yeye
anawachagua watu kwa vigezo vya udugu, na kwa
kupewa rushwa. Natija ya uchaguzi huu ni kuwapa
ajira watu wasiostahili, jambo ambalo
litasababisha utendaji mbovu usio na ufanisi,
utendaji utakaopelekea kufilisika na hatimaye
kufa kwa shirika ambalo ni mali ya umma.
Uharibifu wa mtu mmoja huyu mwenye maradhi
hatari ya rushwa unasababisha kuathirika kwa
jamii nzima ni kwa sababu hii ndiyo Bwana Mtume
–Rehema na Amani zimshukie –akaikemea vikali
rushwa aliposema "Mtoaji na mpokeaaji
rushwa (wataingia ) motoni". At-twabraaniy.
Utamuona leo
daktari anayetupilia mbali maadili ya kazi yake,
anavua utu wake na kuuvaa unyama. Anamuacha
mgonjwa kufa mbele ya macho yake eti tu kwa
sababu hakupewa chai (rushwa). Huu ndio ukweli
na sote tunishuhudia hali hii kila leo. Mdudu
rushwa ameiondosha kabisa huruma ndani ya moyo
wa daktari kiasi cha kuwa maisha ya binadamu
mwenziwe hayana thamani kama hakupewa rushwa. Ni
kutokana na athari hii mbaya ya rushwa ndio
Bwana Mtume –Allah amshushie Rehema na Amani
–akasema "Allah amemlaani mtoaji na
mpokeaji rushwa na mkaa kati yao". Ahmad
Hebu tuangalie
hakimu anayepewa dhamana ya kusimamia haki. Huyu
kwa sababu ya kitu kidogo alichopewa (rushwa)
anampa haki mtu asiyestahiki na kumnyima mwenye
haki au anamfunga mtu kwa dhuluma kwa sababu tu
kuna mtu anataka kumkomoa au anamuachia huru
mtuhumiwa aliyetiwa hatiani na sheria kwa ajili
ya kupewa rushwa.
Hizi ni baadhi
tu za athari nyingi za rushwa kwa jamii. Rushwa
ikienea katika jamii husika, tabia za watu
zitaharibika,utu na heshima vitatoweka na badala
yake unyama,chuki na uadui ndivyo vitaitawala
jamii hiyo kama tulivyoona katika mifano yetu
hai. Mla rushwa ni mtu mbaya na hatari sana
katika jamii. Huyu hana utu, hana haya wala
huruma na ndio maana Bwana Mtume hakumuonea haya
kumshushia laana za Mwenyezi Mungu. Ewe ndugu
yangu uliyelemazwa na maradhi ya rushwa hebu
jiulize na kisha ujihurumie. Jee, unaweza
kuibeba laana ya Mola wako? Kulaaniwa na
Mwenyezi Mungu maana yake ni kutengwa na Rehema
za Mola duniani na akhera , Je, utasalimika
ikiwa hukupata rehema za Mola wako? Kutokupata
rehema kunaamaanisha kupata ghadhabu je ndugu
yangu unao ubavu wa kuhimili ghadhabu za Mola
wako. Ikemee nafsi yako, acha kuanzia leo tabia
mbaya ya kupenda na kupokea rushwa kwa huduma
ambayo unawajibika kuitoa huku ukiitafakari
kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:-
"ANAYEFANYA
MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE,NA MWENYE
KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi)YAKE (vilevile)
NA MOLA WAKO SI DHALIMU (hata kidogo) KWA WAJA
(wake). [41:46]
Chagua
sasa,kuendelea kula rushwa kwa khasara na
maangamivu ya nafsi yako mwenyewe au kuacha kula
rushwa kwa faida na maslahi ya nafsi yako.
Kumbuka "Rushwa ni adui wa haki" na
mla rushwa ni "Adui wa Mungu, Mtume na watu
wote".
|