|
Assalaam Alaykum !
Leo tena Nasaha zako za wiki inakuletea
Mimbari ya Eid, karibu ujikumbushe na kuongeza
maarifa yako juu ya swala ya Eid na siku yenyewe
Eid kwa ujumla.
SWALA YA EID
1) HUKUMU YAKE NA WAKATI WA KUSWALIWA
Swala ya Eid mbili, Eidil-Fitri { Eid ya
mfunguo mosi baada ya Ramadhani} na
Eidil-adh-haa {Eid ya mfunguo tatu baada ya
Hijja}au kama tulivyozoea kuiita "Eid
kubwa" na "Eid ndogo" ni SUNNA
MUAKKADAH. Mwenyezi Mungu ameamrisha katika
kauli yake: "HAKIKA TUMEKUPA KHERI NYINGI.
BASI SWALI KWA AJILI YA MOLA WAKO NA UCHINJE (
kwa ajili ya Mola wako)"[108: 1-2]
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie-
aliswali swala hii na akadumu nayo mpaka
anakufa. Na isitoshe amewaamrisha maswahaba bali
umma mzima kuiswali na ili kulisisitiza hilo
akawapa ruhusa wanawake na watoto kuhudhuria
swala hii. Swala hii ni nembo miongoni mwa nembo
za uislamu ambayo hudhihirisha imani na ucha
Mungu.
Tukivipekuwa vitabu vya historia
hatutashindwa kuona kuwa Eid ya kwanza kuswaliwa
na Bwana Mtume ilikuwa ni Eidil-Fitri katika
mwaka wa pili wa Hijra.
Wakati wa swala ya Eid huingia tangu kuinuka
kwa jua mpaka kupinduka kwake kwake yaani baina
ya saa 1:30 Asubuhi mapaka saa 6:00 Mchana.
Katika kipindi chote hiki inaweza kuswaliwa
swala ya Eid, LAKINI ni vema / bora swaala ya
Eidil-Adh-haa ikaswaliwa mwanzo wa wakati yaani
saa 1:30. Hii ni kwa ajili ya kuwapa watu fursa
ya kutosha kwenda kuchinja wanyama wao wa
UDHUHIA. Swala ya Eidil - Fitri ni ni kinyume
chake, hii ni bora ikacheleweshwa kuswaliwa ili
kuwapa watu fursa ya kuweza kutoa zakatul-fitri
(sadaka ya Fitri). Hivyo ndivyo alivyokuwa
akifanya Bwana Mtume. Amesema Jundub-Allah
amuwiye radhi - "Mtume-Rehema na Amani
zimshukie - alikuwa akituswalisha swala ya
Eidil-Fitri il-hali jua likiwa limepanda kiasi
cha (mtupo wa) mikuki miwili na swala ya
Eidil-Adh-haa kiasi cha mkuki mmoja" .
Al-Haafidh.
2) ADABU/ TARATIBU ZINAZOTAKIWA KUFUATWA
KATIKA SIKU YA EID.
- Muislamu anatakiwa katika siku za Eid
akoge, ajitie manukato (mwanamume) na avae
nguo nzuri za kupendeza. Mwongozo huu
unatokana na kauli ya Anas Ibn Maalik -
Allah amuwiye radhi, " Alituamrisha
Mtume wa Allah - Rehema Na Amani zimshukie -
katika Eid zote mbili tuvae nguo nzuri sana
tuwezazo (kuzipata), tujitie manukato mazuri
sana tuyapatayo na tuchinje mnyama mwenye
thamani kubwa tuwezavyo" Al – Haakim.
" Na Mtume wa Allah - Rehema na Amani
zimshukie - alikuwa akivaa burda (kishali)
cha rangi ya wino (light blue) katika Eid
zote" As - Shaafiy.
- Ni suna kula kwanza kabla ya kwenda
kuswali swala ya Eidil-Fitri kama ambavyo si
suna mtu kula kabla ya kuswali swala ya
Eidil - Adh-haa bali suna ni kuswali kwanza
ndipo ale kama ilivyithibitishwa kutoka kwa
Bwana Mtume.
- Kuleta Takbira kwa wingi tangu usiku wa
Eid zote mbili. Takbira za Eidil - Fitri
huendelea mpaka baada ya swala tu, muda wake
huwa umeisha. Ama zile za Eidil-Adh-haa
hudumu mpaka siku ya mwisho ya kuanikwa
nyama {Alasiri ya mwezi 13 - Mfunguo tatu}
Takbira za Eid ni kusema:- ALLAAHU AKBAR
ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR . LAA ILAAHA
ILLAL-LAAH WALLAAHU AKBAR . ALLAAHU AKBAR
WALILLAAHIL-HAMDU. ALLAAHU AKBAR KABIYRAA .
WAL-HAMDU LILLAHI KATHIYRAA.
WASUB-HAANALLAAHI BUKRATAN WA ASWIYLAA. LAA
ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAU. SWADAQA
WA’ADAU. WANASWARA ‘ ABDAU . WA A’AZZA
JUNDAU WAHAZAMAL - AHZAABU WAHDAU. LAA
ILAAHA ILLAL-LAAHU. WALAA NA-'BUDU ILLAA
IYYAAU MUKHLISWIYNA LAHUD - DIYN WALAU
KARIHAL- KAAFIRUUN.
ALLAAHUMMA SWALLI ALAA SAYYIDNAA MUHAMMAD
WA ALAA AALI SAYYIDNAA MUHAMMAD . WA ALAA
ASW-HAA BI SAYYIDNAA MUHAMMAD WA ALAA
ANSWAARI SAYYIDNAA MUHAMMAD WA ALAA
DHURRIYATI SAYYDINAA MUHAMMAD . WASALLIM
TASLIYMAN KATHIRYRAA.
Takbira hizi ni kwa mujibu wa Mwenyezi
Mungu Mtukufu; " NA MTAJENI ALLAH
KATIKA ZILE SIKU ZINAZOHISABIWA" [ 2;
203 ]
Na kauli yake , "HAKIKA
AMEKWISHAFAULU ALIYEJITAKASA (na mabaya ) .
AKAKUMBUKA JINA LA MOLA WAKE NA
AKASALI" [ 87; 14 -15 ]
Na kauli yake; "....NA KUMTUKUZA
ALLAH KWA KUWA AMEKUONGOZENI ...." [ 2:
185 ]
- Ni suna kwenda msikitini kwa njia moja na
kurudi kwa njia nyingine isiyokuwa ile ya
kwendea. Amesema Jaabir - Allah amuwiye
radhi - " Alikuwa Mtume - Rehema na
Amani zimshukie - alibadili njia inapokuwa
siku ya Eid " Bukhaariy
- Ni suna swala ya Eid kuswaliwa uwanjani
mahali pa wazi ila kama kuna dharura ya mvua
na kadhalika, hapo ndipo inaweza kuswaliwa
msikitini. Hii inatokana na kudumu kwake
Mtume kuiswali jangwani kama ilivyopokewa na
Bukhaariy na Muslim.
- Kadhalika ni suna waislamu kupeana mikono
siku ya Eid. Muislamu amwambie nduguye (
TAQABBALALAAHU MINNAA WA MINKA ) (Mwenyezi
Mungu atutakabalie sisi na nyinyi ibada
yetu.). Hivi ndivyo ilivyopokelewa kwamba
maswahaba wa Mtume wlikuwa wanapokutana siku
ya Eid huambizana: " Taqabbalal-laahu
Minnaa waminkum" Ahmad.
- Hakuna makosa kutanua katika malaji,
vinjwaji na pumbao la halali,. Haya ni kwa
mujibu wa kauli ya Mtume - Rehema na Amani
zimshukie-aliyosema katika Eidil - Adh-haa.
" Masiku ya kuanikwa nyama ni masiku ya
kula na kunywa na kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mtukufu" Muslim.
Masiku ya kuanikwa nyama ni mwezi 11, mwezi
12 na mwezi 13- Mfunguo 3. Na kwa kauli ya Anas
- Allah amuwiye radhi; Mtume wa Rehema na Amani
zimshukie - alipofika Madina aliwakuta wana siku
mbili maalum za kucheza na kufurahi. Mtume
akawaambia; " Mwenyezi Mungu
amekubadilishieni siku mbili hizo kwa ( kukupeni
) siku mbili bora zaidi kuliko hizo; siku ya
Eidil- Fitri na Eidil - Adh-haa" Nasaai.
Na kwa kauli ya Mtume alipomwambia Abu Bakri
alipowakemea wajakazi wawili waliokuwa wakiimba
mashairi nyumbani kwa Mama Aysha siku ya Eid:
"Ewe Abu Bakr kila watu wana sikukuu yao,
na leo ni sikukuu yetu" Bukhaariy
MAWAIDHA YA EID
Ndugu zanguni waislamu, Asslaam Alaykum!
Himda njema zote zinamstahikia Allah na
Rehema na Amani zimuendee Nabii Muhammad,
Maswahaba na aali zake.
Ama baad
Ndugu zanguni waislamu, sote tunakubaliana
kwamba siku ya Eid ni siku ya furaha, ni siku
ambayo mmehalalishiwa kula na kunywa mchana
baada ya kumalizika kwa mfungo mtukufu wa
Ramadhani. Ni siku ya watu kuvaa vizuri. Hebu
itegee sikio pamoja nami kauli yake Mtume -
Rehema na Amani zimshukie: " Inapokuwa siku
ya Eidil-Fitry, malaika hukaa mwanzoni mwa njia
wakalingana: Damkeni enyi waislamu, enendeni kwa
Mola Mkarimu aneemeshaye kisha hulipa thawabu
juu ya neema hizo.
Mmeamrishwa kusimama usiku kuswali (taraweh)
mkasimama na mliamrishwa kufunga mchana
mkafunga. Na mkamtii Mola wenu pokeeni zawadi
zenu. Wanapomaliza kuswali hunadi mwenye kunadi.
Eeh hakika Mola wenu amekwisha kusameheni, basi
rejeeni majumbani mwenu hali ya kuwa mmeongoka.
Nayo ni siku ya zawadi na siku hii huitwa
mbinguni siku ya zawadi"
Siku ya Eid ni siku ya mahafali. Waislamu
wamehitimu mafunzo yao ya mwezi mmoja katika
Chuo Kikuu cha Ucha -Mungu (Swaumu). Leo ndio
siku ya kukabidhiwa na kutunukiwa vyeti wahitimu
na leo ndio siku kila mtu atajua matokeo ya
mafunzo yake kama amefaulu au amefeli. Hili
litajulikana kutokana na namna
atakavyoisherehekea siku yake hii ya Eid.
Ndugu zanguni wapenzi, Katika kumalizika
mwezi mtukufu wa Ramadhani tunapata fundisho
moja kubwa sana, nalo ni kwamba , kama vile
tulivyoshuhudia mwanzo wa mwezi wa Ramadhani na
leo hii tunashuhudia kumalizika kwake. Tujiulize
na tutafakari hili linaashiria nini ? Ikiwa hili
linatoa ishara ya kitu/jambo, basi jambo hilo
litakuwa si jingine bali ni kwamba tujue kwa
yakini kuwa kila chenye mwanzo hakina budi kuwa
na mwisho isipokuwa ALLAH pekee YEYE ndiye asiye
na mwanzo wala mwisho. Tuukiri na kuukubali
ukweli huu usiopingika, tujue na tufahamu kuwa
kama ambavyo kila mmoja wetu alikuwa na siku
yake ya kuja kwake katika ulimwengu huu,
kadhalika anayo siku imngojeayo ya kuondoka
kutoka katika ulimwengu huu umalizikao. Tusome
na tuzingatie: "KILA KILICHOKO JUU YAKE
(ardhi na mbingu) KITATOWEKA (kitaondoka).
INABAKI DHATI YA MOLA WAKO ( tu mwenyewe) MWENYE
UTUKUFU NA HISHIMA" [55: 26-27]
Ndugu zanguni, tujiandae vema na siku hii
ngumu, nzito ambayo haikwepeki, hatuna budi
tutakutana nayo. Siku hii ndio mwanzo wa safari
ya kuhudhurishwa mbele ya mahakama yenye
uadilifu, haki na usawa, kwa ajili ya kuhesabiwa
na kulipwa kwa mujibu wa amali zetu
tulizozitenda hapa duniani bila kudhulumiwa mtu.
Kinachofuata baada ya hapo; "...KUNDI MOJA
LITAKUWA PEPONI NA KUNDI JINGINE MOTONI" [
42:7].
Kuwa katika kundi la peponi au motoni , huu
ni uchaguzi wako mwenyewe na hili litategemea
jinsi utakavyozichanga karata za maisha yako
katika ulimwengu huu. Utavuna pepo/moto kwa
akili, nguvu na mali yako mwenyewe. Tuiogope
ndugu zanguni siku hii; " NA IOGOPENI SIKU
AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE
WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOCHUMA; NAO
HAWATADHULUMIWA[2:281]
Naam, mwezi wa Ramadhani umemalizika na bila
shaka utatushuhudia mbele za Mwenyezi Mungu
Mtukufu kwa yote mema / mabaya tuliyoyatenda
ndani yake. Katika mwezi huu mtukufu sote
tumeshuhudia jinsi misikiti ilivyokuwa ikijaa
waumini katika swala zote za fardhi hata swala
nzito na ngumu ya alfajiri. Misikiti ilikuwa
ikiamrishwa kwa kusoma sana Qur-ani Tukufu, na
kudhukuriwa sana Allah. Takriban wakati wote
usiku na mchana utawakuta waumini misikitini
wakifanya namna kwa namna ibada , na utaviona
vikundi vya ilmu, waumini wasomeshana.
Yote haya tumeyaona ndani ya mwezi wa
Ramadhani, leo mwezi umemalizika na yote
yamemalizika, huyaoni tena hadi Ramadhani ya
mwakani panapo uhai na majaliwa.
Eh! Hasara, msiba na majuto yaliyoje kwa waja
hawa, kana kwamba walikuwa wanauabudu mwezi wa
Ramadhani na sio mola wa mwezi wa Ramadhani.
Mwezi ukiisha hakuna tena kuswali, kufunga,
kusoma Qur-ani wala.... wala.... Hii ni dalili
na ishara ya wazi ya kutokukubaliwa swaumu na
amali zao nyingine walizozitenda ndani ya mwezi
wa Ramadhani. Kwani amali ya mja ikikubaliwa na
kupokelewa, Mola humzidishia mja huyo taufiki na
kutengenea, hapo ndipo utamuona kila siku
anazidi kuendelea kumtii Mola wake.
Ndugu zangu waislamu, ni muhali kabisa kwa
mtu aliyefunga kwa ikhlaaswi, halafu leo baada
ya swala ya Eid akawa anauaga msikiti, haswali
tena hadi Ramadhani ya mwakani ambayo hana
dhamana nayo. Ikiwa hivi swaumu ya mja huyu
haikumfikisha kwenye lengo lake ambalo ni
kumuandaa mja kuwa mcha Mungu. Tusome na
tuzingatie " ENYI MLIOAMINI ! MMELAZIMISHWA
KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA
WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA
ALLAH" [2:183].Ni ukweli usiopingika kwamba
mtu hawezi kuwa mcha Mungu bila ya kushikamana
na swala tano.
Ndugu zanguni, Mwenyezi Mungu aliwaamrisha
Malaika pamoja na Iblisi ambaye alikuwamo
kundini wamsujudie Nabii Adamu - Rehema na Amani
zimshukie - hali ya kumuamkia. Iblisi kwa
ushupavu na upasito aliokuwa nao alikataa
kuitekeleza amri ya Mola wake. Ni kwa sababu hii
tu, Mwenyezi Mungu akamfukuza na kumtoa huko
alikokuwa na akamtenga mbali na rehema zake
(akamlaani) na kesho akhera ataingia motoni
ikiwa ni jazaa ya inadi na kibri chake.
Basi wewe ndugu yangu mpenzi usotaka kuswali,
hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi kuliko Iblisi ?
Pengine utauliza kwanini ? Hii ni kwa sababu
Iblisi alikataa kumsujudia Nabii Adamu (sijida
ya maamkizi si ya ibada), wewe usioswali una
kataa kusujudia sijida ya ibada ya yule aliye
muumba Nabii Adamu. Iblisi alikataa kusujudia
mara moja tu, wewe usioswali unakataa kusujudia
mara 34 kila siku.
Hebu angalia tena adhabu aliyopewa Iblisi kwa
kuacha sijida moja tu, hii inamaanisha mwenye
kuacha sijida 34 kila siku anastahiki kupata
adhabu kali zidi kuliko aliyopewa Iblisi,
sikwambii tena usioswali wiki au zaidi.
Eeh ! Ndugu yangu kiumbe dhaifu wee! Ionee
huruma nafsi yako, acha ukaidi, huiwezi adhabu
ya Mola wako. Badili mwenendo wako sasa kabla
hujachelewa. Tusome na tuzingatie "....NA
BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA
INAYOENDELEA SANA" [ 20:127 ]
Pia kuna khatari kubwa ya kuwa kafiri mtu
asioswali. Isikize kwa makini kauli hii ya Bwana
Mtume - Rehema na Amani zimshukie " YE YOTE
atakaye acha swala kwa makusudi, bila shaka
atakuwa amekufuru".
Ndugu zanguni waislamu inasikitisha sana
jinsi waislamu tunavyoisherehekea sikukuu. Siku
ya Eid ndiyo siku ambayo waislamu wenyewe
wanautukanisha uislamu na kuudhihirishia
ulimwengu kwamba akthari/aghlabu ya wafanyao
mabaya ni waislamu.Mtu alikuwa hawezi kukesha
msikitini kufanya ibada, siku ya Eid atakesha
kwenye ulevi, atakunywa hadi atajimwagia, eti
anasherehekea kumalizika kwa mfungo mtukufu wa
Ramadhani, Sub-hanallah, na huyu si mwingine
bali ni yuleyule muislamu tuliyekuwa naye
msikitini katika kipindi chote cha Ramadhani.
Huyu haisherehekei Eid bali anausherehekea moto
wa Jehannam na huyu ndiye mtu aliyefeli vibaya
kabisa katika mafunzo yake katika Chuo Kikuu cha
Ucha Mungu (swaumu) Siku ya Eid ndiyo siku
ambayo utaona madada zetu wamevaa mavazi ya
ajabu ajabu na kuwa kama mbuzi wasio na mchunga
kwa kuuza utu wao. Ili muradi siku ya Eid, watu
watashindana katika kumuasi Mola wao. Wote hawa
nawaasa kwa kauli hii ya Allah " AMA YULE
ALIYEASI NA AKAPENDA ZAIDI ( akayafadhilisha
maisha ) YA DUNIA. BASI KWA HAKIKA JAHANAMU
NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE NA AMA YULE
ALIYEOGOPA KSIMAMISHWA MBELE YA MOLA WAKE,
AKAIKATAZA NAFSI YAKE NA MATAMANIO (maovu) BASI
(huyo) PEPO NDIO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE. [ 79:
37-41]
Ndugu zangu waislamu funga ya Ramadhani
imemalizika LAKINI hii haiaaamaanishi kuwa
muislamu hana tena fursa ya kufunga hadi
Ramadhani ya mwakani. La hasha bali anayo fursa
ya kujipendekeza na kujikurubisha zaidi kwa
Molaa wake kwa kufunga funga mbalimbali za suna.
Miongoni mwa funga hizo za suna ni kufunga siku
sita za mfunguo mosi (shawwal). Imepokelewa
hadithi na Abu Ayyuub - Allah amuwiye radhi-
kwamba Mtume - Rehema na Amani zimshukie -
amesema, " Atakayeufunga mwezi wa
Ramadhani, halafu akaufuatishia siku sita za
mfunguo mosi itakuwa kama kufunga mwaka
mzima" Muslim.
Ndugu zanguni, hayo ndiyo malipo na ujira
adhimu wa funga ya Ramadhani iambatanayo na
funga ya siku sita za mfunguo mosi. Tumeweza
kufunga mwezi mzima, tutashindwa kufunga siku
sita! Ikiwa tuna nia ya kujipendekeza na
kujikurubisha kwa Mola wetu Mtukufu
hatutashindwa haya shime ndugu zanguni. Mwisho
tunakutakieni Waislamu wote popote mlipo
ulimwenguni kheri, baraka,amani furaha na radhi
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sikukuu yenu
hii ya Eid. Tunawapongezeni nyote kwa kusema;
Wasalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu.
|