i)
ADABU/TARATIBU
ZA KULA NA KUNYWA :
Muislamu
hukiangalia chakula na kinywaji kwa jicho la kukizingatia kuwa ni wasila/chombo cha
kumfikishia katika malengo ya maisha yake ya siku hata siku. Muislamu hakitazami
chakula/kinywaji kwa dhati yake kama ndio upeo wa makusudio na malengo yake. Kwa hiyo
basi, Muislamu haishi ili ale na kunywa bali anakula na kunywa ili aishi. Anakula na
kunywa kwa ajili ya kuhifadhi usalama wa afya ya mwili wake, kwani ni kupitia mwili huu
ndio huweza kumuabudu Mola wake. Ibada hii ndio humfanya astahiki kupata utukufu,
mafanikio na neema za maisha ya milele ya akhera. Muislamu hali au kunywa kwa dhamira ya
kula na kunywa tu, au kwa matamanio, bali hali ila kwa kusikia njaa na kadhalika hanywi
ila kwa kiu. Na hii ni kanuni muhimu ya afya aliyotuwekea Bwana Mtume Rehma na
Amani zimshukie aliposema : Sisi ni watu hatuli mpaka tusikie njaa na tukila
basi hatushibi (kupita kiasi). Lau watu wa leo tungejilazimisha kuifuata kanuni hii,
basi tungeliepukana na maradhi mengi. Kwani asilimia kubwa ya maradhi yanayomsibu huanzia
tumboni, kutokana na kula na kunywa ovyo ovyo. Kwa hivyo basi, muislamu anapaswa
kujilazimisha kufuata taratibu za kisheria katika kula na kunywa kwake. Taratibu/adabu
hizi tutazigawa katika mafungu/sehemu tatu zifuatazo :
a) ADABU/TARATIBU
ZA KUFUATWA KABLA YA KUANZA KULA :
1. Kwanza kabisa
Muislamu ahakikishe anaandaa na kukipata chakula chake kwa njia za halali, kwa kuitekeleza
kauli ya Mola Mtukufu ENYI MLIOAMINI ! KULENI VIZURI TULIVYOKURUZUKUNI
[2:172]
Muradi na mapendeleo ya chakula kizuri ni chakula cha halali
na sio uzuri wa ladha. Kwani ladha hutofautiana baina ya mtu na mtu.
2. Anuie kwa kula
na kunywa kwake kupata afya na nguvu ya kumuabudu Mola wake ili apewe thawabu kwa
atachokila au kukinywa cha nia hiyo. Kwani jambo la MUBAAH hugeuka kwa nia njema kuwa TWAA
ambayo Muislamu hulipwa thawabu kwa kulitenda.
3. Aoshe mikono
yake kabla ya na baada ya kula.
4. Akiweke chakula
chake kwenye sahani/sinia chini na sio mezani, ka kuwa hili la kulia chini hupelekea zaidi
unyenyekevu. Na haya ni kwa mujibu wa kauli ya swahaba Anas bin Malik Allah amuwie
Radhi Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie hakupata kula
juu ya meza.
ZINDUKA : Si haramu kula chakula juu ya meza, bali SUNA ni
kula chini ukiwa umeketi mkekani/jamvini au katika busati na vitu kama hivyo.
5. Akae kwa
unyenyekevu wakati wa kula. Akalie matumbo ya nyayo zake, mguu wa kulia aunyooshe wima na
nyayo yake juu ya ardhi, na aukalie ule wa kushoto kama alivyokuwa akikaa Bwana Mtume.
{kielelezo}Bwana Mtume anatueleza namna ya ukaaji wake wakati wa kula, anasema : Sili
hali ya kuchegemea (kitu), hakika si vinginevyo mimi ni mja (Mtumwa wa Allah) ninakula
kama alavyo mja na ninakaa kama akaavyo mja Abu Dawuud na Tirmidhiy.
6. Aridhie na
kutosheka na chakula kilichopo na wala asikitie kasoro/aibu. Kikimpendeza akile na kama
hakikumridhia basi na akiache bila ya kutoa maneno yasiyo mazuri. Haya ni kwa mujibu wa
hadithi iliyopokelewa na Abuu Hurayrah Allah amuwie radhi - : Mtume wa
Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie kamwe hakupata kukitia aibu/kasoro
chakula akipendezewa hukila na kisipompendeza basi hukiacha Abu Dawuud na Tirmidhiy.
7. Asile peke yake
bali ale pamoja na wenziwe; mgeni, mkewe, wanawe, au hata mtumishi wake. Hii haimaanishi
kwamba kula peke yake ni haramu, la hasha bali ni vyema kula pamoja na wengine. Hili
linatokana na kauli ya Nabii Muhammad Rehema na Amani zimshukie aliposema :
Kusanyikeni pamoja katika chakula chenu mtabarikiwa ndani yake Bukhariy na
Muslim. Kwa hivyo utaona chakula cha pamoja hubarikiwa, kinyume na chakula cha mtu mmoja
peke yake.
b) ADABU/TARATIBU
ZA KUFUATWA WAKATI WA KULA :
1. Muislamu
anatakiwa aanze kula kwa kupiga BISMILLAH kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie Atakapoanza kula mmoja wenu basi na alitaje jina la
Mwenyezi Mungu Mtukufu, akisahau kulitaja jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu mwanzoni mwake
(huko kula) basi aseme (pale atakapokumbuka) BISMILLAHI FIY AWWALIHI WA AKHARIHI (Kwa jina
la Mwenyezi Mungu mwanzoni na mwisjoni) Bukhariy na Muslim.
2. Amalizapo kula
amshukuru Mwenyezi Mungu aliyemruzuku. Kufanya hivyo ni kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie aliposema : Atakayekula chakula na kusema
{kiarabu}: (ALHAMDU LILLAHIL-LADHIY ATW-AMANIY HADHA WARAZAQANIYHI MIN GHAYRI HAWLIN
MINNIY WALAA QUWWAH)
Maana yake : (Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye
amenilisha (chakula) hiki na akaniruzuku bila ya uwezo wala nguvu zangu).
3. Amege tonge dogo
na alitafune vema kabla ya kulimeza. Ale sehemu inayomuelekea ya sahani. Huu ni
utekelezaji wa maneno ya Mtume Rehema na Amani zimshukie alipomwambia
(swahaba wake) Umar bin Salamah : Ewe kijana, mtaje Mwenyezi Mungu (uanzapo kula) na
kula kwa mkono wa kulia na kula katika sehemu (upande) ikuelekeayo Al-Bukhariy
4. Arambe sahani na
vidole vyake baada ya kula, kabla hajavipangusa kwa leso au kunawa. Haya ni kwa mujibu wa
kauli ya Mtume Rehema na Amani zimshukie - : Atakapokula chakula mmoja wenu,
asivipanguse vidole vyake mpaka avirambe Abuu Dawuud na Tirmidhiy.
5. Kikimdondoka
chochote katika akilacho, akiokote na kukipangusa kisha akile. Huu ni mwongozo wa Mtume
Rehema na Amani zimshukie alipotuambia : Litakapodondoka tonge la
mmoja wenu, basi aliokote, alipanguse na kulila na asimuachie shetani Muslim. Kwa
hivyo ni vema kabla ya kula kitandikwe kitambaa kikubwa kisafi au chochote kinachofanana
na kitambaa, ili chakula kitakapodondoka kidondokee hapo.
6. Asikipulize
chakula cha moto na wala asikile mpaka kipoe. Kadhalika asipulizie ndani ya maji wakati wa
kunywa bali apulizie nje ya chombo. Muongozo huu tunaupata kutokana na hadithi iliypokewa
na Anas bin Malik Allah amuwie Radhi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu
Rehema na Amani zimshukie alikuwa akipumua mara tatu katika kunywa Bukhariy
na Muslim. Maana yake anakunywa funda anapumua, kisha anakunywa tena na kupumua kisha
anamalizia kunywa na kupumua. Na hadithi iliyopokelewa na Abuu Said Allah
amuwie Radhi kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani zimshukie
amekataza kupulizia wakati wa kunywa. Tirmidhiy.
7. Asile zaidi ya
uwezo wake, yaani ajiepushe na kushiba sana. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuasa :
NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri) LAKINI MSIPITE KIASI, HAKIKA YEYE
(Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI (wapindukiayo mipaka) [7:31]
Pia kujiepusha kula sana ni kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume Rehema na
Amani zimshukie Hajapatapo mwanadamu kujaza chombo kilicho na shari kuliko tumbo
lake, vyamtosha mwanadamu vijitonge vitavyousimamisha uti wake wa mgongo. Kama hakufanya
hivyo (ikiwa hapana budi kula) basi theluthi moja iwe ni ya chakula na theluthi (ya pili)
iwe ni ya maji na theluthi (ya mwisho) iwe ni ya pumzi Ahmad, Ibn Majah na Hakim.
8. Asiwatazame
machoni wenzake wakati wa kula ili wasione haya, wakashindwa kula. Bali inatakiwa
ayainamishe macho yake kwenye chakula.
9. Asifanye jambo
lolote litakalowachefua wenzake wakati wa kula. Asiukungutie mkono wake katika
sahani, asikiinamie chakula kisije kikadondoka kitu kutoka mdomoni mwake na kuangukia
sahanini. Akiungata mkate kwa meno yake, basi asikichovye kipande kilichosalia
katika bakuli la mchuzi. Kadhalika anatakiwa asizungumze na kuvitaja vitu vichafu vichafu
vitakavyochefua wenzake wakati wa kula kama vile mavi na mfano wake.
c) ADABU/TARATIBU
ZA KUFUATWA BAADA YA KULA :
1. Aurambe mkono
wake, kisha aupanguse kwa kitambaa au anawe.
2. Akiokote chakula
kilichodondoka wakati wa kula, kwani kufanya hivyo ni katika kushukuru neema ya Mwenyezi
Mungu, mtoa riziki.
3. Ayachokoe meno
yake, kisha asukutue ili kukiweka safi kinywa chake ambacho kwacho humdhukuru Mola wake na
huzungumza na wenzake. Pia usafi wa kinywa ni kwa manufaa ya meno ili yaendelee kuwa
salama na imara.
4. Amshukuru
Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kula au kunywa kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume
Rehema na Amani zimshukie Pigeni BISMILLAH mnapotaka kula na mumshukuru
mnapomaliza . Na amesema Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie Atakapomaliza
kula mmoja wenu aseme : {kiarabu}
(ALLAHUMMA BAARIK LANAA FIYHI, WAZIDNAA KHAYRAN
MINHU) (Ewe Mola wa haki tubarikie katika chakula hiki, na utuzidishie
kilicho kheri/bora kuliko hiki)
Na akinywa
maziwa aseme :
(ALLAHUMMA BAARIK LANA FIYHI WAZIDNAA MINU) (Ewe Mola wa haki, tubarikie katika
maziwa haya na utuzidishie)
Kwani
hakitoshelezi katika chakula na kinywaji ila maziwa Ahmad, Abuu Dawuud, Ibn Majah,
Tirmidhiy na Al-Bayhaqi kutoka kwa Ibn Abbas Mola awawie Radhi-. Yaani Maziwa ndio
CHAKULA KAMILI kinachoweza kuchukua nafasi ya chakula na maji.
5. Muislamu
anatakiwa asile njiani huku anatembea wala asile sokoni. Hii inatokana na kauli ya Nabii
Muhammad Rehema na Amani zimshukie Kula sokoni ni uduni